Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii uliyonipatia ya kuchangia mapendekezo ya bajeti kuu, lakini namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii ambayo ameruhusu leo tuweze kuzungumza juu ya bajeti kuu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa bajeti nzuri ambayo tumeiona, tumeisikiliza. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa hiki ambacho kimeandaliwa na kuletwa kwetu kwa ajili ya kutoa maoni yetu. Naamini kwamba tumeletwa duniani kufanya mambo tunayoyafanya yawe endelevu kwa ajili yetu sisi na vizazi vijavyo. Kwa hiyo, naamini kila tunachokizungumza leo lazima kiwe endelevu kwamba tutakitumia sisi na watu wanaokuja wataendelea kukitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, yale tuliyoyakuta tuliyonayo leo na tutakayoyafanya baadaye. Kwa hiyo, naamini kabisa kwa bajeti hii ambayo naiona nilikuwa najaribu kuangalia dhima yake, inatuonesha wazi kwamba, dhima ya bajeti hii ni kuongeza kiasi cha kufufua uchumi na kuimarisha sekta za uzalishaji kwa ajili ya kuboresha maisha. Sasa tunazo sekta za uzalishaji kadhaa ambazo mimi nimekuwa naziangalia kuona kama kuna mabadiliko yamefanyika ili tujue kwamba tunakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona kwenye madini, ukuaji wa sekta ulitoka asilimia 6.7 kwenda 9.6, lakini kwenye mchango wa Taifa inaonekana inatoka 6.7 kwenda kwenye 7.2, inaoonekana kuna kitu kimefanyika. Sasa tunatakiwa tuhakikishe kwamba utekelezaji wa bajeti hii unakwenda kutupeleka mahali ambapo madini yatakwenda kuchangia pato la Taifa kwa kiwango kikubwa kuliko hiki tulichonacho leo na vilevile ukuaji wa sekta uweze kuongezeka. Ukuaji wa sekta utaongezeka vipi? Utaongezeka kwa sababu tutaongeza wigo wa wale wanaoshughulika na shughuli hizi za madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mahali nimesikia watu wanazungumzia habari ya makaa ya mawe, inaonekana hayajafanyiwa kazi, yafanyiwe kazi, lakini kuna mahali kwenye maeneo ambayo mimi natoka, jana nilikuwa napigiwa simu na mwanamke mmoja ananiambia, nina plant yangu, nataka umeme nitaupataje? Kwa hiyo, kuna mahali fulani ambapo watu wa umeme sasa wanatakiwa wapeleke umeme kwenye plant hizo ili uzalishaji uongezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa haya ni mambo mtambuka, basi Wizara zote ambazo zinahusika kwa mfano watu wa umeme wakaweke umeme kwenye hizo plants ambazo ninazisema ili uzalishaji ule uongezeke. Kwa sababu, tunajua kabisa bajeti ya umeme imeongezeka, haya mambo yatakwenda kufanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wale wanaoshughulika na kutoa leseni, Special Mining License, tuongeze wigo huu sasa. Tusichukue muda mrefu sana kuwapatia watu leseni kwa ajili ya kuongeza watu wanaochimba madini. Inawezekana pato letu linaonekana sasa hivi limekua, ni kwa sababu kumetokea mahali fulani mazingira yetu ya vita yale na nini bei yetu ya dhahabu ikapanda au bei ya madini fulani ikapanda, tukaonekana tuna mapato makubwa. Itakapokwenda ku-stabilize mapato yatashuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha pili ambacho nilitaka nikizungumzie ni katika hilo hilo ambalo tumesema, shabaha halisi ya bajeti hii ambayo tunaizungumzia leo imeongezeka. Tunatakiwa kutoka kwenye ukuaji wa 4.7 kwenda at least kwenye 5.3. Kuna mambo fulani ambayo yanatakiwa yafanyike na dhima imeyaonesha wazi. Mfano kilimo, tumepongeza kwa sababu kilimo kimeongezewa zaidi ya Shilingi bilioni mia sita kama na sitini hivi, lakini hoja yangu kubwa hapo ni kwamba, je, machinery yetu iliyozoea kupata Shilingi bilioni 100 tumeiandaa kwa ajili ya kubeba zaidi ya Shilingi bilioni 954? Tusije tukafika mahali tukamtengenezea sifa CAG mwaka kesho akija hapa atuoneshe tu kuna mahali kuna shimo hapa lilitokea, hapa shimo lilitokea. Machinery yetu ya kilimo iko tayari kubeba mzigo huu ambao tumeipatia? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho nilitaka kusema ni sekta ya mifugo na uvuvi ambayo nilitaka niizungumzie. Kilimo wamepata pesa, uvuvi wameongezewa na mifugo ukomo wao kwa Shilingi bilioni 100. Changamoto ninayoiona, sasa nimeona wameandika ukurasa wa 34, wanasema wanakwenda kuchukua Ranch ya Kongwa, hectares 38,000. Sielewi sasa, wakati huo huo kwenye page hiyo wanaonesha wazi kwamba kuna shida, bado mchango wa uvuvi na mifugo haujatosha kwenye Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilitegemea hii Shilingi bilioni 100 iliyoongezeka ikaboreshe NARCO Kongwa, lakini bahati mbaya ni kwamba haiendi kuboresha, wanakwenda kunyang’anywa Kongwa. Sasa sielewi tunakwenda kuboresha mifugo au tuna maana gani? Kwa sababu mapori bado tunayo mengi? Kwa nini wasiende sehemu nyingine tukaiacha Kongwa iboreshwe kwa sababu geographically ranch ilipokuwa located Kongwa pale ni mahali pa kimkakati zaidi. Tukiwaondoa maana yake tumeonesha kwamba, tunawapatia sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa inaonekana tunaondoa mifugo michache iliyo mle ndani, tunaweka mashamba ya alizeti, tunaweka kiwanda cha alizeti kikubwa. Mimi sifikirii kwa sababu tumeongezewa Shilingi bilioni 100, maana yake Shiingi bilioni 40 kwenye mifugo, Shilingi bilioni 60 kwenye uvuvi. Basi twende tukaboreshe maeneo yetu, badala ya kuanza kuyaua sasa, tukiyaua maana yake tutakuwa hatuwezi kwenda. (Makofi)

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na sekta ya kilimo ambayo nilikuwa naizungumza, tuna maeneo mengi. Maeneo ninayotoka yanapitiwa na Ziwa Viktoria, kwa hiyo, nilitegemea sana hizi irrigation schemes, (hii mifumo ya umwagiliaji) tuione mingi kwenye maeneo hayo ili maji ya Ziwa Viktoria yatumike tujenge uchumi wetu. Sina uhakika sana kama alivyosema mchangiaji aliyepita, tusije tukaja mwaka kesho tunapokuja kuzungumza hapa, tukazungumza kitu kingine tofauti na kile ambacho tumekipanga leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, kwa sababu nimesikia kengele imelia, nizungumzie wigo huu mpana uluoongezeka wa TIN Number. Tunapigiwa simu nyingi sana sasa kwamba tumerudisha kodi ya kichwa. Kwa hiyo, naona tu kwamba kuna nia njema ya Serikali kama wachangiaji walivyosema huko nyuma kwamba, TIN Number hizi ni muhimu kila mmoja apate Tax Identification Number. Kwa namna yoyote tutakavyofanya, kwa sababu tunataka kuhakikisha kwamba kila mmoja ana TIN Number, elimu ya kutosha itolewe kwa wananchi wetu ili isionekane kitu kipya kimekuja wananchi wanalalamika wanahisi kama kuna tatizo mbele ya safari, na sisi tukanyamaza kwamba tumeingiza kwenye utaratibu wetu na wananchi wakaona kama wanakwenda kufanyiwa habari ya kodi ya kichwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kabisa Mheshimiwa Waziri kwamba, kitengo kile cha elimu ambacho kipo kwa ndugu zangu wa TRA, kinaweza kwenda kule vijijini kikakaa siku mbili kikarudi Dar es Salaam halafu wanawaambia tumetoa elimu mahali fulani. Ukienda kuuliza elimu yenyewe iliyosemwa huko ndani inaonekena haitoshi. Kwa hiyo, tutumie vyombo vya habari, tutumie majukwaa yote ambayo yanawezekana ili wananchi wapate elimu kwamba TIN Number hii ina maana gani kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maneno haya machache kwa kengele iliyolia naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)