Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nachukua fursa hii kushukuru sana kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia, kipekee sana nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, katika Jimbo letu la Manyoni Mashariki ameweka impact kubwa sana. Nichukue nafasi hii nimshukuru sana Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri wako kwa kazi kubwa kwa kuja na bajeti ambayo ina ubunifu mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nina mambo takribani matatu ya kuchangia, eneo la kwanza nitachangia kuhusu tathmini ya vyanzo vya mapato ambavyo tulipitisha mwaka uliopita, nitachangia kuhusu namba ya mlipa kodi (tax identification number), nitachangia vilevile kuhusu ile asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri inatokana na asilimia 40 ya maendeleo na mwisho nitachangia kuhusu suala la mishahara binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba mwaka jana tulipitisha vyanzo vya mapato, mojawapo ya vyanzo vya mapato tulipitisha tozo kwenye miamala ya simu na wewe ulikuwa kinara uliita tozo ya uzalendo. Pia tulipitisha mfumo wa kubadilisha ukusanyaji wa kodi za property tax, kutoka TRA lakini tukapeleka kwenye mfumo wa LUKU. Sasa sikusikia kwenye taarifa yako Daktari kwamba kwa kiwango gani tumeweza kufanikiwa na hivi vyanzo ambavyo tulivi-propose ili sisi itusaidie kuja na mfumo ambao tunaweza tukaboresha zaidi whether tunahitaji kuendelea na miamala ya simu na efficacy yake ilikuwaje, vilevile kodi ya majengo ni jinsi gani imekuwa effective, niliona hilo nimshauri Waziri anapokuja ku-wind up tujue kwamba to what extent hizo tozo na hizo kodi zimekuwa effective na unashauri nini tuendelee nazo au zibaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni suala la Namba ya Mlipakodi. Kumekuwa na sintofahamu kubwa na kumetokea taharuki kwa wananchi, lakini mimi naomba niwatoe mashaka, nimepitia nchi mbalimbali ambazo zinatumia TIN Number katika mazingira tofauti. Kwa mfano, UK wana kitu kinaitwa National Insurance Number (NINO) ile NINO ndiyo inatumika kama substitute ya TIN Number. Nchi ya Hong Kong wenye hawana ID zingine wanaita Hong Kong Identity Card ileile Hong Kong Identity Card ndiyo inatumika kama TIN number, the same to Pakistan, the same kwa USA.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema nini hapa? Kwanza niseme idea aliyokuja nayo Daktari Mwigulu Nchemba is the valid idea na tumechelewa sana. Tumechelewa kwa sababu gani, nilitegemea kwanza tuondoe utitiri wa vitambulisho tulivyonavyo, mimi nina vitambulisho zaidi ya vitano vyenye Namba nina cheti cha kuzaliwa, nina employers ID number, nina Social Security Number, nina Leseni ya Udereva na zingine huu ni utitiri mkubwa sana. Nchi zingine wanachofanya mtoto anapozaliwa anapewa TIN number ile TIN number inakuwa the same kote huko, ukimwajiri atatumia the same TIN number, kwenye social security atatumia the same TIN number. Lakini kumekuwa na upotoshaji mkubwa kwenye mitandao, watu wanajua hii idea ya TIN number ni kwamba watu wanakuja kulipa head tax, kodi ya kichwa siyo kweli. Kwa hiyo, mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwamba tu-harmonize hii mifumo tusiwe na vitambulisho vingi, kama inawezekana cheti cha kuzaliwa, mtoto anapozaliwa apewe TIN number atakutana nayo akishakua mtu mzima huko atalipia kwenye mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nilipenda kuchangia suala la asilimia 10. Nimewasikia Wabunge wenzangu wakichangia asilimia 10, mimi namuunga mkono Daktari Mwigulu Nchemba. Kwanza ninaishukuru Serikali kutenga ile asilimia 40 ya maendeleo kwenye mapato ya ndani, ambapo asilimia 10 tunaenda kukopesha katika ile 4-4-2. Tukumbuke kwamba hizi fedha tunaenda kuzikopesha lakini hawa watu tunapowakopesha hizi fedha hawana miundombinu ya kufanyia kazi, hakuna masoko, hakuna vibanda vya Mama Ntilie kufanya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amekuja na idea kwamba badala ya kuchukua yote asilimia 10 uipeleke kwenye mikopo, ambayo nitailezea baadae, ame-propose asilimia Tano ya ile hela iende ikaweke miundombinu kwa ajili ya hawa ambao tunaenda kuwakopesha. Unakikopesha kikundi hakina soko, unawakopesha mama ntilie hawana sehemu ya kupika matokeo yake anaenda kutumia gharama nyingi kulipia pango la kile kibanda cha kufanyia biashara. Kwa hiyo, mimi naunga mkono wazo kwamba tuchukue asilimia tano ya mapato yale ya asilimia 10, tukaweka zile infrastructure, lakini kuna multiply effect kubwa kwenye hili, watu wengi watanufaika na lile soko kuliko vikundi. Nitakutolea mfano, katika Jimbo langu la Manyoni Mashariki….

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Matiko Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa mchangiaji kwamba dhana kuu ya asilimia 10 ilikuwa ni kuwainua wananchi kiuchumi, lakini hizi asilimia tano anazosema kwamba zinakwenda kwenye miundombinu ya masoko kwamba watu waende kuuza pale, wengine wanakopa wanafuga nguruwe, wengine wanafuga kuku, products ambazo haziendi kwenye hayo majengo ambayo anaelekeza. Kwa hiyo, nimependa kumpa tu hiyo taarifa kwamba sio wote wanaokopeshwa wanakwenda kwenye umachinga. (Makofi)

SPIKA: Dkt. Chaya.

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, partially naunga mkono hoja ya dada yangu, lakini naomba nimweleze kitu kimoja wale watu wanakopeshwa kwa kutumia revolving system, zile fedha zinarudishwa. Nitatolea mfano, kule Manyoni, tumeshakusanya fedha kutoka kwa wale ambao waliokopa, zile fedha zikirudi wanakwenda kukopeshwa wale tena. Hoja yangu ni nini, hatuna miundombinu ya hawa watu katika kufanya biashara. Kwa hiyo, bado naunga mkono kwamba tutenge asilimia tano kwa ajili ya kuwasaidia kujenga masoko, kujenga vibanda ile fedha ambayo inarudishwa itatumika kwa ajili ya kukopesha na tutaongeza capacity ya kukopesha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ni la mwisho ni kuhusu hii mishahara binafsi, wenzangu wamechangia kuhusu mishahara binafsi na naunga mkono hoja. Kuna matatizo mawili katika mishahara binafsi hususani kwa wale ambao walitolewa kwenye utumishi wa umma, hususani wale ambao walishushwa vyeo vyao. Kwanza kuna hoja kubwa tatu hoja ya kwanza, huyu mtu wakati anateuliwa je, alikuwa ameajiriwa? Hoja ya pili ni kwamba, je, kama alikuwa ameajiriwa? Tatu, je, alikuwa ameajiriwa wapi ni Serikalini au kwenye private sector? Nne, wakati tunamteua nini tofauti ya mshahara wakati anateuliwa na kule alikokwenda? Hizo ndio hoja kubwa nne ambazo tunahitaji kuangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine watu wakishateuliwa anakuwa na mshahara mkubwa, anaamua kwenda kukopa, kwa hiyo, kuna burden ya mikopo ambayo mtu huyu anakuwa nayo. Tatizo ni kwamba na nakubaliana nalo kwamba tumekuwa na watu wengi ambao wapo mtaani, wametolewa kwenye mfumo wanapokea mishahara mikubwa ambayo ni burden kwa nchi. Kwa mfano, katika halmashauri moja wakati fulani kulikuwa kuna Wakurugenzi wanne wote wanapokea mshahara sawa, hiyo ni burden kubwa kwa nchi. Ushauri wangu ya kwanza, tuandae mwongozo mpya ambao sasa utakuja kusaidia idea ambayo Mheshimiwa Dkt. Mwigulu anayo kwamba kama mtu ametenguliwa, je… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Dkt. Chaya kwa mchango mzuri.

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)