Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa hii nafasi ili niweze kuchangia katika hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Kwanza, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake kwa kazi kubwa ambayo wameifanya na namna walivyokuja na bajeti nzuri yenye matumaini makubwa kama yeye mwenyewe alivyosema, kwa kweli tunawapongeza sana. Pia ninampongeza kwa kusimamia uchumi wa nchi yetu ambao ndiyo uhai wa maisha yetu, kwa kweli tunakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan alipokutana na Wabunge mara ya mwisho alituambia kwamba atapeleka mkazo zaidi kwenye sekta za uzalishaji na bajeti hii imeonesha yale aliyoyasema anaenda kuyatekeleza kwa vitendo tunampongeza sana kwa namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta za uzalishaji ziko kama tano, lakini sekta ya kilimo ikijumuishwa kwa mtazamo mpana inajumuisha kilimo cha mazao, mifugo na uvuvi pamoja na misitu. Sekta hii ndiyo imebeba uhai wa Taifa letu, tukifanya vizuri katika hili eneo tunao uwezo wa kupata mapato makubwa tuna uwezo wa kuondokana na umaskini, tuna uwezo wa Pato la Taifa likaongezeka kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kilimo ndiyo tunapata chakula chote na bila chakula chote na bila chakula hakuna kazi inayoweza kufanyika, sote tunategemea chakula lakini kwenye kilimo ndiko tunapata malighafi zote za viwanda, kwenye kilimo ndiyo kwenye ajira nyingi, kwenye kilimo ndiyo tunapata fedha nyingi za kigeni. Kwa hiyo, ina maana madeni yote tuliyonayo ya nje yatalipwa na fedha zinazotokana na sekta hii ya kilimo na sekta zingine za uzalishaji. Kwa hiyo, lazima tuongeze mkazo kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo pia ndiyo biashara kwa hiyo katika hayo maeneo matano ndiyo yamebeba nchi yetu, Watanzania walio wengi wanaishi huko, wanaishi vijijini wanategemea kilimo, wanategemea uvuvi, wanategemea ufugaji wanategemea misitu. Uwekezaji wa Taifa letu lazima ujikite kwenye eneo hilo na Rais wetu amejibu. Kwa mara ya kwanza nafikiri itakuwa ni mara ya kwanza kama sikosei, sasa bajeti ya kilimo yaani kwa tafsiri pana kwa maana ya kilimo cha mazao ya misitu, kilimo cha ufugaji na uvuvi tunazo zaidi ya Trilioni moja, kwa hiyo hili tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uwekezaji huu mkubwa alioufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuamua kuongoza na kuisimamia sekta ya utalii. Utalii wa nchi yetu unaweza ukaleta mchango mkubwa sana, tukiungana na sekta zingine za uzalishaji utalii utaleta manufaa makubwa sana. Ukiangalia sasa hivi utalii kwa mwaka uliopita mwaka 2021 duniani, pamoja na kuwepo kwa ugonjwa wa UVIKO-19 zipo nchi zimefanya vizuri kwenye utalii sana. Lakini ukichukua kwa takwimu za namna ya vivutio vya utalii vizuri Tanzania tulikuwa tunashika nafasi ya pili duniani sasa hivi imeshuka mpaka nafasi ya nane.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwa na nafasi nzuri na kuwa na vivutio vingi bado uwekezaji wetu hautoshi na bado hatujaweza kupata watalii wa kutosha hatujapata mapato ya kutosha. Kwa mfano, ukiangalia nchi inayoongoza sasa hivi kwa mwaka 2021 Ufaransa ndiyo iliyoongoza ilipata watalii milioni 89.4 ikifuatiwa na Spain ilipata milioni 83.7, Marekani ilipata milioni 79.3, China ilipata milioni 65.7, Italy milioni 64, Turkey milioni 51, Mexico milioni 45, Thailand milioni 39, German milioni 39, United Kingdom milioni 39, Tanzania hatujafika hata milioni moja kwa watalii wa nje, kwa hiyo ina maana eneo hili lazima tuwekeze vya kutosha, ndiyo maana Rais wetu ameamua kuja kuhakikisha anaisimamia hii sekta vizuri ndiyo maana akaja na huu utaratibu wa hii filamu ya Royal Tour. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli hii filamu inatutangaza sana kama nchi na mimi nafikiri tujipange katika kuhakikisha kwa kweli utalii ulete mchango mkubwa, hii ndiyo nchi pekee yenye vivutio vingi, tuna milima ya kutosha, tuna mito, tuna mabonde, tuna mbuga za Wanyama, tuna bahari, tuna maziwa, tuna kila kitu, tuna utamaduni! Sasa eneo la kuliangalia tusifurahie tu kwamba hoteli zimejaa tuseme kwamba bado tuwekeze zaidi kwenye hoteli ili tupate watalii wengi wa kuja kwenye mahoteli yetu, watalii wa kuja kwenye mikutano mbalimbali ambao hao ndiyo watakaotuletea fedha nyingi za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunataka utalii wa ndani uongezeke na ndiyo maana mwaka 2018 nilisema kwa mara ya kwanza kwamba Watanzania wajifunze kula Maisha, twende tukale maisha kwenye mbuga zetu. Watanzania wengi hawakunielewa walifikiri labda ni utani, hiyo ni theory ya uchumi! Ili uchumi wetu uchangamke Watanzania tukale maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nafurahi sana kuona Rais wetu ameunga mkono na ameonesha sasa yeye ameshika mstari wa mbele nasi sasa tumuunge mkono. nawapongeza sana umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi juzi walipokuja kwenye Mkutano wao wote waliongozana mpaka Ngorongoro kwenda kufanya utalii wakiunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais, nasi tuendelee kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais. Tutangaze vivutio vyote vilivyopo katika maeneo yote, Rais ametangaza sehemu sasa ni wajibu wetu sasa kutangaza vivutio vingine vyote vilivyobaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Mbozi kuna Kimondo cha aina yake cha kihistoria, kuna maji moto, kuna Ruaha kule kwa mwenzangu kule na maeneo mengine utalii wote Nyanda za juu Kusini nchi yetu hii tuviangalie tutangaze, naamini itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuangalie utalii wa elimu, tunavyo vyuo vingi tuhakikishe tunabadilisha taratibu za udahili ili watu wengi kutoka nchi za nje waje kusoma hapa, watatuletea fedha nyingi za kigeni, huo ni utalii ambao tunauhitaji. Tuna utalii wa matibabu, kufuatana na jitihada ambazo Serikali ya Awamu ya Tano na ya Sita zimechukua kuimarisha huduma za afya kwenye mahospitali yetu, tunapata wagonjwa wengi tunapata watalii wa matibabu. Hili ni eneo ambalo lazima tuwekeze vya kutosha na tuendelee, kuna utalii wa maliasili, kuna utalii wa mali kale na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ambalo nafikiri ni muhimu kwenye uzalishaji ni eneo la viwanda. Viwanda ndiyo uti wa mgongo kwa kilimo chetu tunatakiwa kuwekeza zaidi kwenye viwanda, sasa viwanda hivi bila kuwa na mfuko wa kuchochea maendeleo ya viwanda hatutaweza kufika, nashauri tuangalie namna ya kuweka mfuko wa kuongeza kuchochea viwanda itatusadia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la nne nilizungumzia kuhusu ujenzi wa bandari kavu kule Tunduma na Pemba kwamba ni muhimu sana ile bandari ikajengwa, kwa sababu itatusaidia nchi mbalimbali za kusini mwa Afrika zitakuwa zinachukua mizigo yao maeneo yale. Kwa hiyo, tuijenge ile ili kusudi watu kutoka Zambia, Malawi, Zimbabwe, Congo wachukulie mizigo maeneo yale itatusadia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo suala la mafuta tuongeze uwekezaji. Mheshimiwa Waziri tuangalie sehemu zote ambazo reli inapita reli ya kati, sehemu kule TAZARA inapita kwenye Mikoa mikubwa kama Dodoma tuweke matenki makubwa ya mafuta, mafuta yasafirishwe na treni, yaje hapa yawekwe kwenye hayo matenki, maeneo mengine kama Kigoma au Tunduma tuweke matenki ili kusudi nchi jirani waje kuchukulia mafuta hapa. Tutapata fedha nyingi, naamini zitachangia katika uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri kwa kuja na mifumo ya kusimamia matumizi ya fedha, kwa kweli nimefurahia sana kwa namna alivyokuja lakini amesema pia ameimarisha ukaguzi wa ndani, CAG tumemwongezea fedha na pongezi, lakini naomba niongezee sasa hawa Wakaguzi wa Ndani wana kazi kubwa ndio wanaosimamia fedha za umma, lakini wanahitaji kupatiwa mafunzo ili waelewe na waweze kwenda kufanya kazi vizuri. Sasa hivi utaratibu uliopo, fedha wanazitegemea kutoka kwa Maafisa Masuuli bado kama hatutarekebisha hawataweza kwenda kwenye miradi na kukagua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nafikiri tuliangalie hilo. Tuwatengenezee bajeti yao ili iwatosheleze kama ilivyo kwenye M&E. M&E wana bajeti yao na hawa Wakaguzi wa Ndani wawekewe mafungu kule katika kila mradi wa kwenda kufanya hiyo kazi na kufuatilia, itatusaidia sana. Pia tuwape vyombo vya usafiri, tuwape mafunzo, wataenda kufanya kazi nzuri sana na CAG atakapokwenda itasaidia sana katika kufikia ile hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafurahi sana kuona bajeti imekuja na majibu mazuri na matumaini makubwa, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, nawapongeza wote, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa kusikia kilio cha Watanzania cha kuja na bajeti inayoenda kutoa majibu. Nina uhakika ruzuku na mambo mengine yatasimamiwa vizuri ili nchi hii iweze kupiga hatua kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)