Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami ninakushukuru kwa kuweza kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye hotuba ya mapendekezo ya Serikali ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwa kweli kwa kushukuru na kutambua jinsi Serikali ambavyo imeona iweze kuhakikisha kwamba watoto wa kaya maskini na wenyewe wanapata elimu kama vile wanavyopata wenzao na kwa kuanzisha Mfuko Maalum ambao kwa mwaka huu wa fedha wametenga Shilingi Bilioni Nane na wameelekeza kwamba zitaenda TASAF ili kwa wale watoto wanaotoka kwenye kaya maskini wanaoshindwa kujiendeleza na shule ya sekondari waweze kwenda kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika hili napenda kushauri. Pamoja kwamba mna nia njema na imeelekeza kwamba database inapatikana TASAF na kutoka kwa Wabunge na Madiwani, napenda kushauri kwamba wale Maafisa Maendeleo ya Jamii ndiyo ambao wanajua na wako pale wanajua hizi kaya maskini wanaweza kuwa na database nzuri. Huko nyuma tuliwahi kushauri kama ingependeza TASAF ingeweza kutoka Utumishi ikaenda ikawa chini ya hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii maana yake ndiyo wanaozitambua hizi kaya maskini, ndiyo maana hata tunaweza kuona kunakuwa na changamoto nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi ili kuweza kuona hizo Shilingi Bilioni Nane zisiwe misused ziweze kwenda kwa walengwa ambao ni walengwa hasa ambao wanatakiwa waweze kupata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia na hili suala la kuondoa ada kwa Kidato cha Tano na cha Sita ni jambo jema, lakini tuangalie sasa ni vipi tunafanya elimu inakuwa bure kuanzia shule ya msingi, sekondari na hata kidato cha tano na cha sita, siyo kuondoa ada tu wakati unaacha mlundikano mkubwa wa michango ambayo wazazi wanashindwa kumudu na watoto wanapelekea kutokwenda shule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine sasa najielekeza kwenye mchango wangu ni kuhusu kuhusiana na hali ya umaskini kwa Taifa letu. Mpango wa maendeleo wa miaka mitano uliainisha kabisa kufikia mwaka 2025 tuwe walau tumefikia asilimia 22, tupunguze umaskini wetu kwa asilimia 22. Kwa data zilizopo mwaka 2018 kiwango cha umaskini kilikuwa ni asilimia 26.4, kwa uwiano wa kwamba vijijini 2018 ilikuwa ni asilimia 31.4, tunagemea kwamba ikifika 2025 basi tuwe tumeshuka kwa vijiji kufika asilimia 28.1. Kwa Mijini kutoka asilimia 15.8 mpaka asilimia 13.2 kwa mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia sasa umaskini wa mahitaji maalum kwa Watanzania kwa kipindi cha miaka 10 umepungua kwa asilimia 1.8 tu. Kwa maana mwaka 2012 ilikuwa ni asilimia 28.2, mwaka 2021 ilikuwa ni asilimia 26. Ukiangalia hapo tumeweza kumudu kupunguza umaskini kwa asilimia 1.8 tu kwa miaka 10, tumepunguza kwa asilimia 1.8. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa nini nimesema hii? Ili tuweze kuondoa umaskini kwa Mtanzania lazima tuhakikishe kwamba tumemuinua kiuchumi. Sasa ukiangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameainisha kabisa kwamba anaenda kupunguza kwenye zile asilimia 10 ambazo zilikuwa zinamuinua, makundi maalum yale ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, anaenda kupunguza asilimia tano anazipeleka kwenye miundombinu na masoko ya wamachinga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii inakuwa inazidi kurudisha nyuma katika kuhakikisha kwamba unamuinua Mtanzania mmoja mmoja aweze kujiinua kiuchumi. Ninashauri tu kwamba, lengo linaweza kuwa lipo vizuri, lakini mosi halitakuwa na uwiano katika Halmashauri zenye mapato makubwa na zile Halmashauri hazina mapato kabisa. Leo kwa mfano kule Tarime tukijikakamua sana Tarime Mjini ni kati ya shilingi milioni 900, shilingi bilioni 1.1, shilingi bilioni 1.3; ambapo asilimia 10 ni shilingi milioni 130, asilimia tano unazungumzia shilingi milioni 50 mpaka milioni 75. Kusema hawa watu wajenge masoko na miundombinu kwa shilingi milioni 50/50 hizo wadundulize kwa miaka takribani 20 wakati huo hata yale makundi maalum umewanyima hizo fedha, then miundombinu inakamilika hawajaweza kujiinua kiuchumi, sasa hayo majengo wanaenda sasa wanaingia popo, maana yake yanakuwa hayana watu ambao umewa-empower kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukilinganisha na Dodoma Jiji mapato yao labda shilingi bilioni 40, shilingi bilioni 50 asilimia 10 kwao it makes sense inakuwa ni shilingi bilioni tano. Ukichukua plus shilingi 500 hapo ni shilingi bilioni 2.5, hawa at least is viable kwao. Kwa hiyo, tuliangalie hili wazo, it’s not practical at all. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine Serikali lazima itafute fedha, ijenge miundombinu hii ya masoko ambayo yatakuwa na uniformity Tanzania nzima. Kama unajenga Dodoma soko la machinga complex kama hili ambalo tumeona, basi na Mwanza lijengwe na Tarime lijengwe na kwingineko kote. Inaweza ikapungua tu ukubwa lakini uwe na uniformity ya muonekano ulivyo. Leo ukisema tudundulize shilingi milioni 20, shilingi milioni 30 ndiyo unakuta yaani visoko vya ajabu ajabu. Kwa hiyo, hili mimi napingana nalo na naishauri Serikali iende iwaze vema katika hili, kuleta usawa kama tulivyofanya kwenye COVID-19 ile fedha tuliyopata shilingi 1.3, mkatoa fedha zinaelekezwa na zikaonesha miundombinu ilipo na kila mtu ana-appreciate sasa hivi anaona, its tangible unaweza ukaiona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia kuhusu capital goods. Katika zana ile ya kumuinua Mtanzania kiuchumi mmoja mmoja ili mwisho wa siku tuone kabisa uchumi wa Tanzania unakua, amesema kwamba capital goods ya shilingi milioni 60 kuendelea ndiyo atapata msamaha wa kodi VAT. Mimi nashauri na nashauri hili hata tuweze kuiga kwenye nchi za South East Asia zenye tight economy, wenzetu wale waliwekeza kwenye viwanda vidogo na vya kati kwa kuviwezesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tupunguze hii fedha, irudi mpaka shilingi milioni 20 ambayo ndiyo capital goods iwe hivyo, waweze kupata msamaha wa VAT, tutaweza kuibua Watanzania wengi ambao hata hizi fedha ambazo tunazikopesha kwenye Halmashauri zetu, kuweza kuwapa hivi vikundi vya milioni 20 kuweza kuagiza hivyo vifaa, ila sasa wanavyoleta wapitishie, wahakikishe kwamba wanafanya incubation SIDO kwa mwaka mmoja kuweza kupata mafunzo. Wakati huo wa kufanya mafunzo unakuta wameshaingia kwenye operation ili sasa kuweza hata ku-avoid hizi charges ambazo ni tozo, kodi mbalimbali kutoka kwenye mamlaka mbalimbali kwa mwaka mmoja wa mpito hao watu utakuwa umewainua sana. Baada ya mwaka mmoja wanakuwa wameshaji-establish na wanaweza kulipa na kodi ya Watanzania, kinyume na hapo hatutaweza kuona chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine pia wameweza kuainisha kodi ya mfuto kwa lori na mabasi. Mmesema shilingi milioni 3.5, tuwe na uhalisia. Haya malori kwanza hamjaya-categorize, yaani hauwezi kusema unaweka kodi ya mfuto ya shilingi milioni 3.5 kwa lori la tani nne kwa lori la tani 10 sijui tani ngapi ni kuwafanya hawa watu waondoke kwenye hii biashara, ukizingatia operation cost ziko juu. Mafuta yamepanda, vipuri vimepanda, mtapandisha kodi mwisho wa siku hizi shilingi bilioni 141 hamtaziona, zitakuwa kama kodi za simu tu. Tukiwa na matarajio zitafika Shilingi Trilioni 1.02, tunaishia kupata hata shilingi bilioni 300 hazifiki, kwa sababu kodi imekuwa kubwa, watu wame-pull out. Ndiyo kitakachotokea hapa Mheshimiwa Waziri! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wata-pull out, watu wa malori wataacha biashara ya malori, watu wa mabasi wataacha biashara ya mabasi, mwisho wa siku hata zile kidogo mlikuwa mnapata msizipate! Ninashauri, kwanza mzi-categorize labla kuanzia tani kadhaa mpaka kadhaa labda walipe shilingi milioni 1.5 na zile kubwa hebu walipe shilingi milioni 2.5 ili kuhakikisha kwamba wote mnawaweka on board.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ujenzi, tumeona kwanza ilivyo sasa hivi bei za vifaa vya ujenzi zimepanda ukilinganisha mwaka jana na mwaka huu. Kwa mfano, Tarime bei ya nondo kwa mwaka jana Machi, nondo milimita 12 ilikuwa shilingi 21,000, sasa hivi Machi - training za TPSF walikuja kutupa semina juzi ni shilingi 27,000 ongezeko la asilimia 28.5. Milimita 16 ilikuwa ni shilingi 34,000 sasa hivi ni shilingi 44,000 ongezeko la asilimia karibia ngapi huko. Ukija kwenye mabati ilikuwa 28-gauge ilikuwa ni shilingi 26,000 sasa hivi ni shilingi 40,000 ongezeko la asilimia 53 na mengine mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mmeweka kodi, kwamba mnaweka kodi kwa wanaoingiza finished goods ambayo ninakubali, kwamba mnataka mlinde viwanda, lakini hivi viwanda raw material zinatoka nje, zile raw material zenyewe zinakodi kubwa at the end of the day watakuwa hawana hiyo importation, achilia mbali hamjafanya assessment kujua kama production capacity na surplus demand ya Watanzania wanavyohitaji. Kwa hiyo, kwenye raw material goods zinazokuja zina kodi, mwisho wa siku operation cost ikiwa kubwa bado vifaa hivi vitakuwa vikubwa sana na ile dhana ya kuwa na maisha bora kwa Mtanzania haitakuwepo, hatutaweza kujenga makazi bora. Mtu hawezi ku-afford kununua nondo kwa shilingi 36,000 tena baada ya Julai itakuwa shilingi siyo 36,000 ni shilingi 40,000 huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, white cement tulikuwa tunanunua kwa shilingi 33,000 sasa hivi hapa Dodoma ni shilingi 48,000 nani ambaye ata-afford? Watajengea fito, watatumia mbao badala ya kutumia chuma na kila kitu, na hayatakuwa makazi bora. Kwa hiyo, nashauri wakati tunaangalia hizi kodi Serikali iangalie kodi ambazo hazimkandamizi Mtanzania bali zinaenda kumsaidia kumuinua, lakini hata viwanda vyetu kwenye hizo imported raw materials mpunguze kodi, muwape incentives ili waweze kuzalisha visiweze ku-pull out of the market. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mengine nitayachangia kwa maandishi. (Makofi)