Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami kuchangia hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa bajeti nzuri sana ambayo ametuletea mwaka huu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wakati anatoa hotuba yake kuna sehemu nyingi sana alizoelekeza na alizosema za kupunguza matumizi, lakini kuna sehemu moja ambayo hakuitaja ambayo naona ni ya muhimu sana ya kupunguza matumizi katika nchi yetu. Eneo hili ni kupunguza matumizi ya Serikali ya eneo la riba na faini ambazo inatozwa Serikali kutokana na ucheleweshwaji wa malipo kwa wakandarasi na wazabuni. Eneo hili ni eneo muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wakandarasi wana charge interest kwa Serikali kwa sababu tumechelewesha kuwalipa. Kama hatutabana hii sehemu, maana yake tutaendelea kuiingizia Serikali hasara, tunaendelea kupandisha miradi thamani yake, lakini pamoja na hayo, Serikali inazidi kupata hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mifano. Ukisoma ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha 2020/2021 iliyotolewa Machi 22, inaeleza; ukisoma ukurasa wa 52 na 53 wa Hesabu za Mashirika ya Umma, utaona tulichajiwa interest na faini ya Shilingi bilioni 95.2 ambapo TANESCO ilikuwa shilingi bilioni 10.4, ATCL ilikuwa shilingi bilioni 16.8 na Bodi ya Mikopo ilikuwa shilingi bilioni 68. Fedha hizi ni nyingi kwa Serikali. Ukienda kwenye Hesabu ya Serikali Kuu, utakuta TANROADS walichajiwa shilingi bilioni 68.7 na TARURA walichajiwa shilingi bilioni 0.88 sawa na shilingi milioni 880. Fedha hizi ni nyingi, lazima twende tukaziokoe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sasa Wizara kutazama kwa kina Hazina ili kuweza kutoa mlolongo uliopo mkubwa katika namna kubwa sana ya ku-approval malipo kwa Wakandarasi wetu. Tuki-solve hili eneo tutaokoa fedha nyingi sana kwa Taifa letu, tutaokoa fedha nyingi sana kwa nchi yetu. Namaanisha nini? Ukienda kwa mfano, Kamati yetu ilienda pale TPA tukakuta wamepigwa faini ya kuchelewa kulipa, ya shilingi milioni 980. Fedha hizi ni nyingi, lakini ukiuliza sababu utaambiwa kwamba Hazina ilichelewesha malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia, tunapata mikopo ya watu wa Benki ya Dunia, tunaposaini mikataba, yaani financial agreement, Benki ya Dunia huwa inaleta fedha zote inazipeleka Hazina. Sasa kigugumizi cha kulipa Wakandarasi kinatoka wapi? Kwa nini hatuwezi kulipa wakandarasi kwa wakati ili kuondoa hii gharama ya kulipa interest? Implication yake ni nini katika hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, implication yake ni kwamba inawezekana kuna viongozi kwenye ofisi wanachelewesha kwa makusudi ili watakapotoa fedha hizi waweze kupata mgawo. Hii ndiyo implication ya tatizo hili. Implication ya pili, Wakandarasi wameshatugundua sasa kwamba Watanzania wao hawalipi kwa wakati, tutachaji interest. Kinachofanyika sasa wanapofanya quotation ya kazi wana-quote kidogo wakijua kwamba watakuja wafidie pale kwenye interest.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni muhimu sana Wizara ya Fedha kuliangalia. Nendeni pale Hazina, kama kuna issue zinasumbua, fumueni utaratibu, leteni tuwapitishie hapa, tuokoe fedha nyingi ambazo tunaingia gharama bila sababu za msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la pili ambalo nataka kuchangia, ni kuimarisha mashirika ya Serikali yanayozalisha na kupata kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuchukulie mfano Shirika letu la TPDC, katika uagizaji wa mafuta mwezi Mei, 2022 mafuta yaliyoingia nchini ya diesel yalikuwa metric ton 346,631. Katika hii Shirika letu la TPDC lilipewa metric ton 111,000 sawa na asilimia 32, ukiuliza wanakuambia hawana mtaji! Leo lazima tukubaliane tupeleke mtaji katika Shirika letu ili liweze kuagiza mafuta mengi na tuweze kupata faida Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma taarifa ya fedha utaona kwamba tayari wameshapleka gawio Serikalini zaidi ya Bilioni Tisa katika miaka mitatu, sasa kama hatuwezi kuwapelekea mtaji watapata wapi gawio la kuleta Serikalini ni lazima sasa tuone namna ya kuwapa fedha ili waweze kufanya biashara na tuweze kupata gawio Serikalini. Haya ni mambo ya msingi yatakayoenda kutupatia fedha katika nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo ukiangalia kuanzia 2004 Julai, mpaka Mei, 2022 TPDC wameokoa Trilioni 41 wa kutumia gesi asilia, lakini ukisoma taarifa inaonesha mpaka sasa hivi wanaotumia gesi asilia ni asilimia 10 bado asilimia ni ndogo sana. Kama tumeweza kuokoa Trilioni 41.3 sasa haya si ni mahesabu tu ya kawaida comrade Mwigulu, kwamba sasa tupeleke fedha nyingi TPDC ili tuweze kuokoa fedha nyingi na baadae tupeleke fedha kwenye mzunguko ndiyo logic ya hii Habari! Kwa hiyo tulione suala hili ni la msingi sana, kama tumeokoa Trilioni 41 na bado ni asilimia 10, Je, tutaokoa kiasi gani kama tutafikisha asilimia 60 hii ni hesabu ya kawaida twendeni tukaliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la Tatu ni kuangalia sekta za uzalishaji. Ninaipongeza sana Serikali kwa kuja na mkakati wa sekta ya kilimo kwa ajili ya uzalishaji. Niseme tu kwamba sababu mojawapo inayosababisha ongezeko la bei kwenye bidhaa mbalimbali ni kutokuwepo uzalishaji mkubwa wa mazao ya nchi husika. Tusipozalisha kwa wingi hapa nchini maana yake bei za mazao zitaendelea kuwa kubwa kwa sababu tunategemea kuingiza kutoka nje. Nini kifanyike, tunatakiwa tuzalishe kwa wingi hapa nchini ili tuweze nasi kuuza kwa wenzetu, tukienda mbali zaidi tuweze kutumia hapa nchini kwetu tuzalishe final product na hizi final product zikaweze kutumika katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano kule Simiyu tunalima sana pamba lakini tunalo andiko kubwa ambalo limekuja Wizara ya Fedha la kutengeneza kiwanda kikubwa Simiyu kitakachozalisha vifaa tiba vitokanavyo na pamba. Vifaa tiba hivi vinaenda kuokoa fedha zaidi ya Bilioni 147 ambayo tunatumia sasa kuagiza vifaa tiba huko nje. Sasa kwa nini tusizalishe hapa tutengeneze kiwanda, tuzalishe sisi wenyewe na tutumie, hii itaokoa fedha nyingi ambazo tunapeleka kule nje. Pia zaidi ya wananchi 1,000 wanaenda kupata ajira, kule Busega watapata ajira, kule Bariadi watapata ajira, kule Iramba watapata ajira. Kinachotakiwa sasa kufanyika ni kuwekeza eneo hili ili wananchi wetu waweze kupata ajira na tuokoe fedha nyingi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ndiyo itakuwa sasa mantiki ya kuwepo kwa reli, huwa najiuliza swali moja huko nyuma kwamba kwa nini tunajenga reli wakati hatujaenda kuwekeza katika sekta za uzalishaji, hii reli inaenda kusafirisha nini? Lazima tuwe na mipango, reli siyo ya kusafirisha watu peke yake, reli ni ya kusafirisha pia mizigo ya kusafirisha mazao. Mantiki ya kutengeneza reli ni pamoja na usafirishaji kama tunatengeneza reli kwa ajili ya kusafirisha watu hatutarudisha huo mkopo. Ni lazima sasa twende mbali zaidi tunatengeneza reli na mwisho wa siku huko reli inakoenda kuna uzalishaji gani. Kama reli inaenda Mwanza kuna uzalishaji gani kule Mwanza, kama reli inaenda Kigoma kuna uzalishaji upi kule Kigoma ambao sasa tutatumia katika suala zima la usafirishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)