Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika bajeti hii iliyoletwa mbele yetu na Waziri wa Fedha. Kipekee napenda kuwashukuru viongozi wa Wizara hii, Waziri, Mheshimiwa Mwigulu pamoja na Mheshimiwa Hamad Chande kwa namna ambavyo wamekuwa wakiendelea kufanya kazi vizuri. Pia nawapongeza Katibu Mkuu wa Wizara hii na Manaibu wote kwa namna ambavyo pia wamekuwa wakitekeleza majikumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee zaidi namshukuru Mheshimiwa Rais wetu kwa namna ambavyo amekuwa akifanya mambo mzuri, nami kama mwakilishi wa Mkoa wa Songwe, ninayo mengi mazuri ambayo najivunia ambao Mheshimiwa Rais ameweza kufanya kwa ajili yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitapenda kuongelea masuala machache ambapo suala moja kubwa ni kuhusu mkataba huu ambao umesainiwa wa uuzaji wa makaa ya mawe, ambapo nchi yetu ya Tanzania itaenda kuiuzia makaa ya mawe nchi ya Switzerland, na tumesaini mkataba wa kuuza tani 60,000 za makaa ya mawe kwa hiyo nchi ya Switzerland. Kwa sisi watu wa Mkoa wa Songwe hususan Wilaya ya Ileje, ni fursa nzuri sana ambayo kwa kweli tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutusaidia kuweza kuipata hii fursa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu Wilaya ya Ileje ni moja ya wilaya ambazo zinamakaa ya mawe mengi sana katika nchi hii. Kwa taarifa ambazo zipo na zilizofanyiwa utafiti zinaonesha kuna reserve ya tani milioni 100 ya makaa ya mawe katika eneo hili kitu ambacho kwa kupitia huu mkataba uliosainiwa, tani 60,000 tutauza kwa 4.4 billion inaonesha kwamba kama tutafanikiwa kuuza haya makaa yote ya mawe ambayo ni tani milioni 100, kwa nchi yetu tunaweza tukaingiza kiwango cha Shilingi bilioni 6,900. Nadhani ni pesa nyingi sana ambapo kama nchi tunaihitaji kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba huu uliosainiwa utekelezaji wake unaenda kuanza ndani ya mwezi huu. Kwa namna hiyo, kupitia huu mkataba ambao ni wa miaka mitano, ina maana ya kwamba tutaweza kuvuna tani milioni 3.6 tu, kitu ambacho tunaona kwamba bado tunayo fursa ya kutafuta mikataba mingine mingi zaidi ili haya makaa ya mawe yaweze kutumika na kuliletea Taifa letu kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema nini? Kweli tumepata mkataba, lakini tunafahamu kwamba haya makaa ya mawe yaliko bado miundombinu haijakaa vizuri hususan kwenye barabara. Nilitamani kuiomba Wizara hii iweze kuweka kipaumbele cha ujenzi wa barabara hii ya kilometa saba ambayo fedha yake imetengwa kupita TARURA, badala utekelezaji uende kufanyika kupitia TARURA, tulitamani kwamba utekelezaji huu ufanywe na TANROAD ili iweze kufanyika kwa haraka sana kulingana na umuhimu wake ambao upo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kama barabara haitakaa vizuri ina maana uzalishaji na usafirishaji wa haya makaa ya mawe itakuwa ni changamoto kubwa. Kwa hiyo, kwa maana ya ujenzi wa kiwango cha lami kupitia TANROAD utafanyika kwa haraka kitu ambacho tutakuwa tumeisaidia nchi yetu kurahisisha uuzaji wa haya makaa ya mawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema nini? Mpaka sasa hivi hii barabara ya kilometa saba imekuwa haitumiki. Kwa hiyo, wanatumia barabara nyingine mbadala ambayo ina kilometa 36 ambapo kwenda na kurudi unakuta kilometa 72, kitu ambacho kinaongeza gharama za usafirishaji wa yale makaa mpaka ile selling point ya haya makaa ya mawe. Ukiacha hivyo, pia ule mzunguko wa usafirishaji wa makaa ya mawe unachukua muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, najaribu ku-justify kwamba ujenzi wa hii barabara kwa kilometa saba kwa Serikali itaweza kuipunguzia gharama zisizokuwa za lazima. Kwa hiyo, nawaomba kwamba ile fedha iliyotengwa TARURA ihamishiwe TANROADS ili zoezi liweze kufanyika kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha hilo suala la barabara, pia tunafahamu kabisa kwamba pale Kyela kuna Ziwa Nyasa ambapo tumekuwa na mkakati wa ujenzi wa meli na meli zilizojengwa mpaka sasa hivi kwa usafirishaji wa mizigo hii zinaonekana ni ndogo, kama kweli Serikali ikiamua kuwekeza kwenye ujenzi wa meli nyingine mpya kubwa ya mizigo, itarahisisha usafirishaji wa haya makaa ya mawe kuelekea Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kabisa kupita Ziwa Nyasa kwenda Mtwara ndiyo inakuwa njia nyepesi ya usafirishaji wa mizigo kuliko kusafirisha haya makaa ya mawe kupitia barabara ya kutoka Kyela, Mbeya, Makambako mpaka Songea kuelekea Mtwara. Kwa hiyo, naishauri Wizara ione umuhimu wa kuwekeza katika Ziwa Nyasa, kujenga meli nyingine mpya kubwa ya mizigo ili tuweze kusafirisha kwa urahisi na kwa namna hiyo tutakuwa tunazilinda barabara zetu ambazo tunazijenga kwa gharama kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuliongea hilo, natamani kuongelea katika kipengele cha TAZARA. Ninaongelea TAZARA kwa uchungu mkubwa kwa namna ambavyo imeharibika, imechakaa. Kitu ambacho tunajua, kama tuliweza kukaa awali, tukatengeneza hiyo sheria ambayo ipo na tukawa tunaitekeleza na sasa inaonekana kwamba hiyo sheria inakuwa kama haitupi fursa ya uwekezaji sisi kama Watanzania, tuone namna ya kuweza kupitia hii sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, natamani kuona Serikali inachukua hatua kwenye kufuatilia utekelezaji wa hiyo sheria ambayo inaifanya Tanzania ishindwe kuendelea kuwekeza katika TAZARA. Kwa namna hiyo, kama sheria ikibadilishwa tunaamini tutanunua mabehewa lakini pia tutawekeza kwenye repair ya hii reli ya TAZARA. Hivyo, Serikali iione TAZARA kwa jicho la kipekee. Kwa sababu tunaamini kabisa lengo la ujenzi wa TAZARA ilikuwa ni kusafirisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kuelekea nchi za SADC. Kwa namna hiyo na tunafahamu kabisa asilimia 70 ya mizigo inayoingia bandarini inaelekea nchi ya Malawi, Zambia na Congo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niiombe Serikali ilichukue hili kwa kipekee iweze kupitia hiyo sheria na kupitia kama tutaweza kuboresha utendaji kazi wa TAZARA. Tuweze kufikiria ni kwa namna gani tutengeneze bandari kavu katika eneo la Mpemba pale Tunduma. Tunajua kabisa bidhaa nyingi wanaonunua ni watu wa hizi nchi za SADC, kwa nini tusione umuhimu wa kujenga hii bandari kavu pale? Kwa sababu tutakuwa tumerahisisha mambo mengi, kwa sababu barabara zetu hazitaharibika lakini mizigo itafika kwa wakati. Uratibu wa mizigo utakuwa ni kwa haraka kwa sababu itakuwa ipo specifically kwa eneo la watu wa SADC. Kwa hiyo, ipo haja ya kuona Serikali inachukua hatua kwenye ujenzi wa dry port Tunduma pia kwenye utengenezaji wa hiyo meli, hii itachangiza uanzishwaji wa free market katika eneo la Tunduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)