Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba ya bajeti iliyoko mbele yetu. Kwanza, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya na uzima, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazozifanya ndani ya nchi yetu, pamoja na viongozi wote wanaomsaidia Mheshimiwa Rais, kuanzia Makamu wa Rais mpaka Mwenyekiti wa Kitongoji kwa sababu wote wanafanya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru sana wananchi wa Tanzania ambao ndiyo walipakodi niwaombe waendelee na moyo huohuo. Ninampongeza pia Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya, Naibu Waziri na Katibu Mkuu na hasa wananchi wa Hai wamenituma niwashukuru kwa jambo zuri waliloliratibu la kuweza kupata Milioni 400 pale kwenye Kituo chetu cha Afya Kisiki wanasema ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nipongeze hotuba hii kwa kweli imekuja na mambo ambayo yanagusa wananchi, moja ya eneo ambalo linagusa mwananchi moja kwa moja ni kuondoa ada kwa Kidato cha Tano na cha Sita tunashukuru sana. Pia kubadilisha utaratibu ule wa manunuzi ambao mfuko wa simenti ukiitwa wa Serikali bei yake inapanda saa hiyohiyo, kwa hiyo jambo hili linaenda kunusuru fedha nyingi za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ule utaratibu wa magari mliouleta na lenyewe ni jambo lenye tija sana ninawapongeza. Mimi nitangulie kutanguliza maombi kadhaa kabla ya kuingia kwenye mchango wangu, mimi niombe Mheshimiwa Waziri mkatazame namna ya kupata fedha kwenye remittance wale Watanzania wanaofanya kazi na wanaishi nje ya nchi ya Tanzania, ni namna gani tunaweza kupata pesa kwao. Wenzetu wa Bangladesh asilimia 12 ya Pato lao la Taifa wanapata kutoka kwenye remittance, mimi niombe mkakae na wataalam muone namna ambavyo tunaweza tukapata fedha hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi la pili mmeweka fedha kwenye mazao mengine ya ruzuku, zao la kahawa mkaacha! Zao la kahawa hili linatuletea fedha nyingi za kigeni niombe Mheshimiwa Waziri utakapokuja kuhitimisha hapa nenda kaa na wataalam wako uone namna ya kuongeza zao la kahawa na lenyewe liweze kupata ruzuku. Pia niombe nimekuwa nikisema mara kadhaa, sasa hivi huku mbele nitachangia kuhusu Wizara ya Kilimo. Tumeweka fedha nyingi pale na tunataka kuongeza thamani mazao yetu lakini mazao haya wateja wetu wako nje ya nchi na mazao ya mbogamboga usafiri wake mzuri ni usafiri wa ndege, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri unikubalie kwamba kiwanja cha ndege cha Kilimanjaro, ndege zile za mizigo tu zitue maegesho yawe bure na kutua ndenge kuwe bure ili tuweze kuvutia ndege nyingi za mizigo zije pale zichukuwe mazao yetu haya ambayo tumeweka fedha nyingi yaweze kupata wateja nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ni ombi ofisi ya ombudsman tuliosema ambao ni msuluhisho wa masuala ya kikodi, tuombe Tarehe Moja ianze na siyo lazima ianze na watumishi wote, mnaweza kuanza na watumishi wachache ili mradi tu waweze kuanza na mkisema muanze kuhangaika ofisi hapo Chuo Kikuu cha UDOM kuna maofisi wapelekeni hapo waanze kazi mara moja ili kuondoa adha kwa wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kuhusu Wizara ya Kilimo, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kusikia maoni yetu Wabunge, kutoka kwenye Bilioni 294 hadi Milioni 954 haya ni mapinduzi makubwa sana kwenye Bajeti ya Kilimo. Tafsiri yake ni kwamba tunaenda kuongeza pato la Taifa, kwa sababu formula ni kwamba unapoongeza uzalishaji maana yake Pato la Taifa letu linaenda kukua. Ninamuomba Mheshimiwa Waziri fanya ufanyavyo fedha hizi zije kama zilivyo, kwa sababu kama tutapanga hapa halafu hazitakuja tutakuja kualaumu Wizara ya Kilimo kumbe hakupeleka fedha. Ili kusudi tuhakikishe kwamba tunaenda kupata mbegu ya Kitanzania, wataalam wetu hapa Tanzania kwenye taasisi inayoshughulika na mbegu wafanye utafiti tupate mbegu za kwetu ambazo ni rafiki na ikumbukwe Mheshimiwa Waziri hii ni biashara shindani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapoenda kuchukuwa mbegu huko hatukatai ni vizuri ni majirani zetu lakini tuko kwenye ushindani wa kibiashara, tuhakikishe fedha inayotengwa kwa ajili ya utafiti wa mbegu inakwenda kwa wakati, kwa sababu mbegu ndio kitu cha kwanza kinachotangulia. Fedha zilizopangwa kwa ajili ya skimu ziende ili mwisho wa siku tuweze kufanya kilimo biashara lakini chenye tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine zuri Wizara ya Kilimo imetenga fedha kwa ajili ya kutengeneza vile viwanda vya kuongeza thamani ya mazao common use facility, niombe hizi fedha ziende mara moja ili zikajengwe bahati nzuri na sisi Hai ni wanufaika kitajengwa pale Hai. Tuweze kujenga wakulima wetu waende wafungashe mazao yao, wauze yakiwa yameongezwa thamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine tumekuwa tukipewa taarifa hapa kwamba nchi yetu ina dalili ya kupata mafuta lakini tayari tumekwisha kupata gesi, nimezungumza na wataalam wakasema tunahitaji Bilioni 40 kufanya utafiti kisima kimoja, hivi kwa nini tusifunge mkanda tukaamua sasa tutenge fedha za kutosha tufanya utafiti tuangaike na haya mafuta kwa sababu tuna uhakika tukiyapata tutainua uchumi wetu na tutaondokana na matatizo makubwa kama ambayo yametukumba hivi karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mungu ametujalia na dalili zinaonekana mimi niombe sana Mheshimiwa Waziri inawezekana sio bajeti hii pale utakapopata pesa nyingine, nje ya bajeti tunayoipitisha hapa, kipaumbele kiwe ni namna gani tunaweza kufanya utafiti, tuwe na mafuta yetu, tuwe na gesi yakujitosheleza ya kwetu itatusaidia sana. Pia sambamba na hilo nchi hii imejaliwa madini mengi, mimi niombe namna ambavyo tunaendesha biashara hii ya madini bado haijawa yenye tija ya kutosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tuna shida gani ya kuchagua Mikoa Mitatu au Minne tukasema Mkoa wa Mbeya, Geita, Mikoa inayofanana na hiyo yenye madini mengi, tukaenda kufanya tathmini geological survey tukapata ripoti ya madini tuliyonalo tukauza leseni ambazo zimefanyiwa utafiti kuliko hivi sasa hivi tunauza leseni ambazo hazijafanyiwa utafiti ninajua ni gharama kubwa lakini sisi tu-invest pale hela ile itarudi ukizua leseni ambayo imefanyiwa utafiti utapata fedha ya haraka halafu ambayo haina risk yeyote lakini tuwe tumefanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niombe nimekuwa nikisema Mheshimiwa Waziri wewe ni mtaalam wa uchumi nchi hii tuna shida gani ya kutengeneza National agenda za kwetu tuwe na mipango ya miaka 100? nchi hii imejaa wachumi wengi wako Vyuo Vikuu, na nitumie nafasi hii kuwaomba Wachumi nchi hii waje na andiko la kutusaidia ni namna gani tunaweza tukawa na mipango yetu ya miaka 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunayo maono nakubali ya miaka 20, lakini tunayo maono ya miaka mitano, mwaka mmoja mmoja lakini tutoke hapo ili kuweka nguzo ya uhakika tunaposema Serikali yetu tunataka tuimarishe kilimo basi tuweke mipango ya muda mrefu ambayo itafungwa kisheria, yeyote atakayekuwa Kiongozi wetu atasimamia mipango hii bila kuipindisha. Mheshimiwa Waziri naomba kipindi chako wewe ni Mchumi hebu anzisha jambo hili ili tuone litafikia wapi, watakuja wengine watakuja wataendelea ulipoishia wewe lakini usikubali kuondoka kwenye Wizara hii sasa hivi bila kuacha mpango huu umekaa vizuri. Nchi hii iwe na mipango ya muda mrefu miaka 100 na tufanye mabadiliko ya sheria jambo hili linawezekana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme kuhusu watumishi ambao tumesema hapa, kwamba watumishi wale ambao wako kwenye uteuzi, wakitoka kwenye teuzi zao warudi kwenye utumishi wa umma wa kawaida. Nashauri kwa kuwa mtumishi huyu atakuwa ameondoka kwenye utumishi wake wa umma wa kawaida akaenda kwenye uteuzi kuna miaka ambayo hakupanda madaraja, anaporudi basi apewe kwanza promosheni zake kwa kipindi kile ambacho alikuwa nje ya utumishi halafu ndiyo abaki pale, kuliko kumrudisha huku amefanya kazi labda alikuwa Afisa Utumishi akateuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya amekuwa Mkuu wa Wilaya kwa miaka ishirini au miaka kumi akirudi akaanzie tena daraja la pili, hii siyo sawa. Apandishwe promosheni zake kwanza, halafu ndiyo ambapo anaweza kubaki kwenye cheo chake.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine niombe sana, kule Hai walifanya tathmini muda mrefu sana ya Daraja lile la Kikafu ambalo ni Barabara ya Moshi – Arusha, wananchi wamesimama muda mrefu hawajalipwa fidia zao na nimepita kwenye hotuba ya Waziri, sijaona mahali ameweka. Nimwombe Mheshimiwa Waziri atafute fedha hii na bahati nzuri mradi ule ni wa wadau, atafute fedha hii alipe wananchi wale fidia na lile Daraja la Kikafu liweze kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe jambo lingine, Chuo chetu cha SUA tafadhalini sana. wamezungumza Wabunge hapa, ifike mahali Mheshimiwa Waziri apokee maoni yetu, Chuo cha SUA kiwe Chuo cha Kilimo kweli kweli, wawapelekee fedha wafanye kazi yao…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Mafuwe, kengele ya pili hiyo.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naomba kuunga hoja mkono. (Makofi)