Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni hii ili niweze kuchangia na kutoa maoni yangu hasa zaidi kuhusu bajeti iliyopo mbele yetu na kuifanyia maboresho kwa manufaa ya nchi yetu. Kwa namna ya pekee kabisa niwapongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake Mheshimiwa Chande tumefanya kazi wote pamoja kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara, ni mtu makini na hawa wote ni watu makini sana na wasikivu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti iliyopo mbele yetu ni nzuri sana na kwa vyovyote vile imeonesha nia njema kabisa ya Mheshimiwa Rais kutaka kulisongeza Taifa hili mbele. Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara, kwa hiyo nitaongea kidogo kwenye upande wa biashara mambo ya kodi, tozo na mengine kwa maana ya kutaka kuboresha bajeti hii. Kwa namna ya pekee kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais pamoja na Wizara yetu ya Utalii kwa sababu hivi karibuni tumeona Mheshimiwa Rais amesafiri nchi nyingi hapa duniani kwenda kufanya kazi ya kutangaza vivutio vyetu vya utalii kwenye ile sinema maarufu kabisa inayoitwa Royal Tour. Hata hivyo, jambo ambalo nataka niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba kwenye Bunge lililopita kila mara tulikuwa tunaongea suala la vita ya kibiashara na tulikuwa tunajaribu ku-site namna ambavyo majirani zetu wanajaribu kutumia vivutio vyetu na kuvitangaza kama vivutio hivi ni vya kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vyovyote vile namna mama alivyofanya kazi nzuri kwenye hii sinema ya Royal isingekuwa rahisi majirani zetu kukaa kimya na kuona kwamba sisi sasa tunataka kwenda kuwa sehemu kubwa ya utalii katika Afrika ya Mashariki. Kwa hiyo lazima tutapigwa madongo kwa kila kona na sisi kama Watanzania lazima tuwe na uwezo wa kuwajibu lakini na kuongeza zaidi vivutio kwa maana ya biashara yetu ya utalii iwe kubwa zaidi kuliko nchi za jirani, kwa sababu sasa hivi tumeamua kueleza sisi wenyewe kwamba sisi kama Watanzania ndio wamiliki wa Mlima wa Kilimanjaro, sisi kama Watanzania ndio wamiliki wa Ngorongoro, sisi kama Watanzania ndio wamiliki wa Loliondo. Kwa hiyo ukishuka Uwanja wa Kimataifa wa Dar es Salaam, ukishuka Uwanja wa Kimataifa wa KIA uliopo Kilimanjaro kwa vyovyote vile utafika Kilimanjaro, utafika Loliondo, lakini pia utafika na Ngorongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zamani walikuwa wanasema ili ufike Mlima Kilimanjaro unatakiwa ukashuke kwenye uwanja wa nchi za jirani ili iweze kuwa rahisi kutoka kule kurudi hapa. Ninachoomba sasa ni kuboresha miundombinu ili tuweze kwenda sambamba na hizi kelele zinazopigwa na majirani zetu tusizichukulie poa poa kidogo, Mheshimiwa Waziri wa Utalii aongeze juhudi kwenye kuhakikisha sasa vivutio vyetu vya utalii vinatangazwa zaidi duniani kwa ajili ya manufaa ya Watanzania ili tuweze kukuza uchumi wetu tuweze kupelekwa kwenye nchi ya daraja la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kuna NGOs nyingine na wanaharakati hata Watanzania na wenyewe wamekuwa sehemu ya hujuma zinazofanyika kwa maana ya Ngorongoro lakini pamoja na Loliondo. Kwa hiyo tuwe makini sana tusichanganye mambo haya. Harakati pamoja na haki za binadamuh lakini harakati pamoja na biashara na lazima tutambue kwamba sasa hivi tupo kwenye vita ya kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine tumeona sasa hivi nchi yetu kumekuwa na inflation na hii inflation imesababishwa na kupanda kwa bei ya bidhaa. Ukiangalia vizuri imegawanyika katika namna mbili kuna sababu zetu wenyewe za ndani na kuna sababu za nje. Sababu za nje kila mara tulikuwa tunasema vita lakini pia na upatikanaji wa malighafi za kuzalishia, vitu vingi sisi tulikuwa tuna import.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa na sisi tuwe exports kwa maana tufanye kazi kwa nguvu kabisa tuhakikishe Mradi wetu wa Liganga na Mchuchuma unaanza mara moja ili tuweze ku-export chuma, tuweze kupata fedha za kutosha kufanyia miradi yetu ya ndani. Pia tuangalie, kuna tozo mbalimbali zinazotozwa kwenye bidhaa ambazo zinazalishwa hapa nchini lakini pamoja na bidhaa ambazo zinatoka nje ya nchi, tukiamua kurekebisha tozo hizi kwa vyovyote vile gharama za uzalishaji za ndani zitashuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, niwaombe Waziri amemaliza ku-present hii taarifa yake lakini kuna mambo tuyaangalie. Sasa hivi ni zaidi ya miaka minne, mitano, nafikiri toka VAT iliposhushwa kutoka asilimia 20 ikawa hadi 18 hawajagusa tena VAT lakini pia hawajagusa tena corporate tax. Tukiamua kushusha vizuri VAT labda kufikisha asilimia 16, tukashusha corporate tax hadi kufika asilimia 24, kutakuwa na compliance kubwa, watu wengi wataweza kulipa kodi na mauzo yataongezeka na hii itakwenda kuchangia kwenye kuongeza ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze hapa wakati Waziri anatoa taarifa yake alikubali kabisa kwamba sasa hivi Sheria ya Korosho ambayo ilikuwa ina-hold export levy amekubali sasa kurudisha, lakini tuiboreshe zaidi. Ilipoondolewa wakati ule ilikuwa ni asillimia 65 ambazo asilimia 50 zilikuwa zinarudi Serikali Kuu, lakini 15 zilikuwa zinakwenda kusaidia kwenye vituo vya utafiti na maeneo mengine. Sasa hivi imerudi ni fifty fifty, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri tutengeneze kanuni bora kuona namna ya kutumia fedha hii. Sisi tunatamani sana fedha hii ingekwenda kupelekwa kama ruzuku kwenye pembejeo zinazosaidia kuzalisha korosho, lakini fedha imepelekwa Wizarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizarani kuna mazao mengi sana, madhumuni ya fedha hii ilikuwa inakatwa ili ikasaidie wakulima wa korosho pamoja na kwamba sasa hivi wakulima wa korosho wamekuwa mtambuka nchi nzima watu wanahamasishwa kulima korosho, sio jambo baya, lakini ikasaidie tu kuendeleza zao la korosho.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kuna suala la blueprint. Mheshimiwa Waziri wakati analeta taarifa yake ameongea sana kuhusu suala la blueprint na kwamba kuna kodi zile mbalimbali karibu 15, nafikiri wameamua kuziondoa ili kuweza kuona zinawafanya wawekezaji kuvutiwa kuja nchini kwetu kuwekeza kwa sababu ya kutengeneza mazingira rafiki ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe kwamba speed inayotumika sasa hivi kwenye kutekeleza mambo mbalimbali yaliyomo ndani ya blueprint ni ndogo sana. Niombe Wizara iongeze speed kwenda kuhakikisha na zile kero zinazotajwa na wafanyabiashara wanaokuja kuwekeza hapa Tanzania nazo zinaondoka, mojawapo ikiwepo hii ya city levy. city levy inapangwa na halmashauri zetu lakini city levy sheria inataka kuanzia asilimia 0.01 hadi 0.03. Kutokana na kuwa na vyanzo vichache vya mapato Halmashauri nyingi zinaamua kukamua wafanyabiashara. Wengi wanang’ang’ania kutoza asilimia 0.03 wakati ruksa ni kuanzia asilimia 0.01 hadi 0.03.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa karibuni tulifanya ziara Bukoba, tulitembelea viwanda pale na tukaenda kwenye Kiwanda cha AMIMZA kwenda kujionea wenyewe wanaozalisha kahawa lakini pia tulifika kiwanda cha sukari, hii mitaji imekuwa ni kero kubwa sana. Nimwombe Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up basi atuambie kwamba ni nini, kodi hii lazima iwe ya pamoja,haiwezekani ukienda Mtwara ukute asilimia mbili, ukienda Bukoba ukute asilimia tatu, ukienda maeneo mengine, inakuwa inatofautiana. Kwa hiyo lazima nchi nzima iwe uniform, kama asilimia 0.01 kwa ajili ya city levy iwe hivyo, kama ni asilimia tatu basi iwe hivyo, lakini utofauti unaoletwa kwa kila halmashauri sio mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la capacity charge. Kuna tozo ambayo ipo kwenye umeme inaitwa capacity charge, kwa kawaida wazalishaji ukienda kwenye kahawa tuseme labda tutumie mfano, lakini ukienda kwenye viwanda vya korosho huwezi kuzalisha kwa mwaka mmoja, kuna kipindi fulani ambacho wanafunga uzalishaji. Sasa unapofunga uzalishaji bado Serikali au kwa maana ya TANESCO wanaendelea kukutoza gharama za umeme kwa asilimia 75 katika mwezi wa kwanza kutokana na previously bili yako. Bili uliyolipa mwezi uliopita tunazota asilimia 75 mwezi huu, halafu ukiacha tena kuzalisha au kutumia umeme, mwezi unaofuata unatozwa asilimia 50. Hii imekuwa kero kubwa sana kwa wafanyabiashara, kwa hiyo tunaomba sasa tuachane na hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine tumeona walifanya marekebisho hapa sasa hivi crude oil, nafikiri itaingia kwa asilimia sifuri, lakini tuangalie na viwanda vya ndani. Unapoamua kuruhusu wafanyabiashara wa nje kuingiza mafuta pasipo kutoza kodi, tafsiri yake unakwenda kusababisha upotevu wa ajira au uzalishaji, lakini tuangalie namna gani hili jambo tunakwenda kulifanya. Kwa vyovyote vile kama sisi Wajumbe wa Kamati ya viwanda na biashara tulikuwa tunajadili ili mara nyingi, utakapomruhusu mwekezaji wa nje aingize ndani mafuta ghafi kwa asilimia sifuri, ndio nia ni njema kutaka kupunguza gharama za mafuta hapa nchini, lakini tuone namna gani tunakwenda kuathiri viwanda vinavyozalisha mafuta hapa nchini kutokea level ya chini, maana yake kwamba wao wananunua alizeti, watakwenda kuzichuja mafuta, watafanya refinery baadaye wanaziingira sokoni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoleta crude oil kwa asilimia sifuri, watu wataondoka. Tulikitembelea kiwanda kimoja Dar es Salaam, siwezi kutaja jina, lakini alikuwa analalamika kwamba wanaoleta mafuta toka nje wana-declare kwamba ni crude oil, wanafikia kwenye process, labda katikati ya process nzima ya uzalishaji. Kwa hiyo unaweza ukakuta gharama yake ni chini zaidi kuzalisha na kikubwa anachofanya ni kusafisha na kufanya packaging, lakini wale watu wana watu wanaonunua alizeti mitaani, wana watu wanaosafirisha alizeti kuleta viwandani, lakini pia kuna watu wanaofanya kazi ya kupepeta, kuchekecha hizo alizeti mpaka zinakuwa mafuta. Kwa hiyo tuone namna gani tutavisaidia viwanda vya ndani pamoja na nia njema ya Serikali kutaka kupunguza hizo gharama za uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la kodi kama ambavyo nimesema hapo, tunapoweka kodi nyingi kwenye viwanda, kwa vyovyote vile vitapunguza ajira, tunapoamua kusaidia viwanda kwa kupunguza kodi na sehemu kubwa ndio tunayosema VAT, tumeona hapa Serikali imeamua kufanya VAT refund hapa karibuni, lakini pia tumeiona Serikali inajaribu bado kutaka kuwasaidia wale wawekezaji wa ndani. Mfano, nilioutoa kwenye mafuta unafanana pia mfano huo kwenye viwanda vya bati.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona sasa hivi kuna viwanda vingi sana vya bati vimeingia Tanzania, lakini wenzetu nitataja kwa jina ALAF, wao ALAF wanachokifanya wananunua rollers zile bar rollers, mara nyingi ukiangalia ukiwa unatoka bandarini unaziona na wao wanaanza process kuanzia ya kwanza kuchukua zile chuma, kuzibonda, kuzi-size, kuzipiga rangi na baadaye kuziweka migongo na kuzikata, lakini kuna viwanda ambavyo wanaingiza hizo material zikiwa tayari karibu na kuwa semi-finished, wakifika hapa Tanzania kazi wanayoifanya ni kupiga rangi na kuweka migongo na kuzikata na kuziingiza sokoni. Kwa hiyo unaweza kuwa na kiwanda cha bati chenye watu 20…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi na mengine nitayaleta kama mchango wangu kwa maandishi. Ahsante sana. (Makofi)