Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii na mimi niweze kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ya Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu na nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake nzima kwa hotuba nzuri iliyobeba dira, dhamira, maono na mwelekeo na huruma ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania, inatia moyo na tunachoweza kufanya ni kuendelea kumuombea Mheshimiwa Rais Mungu amuweke kwasababu kuna mahali tunapoelekea na kuna mwanga mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nimpongeze kwa kuyatafsiri yote haya malengo ya Mheshimiwa Rais kwa matendo katika kipindi cha mwaka mmoja huu, kusema kweli ile kauli ya unaupiga mwingi na wewe inakuhusu moja kwa moja. Mara nyingi mimi nasema Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu unakuwa huna baya isipokuwa inapokuja mambo yako ya ‘Utopolo’ tu lakini huko kwingine upo safi kabisa. Hongera! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ni nzuri hata hivyo kuna maeneo kadhaa ambayo mimi nahisi naweza kuweka senti hamsini zangu. Kwanza kabisa ni katika ukurasa wa 69 ambapo Mheshimiwa Waziri anapendekeza kuhusiana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri zetu kwamba tuikate kwa asilimia 50. Asilimia Tano iende kwenye kutengeneza miundombinu ya masoko ya Wamachinga. Kwanza, mimi niseme msingi wa sera ile, msingi wa ule mwongozo ilikuwa ni kuwawezesha wananchi kiuchumi, kuwakwamua kwenye umaskini, kuwaunganisha na Serikali yao moja kwa moja kwa kuwahakikishia kwamba hali zao za kiuchumi binafsi zinaimarika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ile imekuwa inafanya shughuli nzuri ina changamoto za hapa na pale lakini naamini suluhisho la changamoto zile si kuikata kwa asilimia 50 na kuirudisha kwenye Halmashauri, hili jukumu la kujenga miundombinu ya masoko ya wamachinga ni jukumu la Serikali, Serikali isilikimbie inabidi ilifanye kwa namna yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuchukua asilimia Tano kati ya asilimia 10 zile na kuirudisha Serikalini ni kuwapora akina Mama, Vijana na Watu Wenye Ulemavu fedha ambazo tulikuwa tumeshawaahidi na zinawasaidia kwelikweli. Mimi kwa mfano, Muheza pale mapato yetu ya ndani ya Halmashauri ni takribani shilingi bilioni 2.1 kwa hiyo, kiutaratibu tunatakiwa kutoa shilingi milioni 210 kila mwaka kwa ajili ya kuyawezesha makundi haya. Sasa pamoja na mzunguko na marejesho tunakaribia kutoa shilingi milioni 500. Makundi ambayo yananifuata mimi binafsi, makundi ambayo yanamfuata Mkurugenzi, yanamfuata Mkuu wa Wilaya kumuomba awasaidie kupata mikopo hii kwa ajili ya kujisaidia kwenye shughuli zao za kiuchumi ni mengi mno hata hiyo hela yote ambayo tunayo haiwezi kufika nusu ya haja tuliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, kusema ukweli Mheshimiwa Waziri wa Fedha ninakuomba hii asilimia Tano tusiiguse huku, tusipite njia hii haitoki na Serikali isikwepe kama kuna lolote ambalo lingeweza kufanyika kwanza, ningehisi kwamba ungetoka mwongozo mwingine wa hii fedha iongezwe kwa sababu inawasaidia moja kwa moja inamsemea vizuri Mheshimiwa Rais, inaisema vizuri Serikali, inasema vizuri Wabunge, Madiwani na Halmashauri zetu. Kwa hiyo, badala ya asilimia 10 pengine ingeenda kuwa asilimia 15. Serikali ifanye jukumu lake la kujenga miundombinu kwenye masoko ya wamachinga kwa fedha ambazo yenyewe itazipata wapi hatujui, lakini ihakikishe kwamba fedha hii haiguswi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama kuna uwekezano tena Serikali itoe ruzuku kwa Halmashauri zetu ambazo zinaingiza mapato kwa kiwango ambacho kimekusudiwa, kimekadiriwa basi zipewe ruzuku kwa ajili ya kufanya miundombinu hii ya wamachinga na siyo kutoa kwenye fedha hizi ambazo tulishaahidi makundi haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, pendekezo hili Mheshimiwa Waziri mimi niseme kwamba sikubaliani nalo na ninapendekeza tuachane nalo moja kwa moja lisirudi wakati wa majumuisho yako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nimemsikia pia akisema kwamba Pato la Wastani la Mtanzania kwa sasa ni Shilingi Milioni 2.8 na hii inamaanisha ni kama 233,000 kwa mwezi, hatupo vibaya kusema kweli dola elfu moja mia moja na kitu, lakini tunaweza kuimarisha kwa kulainisha zaidi mazingira wezeshi yanayomfanya Mtanzania wa kawaida kujiongezea kipato chake, kwenye hili bado hatujafanya vizuri sana kuna maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mfano; kule kwetu Muheza kuna Tarafa inaitwa Amani katika vijiji vya Fanusi, Magoda, Kisiwani na Kavaa kule Amani tulikuwa tunafanya miradi ya ufugaji wa vipepeo kabla ya mwaka 2016, halafu likatoka zuio 2016 la kuzuia miradi ile isifanyike, najua ukisema miradi ya vipepeo watu wanajua kama mnachukua vichujio vile mnaenda kukamata kwenye maua haipo hivyo ni miradi mikubwa ambayo ilikuwa inawasaidia sana wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kaka yangu Mheshimiwa January Makamba alipokuwa Waziri wa Mazingira alishatembelea miradi ile, somo yangu Mheshimiwa Hamisi Kigwangalla alipokuwa Waziri wa Maliasili alishajionea na juzi Mzee wangu Mheshimiwa Jerry Silaa akiongoza Kamati yake ya Uwekezaji walipita pia kule, na wote wamekuja na positive feedback kwamba miradi ile kwanza haina athari za kimazingira, vipato vya wananchi vinaongezeka, shughuli za kijamii kama maji na madarasa yamejengwa na miradi ile pia vilevile na inatusaidia kulinda misitu kwa sababu wananchi wanapata shughuli nyingine za kiuchumi za kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 mpaka sasa hivi ni miaka takribani Sita, pengine mwongozo ulitoka haraka haraka kwa sababu ulikuwa unataka kulinda swala, pundamilia na twiga wetu wasitoroshwe na ukawa haukupata muda wa kutofautisha kati ya pundamilia na vipepeo, lakini mimi ninachosema ni kwamba imechukua miaka sita sasa kwamba wataalam wetu wameshindwa kufanya kazi yao ya kuweza kutofautisha kati ya wanyama ambao wanatakiwa kulindwa wasitoroshwe kwenye nchi hii na hawa Vipepeo wanaoishi kwa siku 14. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mzigua mmoja hapa nyuma yangu anasema kwamba tunakaa kwa miaka Sita tunabishania kuhusiana na wadudu ambao wanaishi kwa siku 14. Miradi ile ilikuwa inawasaidia wananchi wa maeneo husika wanapata mpaka kiasi cha shilingi milioni moja kwa mwezi, sasa katika nchi ambayo pato la Mtanzania ni shilingi milioni 2.8 kwa mwaka mtu mmoja anapata milioni 12 kwa mwaka na bado tunamzuia, tunamfanyia roho mbaya tu ili mradi asifanye biashara hii kwa sababu ya uvivu tu wakushindwa kutenganisha kati ya swala na vipepeo hii siyo sawa! Hili eneo hatujafanya vizuri Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine unaona kama kuna masihara yanafanyika mpaka juzi Kamati ya Bunge ya Uwekezaji inayoongozwa na Mzee wangu Jerry Silaa ilitoa maagizo ya kwamba suala hili lifanyiwe kazi na miradi ile ifunguliwe, vipepeo waendelee kusafirishwa lakini mpaka sasa hivi hamna hata mtu mmoja aliyetingisha hata unywele! Sasa hii maana yake ni kama ni dharau kwa Bunge vilevile kwasababu kutenganisha kati ya vipepeo na Swala kusema kweli ….

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa taarifa mchangiaji kwamba siyo tu miradi ya kufuga vipepeo ina faida na tija kubwa kwenye maisha ya wafugaji ambao ni wananchi wa vijiji alivyovitaja, bali pia miradi hiyo inafaida kubwa sana kiuhifadhi na kimazingira. Pia miradi ya vipepeo haihusiani kabisa na sababu zilizopelekea kuzuiliwa kwa wanyama kusafirishwa nje ya nchi ambazo nyingi zilikuwa ni kelele na vilio vya wananchi baada ya kusikia kwamba Twiga na Pundamilia wanasafirishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa apokee taarifa hiyo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwinjuma taarifa hiyo.

MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kigwangalla will always come to my rescue, ahsante sana naipokea taarifa hii kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilichokuwa najaribu kusema ni kwamba hata watoto wa Darasa la Nne wangeweza kutofautisha kati ya Swala, Pundamilia na Vipepeo bila wasiwasi wowote, sasa sisi tuna watalaam ambao kabisa wamesomeshwa na hela za kodi za wananchi wa nchi hii, wameshindwa kufanya shughuli hii wakaandika madokezo na kupendekeza kwamba miradi ile iruhusiwe kwa miaka Sita, haya ni masihara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Bunge lako Tukufu miongoni mwa mambo ambayo tunatakiwa kuyafanya ni kuhakikisha tunawalegezea mazingira wananchi ya kujiingizia vipato vyao binafsi, hili likiwa mojawapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi naomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)