Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru sana kupata nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Bajeti Kuu ya Serikali na nitajielekeza kwenye maeneo matatu, kwenye upande wa maduka ya kubadilisha fedha, kubana matumizi ya Serikali na Tanzanite.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, BOT ina double standard, tunafahamu kwamba kwa muda mrefu imekuwa inapuuza maelekezo ya Serikali. Tumemsikia Waziri wa Fedha kupitia Bajeti ya Wizara ya Fedha ameonyesha umuhimu wa maduka haya ya kubadilisha fedha hasa kutokana na kazi nzuri aliyoifanya Rais wetu kwenye sekta ya utalii. Kuna Kampuni inaitwa Kadoo Bureau De Change inafanya kazi zake Dar es Salaam na Arusha imepewa kibali na BOT, pia kampuni nyingine nyingi zenye sifa zilizoko Arusha zimenyimwa leseni na BOT kwa sababu ambazo hazieleweki na vigezo wameshakidhi, inaonekana kwamba huyu mwenye hii Kampuni wa maslahi naye ndiyo maana wamemuachi na kuzuia wengine ili aweze kufanya biashara peke yake. Tunadhani hili jambo siyo sawa na siyo jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Rais ametoa malekezo akiwa Kagera, kwamba wenzetu wa TRA wanapofuatilia kodi wasiende miaka zaidi ya miwili, lakini kwenye hawa wetu Bureau bado wanakwenda kuwauliza taarifa za mwaka 2015 mpaka 2016 ili tu kuwatafutia sababu na mwisho wa siku wawanyime fursa hiyo ya kufanya biashara kama wenzao wanavyofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi utalii umeongezeka hoteli zimejaa mpaka mwezi Desemba na kuendelea, Ndege nyingi zinaingia usiku tunategemea watalii wanapofika wasipate changamoto ya kubadilisha fedha. Kwa sababu ukileta urasimu wa namna hii mnasababisha pia wakati mwingine kuwa na black market katika maeneo mbalimbali, badala ya ku-change fedha kwenye maeneo rasmi wana-change kwenye maeneo binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia changamoto nyingine kubwa katika jambo hili ambalo tunaomba BOT waliangalie ukiritimba nao ni mkubwa sana. Unapokwenda Benki kwenda kubadilisha fedha ni tofauti na kwenye Bureau wanataka wajue je unayo akaunti, je kama hauna akaunti umetoka wapi na maswali mengine mengi, lakini ukienda kwenye Bureau taratibu zinakuwa rahisi zaidi. Tunaomba BOT waache urasimu, kama wana watu wao wanawataka wawape lakini pia na Watanzania wengine wenye sifa wapewe kama watu wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kuhusu kubana matumizi ya Serikali. Kwanza naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na kwa usimamizi wako Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yako yote, kwenye kuhakikisha magari ya Serikali kwa kiwango kikubwa mnakwenda kuyadhibiti kwa sababu ni kweli gharama zimekuwa kubwa. Lakini kuna eneo jingine pia naomba tuliangalie, angalia kwenye Halmashauri zetu, ukienda Halmashauri za Dar es Salaam, Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam mapato yao ya jumla makisio yao ni bilioni 81, lakini mapato yasiyolindwa ni bilioni 62.2 ukichukua asilimia 70 ambayo inatakiwa iende kwenye maendeleo ni sawasawa na bilioni 43.587, lakini other charges, yale matumizi ya kawaida posho, kaweka mafuta kafanya hivi ni Bilioni 18 kwa Halmashauri moja kwa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Halmashauri kama ya Dodoma makisio yao ni Bilioni 55, mapato yasiyolindwa ni bilioni 44, ukichukua asilimia 60 ni bilioni 26, other charges matumizi yale ya kawaida ya kila siku ni kama bilioni 17. Ukichukua Halmashauri ya Kinondoni hivyo hivyo bilioni 57 ya asilimia 46, maendeleo 32, matumizi ya kawaida bilioni 14. Ukienda Jiji la Arusha mapato yetu ni bilioni 30 makisio, mapato yasiyolindwa bilioni 24, asilimia 70 kwenye maendeleo ni bilioni 17, matumizi ya kawaida ni bilioni saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona mfano mmoja Jiji la Arusha kwa mapato haya ya Bilioni Saba tu wameweza kuingiziana fedha kwenye akaunti binafsi, tumeona aliyekuwa Mkurugenzi wakati huo Ndugu John Pima kachukua milioni 103, kamuingizia Mchumi Innocent Maduhu milioni 103 kwenye akaunti yake binafsi. Mchumi kachukua milioni 25 kaenda kununua gari Subaru kwa matumizi yake binafsi na ushahidi upo. Mkurugenzi kachukua fedha kamuingizia kijana anaitwa Ndugu Alex milioni 65, mwingine milioni 65, unaona hizi fedha ambazo mnazijazia hizi Halmashauri na hizi asilimia zenu zinakwenda kunufaisha watu na siyo kunufaisha wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba tunaomba Wizara ya Fedha wakae na TAMISEMI badala ya kusema waangalie asilimia waangalie matumizi halisi. Ukichukua hizi bilioni 18 za Halmashauri ya Dar es Salaam ni sawasawa na ukichukua Halmashauri ndogo 14, ukichukua Halmashauri ya Mbulu, Halmashauri ya Gairo, Halmashauri ya Butiama, Halmashauri ya Rorya, Kigoma, Kakonko, Buhigwe, Nsimbo, Bumbuli, Mbogwe, Mlele, Momba, Madaba na Halmashauri ya Ileje. Halmashauri 14 hizi matumizi yao ya kawaida kwa mwaka mzima ni bilioni 9.9. Matumizi yao ya kawaida kwa miaka miwili ndiyo matumizi ya Jiji la Dar es Salaam ya kuweka mafuta, kulipana posho na masuala mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani hapa kuna haja ya Serikali kwenda kuangalia kazi nzuri kwenye magari lakini turudi pia kwenye matumizi ya kwenye Halmashauri zetu. Rais anafanya kazi kubwa sana, anakwenda kutafuta hela Dunia nzima, anabana matumizi kila mahali, lakini Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Fedha msaidieni Rais kupitia matumizi haya ya Halmashauri zetu ili tuweze mwisho wa siku kupata fedha za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasi Arusha hapa kwa nilivyoangalia wanavyo kulakula hawa wakipewa hata Bilioni Tatu, Nne zinawatosha, hii Bilioni Tatu nyingine au Nne zinazobaki tuende tukajenge barabara kwa sababu changamoto ya barabara ni kubwa sana, tukanunue vifaa kwenye Vituo vya Afya na tukapeleke huduma mbalimbali kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, nilikuwa naomba pia kutoa mchango wa mawazo kwenye eneo hilo na ni imani yangu kwamba wenzetu wa TAMISEMI watatusaidia. Kwa sababu hizi hela zinaliwa sana nikitaka niseme mnyororo mzima hapa wa namna ambavyo hizi hela za Arusha zilivyoliwa na zilivyogawana hapa ndani kuna wengine tutapoteana kwa sababu changamoto ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la tatu ni kuhusiana na Madini ya Tanzanite. Hili jambo nimekuwa nalisema kila siku na kila nikilisema nadhani sieleweki. Watu wa Arusha hatukatai madini ya Tanzanite kuuzwa Mererani kwa sababu Mererani ndiyo yanakochimbwa. Tunachokisema sisi yakishachimbwa yale madini kwa sababu lengo la kujenga ule ukuta ni kuzuia utoroshaji, yakishichimbwa na Serikali iko pale na vyombo vyote viko pale waangalie kodi zote za Serikali ambazo mwekezaji anatakiwa kuzilipa, kwa sababu akishalipa anaruhusiwa kusafirisha haya madini kupeleka kote Duniani. Akitaka kupeleka India anapeleka, akitaka kupeleka Marekani anapeleka na sehemu nyingine zote, lakini eti haruhusiwi akishalipa tozo zote kupeleka Arusha, kupeleka Dar es Salaam, kupeleka Mwanza, kupeleka na Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanachokifanya wafanyabiashara anakwenda pale Mererani anachimba madini yake, anapata vibali vyote, anafungua Ofisi yake Dubai, anafungua Ofisi yake India, anafungua Ofisi yake Kenya, anasafirisha madini anakwenda kuyachakata kule halafu anakuja kwenye border zetu anayapitisha kuja kuyauza Arusha na maeneo mengine. Sasa tunayafanya haya kwa kumunufaisha nani? Sisi hatukatai mambo haya kupelekwa Mererani lakini tuangalie mtu akishalipa kodi kama anaruhusiwa kupeleka India kwa nini haruhusiwi kupeleka Arusha, kupeleka Dar es Salaam, kupeleka Mwanza, Zanzibar na maeneo mengine? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wakati huu wa utalii, watalii ni wengi sana mtu anakuja amekwenda kuangalia Pundamilia, kaangalia Simba na wanyama wengine, akitaka kurudi nyumbani anataka arudi na zawadi, anakwenda kununua Tanzanite kama zawadi anapeleka kwa ndugu zake kule nchi alikotoka. Leo haruhusiwi kufanya kitu cha namna hiyo! Kwa hiyo, naomba Wizara ya Madini waliangalie jambo hili kwa uzito unaostahili, kwa sababu kwa kweli changamoto hii ni kubwa na mambo haya yanahitaji uzalendo wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa fursa hii. (Makofi)