Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ushetu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na kuweza kuendelea kutusimamia na kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais. Pia nikushukuru sana wewe binafsi kwa jinsi ambavyo unaendesha Bunge kwa hekima kwa busara. Nimshukuru sana vile vile Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa bajeti kubwa ambayo amevunja rekodi kati ya Marais wote waliowahi kuitawala nchi yetu, bajeti yake imejikita sana kuwasaidia wananchi wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kusamehe kodi kwa wafanyabiashara ambao sasa wamepewa wigo mpana wa kuendelea kufanya shughuli zao na kuwahudumia wananchi wetu. Kipekee sana nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Naibu wake, niseme kwamba amevunja rekodi hasa kwenye suala la kubana matumizi ya magari na amevunja rekodi kusimamia haya magari. Kwenye hotuba yake kama alivyosema ni kweli unakuta gari nyingi zinazunguka barabarani wakati mabosi wao wamepanda ndege kwenda Dar es Salaam, wamepanda ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Bukoba, wamepanda ndege kutoka Bukoba kuja Dodoma, halafu magari sasa yanawafuata kule gharama zake zinakuwa kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa hili, ningeomba sasa fedha hizi ambazo wanaenda kuziokoa, Mheshimiwa Waziri zielekezwe mahospitalini, zielekezwe kuwahudumia akinamama hospitalini. Fedha hizi zikienda hospitalini zitawasaidia sana akinamama wanaoenda kujifungua. Bado akinamama wanaambiwa kwenda na gloves hospitalini, bado akinamama wanaambiwa kwenda kununua dawa zingine, hatujajua na naomba hili niweze kulisema hapa hadharani, akinamama wanapoenda hospitalini wanaandikiwa vitu vingi vya kwenda navyo, sasa tunataka tujue ni vitu gani akinamama wanatakiwa aende navyo, akinamama hao hospitalini wanahangaika sana, akinamama hao hospitalini wanateseka sana. Pia watoto wadogo hopitalini wanapoenda wanateseka sana na kunakuwa na changamoto moja ambayo tunakutana nayo sisi hasa kwenye majimbo ya vijijini ni gharama gani ambapo mama anatakiwa afanye operation ni kiasi gani anatakiwa alipe. Kwa sababu katika maeneo mengi unakuta akinamama wanapofanyiwa operation gharama zinakuwa kubwa, wengine wanafanyiwa operation mpaka kwa 150,000, wengine operation mpaka kwa 400,000, wengine anafanyiwa operation mpaka kwa 500,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna issue ambayo naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha aiangalie vizuri, anafika mama hospitalini anaambiwa apumzike mpaka mfumo ukae sawa, mfumo umegoma, daktari ana-chat na simu, nurse ana-chat na simu, eti kwanza mfumo umegoma, sasa tujiulize ndugu zangu Wabunge tuko hapa, hivi uchungu unasubiri mfumo? Tuambizane hivi mtoto anapotaka kuzaliwa anasubiri mfumo? Ningeomba suala hili Mheshimiwa Waziri aliangalie, akinamama wanateseka, akinamama wanapewa rufaa kwenye hospitali zetu, kwenye zahanati zetu, wanaenda kwenye hospitali za rufaa, kwenye vituo vya afya, mtu anapopewa rufaa hali yake siyo nzuri, anafika pale anaambiwa mfumo haujakaa vizuri. Niombe, akinamama wanapoteza maisha katika hili suala la mfumo, tunaomba tuliangalie, anapofika mama kwa udharura wake ashughulikiwe kwanza wakati mfumo wao wanauandaa badala ya kuambiwa kaa hapo mfumo haujakaa sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Waziri wa Fedha, Dkt. Gwajima alitangaza suala hili kwamba vifo vinavyotokana na akinamama wajawazito na watoto lazima wajiridhishe Wizara ya Afya, lakini cha ajabu maneno haya yanaishia kwenye mtandao tu, hakuna anayeshuka chini kwenda kulifuatilia hili. Naomba hili suala lifanyiwe kazi hasa katika majimbo ya vijijini, ni changamoto kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia juzi kwenye hotuba ya Waziri wa Fedha, ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ameondoa tozo kwenye vifungashio vya pamba, akaondoa tozo kwenye vifungashio vya korosho, lakini hajaondoa tozo kabisa kwenye vifungashio vya zao la tumbaku, zao ambalo linaingiza fedha nyingi za kigeni hapa nchini. Mwaka huu tu zao la tumbaku pekee fedha ambazo zinakopwa benki ni zaidi ya dola milioni 86 ambazo zinaenda kuwahudumia wakulima na Mheshimiwa Rais ameweka ruzuku, lakini kuna tozo ambazo ziko kwenye vifungashio hasa magunia, kuna asilimia 35 ambayo ni ya import duty, ni gharama kubwa sana kwenye magunia haya ambayo wakulima wanaenda kutumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna VAT 18%, ukiipiga kwa magunia tu kwa bei ya dola 720 kwa pensheni cross inaingia kwenye dola 1146.96 kabla ya gharama za usafirishaji bado gharama za bandarini ukijumlisha gharama yake na gunia inakuwa na bei kubwa sana, lakini magunia haya yanaenda kutumiwa na wakulima wetu, magunia haya wanaenda kufungia tumbaku wakulima wetu na ndiyo wanazitumia wakulima wetu kuvunia tumbaku na mwisho wa siku tumbaku hii ndiyo inayoingiza fedha nyingi za kigeni.
Mimi ningeomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha hili suala la upande wa import duty kwenye magunia yetu vifungashio vya tumbaku viweze kupunguzwa viweze kuondolewa ili wakulima sasa tuwape favour ya kuongeza bei waweze kuona faida kwenye zao la tumbaku. Vile vile kuna tozo ya mionzi, tozo ya mionzi ni 0.2 kwa kilo kwa kila tumbaku inayosafirishwa nje ya nchi, lakini hawa watu mbaya zaidi hawako bandarini ofisi yao iko Arusha, ina maana mtu anaposafirisha tumbaku mpaka wapigiwe simu kutoka Arusha waende Dar es Salaam kutoa kibali, sasa inachelewesha usafirishaji na gharama yake inakuwa kubwa kinachofanyika sasa wanunuzi wanapunguza bei.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimwombe na nimshauri Mheshimiwa Waziri, tuangalie cha kufanya, tukiondoa hii kodi ya mionzi, tukaamua kuwekeza kwenye mjengeko wa bei, kwanza tukiondoa wanunuzi wataongeza bei, tumbaku yetu inanunuliwa wastani wa dola moja mpaka dola 1.6, lakini wenzetu Nchi za Malawi, Zimbabwe na washindani wetu Zambia, bei yao sasa iko kwenye dola tatu, dola tano mpaka dola nane kwa sababu kodi hizi nyingi wameziondoa. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kodi hizi aziondoe, halafu aziweke kwenye mjengeko wa bei. Mfano tu kama uzalishaji tukaenda tani 60 mpaka tani 200, tukiweka dola mbili tu kwenye kila kilo, tuna uwezo wa kukusanya zaidi ya dola 800,000 kwa mwaka. Ukibadilisha kwa fedha kwa rate ya leo, tuko kwenye zaidi ya trilioni moja. Sasa hebu tuangalie asilimia 0.2, hatukusanyi fedha nyingi usumbufu kwa wanunuzi, matokeo yake wanunuzi wetu wanaendelea kupunguza uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo linanisikitisha sana, zao la tumbaku linaingiza fedha nyingi sana, lakini juzi Waziri wa Afya amesema anaendelea kupiga marufuku matumizi ya tumbaku Tanzania na ni zao la kimkakati kwenye Serikali yetu. Hata kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, ukurasa wa 41 linasema Serikali inahakikisha kufikia mwaka 2025, tutatoka kwenye tani 60,000 tutaenda kwenye tani 200,000, sasa tutafikaje kama wakulima tunaendelea kuwachanganya hivi? Waziri anasema anapiga marufuku matumizi ya tumbaku, kwenye ilani inasema inahitaji kuongeza uzalishaji, tuondoke na lipi? Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo sasa ndiyo msahafu wetu wa Chama Cha Mapinduzi unasema tuongeze uzalishaji, lakini wengine tunasema tunapiga marufuku matumizi ya zao la tumbaku, wakulima hawa tunawachanganya na wanunuzi ambao wanaingia kutoka nchi za nje. Hivyo, ningeomba sasa tuangalie wapi ambao tunaweza tukasimama.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni riba za benki. Bado riba ya benki kwenye sekta ya tumbaku ni kubwa sana, bado ni asilimia saba kwa dola, ukizibadilisha leo ni zaidi ya asilimia 18 ya riba. Ningeomba mabenki yaendelee kupunguza riba, ni kweli juzi wametangaza ni asilimia tisa lakini asilimia tisa haiwafaidishi wakulima wadogo wadogo bado ni changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine masharti bado hawajayapunguza, unapunguza riba lakini masharti yanakuwa makubwa kwa wakulima wetu. Tungeomba sasa mabenki pamoja na kupunguza riba, wanaendelea kupunguza riba, lakini masharti yaendelee kupunguzwa ili wakulima wadogo wadogo waweze kukopa, wakulima wetu vijijini waweze kukopa, wafanyabiashara wadogo wadogo waweze kukopa na waendelee kufaidika, lakini tunaposema riba imepunguzwa lakini masharti yanaendelea kuwa magumu, haisaidii.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kukushukuru sana, kwa kweli suala la riba ya benki ni changamoto kubwa sana. Naomba sana sekta ya pamba inaingiza fedha nyingi pia na yenyewe naomba kodi zake ziendelee kuondolewa ili wakulima wetu wanaolima pamba waweze kufaidika na pamba. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuunga mkono hoja, nawapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri, wanaupiga mwingi na wanamshauri vizuri Mheshimiwa Rais, Ahsanteni sana, hongereni sana. (Makofi)