Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema. Pia nachukua fursa hii kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Pia nakipongeza Chama changu cha Mapinduzi kwa maelekezo yote ambayo Katibu Mkuu anatupatia, tunamshukuru sana. Nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pamoja na timu nzima ya Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na elimu. Naipongeza Serikali, kwani kama kuna eneo ambalo wametutua mzigo sisi wazazi ni ili eneo la elimu bila malipo kwa Watoto. Ila elimu imegawanyika sehemu mbili; tuna elimu nyoofu na alternative education. Elimu nyoofu kutoka Darasa la Kwanza mpaka Kidato cha Sita, watoto hao watasoma bila kulipa ada, na akienda Chuo Kikuu maana yake anapata mkopo. Hao alternative education, ni wa vyuo vya kati na wote tunawahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nataka niiombe Serikali, tunajenga sana VETA, lakini pia tuna vyuo vya kati vya kutosha na vijana wengi wanakwenda hata akipata Division One anataka kwenda chuo cha kati akasome Nursing, Maabara, Ufundi wowote ili aweze kupata ujuzi. Nchi yetu leo inawahitaji vijana wenye ujuzi ili tuweze kutoka hapa tulipo, lakini tukimsubiri kijana amalize aje na maarifa, hilo ni jambo moja, lakini jambo la pili, amkute kijana mwingine mwenye ujuzi yuko tayari anaendelea na kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niiombe Serikali, Mheshimiwa Waziri amesema vizuri, tutawasaidia pale itakapopatikana fedha, lakini tunaweza kutumia utaratibu mzuri tu, kwa sasa tukapunguza ada ambayo inatolewa kwenye vyuo vyetu vya kati ili wazazi waweze kuwasomesha watoto wao walio wengi na sisi tunawahitaji. Nataka niombe eneo hili tulifanyie kazi, nami nimekuwa pioneer sana wa kuhakikisha vyuo hivi vya kati tunavithamini sana, na ili uchumi wetu uendelee, unahitaji vijana wenye ujuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine hapa ni la MSD, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba. Serikali imetenga Shilingi bilioni 200, ni jambo jema sana, na niipongeze sana. Mwaka 2021 walitenga Shilingi bilioni 218, wametoa zaidi ya Shilingi bilioni 160, hili ni jambo kubwa sana, nimpongeze sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni imani yangu fedha iliyobaki wataimalizia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunazungumzia maisha yetu, tunazungumzia afya ya Watanzania, upatikanaji wa dawa umekuwa bado ni changamoto. Hii Shilingi bilioni 200 inayowekwa, inawekwa kwa projection ipi? Nataka hapa Serikali tujaribu kuangalia, maoteo ya dawa yanatoka wapi? Ukiangalia katika zahanati tulizonazo, zaidi ya zahanati 7,000 za Serikali hakuna mfamasia wala pharmaceutical technically hakuna, unawezaje kupata maoteo ya dawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kama huna wafamasia; nchi nzima una wafamasia asilimia 22 tu, na wanafanya kazi kubwa, lakini tuna deficit ya wafamasia asilimia 78 zaidi ya wafamasia 35 wanatakiwa kuwepo nchini. Nataka kuishauri Serikali katika eneo hili, wanaofanya kazi ya dispensing kule kwenye zahanati zetu kutoa dawa, ni medical attendant. Medical attendant wameajiriwa kama wahudumu wa afya, siyo kama manesi, siyo kama watoa dawa, lakini wanafanya kazi zote kwenye zahanati zetu. Leo tunapozungumza hivi, sasa Serikali inapaswa kuwekeza hapa; ukiona dawa nyingi zime-expire ni kwa sababu yule medical attendant hatujamfanyia training, awezi kujua inventory ya kuingiza na kutoa dawa. Hata dawa zile tunazozileta leo, maana yake anapaswa afanyiwe training. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo nataka Serikali ilitazame vizuri jambo hili. Medica attendant kama hujamfanyia capacity building, wewe unawezaje kupata maoteo ya dawa? Unawezaje kujua dawa leo Watanzania wanataka dawa, unatenga Shilingi bilioni 200? La hasha! Lazima tuwe na projection inayotokana na hao watu. Tukawafanyie capacity building, tutenge fedha, tuwape uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo moja kubwa, wengi wanasoma mwaka mmoja na certificate ili tu-cover hili, lakini Serikali imefuta NTL Level IV. NTL Level IV ilikuwa inawawezesha vijana wetu kuweza kusoma certificate kwa mwaka mmoja na wakaenda ku-cover haya ma-gap. Unampeleka NTL Level V ambayo inamtaka kwenye somo la sayansi awe amepata C, sasa kwa mazingira gani ya shule zetu tulizozianzisha na maabara zetu hazina vifaa, mtoto anaweza akapata C halafu akarudi kwenda kusoma alternative education? Hili jambo bado ni gumu sana. Bado huyu atakayepata C, kwa nini asiendelee na elimu ambayo ni ya bure ya kidato cha tano na sita na huko atapata mkopo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali tuje na mpango na Wizara ya Afya waje watuambie wanapata wapi maoteo ya dawa? Inawezekana mahitaji yetu ya dawa ni karibu shilingi bilioni 500, tunatenga shilingi bilioni 200, ndiyo maana tatizo hili linaendelea kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine muhimu sana ni suala la utalii. Hakuna ubishi baada ya janga la Corona utalii wetu ambao ulikuwa unachangia GDP ya asilimia 27 umeshuka mpaka asilimia 17. Hili jambo limekuwa ni kubwa mno, ambapo sasa mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu ameamua kuingia field na kuja Royal Tour kwa ajili ya kuonesha kwamba utalii wetu ndiyo sehemu kubwa ambayo sisi tunaitegemea ili iweze kuongeza kipato kwenye uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa tumeshuka, nini sasa kinafanyika? Watalii wanataka mambo mawili tu. La kwanza, political stability, wanataka hali ya usalama na amani. Jambo la pili, wanataka ukarimu. Sasa leo tunapokwenda kuimarisha utalii wetu ambao tunajua kabisa ndiyo msingi wa pato letu, ndiyo unachangia kwa kiasi kikubwa ili tufike kwenye GDP ya asilimia 30. Lazima sisi Watanzania tuwe pamoja. Utalii hapa huwezi kuzungumza Ngorongoro na Loliondo peke yake, utalii hapa kama tunatokea sehemu ambayo inaonesha hakuna usalama, maana yake watu hawawezi kwenda Moshi, hawawezi kwenda Manyara, hawawezi kwenda Mara, hawawezi kwenda popote. Tayari Tanzania itakuwa inaonekana, huku kuna tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri maeneo machache. Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa maelekezo mazuri, nami nampongeza sana kwamba wale ambao wako tayari kuondoka, wanaondoka na mazingira yameandaliwa. Hili ni jambo jema sana. Hili la kwanza; la pili, ni lazima tuajiri Maafisa Maendeleo ya Jamii ili ku-improve relationship ya wakazi wa eneo hilo. Watu wanapotoka kwenda eneo lingine, bado tunaweza kuzalisha eneo lingine kule kama hatujaweka mkakati kuwa na Maafisa Maendeleo ya Jamii; na wale wanaobaki kama hatuweka mkakati kuwa na Maafisa Maendeleo ya Jamii, tusitarajie kwamba tutakuwa na mahusiano mazuri. Bado hapa hali ya usalama itakuwa hatarishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la utalii; utalii ni biashara, lazima tuajiri ma-CEOs. Sasa kama mtu anabaki na game reverse, yeye abaki kwenye conservation, lakini tuajiri ma-CEOs ili waweze kutusaidia kufanya biashara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, hili eneo ni muhimu sana. Nasi Watanzania tuungane kwa pamoja bila kujali tofauti zetu, lakini tunataka kuinua uchumi wetu. Uchumi huu kwenye utalii ndiyo eneo kubwa sana tunatakiwa tulisimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ulikuwa Waziri wangu, ulinituma kwenda kwenye ile timu ya Mawaziri nane. Kama kuna eneo la uhifadhi tulilisimamia lilikuwa la Lake Natron. Lake Natron tumelitenga kama eneo tengefu. Eneo tengefu linakuwa na pande mbili; upande wa kwanza litahifadhiwa, lakini upande wa pili matumizi ya binadamu yanaendelea, kama tunavyofanya kwenye Ziwa Rukwa. Kwa hiyo, sasa ile ripoti ambayo ilikuwa ya Mawaziri nane wakati ule, ndiyo ripoti pekee inayoweza kutoa suluhu ya haya matatizo ambayo yanaendelea sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niguse eneo lingine la CAG. CAG ametengewa fedha kwa ajili ya kuongeza kazi yake anayoifanya na anafanya kazi nzuri sana, lakini CAG anafanya compliance. Sasa tunamwongezea fedha kwa ajili ya kwenda kufanya postmortem. Nadhani mnanielewa ninavyozungumza postmortem. Tayari postmortem unaenda kuangalia huyu marehemu amekufa kwa sababu ya nini? Unaenda kuangalia chanzo cha kifo cha marehemu, badala ya kwenda kumsaidia huyu asiweze kufa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa fedha tuliyotenga imwezeshe CAG kuwa pro-active. CAG hawezi kubaki kuwa reactive. Tumefanya vizuri kwa Internal Auditor tumefanya vizuri sana wawe wanafanya kazi kwa wakati wote, lakini CAG anapoenda kufanya kazi, sisi mzunguko utoke kwenye Kamati, ije Bungeni, tufanye maazimio; too late to catch the bus.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali hii, fedha tuliyotenga tumsaidie CAG aende awe pro-active ili atusaidie matatizo yasitokee, tusije tukawa tunasubiri matatizo yanatokea, tunakuja kujadili matatizo yameshatokea. Mtu unayeenda kumhukumu, hayupo; ameshahama, ameacha kazi, amestaafu. Huko hatuwezi kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie eneo muhimu sana. Mwaka 2021 Mheshimiwa Waziri alieleza juu ya Madiwani, kaeleza vizuri sana. Hawa wanafanya kazi nzuri na uzalishaji ni mkubwa na ndio wanaosababisha mapato ya ndani yanakuwa makubwa. Akatumia neno zuri sana, Wabunge wakaazi wa kata, na akasaidia, lakini ukiacha Halmashauri 16, nyingine zote Serikali iliamua kulipa posho yao na mpaka leo hatuna mgogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niiombe Serikali eneo jepesi sana. Own source zetu tunazozalisha kwa kiwango kikubwa kwenye mapato yetu ya ndani hatuwezi kushindwa kuweka responsibility allowance kwenye own source. Tunataka Serikali itoe tu maelekezo ya fedha ya madaraka kama tunavyotoa kwa Maafisa Elimu wa Kata, kwa Watendaji wa Kata, kote Serikali inatoa. Ila Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata, yeye hana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiweka responsibility allowance kwenye own source zetu ambayo ianze tu kuanzia Shilingi 200,000/= na kuendelea kulingana na mapato yao; ukiweka Shilingi 200,000/= kwa Singida Mjini, maana yake utakuwa unatenga Shilingi 4,600,000/=, haiwezi kushindikana. Naiomba Serikali iweze kuliangalia eneo hili ili liweze ku-promote, ili liweze kuwasaidia hawa wafanye kazi kwa ufanisi. Hapa tunazungumza uwajibikaji wa pamoja na uwajibikaji huu lazima twende kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwa haraka ili tufike mahali tukubaliane. Sisi ni wazalishaji wa alizeti, Serikali leo imeamua kuwekeza kwenye eneo hili. Tuna kiwanda kikubwa sana cha Mount Meru ambacho tangu kimeanza kazi hakijawahi kutosheleza mahitaji. Kwa nini? Ni kwa sababu viwanda vyetu vingi vinavyoanzishwa, hawa wawekezaji wanaokuja kuanzisha hawafanyi contract farming. Wewe unaacha mimi nizalishe, leo mimi naenda kwenye njaa, siwezi kulima alizeti kwa wingi kwa sababu ni zao la kibiashara, nitalima zao la chakula ili niweze ku-survive. Sasa nini kinatakiwa kifanyike?

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali itoe malekezo kwa wawekezaji wote hawa wanaoanzisha viwanda wawe na contract farming. Nenda umsaidie mwananchi mwenye eneo, mpe pembejeo, hakikisha unamsaidia, unawapa na watalaam na kila kitu, uzalishaji utaongezeka, na soko hili la mafuta litakuwa ndiyo soko kubwa ambalo litawasaidia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna ubishi kwamba asilimia 10 imewasaidia sana Watanzania. Leo tunapoenda kuigawanya; tano inaenda kwenye eneo ambalo ni wajibu wa Serikali, suala la kujenga masoko ya Wamachinga, hii ni kazi ya Serikali, lakini asilimia 10 ni fedha ambayo tumeiandaa sisi. Tumekusanya kwenye vyanzo vyetu, tumeamua sasa asilimia 10 iwasaidie akina mama, vijana na pia watu wenye ulemavu. Mpaka sasa hamjatuambia, tumefanikiwa kwa kiwango gani? Tumefeli wapi? Hatuwezi kukimbia tatizo. Ila kama ndivyo, mtuambie tumeamua kwenda huku kwa sababu hawa watu wamewezesha. Sasa kama tunaamua kuweka TIN, umeweka TIN halafu unaenda kuwapata watu gani wanaoweza kufanya productivity kama sio hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, hii asilimia 10 tena sisi tulikuwa tunawaza iongozwe, kwa sababu mapato tunakusanya wenyewe, sasa tunaitoa 5% inaenda kufanya kazi ya Serikali ambapo kazi hii ni wajibu wake Serikali kujenga masoko, kufanya nini, kutenga na kila kitu. Naiomba Serikali kwenye eneo hili tuachieni sisi tuka-improve maisha ya watu wetu, kwa sababu ndiyo eneo kubwa ambalo linatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya Serikali. Ahsante sana. (Makofi)