Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa hii ya kuchangia kwenye Bajeti Kuu ya Serikali. Napenda kuanza kwa kuipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea bajeti ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti Kuu ya Serikali napenda kuchangia katika maeneo manne ambayo yaligusiwa katika hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali. Eneo la kwanza ni matumizi ya TEHAMA na internet. Naipongeza Serikali kwa kutambua umuhimu wa matumizi ya TEHAMA na internet katika utekelezaji wa kazi zake na uamuzi huu utapelekea kuongeza chachu katika kufikisha huduma ya TEHAMA na internet katika maeneo yote nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tufanikishe hilo kwa uharaka, napenda kurejea ushauri niliotoa wakati nachangia kwenye bajeti ya Wizara inayosimamia masuala ya TEHAMA kwamba wakati umefika sasa Serikali itambue community networks kama njia mbadala ya kufikisha huduma ya internet kwenye maeneo ambayo bado hayajaunganishwa. Katika hili nina habari njema, wiki iliyopita katika Mkutano Mkuu wa Maendeleo ya Mawasiliano Duniani uliofanyika Kigali na nashukuru kwamba Mheshimiwa Waziri Nape Nnauye alikuwepo kwenye mkutano ule, Nchi zote Wanachama wamepitisha Azimio namba 37 ambalo limetambua community networks kama njia mbadala ya kufikisha haraka huduma ya TEHAMA na internet kwenye maeneo ambayo bado hayajaunganishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kusisitiza kwa Serikali, ili tutimize dhamira hii ya Serikali ya kutumia TEHAMA na teknolojia katika maeneo yote ikiwemo maeneo ya pembezoni, basi wakati umefika pia na Tanzania tutambue rasmi community networks kama njia mbadala.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo langu la pili, napenda kuishukuru Serikali kwa kuamua kuanzisha dirisha maalum la kuhudumia watoto wanaotoka kwenye kaya maskini katika Mfuko wa Maendeleo wa TASAF. Hapa narejea wakati nachangia katika bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, nilipendekeza kwamba Serikali ione namna gani ya kutumia Mfuko huu wa TASAF kuwezesha watoto wa kike wanaotoka kwenye kaya maskini wapate msaada wa taulo za kike ili wasiendelee kukosa shule kwa sababu ya kuwa kwenye hedhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akihutubia, alisema kwamba dirisha hili jipya kwa ajili ya watoto wanaotoka kwenye kaya maskini litatumika kuwawezesha watoto wanaotoka kwenye kaya maskini kupata mahitaji maalum. Hivyo ningeomba kwa unyenyekevu mkubwa wakati Mheshimiwa Waziri anakuja kuhitimisha hoja yake atuainishie bayana haya mahitaji maalum ni yapi na naendelea kusisitiza katika hayo mahitaji maalum ni muhimu sana suala la msaada wa taulo za kike kwa watoto wa kike wanaotoka kwenye kaya maskini lijumuishe ili mtoto wa kike asiendelee kukosa shule kwa sababu ya kuwa kwenye hedhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo langu la tatu, naishukuru sana Serikali kwa kupendekeza maboresho kwenye Sheria ya 148 ili kuwezesha Serikali kukusanya kodi za biashara za mtandao (online businesses) pamoja na digital services. Suala hili nilishauri hapa Bungeni mwaka jana na hii inadhihirisha kabisa kwamba kwa hakika Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ni Serikali iliyo sikivu na inaendelea kutupa moyo sisi Wabunge kuendelea kuishauri Serikali kwa ari na nguvu ili kuhakikisha kwamba tunachangia maendeleo endelevu ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili Serikali iweze kukusanya kodi ipasavyo, lazima pia tufanye maboresho kwenye Sheria ya VAT ili TRA waweze kutoza kodi makampuni ambayo yamesajiliwa nje ya nchi. Nitatoa mfano mdogo, DSTV wanatoa huduma hapa Tanzania, lakini hapa Nhini Tanzania kuna agent, pesa zote tunazolipa katika kuangalia DSTV zinalipwa Afrika Kusini na kanzidata ya wateja wa DSTV ipo Afrika Kusin. Kwa mantiki hiyo ni ngumu kwa Serikali yetu kupitia TRA kupata uhakika DSTV ina wateja wangapi hivyo kujua inatakiwa ilipwe VAT ya kiasi gani. Kwa hiyo pamoja na kwamba tunaenda kufanya maboresho ya hii Sheria 148 ni lazima Serikali ifanye haraka kuleta ile sheria ya data protection ili ndani ya ile sheria iwe ni lazima kwa kampuni hizi za kibiashara kutoa taarifa zao za wateja (sharing of debtor), kati ya hizi biashara na Serikali ili tuweze kupata uhakika maana zile data ni data za Watanzania iweje ziwe nje ya nchi na sisi ndani ya nchi tusiwe na access nazo. Kwa hiyo Sheria ya Data Protection ije ili tuweze kuhakikisha kwamba, kunakuwa hakuna mianya yoyote ya ukwepaji wa kodi katika biashara ambazo aidha zinafanywa online business ama zinatoa digital services au zinatoa huduma kwa kutumia satellite.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo langu la nne, naipongeza sana Serikali kwa uamuzi wa kwamba kila mtu kuanzia umri wa miaka 18 apate usajili wa TIN, kwa sababu usajili huu wa TIN utawawezesha vijana wetu kujiajiri ikiwemo na kupata leseni za udereva. Hata hivyo, natambua pia moja ya lengo la kufanya hivi ni kuongeza wigo wa walipakodi kwa maana ya kwamba kuanzia vijana wa miaka 18 watakapofikisha kipato kile ambacho kinaweza kutozwa kodi, basi wataweza kulipia kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa kwa unyenyekevu kabisa na kwa kutambua kwamba tunayo changamoto ya ajira kwa vijana, naomba kupendekeza kwa Serikali itoe msamaha wa kodi kwa biashara mpya zitakazoanzishwa au biashara zitakazorasimishwa za vijana kati labda umri wa miaka 18 mpaka 30 ili vijana ambao wamemaliza shule wanahitimu vyuo vya kati, wanahitimu Vyuo Vikuu waweze kujiajiri. Jambo hili linawezekana, Serikali inaweza ikatoa msamaha wa kodi kwa vijana walau kwa miaka mitatu ili itoe hamasa kwa vijana hawa kuanzisha biashara zao na kurasimisha. Naamini jambo hili linawezekana kwa sababu ikiwa Serikali inatoa misamaha ya kodi kwa wawekezaji kwa nini ishindwe kutoa misamaha ya kodi kwa vijana wetu wa Kitanzania ambayo itakuwa ni chachu ya wao kujiajiri, lakini vivyo hivyo itakuwa ni njia ya kupelekea kuongeza wigo wa walipakodi hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuhitimisha, naomba kwa unyenyekevu mkubwa sana nirejee suala la umuhimu wa Serikali kuweka msamaha wa kodi ya VAT kwenye pump za maji zinazotumia nishati ya jua (solar water pumps). Wakati Serikali inaendelea kupeleka jitihada ya kufikisha maji vijijini, inaendelea kufanya jitihada ya kufikisha umeme vijijini, ni muhimu sana kwa Serikali kuweka mazingira ambayo yatarahisisha upatikanaji wa maji, hivyo kufanikisha dhamira ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwatua akinamama ndoo kichwani. Vivyo hivyo suala hili la solar water pump pia lina mchango mkubwa sana katika sekta ya kilimo kwa maana ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, siku ya tarehe 9 mwezi Juni mwaka huu 2022 katika ziara ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Kagera katika mkutano wa kati yake na wananchi wa Bukoba mjini na Mkoa wa Kagera kwa ujumla niliwasilisha ombi kwake Mheshimiwa Rais la kuona namna gani ambavyo Serikali itaweka msamaha wa kodi kwenye hizi solar water pumps. Wakati anahutubia Mheshimiwa Rais alifanya rejea kwenye suala hili la VAT kwenye solar pumps. Mimi binafsi naamini kitendo cha Mheshimiwa Rais kufanya rejea kwenye suala la VAT kwenye solar pumps ni kiashiria tosha kwamba Serikali lazima iangalie jambo hili kwa jicho la kipekee.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri Dkt Mwigulu Nchemba atakapokuja kuhitimisha hoja yake, lakini pia katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2022/2023, jambo hili la msamaha wa kodi kwenye solar pumps ni jambo ambalo linahitaji liwekewe uzito. Natarajia kwamba ni jambo ambalo litakuwemo na Serikali italichukua kwa uzito wake ili kuhakikisha kwamba tunawatua akinamama ndoo kichwani, lakini pia tunahamasisha kilimo cha umwagiliaji ambacho ndiyo sera ya Serikali hii ya Awamu ya Sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na naunga mkono hoja. Ahsante sana.