Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. JUMANNE I. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie katika bajeti hii ya Serikali. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye nchi yetu. Pamoja na kumshukuru Mheshimiwa Rais, lakini ni lazima tuendelee kuwapongeza juzi tu tumetoka kumpongeza Mheshimiwa Waziri, kwenye sekta ya Wizara yake ya Fedha kazi ambayo wanaendelea kufanya kama Wizara pamoja na watendaji wao. Kwa hivyo, leo nitajielekeza katika maeneo kama mawili, matatu kwa haraka jambo la kwanza ni lile ambalo limesemwa na wengi la asilimia 10. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo hapo kwenye asilimia 10. Wengine wanajaribu kutofautisha kati ya Miji yenye mapato makubwa na halmashauri nyingine. Mimi natoka Dar es Salaam unakotoka wewe, kwenye Wilaya yetu ya Ubungo tunasema asilimia 10 bado tunaweza tukasema ina asilimia 50 kwenye mafanikio na nimewahi kusema humu ndani. Tunatamani kujua uhakiki na tathmini ya ujumla katika kipindi chote ambacho asilimia 10 imefanya kazi, hiyo itatupa matokeo. Niliomba hapa TAMISEMI wakafanye hili jambo, leo tungekuwa tunajua kwa nini tano, ingekuwa wanatuambia vizuri kwa nini wanazipunguza, tumefanikiwa kwa kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu humu ndani bado zipo taarifa nyingi zimeshapotea fedha nyingi katika hizo asilimia 10. Sasa tunakuwa katika mazingira ya kwamba hatuwezi kufanya maamuzi, je, ni kweli tukubali zipungue au tubaki hapo hapo au tuongeze kama wengine ambavyo wanaona? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia liko jambo tumezungumza juzi na nilikuwa na swali la nyongeza juu ya vijana wengi zaidi ya miaka 35, akinamama wameingizwa katika umri ambao hauna mpaka. Vijana kundi la akinadada wapo katika umri wao katika ujana na pia na wanawake, lakini vijana mwisho miaka 35. Tunajua wajasiriamali hapa ambao tunawazungumza wengi ni zaidi ya miaka 35 mpaka 40 ndio wengi na huo ndio ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiona azma hii ya kuhamisha asilimia tano ni kama vile, wanakwenda kuwatafuta wajasiriamali ambao wengi wamezidi miaka 35. Kwa hiyo, kama huo ndio muono ni jambo jema, lakini inaweza kubaki 10. Katika halmashauri zenye uwezo, ninayotokea mimi nikikubali kwamba 10 zibaki, lakini jambo hili lenye nia njema na wajasiriamali wa zaidi ya miaka 35 waongezewe hiyo tano. Kwa hiyo, ningefurahi kabisa ingeenda hata asilimia 15, kumi zingebaki na tano zingeongezwa, lakini kwa nani wakafanye tathmini. Wale wenye mapato madogo waachwe vile walivyo, wenye mapato makubwa waende kwenye 10 wajumlishiwe na tano ziweze zikawasaidie au hiyo miundombinu ya hao wengine. Ziada kwenye hili niwaombe sana hebu tukaongeze/tukafungue ule umri pale kwenye hii mikopo, tukaufungue ufike miaka 40 inaweza ikatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye asilimia 10 kuna shida moja ambayo hatuizungumzi. Wananchi wengi wanalia, wapiga kura wetu wengi wanalia. Tunazungumzia asilimia 10 (4:4:2) au hiyo (2:2:1) kwa wajasiriamali wenye biashara, lakini wale ambao wanataka kuanza biashara hatuwataki kabisa na ambao ndio wengi. Sasa hao wanataka kuanza biashara, wanataka mtaji mdogo na sisi hatuwezi kuwapa, tunasema lazima uanze na biashara, ndio maana kuna udanganyifu sasa. Wanatafuta duka la mtu wanakwenda watano, 10 wanasema tukae humu kwako, ili iweze kuja kwa mtu mmoja wakagawane vipande vipande, hii haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Maafisa Biashara, tunao wengi tu katika kila halmashauri yupo, ana kazi gani kama hawezi kutoa elimu juu ya kuanza biashara na akaweza kuisimamia biashara iliyoanza? Uoga wetu ni nini kama nchi? Uoga wetu ni nini katika hili? Ione hii, tushauri Wizara katika bajeti yetu hii, hebu tuone jambo hili, tufungue pale miaka 40, lakini tukaone mitaji hii inayotolewa iende kwa kuanza biashara na sio kwa mwenye biashara. Inasababisha kuwa na manung’uniko makubwa makubwa sana na fedha zinakwenda kwa watu wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye jambo la asilimia 10 hapa naweza nikachomeka jambo ambalo limezungumzwa sana na watu. Kuna jambo la mapato dhidi ya matumizi kwenye halmashauri zetu. Mdogo wangu Mheshimiwa Gambo hapo kaisema katika njia fulani kaifananisha Dar es Salaam na mimi ndio maana naamua nirudi hapo. Ni kweli tunayo hayo mapato, lakini nasema hata hayo mapato ambayo tunayapata ya ndani bado ni madogo kwa sababu, ipo kauli ya Serikali ambayo huwa inatolewa au mpaka sasa imeshawahi kutolewa kwamba matumizi ya Waheshimiwa Madiwani kwenye allowances au hizo capacity building ili waweze kwenda kutoa hamasa ya kukusanya mapato inatolewa kauli moja tu halmashauri zote posho zitafanana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo hapo Wazii ametamka mwenyewe kuna halmashauri zaidi ya 19, kukusanya tu wanakusanya shilingi 500,000,000, huyu mwingine anakusanya shilingi 8,000,000,000, unasema wote wakatumie shilingi 200,000 tunawezaje hivyo? Hatuwezi kufanana, kama tunatofautiana kwenye kuzitafuta, tutofautiane pia kwenye kuzitumia. Hili ni jambo muhimu sana, inakatisha tamaa. Leo Waheshimiwa Madiwani wanalia kwa sababu wanafananishwa na kule kwa ndugu yangu Tunduru, hakusanyi, hana uwezo wa kukusanya, lakini Ubungo nakusanya. Hivyo, kama nakusanya waacheni Madiwani waendelee kutafuta mianya mingine iliyopotea ili waongeze mapato zaidi lakini na wenyewe waone au wapewe hizi capacity building tofauti kutokana na wanavyokusanya na sio kufananishwa kwa sababu tunatofautiana jinsi ya kutafuta. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. JUMANNE I. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la TARURA, ukurasa 25 wa taarifa unasema vizuri na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, zipo tozo nyingi ambazo zimeingia na kutoka. Tumeingiza mwaka jana ya simu, lakini tumeitoa haraka, kwa hiyo tuliingiza ili ikapunguze gharama za smartphone ili tuweze kupata fedha kupitia bando na vitu kama hivyo na data, lakini ujanja ujanja wa wafanyabiashara wamekataa kupunguza. Mwaka huu nimfurahie sana Mheshimiwa Waziri ameirudisha tena, tunakwenda sawa, tukikupa ili twende sawa unakataa tunarudi tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo la tozo ya mafuta fuel levy, jambo hili limebaki hivyo hivyo na limetusaidia, kwenye bajeti ya barabara unaweza ukaangalia kabla ya tozo Mfuko wa barabara peke yake kwenda TARURA zile asilimia 30 ulikuwa unapeleka shilingi bilioni 243.15, lakini baada ya Mheshimiwa Rais kuona umuhimu wa kuweka tozo, imekwenda kuongeza shilingi 322.16. Unaweza ukaiona imekwenda ku-double ukiondoa vyanzo vingine vya barabara ambavyo vinatupeleka kama Shilingi Bilioni 781, lakini tayari shilingi bilioni 600.66 kama asilimia 66 zaidi ya shilingi trilioni 1.1 zimeshatoka. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mtemvu.

MHE. JUMANNE I. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwa leo nimeyasema hayo machache, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)