Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Aloyce John Kamamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia na kuwa mtu wa kwanza kwa muda huu wa jioni. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa, nzuri sana ambayo ameifanya hasa katika kupeleka fedha nyingi katika ujenzi wa madarasa, hospitali na barabara. Yapo maeneo mengine ambayo tangu dunia inaumbwa hayajawahi kupata barabara lakini kupitia Mheshimiwa Rais maeneo hayo sasa yamepata barabara, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kwa kugusa eneo la kilimo na nianze kupongeza Serikali kwamba kupitia bajeti yake ya mwaka huu, Serikali imeweza kuongeza fedha nyingi kutoka Bilioni 200 kwenda Bilioni 900 tunapongeza sana Serikali kwa fedha hizo ambazo zimepelekwa. Lengo la Serikali nafahamu kwamba ni kuongeza chakula lakini vilevile kujibu changamoto inayokabili Serikali hasa ya mafuta ya kula.

Mheshimiwa Naibu Spika, zao mojawapo ambalo Serikali imeweza kuliona na kuliweka ni zao la Chikichi. Kwetu Kigoma zao hili linakubali. Kwa hiyo niombe sana Serikali iongeze nguvu ya kutosha kwa kupeleka wataalamu wa kutosha wa mbegu ikiwa ni pamoja na mbegu ya chikichi katika eneo hili. Hii iende sambamba na kupeleka mbegu za kutosheleza kuweza kukidhi mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ardhi Kigoma ipo, ardhi siyo changamoto, lakini vile vile Kigoma mvua si tatizo, kwa hiyo eneo hilo linaruhusu moja kwa moja zao hilo kuweza kukubali, kwa hiyo naomba sana Serikali iangalie eneo hilo. Vilevile nasisitiza zao la chikichi kwa sababu zao la chikichi kupitia chikichi tunapata mafuta, kupitia chikichi tunapata sabuni, kupitia chikichi tunapata chakula cha mifugo na mazao mengine yote. Kwa hiyo, ili tuweze kufanikiwa naomba sana Serikali iongeze nguvu zaidi katika zao hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kukidhi zao hilo ambalo linaongeza mafuta lipo zao la alizeti. Kakonko tunalima zao hili vizuri sana, lakini changamoto ni upatikanaji wa mbegu, upatikanaji wa mbolea, niombe sana Serikali iandae mbegu mapema, iandae mbolea mapema, iweze kupeleka katika maeneo haya ili Kakonko na Mkoa mzima wa Kigoma tuweze kupata mafuta ya kutosha kupitia alizeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo miundombinu hasa ya barabara, barabara ni uchumi, lakini barabara ndiyo mishipa ya kuongeza uchumi katika nchi. Mkoa wetu wa Kigoma ikiwa sambamba na Mikoa mingine ipo mikoa ambayo haijaweza kuunganishwa kwa njia ya barabara hasa barabara ya lami. Kigoma haijaunganishwa na Tabora, Kigoma haijaunganishwa na Katavi, Kigoma haijaunganishwa na Mikoa ya Mwanza na Kagera. Niombe sana fedha zipelekwe haraka ili ujenzi uweze kukamilika na hatimae Kigoma kama Mkoa nao uwe umeweza kuunganishwa katika maeneo hayo.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ipo reli ya kisasa ya Standard Gauge. Nashukuru sana kwamba Serikali imeweza kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kutoka Uvinza kwenda mpaka Burudi katika Mji wa Itega na kwenda sambamba mpaka Congo. Najua kwamba Serikali imeweka katika mpango niombe sana Serikali iweze kuongeza fedha za haraka na ujenzi uweze kuanza mara moja kwa sababu barabara hiyo reli hiyo inahitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu bila malipo. Serikali imeweza kupeleka fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba elimu kuanzia Msingi hadi Kidato cha Sita inatolewa bure kwa maana gharama zote zinakwenda upande wa Serikali. Vipo vyuo vya elimu ya kati wapo wanamaliza Kidato cha Nne wanakwenda kusomea ualimu, wapo wamemaliza kidato cha nne wanakwenda kusomea ufundi, wapo wamemaliza kidato cha nne wanakwenda kusomea udaktari na kadhalika. Hawa Serikali inawaangalia kwa kiasi gani? Maana tunaona kwamba Serikali imechukua eneo la huku chini shule ya Msingi na Sekondari Kidato cha Tano na Sita, imekwenda mpaka Chuo Kikuu lakini hapa katikati ambapo pana watoto wa Watanzania wengi Serikali haijaweza kupaona. Naomba Serikali iangalie eneo hilo wapo Watanzania wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, watoto hawa ambao wanakwenda kwenye vyuo elimu ya kati hawana tofauti na hawa ambao wanakwenda Kidato cha Tano na Sita na kwa taarifa vijana wengi sasa badala ya kwenda hata kwenda kwenye vyuo na kadhalika wanatamani sasa kwenda Kidato cha Tano na Sita kwa kuwa Serikali imeamua kwamba iwe elimu bure. Kwa hiyo, niombe kwa kuwa hawa vijana wanakwenda kusomea taaluma wanasomea ufundi, wanasomea u-nurse, wanasomea udaktari ambao wanatoka moja kwa moja na kuweza kujiajiri, naomba Serikali iweze kupeleka fedha katika maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ajira ya watumishi. Ni ukweli kwamba Serikali imejenga madarasa mengi safi, lakini imejenga vituo vya afya safi, imejenga hospitali nyingi safi, imejenga zahanati safi, lakini ni sawa na chakula kizuri ambacho hakina chumvi. Watumishi wanahitajika, Waalimu wanahitajika, Madaktari wanahitajika, sasa sijaona vizuri ni kwa kiasi gani Serikali inapeleka nguvu kubwa zaidi katika kuajiri hawa watumishi ili waweze kufanyakazi kwenye shule zetu za msingi, kwenye hospitali zetu, kwenye zahanati zetu na kadhalika.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala la barabara ambayo inatuunganisha Tanzania na Burundi. Taarifa zilizopo ni kwamba nchi ya Burundi imehamisha Makao Makuu kutoka Bujumbura kuja Mji wa Kitega na Mji wa Kitega uko kilomita kama 150 kutoka mpaka wa Muhange, lakini hatuna barabara sasa ambayo inatuunganisha Tanzania kwa barabara ya lami kutuunga na nchi ya Burundi hasa kwa kwenda Makao Makuu ya nchi ambayo ni Kitega. Barabara ambayo inastahili kutuunganisha ni barabara ya kutoka Kakonko kwenda mpaka kwenye mpaka wa Muhange. Niiombe Serikali ilifanyie kazi hili kwa kupeleka fedha za kutosha, barabara hiyo ijengwe na niombe sana Waziri wa Fedha upeleke wataalam kwenye mpaka huo wa Muhange ambao wanajua kwamba barabara ikishajengwa na wataalam hao wakipatikana watakusanya fedha, kwa hiyo hiyo fedha ambayo utakuwa umeitumia kujenga barabara nina hakika fedha hizo zitarudi bila kuchelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara za Mji wa Dodoma. Dodoma ni Makao Makuu ya nchi, ni Jiji sasa, hatutegemei kwamba Dodoma itarudi iwe Manispaa au iwe Mji Mdogo lakini barabara zake ni tatizo. Ukiangalia sasa hivi Kiongozi yeyote wa Kitaifa awe Spika, awe Naibu Spika awe Waziri Mkuu awe Rais anapita Mji wa Dodoma unakuwa ni tatizo sehemu ya kupita. Sasa ni juu ya Serikali kuamua kulidhibiti tatizo hili mapema, isije ikawa kwamba baada ya muda ni mrefu sasa ndiyo tunaanza kufikiri kujenga barabara za kupitisha labda upande mmoja barabara tatu au nne upande mwingine barabara tatu au nne ni vema zikaanza kujengwa sasa ili kudhibiti tatizo la jam kwa maana ya wingi wa magari katika Mji wetu wa Dodoma. Kwa hiyo, napendekeza ijengwe barabara mapema ya kuweza kupitisha malori, badala ya malori kupita katika Mji wa Dodoma katikati basi malori hayo yaweze kupita pembeni kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa niendelee kupongeza Wizara ya Fedha kwa bajeti nzuri sana, ambayo imeiweka ina vipaumbele vyote muhimu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Serikali yetu inafanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja nashukuru sana ahsante. (Makofi)