Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye hotuba hii ya Bajeti. Nikianza na hotuba hii ya bajeti, nimeiona imejikita kwenye mambo mengi ikiwemo utalii, uvuvi na mambo mengine. Si mbaya kwa sababu tayari tunatafuta keki pana zaidi kwa ajili ya kugawanya mgawanyo wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi sijaona kipengele muhimu sana cha diplomasia ya uchumi. Kinachofanyika katika Taifa letu, Mama Samia Suluhu Hassan amekuwa kama assist kwenye ulingo wa mpira. Sasa wanatakiwa ma-striker wa kufunga magoli, hivyo, kila mtu acheze kwenye nafasi yake. Wakati tukiimba royal tour inaleta matokeo ni lazima sasa twende kwenye diplomasia ya uchumi tuangalie tutapataje watu kupitia royal tour, wawekezaji pamoja na fursa mbalimbali katika Taifa letu. Yeye amecheza nafasi yake na sisi tunatakiwa kucheza kwenye nafasi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikisema hayo, naenda moja kwa moja katika balozi zetu. Huwezi kuongelea diplomasia ya uchumi kama usipogusa balozi zetu nje ya nchi. Sasa hivi kuna shida kubwa katika balozi zetu nje ya nchi ambapo kuna uhaba mkubwa wa watumishi. Wale watu wanatakiwa wawe ndiyo reception yetu ya kupokea watalii, wawekezaji na watu wanaokuja kutafuta fursa na kutafuta sisi fursa kwenda nje, lakini kuna uhaba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukaguzi wa CAG wa Machi, 2022, inaonekana katika balozi sita kuna upungufu wa watumishi 26. Kiwango hiki ni kikubwa kwa sababu walitakiwa wawe watumishi 62 lakini wapo watumishi 38 tu. Hawa ndiyo tunaowategemea wawe reception yetu ya kupokea watalii na kupokea wawekezaji, hili ni janga. Wakati tunakwenda katika nchi ya Kongo, pia tulikutana na hii kesi ya upungufu wa watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilishauri, nikasema katika balozi zetu huwezi kuuza bidhaa zako ukazifungia chumbani, ni lazima uzitangaze. Katika balozi zetu hakuna kitengo ambacho ni cha habari. Ukiangalia blog mbalimbali za Wizara, ukiangalia kwenye social media huoni utangazaji wa fursa za kiuchumi za Tanzania kama ilivyo, huoni watu wamejipambanua. Tunahitajika kujipambanua zaidi kama Tanzania, tusisubiri mtu mmoja atangulie mbele halafu sisi tukarudi nyuma. Tutakuwa tunaharibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia katika suala zima la watumishi. Kama watumishi hawapo wa kutosha, ule mzigo unakuwa ni mkubwa, ufanisi unakuwa duni. Kwa hiyo, naomba wakati Waziri anakuja aweze kutuwekea mkakati bayana ni namna gani tunaenda kujaza hizi nafasi za watumishi katika balozi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, athari hii imekwenda moja kwa moja kwenye utekelezaji wa dhana ya kidiplomasia katika balozi zetu. Mwaka 2020/2021, balozi sita nje ya nchi zilishindwa kutekeleza dhana hii kwa kukosa bajeti. Siyo kwamba zilikosa hakuna, hazikupelekwa, zilitengwa na Bunge lako Tukufu lakini hazikupelekwa nje ya nchi. Nikifika hapa naunga mkono kile kipengele cha ufuatiliaji kwa ajili ya kuangalia bajeti tunazotenga, je, zinafika kwa wakati na zinafika kama tulivyozitenga? Otherwise tutakuwa tunakaa hapa na tunachokisema kinapotelea hewani, bila kipengele hicho hatuwezi kuvuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda niainishe balozi ambazo zilishindwa kutekeleza hii dhana ya diplomasia ya uchumi nje ya nchi kwa vitendo kwa kukosa bajeti. Bunge lako tukufu 2020/2021, lilitenga shilingi 116,200,000 kwenda Ubalozi wa Kinshasa Congo, lakini fedha zilizopelekwa ni Sh.13,000,000, sawa na asilimia 11, tunatokaje hapa? Balozi ya Lilongwe ilitengewa shilingi 57,000,000, zilipelekwa shilingi 12,000,000 sawa na asilimia 21. Tunaondokaje hapa kwenda mbele? Ubalozi wa Doha ulitengewa shilingi 75,600,000, tulipeleka shilingi 10,000,000 tu, sawa na asilimia 14. Tuna move vipi kwenda kufunga magoli, vita iliyopo sasa hivi kwenye Taifa ni vita ya kiuchumi siyo vita ya mtu kwa mtu. Tunaingiaje kwenye ushindani wa kiuchumi kama reception yetu imefungwa na hakuna pakupita? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, Addis Ababa tulitenga shilingi 138,000,000 zimepelekwa shilingi 2,000,000 tu, shame. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni sawa na asilimia 1.8. tunakwenda wapi? Ubalozi wa Washington DC tulitenga shilingi 144,000,000,000 lakini zilizopelekwa ni shilingi 8,000,000, sawa na asilimia saba. How can we move kama nchi kama tunakwenda kufanya mambo kama hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo niende kwenye kipengele cha pili. Hawa watu Mabalozi wetu, watumishi wetu wa ubalozi ambao ni pungufu wamebeba mzigo mkubwa lakini wawakilishi hawa wanadai Serikali, kuna nini hapa?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Njau kuna neno umelitamka ambalo si neno la Kibunge ni neno la kuudhi. Huwezi kusema Serikali imefanya kitu halafu ukatamka neno hilo la shame. Kwa hiyo, naomba ulifute.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nalifuta.

NAIBU SPIKA: Hapana, tamka kwa maneno yako kwamba hilo jambo unalifuta.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme ni aibu. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

NAIBU SPIKA: Futa neno lako hilo. Futa neno lako hilo. Si umeshafuta?

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nimefuta.

NAIBU SPIKA: Haya, ahsante. Tuendelee. (Makofi)

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, badala yake niseme inasikitisha sana. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea. Madai ya watumishi katika balozi zetu ambayo ni sebule (reception) ambayo tunawapokea wawekezaji na watalii, tuwaangalie kwa jicho la huruma. Kwenye ripoti ya CAG imeainisha balozi nne ambazo zinadai Shilingi milioni 684.17, ni fedha nyingi. Labda niziainishe kwa haraka haraka; ni Ubalozi wa Paris, Ufaransa ambao unadai Shilingi milioni 83.2; Ubalozi wa Kuala Lumper, Malaysia unadai Shilingi milioni 67.3; Ubalozi wa Kinshasa, Congo unadai Shilingi milioni 243; Ubalozi wa Pritoria, South Africa unadai Shilingi milioni 290. Jumla yake ni Shilingi milioni 684.17. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu wenye mzigo mkubwa ambao hawatoshi, lakini bado wanadai marupurupu, wanadai posho zao na malimbikizo yao ya mshahara, na bado wanatakiwa waende mbele kupambana; nafikiri kama sijakosea, kwenye Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 zinaelekeza, kama kuna watumishi wanadai malimbikizo, marupurupu, posho, kupanda vyeo, walipwe mara moja. Kanuni hii imekiukwa kupitia balozi hizi. Tunaendaje kuwabana wakafanye kazi kubwa namna hiyo wakati hata fedha zao hawajapewa?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa aeleze ni mkakati gani madhubuti wa kwenda kulipa madeni haya ili balozi zetu ziweze kufunguka na Tanzania iweze kupata neema?

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunaongelea haya, ni kwa maslahi mapana ya Taifa letu, ni kwa maslahi ya nchi yetu ambapo tumeona Kiongozi Mkuu Jemedari ametangulia mbele na wengine wapo nyuma wanarudi nyuma, tukamshike mkono twende wote pamoja. (Makofi)

(Hapa kengele ililila kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)