Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Issa Ally Mchungahela

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lulindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na afya kuweza kutekeleza majukumu yangu ya kila siku, pili nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii kulihutubia Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru mzalendo Namba Moja Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa uzalendo wake aliouonyesha ni uzalendo mkubwa sana, siku tulipoingia mkataba wa LNG ule hodhi, Mheshimiwa Rais alifanya kitu kikubwa sana ambacho aliitangazia Dunia kwamba yeye anafahamu sana diplomasia ya uchumi. Mheshimiwa Rais alisimama na kuwaambia wawekezaji kwamba wanapokuja Tanzania wahakikishe kwamba wanayo dhamira ya dhati ya kufanya biashara nasi na kwamba mkataba ule usije ukawa ni shere ya kutufanya sisi tuendelee na jitihada zetu zakutafuta mtu wa kutusaidia kushughulika na biashara ile. Ikawa wao wanaishikilia kwa maana waendelee kufanya biashara ile kwenye maeneo mengine walikowekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kauli hii imetoka mdomoni mwa Mheshimiwa Rais ni kauli nzito sana ile ni message ambayo inatakiwa watu wote tuzingatie kwa sababu ni message inayoonyesha uzalendo wa hali ya juu na kuonesha ni kwa jinsi gani yuko serious hasa katika suala hili la uwekezaji. Message kwa mtindo upi? Kwamba Tanzania kama nchi ni nchi tajiri sana na ina madini mengi lakini ina vitu vingi sana vitakavyoweza kutusaidia tukiamua kuvitendea kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lmessage ile ilikuja kwa Watendaji pia kuwa wakati wanatengeneza mikataba wawe makini sana kwa sababu failure inaleta hasara kubwa sana katika nchi, lakini message kwa dunia na wawekezaji kwamba wanapokuja Tanzania wajue kwamba biashara ya uwekezaji Tanzania ni very serious siyo kitu cha mchezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kauli ile ilinitia nguvu kama nilivyosema kuhutubia Taifa, dhana hii ya kuhutubia Taifa kuna baadhi hawaielewi lakini siwezi kuwalaumu kwa sababu ni dhana yenye maana pana sana pia ni mtambuka. Kwa kifupi tu ni kwamba ni dhana inayoendana na falsafa ya kuchunga fedha, falsafa ambayo inafanya kazi vizuri sana katika mazingira ya jamii yenye itikadi ya kizalendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema ni itikadi maana yake siyo wimbo wa kizalendo kwa maana itikadi ni dini na dini ni kuamini na kuabudu. Kwa hiyo, Watanzania lazima tuamini na kuabudu kwenye itikadi hii, tukifanya hivyo itatusaidia sisi kufanya yale tunayokusudia kuyafanya kwa maslahi ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tumepungukiwa sana na hii dhana ya uzalendo, tumekuwa hatuwezi kuweka maslahi ya Taifa mbele na hii imetokana na jinsi tulivyopita katika mapito mbalimbali kuelekea kutengeneza uchumi wa nchi hii, mapito ambayo yameleta athari mbalimbali ambazo hasi pamoja na athari chanya, sitazungumzia athari chanya kwa sababu zimegusa watu wachache lakini athari hasi zimegusa watu wengi kwa maana jamii nzima. Athari hasi zimetengeneza mitazamo hasi pia kwa jinsi tunavyoangalia mambo mbalimbali ya muhimu sana yanayohusu maendeleo ya nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tukiangalia dhana ya elimu, jamii ya nchi hii kutokana na athari zilizojitokeza inaiangalia elimu kuwa ni chombo cha kutengeneza fursa ya ajira ambayo itatengeneza fedha, kwamba mtu anayetafuta ajira ni lazima aje kuajiriwa baadaye lakini ajira hiyo impe fedha. Sasa mtizamo huu ukiuangalia umeleta msukumo ambao unaleta changamoto sana katika utendaji wa masuala mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, unakuta kwamba kila mtu anayetaka kusoma, anataka kusoma masomo ambayo anasema ni yenye mlengo wa deal, masomo yatakayo mpa ulaji na hata wazazi wamekuwa wakiwasukuma watoto wao kusomea masomo ya namna hiyo na kuacha masomo mengine, pia msukumo wa kikazi uko katika kutafuta fedha kwa maana mtu anahangaika kutafuta kwa njia yoyote ile, bila kujali hata kama fedha hiyo inapatikana kwa taratibu unaostahili au lah. Kwa hiyo, kumekuja na mtazamo kuwa mwajiriwa akimuibia mwajiri wake hata kama wizi huo utasababisha kufilisi kampuni au kama utasababisha kuyumbisha uchumi wa nchi, mtu huyo anaonekana kuwa ni mtu mjanja. Sasa suala hili ni baya sana ndugu zangu watanzania, tunatakiwa kwa makusudi kabisa tuwe na jitihada za kuepukana nalo jambo hili, tufanye jitihada kubwa sana kuwasomesha watoto wetu kuwaelimisha lakini kuwaelimisha kizazi chetu na jamii nyingine kwamba tunatakiwa tuifikirie nchi kwamba ndiyo pekee yenye maslahi, wewe usifikirie kwamba nchi itakufanyia nini lakini fikiria kwamba wewe utaifanyia nini nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwamba kumekuwa na mtizamo wa masuala tofauti tofauti, pia kumekuwa na changamoto sana katika usimamizi wa bajeti kwa mfano, Serikali kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi imelazimika kwa namna moja ama au nyingine kutekeleza miradi mkakati. Miradi hii kama tutaangalia mapato yetu ya ndani hatuwezi kuitekeleza au itachukua muda mrefu sana kuitekeleza, lakini kutokana na hiyo Serikali inalazimika kwenda kukopa. Mheshimiwa Rais kwa mfano, ameenda nje akajitahidi kukopa zile fedha zikija hapa ni fedha zinatakiwa ziende moja kwa moja katika miradi mkakati, kwa sababu kama hazitaenda huko zitatupa madeni makubwa ambayo itakuwa ni mzigo mkubwa kwa Serikali, nataka jambo hili lieleweke tukiangalia kwa mfano kwenye bajeti tunaweza tukalielewa jambo hili vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya Mwaka 2019 kwenda 2020 tulikuwa na bajeti ya kulipa Deni la Taifa takribani Trilioni 9.3 lakini bajeti ya Mwaka 2020 kwenda 2021tulikuwa na amount ya kulipa Deni la Taifa trilioni 10.4 bajeti ya mwaka 2021/2022 tulikuwa na bajeti ya kulipa Deni la Taifa shilingi trilioni 10.6 lakini kwenye bajeti ya mwaka huu kuna mapendekezo estimation ya kulipa Deni la Taifa takribani trilioni 9.093 ukijumlisha hii yote kwa miaka minne utakuta ni zaidi ya trilioni 39 fedha ambayo ni nyingi sana yaani ni bajeti nzima ya mwaka mzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unaweza ukaona kwa jinsi gani hapa fedha nyingi sana kama hii ingeweza ikatumika katika masuala mengine kwa mfano, tungekuwa tunatumia ile trilioni kumi ya kila mwaka kuchanganya na fedha nyingine ya maendeleo utaweza ukaona kwa jinsi gani fedha hii ingeleta tija kubwa sana, lakini kwa sasa hivi fedha hiyo tunalipa deni, hapo ndipo linapokuja umuhimu wa sisi kusimamia hii fedha ya madeni tunayoikopa kutoka nje ili kusudi ifanye kazi inayostahili pia kusimamia ni pamoja na kuhakikisha tunapunguza changamoto zozote zile za kuongeza riba katika madeni hayo, kama hatuwezi kufanya hivyo maana yake tunaingizia hasara nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye usimamizi, kuna suala la kwamba, Wabunge wanatakiwa kusimamia. Tukiangalia hapo kuna changamoto, changamoto ipo kwamba je, Mbunge anasimamiaje? Mipaka yake ya kusimamia ni nini, nini anatakiwa asimamie, nini hatakiwi kusimamia. Akienda kuangalia akakuta kuna changamoto anaziripoti kwa nani?

Je, Mbunge kama kazi hii ya kusimamia anatakiwa kuisimamia, anawezeshwa, ana uwezo wa ku-move kutoka eneo moja kwenda lingine kusudi kuangalia miradi hii jinsi inavyofanyika?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia pia usimamizi unapwaya kwa wenzetu Madiwani ambao ni muhimu sana. Tukiangalia Madiwani wao ndiyo wana nafasi kubwa ya kusimamia kwa sababu miradi hii inafanyika katika maeneo yao. Lakini Diwani ndugu zangu yuko hohehahe. Tukiangalia kimshahara, Diwani ni kama hana mshahara. Hata posho anayopewa Diwani haitoshi kabisa, kiasi kwamba suala la usimamizi kwake yeye linakuwa ni suala nyeti kabisa kwa sababu kuna wakati anaweza akatishiwa hata na Mtendaji kwa sababu tu hana kipato kizuri kiasi cha kumfanya Mtendaji amshawishi Diwani kufanya kitendo kibaya cha kuweza kubadili fedha ambayo inatakiwa kusimamiwa ikatumika vinginevyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye hili, ninalo la kuishauri Serikali. Tujaribu kufumba macho tuweze kumwezesha Diwani, kwa sababu Madiwani katika halmashauri 185 za nchi hii, kuna Madiwani 5,774 kiasi kwamba tukiamua tukatoa shilingi milioni moja kama mshahara wa Diwani kwa mwezi, tuna uwezo wa kumpa... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante, kengele ya pili hiyo. Mheshimiwa Kengele ya pili hiyo, ahsante.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sekunde mbili, tatu nimalizie, kwamba tukiweza kumlipa Milioni moja kila Diwani, tuna uwezo wa kulipa…

NAIBU SPIKA: Ahsante, mengine utaandika. Unaruhusiwa kuandika. (Makofi)

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.