Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hii hotuba ya Waziri wa Fedha. Ndugu yangu, mjukuu wangu Dkt. Mwigulu namshukuru sana, kwa namna jinsi ambavyo hotuba yake imejielekeza na inaonesha kwamba ni hotuba ambayo inaweza ikasaidia katika kuwakomboa Watanzania hasa kiuchumi. Maana kati ya shida kubwa ambayo tuliyonayo kwa Watanzania kwa sasa tuna tatizo kubwa sana la ajira katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kila mwaka nchi yetu inazalisha watoto zaidi ya milioni mbili ambao wanaingia katika soko la ajira. Sasa shida inakuja kwamba ajira inatupa taabu sana. Sasa umesema vizuri na ukaonesha kwamba kwa mwaka huu peke yake zaidi ya Shilingi Bilioni 900 zimeongezeka kwenye upande wa kilimo, lakini vile vile na kwenye mifugo, kwenye uvuvi na katika maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninachokifahamu katika hii Serikali yetu, wakati mwingine tunazungumza kitu kingine, lakini kwenye utekelezaji vinakuja vitu viwili tofauti. Tusipoangalia mwaka kesho hii hotuba tunaisifia tutakaporudi hapa bado itakuwa haionekani katika macho ya watu, kwa maana kwamba ni kwa namna gani imeweza kuwasaidia Watanzania. Nitoe mifano michache ambayo inaonekana dhahiri. Leo tukizungumza upande wa mifugo, Tanzania ni nchi ya tatu katika Afrika kwa kuwa na mifugo mingi, lakini cha ajabu ni kwamba pamoja na kwamba ni nchi ya tatu kuwa na mifugo mingi ni nchi ambayo mifugo haioneshi kuchangia katika kuondoa umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba, wale wafugaji wenyewe ni maskini na mifugo yao yote bado ina hali duni. Sasa ukija kutafuta kwamba sababu ni nini Watanzania ng’ombe wengi tulionao tuna ng’ombe aina ya Zebu. Ng’ombe aina ya Zebu mchungaji au mfugaji anamfuga zaidi ya miaka mitano, akija kumuuza anauza shilingi 300,000. Sasa nini kifanyike, tunahitaji kuhakikisha kwamba tuna-improve ile mifugo yetu na katika ku-improve ile mifugo yetu ni pamoja na kuleta mbegu za kisasa. Leo ukienda katika mashamba ya Serikali tuna mifugo mfano aina ya Borani, hawa ni ng’ombe ambao wanakuwa haraka wana nyama nyingi ambao wanaweza wakatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nimekwenda kwenye shamba mojawapo la la mifugo kwenye haya mashamba ya Serikali, unamkuta leo anauza dume mmoja wa miaka miwili shilingi 3,500,000. Mimi ni mfugaji, leo ukiangalia ng’ombe wangu mimi ambaye ni mfugaji, ng’ombe wangu ni bora kuliko wale walioko kwenye mashamba ya Serikali. Nilikuwa nauza ng’ombe dume wa miaka miwili kwa shilingi 2,000,000 lakini nimekuja nimegundua kumbe huku Serikalini wanauza shilingi 3,500,000. Sasa matokeo yake na mimi naye nimepanda badala ya kuuza shilingi 2,000,000 nauza shilingi 3,000,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa shida iliyopo ili yule mfugaji aweze ku-improve mifugo yake, tafsiri yake, lazima auze ng’ombe 10 apate shilingi 3,500,000 ili aweze kununua dume moja. Hivi katika utaratibu huo ni dhahiri kwamba mifugo haiwezi kusaidia katika kunyanyua kipato cha wafugaji, lakini na kunyanyua kipato cha Watanzania. Hata ungeenda kwenye upande wa uvuvi maana unajua ni rahisi sana tukapeleka fedha kwenye kilimo, lakini tusipeleke fedha kwenye ukulima na hilo tunahitaji tuliangalie sana kwamba tunahitaji hizi fedha ambazo tumezipeleka ziweze kuwafikia wale ambao ni walengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hata kule kwenye uvuvi kuna vizingiti vingi yaani leo mtu akitaka kufungua kizimba chake kule cha ufugaji bora wa samaki, bado utakuta mambo ya NEMC yanamsumbua, upatikanaji wa vibali unakuwa na mlolongo mrefu kwa hiyo matokeo yake mtu anakata tamaa. Kwa hiyo, hayo yote ni mambo ambayo tunahitaji tuyaangalie ili tuweze kufikia malengo. Sasa niseme sisi ndio viongozi tuliopo na kazi ya viongozi ni kufanya mambo yatokee wala tusisubiri mambo yatokee. Sasa nizungumzie kwenye suala la kilimo na kwa kuwa tuna tatizo kubwa la ajira katika nchi yetu na hasa kwangu kule Musoma, vijana wetu wengi hawana ajira na tumesema kilimo kinaweza kikaleta impact kubwa, nini kifanyike? Pale kwenye Wilaya yetu ya Musoma tuna eneo kule linaitwa Bugema, zipo hekari zaidi ya 20,000, nasema tuanze mwaka huu na hekari 5,000 peke yake, ili mwaka kesho tukisimama hapa tuwe na vitu vya kuzungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tukilima zile hekari 5,000 peke yake katika hekari 20,000 tutaleta ajira zaidi ya 10,000, nini kifanyike? Mheshimiwa Waziri wa Fedha atupatie fedha, nitashirikiana na Mbunge mwenzangu wa Musoma Vijijini Profesa Muhongo, pamoja na DC wetu pamoja na halmashauri zetu, twende tukalime zile hekari 5,000 tu kuanzia mwaka huu na ukulima wenyewe ni very simple. Tutatangaza nani anataka atulimie zile hekari 5,000, atakwenda atalima tutamlipa fedha, nani anataka ku-irrigate zile hekari 5,000, ni rahisi kupatikana, atafanya kazi ya ku-irrigate na tutaanza kulima alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukilima zile hekari 5,000, bahati nzuri kutokea pale kwenye shamba kilometa 80 tunacho kiwanda cha kuweza kusindika mafuta. Tafsiri yake ni nini? Piga hekari 5,000 zote ulime alizeti na umwagilie, matokeo yake ni kwamba, tutapata mafuta mengi sana katika nchi yetu, hilo ni la kwanza. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba kuanzia mwezi wa Septemba mwaka huu mpaka mwezi Januari tayari tutakuwa tumepata mafuta mengi kwa ajili ya Watanzania, lakini hiyo haitoshi vijana wetu zaidi ya 10,000 watakuwa wamepata fedha na watakuwa wamepata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi mwaka kesho tunavyoanza katika kile kipindi cha miezi sita kuanzia mwezi Januari mpaka mwezi Juni, utaratibu ule ule tunatangaza nani anataka kutulimia hekari 5,000 atalima, nani anataka ku-irrigate hekari 5,000 ata-irrigate. Wale vijana wetu watafanya hiyo nguvu kazi ya kazi zote zinazofanywa kwa mikono. Tunahangaika masuala ya mbolea, kule kwetu wafugaji wako wengi wana makundi makubwa ya ng’ombe, maana yake ni kwamba ile mbolea yao tutapeleka ma-tipper, vijana watapakia watapeleka kule mashambani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kazi zote za mikono wale vijana watafanya na kwa kufanya hivyo tukilima mpunga hekari 5,000, ni eneo kubwa ambalo litasaidia vijana wetu kuwa na ajira na maisha yao yakawa mazuri. Kwa hiyo tunadhani kwa kufanya hivyo itatusaidia sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mathayo.

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)