Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kuweza kunipa nafasi nami niweze kuchangia mawazo yangu kidogo kwenye hoja ya bajeti iliyowasilishwa na Waziri hapa kwenye Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuweka hapa muda wote ili tuweze kuweka mipango yetu katika tafsiri ya fedha na nina uhakika fedha tulizozitenga na bajeti ilivyosomwa na mambo yaliyoko ndani ya bajeti kama yakisimamiwa vizuri, utekelezaji ukaleta tija, basi Watanzania wanaweza kuguswa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitazama bajeti hii wako watu watakaofurahi na kuna watu ambao wameguswa hawataweza kufurahi. Kwanza niongezee kwa Mheshimiwa Esther pale aliposema kuhusu watoto wetu wa kidato cha tano na kidato cha sita kuwa katika elimu bure. Niende kwenye ukurasa wako Mheshimiwa Waziri wa 159, pale ulipoweza kuweka fedha ya maendeleo. Umetoa Shilingi Bilioni 346.5 na ukasema itagharamia elimu ya msingi bila ada.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa neno hilo elimu ya msingi sijajua unamaanisha basic education kwamba Tanzania tunapaswa kupeleka mpaka form five na six au vipi, labda uiangalie vizuri statement hii sijaielewa vizuri unaposema elimu ya msingi bila ada sidhani kama unaongeza na watu wa form five na form six. Basi kama ni aina fulani ya Kiswahili au Tanzania tuambiwe sasa basic education ni nini na je, hizi shilingi bilioni 346 zime-include na form five na six? Kwa sababu ni mpango mpya na watoto wengine wameshaenda shuleni. Tunachoomba ni kwamba, Serikali sasa iwe na mpango mzuri kuhakikisha kwamba jambo hili linatekelezeka vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili nakwenda na kurasa zako, ukurasa 107 na bahati nzuri kifungu ni 107 ambacho kinasema, kubadili sheria Serikali za Mitaa ile 10 percent. Tunapaswa tuiseme wote na hasa sisi wanawake kusema ukweli. Napenda kuuliza ni kwa nini Serikali imegeuza Mfuko huu kama shamba la Bibi? Mfuko huu unatolewa na Halmashauri na umelenga kusaidia makundi maalum, ukitazama tangu sheria hii iwepo hatujapima hata tija na hasa kwa watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napendekeza Serikali itafute Mfuko mwingine, Halmashauri hizi kumbuka mmeshazinyang’anya mapato yote. Mmezinyang’anya mapato yote, majengo, mabango na kila kitu. Kwa hiyo, Halmashauri nyingine zinachechemea. Sasa kila kitu kinachokuja, kila Wizara Halmashauri, kila Wizara hata Bajeti Kuu inasukuma mzigo wa machinga kwa Halmashauri, kwa kweli jambo hili siyo sahihi na kwa upande wangu mimi sikubali kabisa kwamba, hakikisheni huu Mfuko unabaki jinsi ulivyo. Kama mnaamua kutenga ile percent ya vijana kupeleka kwa machinga, mkumbuke wanawake walio wengi siyo wamachinga, basi wasikope Halmashauri muwape Mfuko wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema katika kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali. Umesema maneno mengi, umesema mengi kuhusu magari, mambo ya manunuzi. Napenda kukuongezea vitu kama viwili pale. Kwanza katika manunuzi na hasa katika tenda, Mheshimiwa Waziri uandike hapo, kuna kitu kinaitwa correction of error, pale kwenye tender, pale mtu anapo-tender, labda mmesema kwamba ya chini ni shilingi bilioni moja, lakini anapewa kwa sababu sheria inasema apewe mtu aliye-tender kidogo, hiyo sheria inatoa mandate kwa watoa tender kwenda kurudia zile hesabu za BOQ.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta mradi kama ulikuwa wa shilingi bilioni moja, ile correction of error inakwenda shilingi milioni 500. Sasa tunashangaa na tumeiona hii kwa sababu niko kwenye Kamati ya LAAC na tunakagua miradi, tunakumbana na vitu vya namna hiyo, ni upotevu mkubwa wa fedha, kwa hiyo, uiangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna majengo mapya ya Halmashauri. Kuna maeneo mapya ya utawala. Sasa maeneo haya yanapaswa kujenga ofisi, is well and good. Ofisi zenyewe zinajengwa lakini Serikali iweke limit ya fedha. Tumeenda katika ziara zetu, tumeenda kwa mfano katika Halmashauri ya Busokelo, tumekuta wamejenga jengo lina vyumba 203 plus one. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unaweza kujiuliza, Halmashauri inajenga vyumba 203, unajenga na hoteli za kulaza watu mle ndani? Kwa hiyo, tunapenda ofisi zijengwe, ziwe na standard na kiwango fulani cha fedha na ramani ambayo itawezesha nyumba hizi kuwa nzuri. Pia tufikirie huduma zaidi inayotoka kwenye majengo hayo kuliko thamani yake na show. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mtazame namna hiyo kuweza kupunguza kuwe na standard kwamba nyumba itajengwa kwa shilingi bilioni mbili basi iwe shilingi bilioni mbili na ramani ziangalie na mahitaji. Kwa hiyo, hakuna sababu ya kujenga yale bungalows makubwa ambayo hayana maana. Unaenda kuangalia ofisi ya Mkurugenzi unashangaa kwamba inawezekana hata wewe Waziri wa Fedha hiyo ofisi huna, kwa sababu…..! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nije sasa kwenye force account. Hii force account katika kutengeneza miradi siyo kitu kibaya. Kinachohitajika Halmashauri ziwe na Wahandisi ambao wanaweza kusimamia. Kipindi fulani nimeshachangia hapa nikasema, Serikali, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Elimu ishirikiane ili wapeleke vijana wetu VETA, wale technicians wajifunze mambo ya kujenga, mambo ya barabara. Hata ukienda kwenye Chuo cha VETA - Dodoma hapa, bahati nzuri mimi nimepeleka watoto wengi kusoma hapo. Wanavyo vitengo vya ujenzi (mason), wanavyo na vitengo kabisa vya kujenga barabara. Sasa tunakosa wasimamizi, huku chini Halmashauri zetu hazina Engineers lakini force account inasaidia kujenga miradi mingi kwa gharama ndogo pia tutazame sasa kile kiwango cha miradi, kama miradi inafikia bilioni sita na kuendelea tunaweza kuweka Mkandarasi, lakini kama miradi ile ni ya kujenga madarasa, kuna wengine kwa kweli wamefanya vizuri, kwa mfano tulienda Mbeya Mjini wametengeneza hospitali nzuri kabisa kwa force account, ukifika pale unaridhika na maeneo mengine ambayo tumepita, kwa hiyo nina uhakika kwamba tunaweza kuendelea na force account lakini pawe na usimamizi, hakikisheni ndani ya Halmashauri kunakuwa na Engineers. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, force account inasaidia kujenga miradi mingi kwa gharama ndogo, lakini pia tutazame sasa kile kiwango cha miradi kama miradi inafika bilioni sita na kuendelea, tunaweza kuweka mkandarasi, lakini kama miradi ile ni ya kujenga madarasa, kuna wengine kwa kweli wamefanya, ukienda pale Mbeya Mjini wametengeneza hospitali nzuri kabisa kwa force account, ukifika pale unaridhika na maeneo mengine ambayo tumepita.

Kwa hiyo, nina uhakika kwamba tunaweza kuendelea na force account lakini pawe na usimamizi, Serikali ihakikishe ndani ya halmashauri tunakuwa na ma-engineer. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba Serikali imeongeza mishahara ni kitu kizuri, lakini mishahara hii iwatazame hata askari. Yapo malalamiko mengi na askari hawawezi kusema, hawawezi kuja hapa, kwa mfano Maaskari Magereza, wanalalamika hawajalipwa posho za chakula, posho za maji, umeme, pango, per diem nauli za likizo uhamisho na kadhalika. Kwa sababu ukiwatazama askari magereza kazi zao ziko kule kule ndani, sio watu wanaosafiri sana, kwa hiyo Serikali iwatazame hata kwenye mshahara yao, kwa sababu Serikali imeongeza mishahara iwaangalia kwamba ni watu ambao wanatunza watu wetu ambao, tuwaite wa kurekebisha tabia tusiwaite wafungwa, wanakwenda kurekebishwa tabia zao huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali iwaangalie, hawajalipwa hizi posho karibu kuanzia 2018/2019, 2019/2020, 2020/2021. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri awafikirie atakapopandisha mishahara, ahakikishe Askari Magereza kama siyo wote, lakini wafanye assessment waone ni wangapi ambao wamelipwa na ambao hawajalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimalizie kwa kusema kwamba bajeti hii itoe majibu kwa kutengeneza miundombinu imara na hasa barabara, madaraja, yasimamiwe vizuri na wawe na wataalam ambao wanafanya upembuzi yakinifu ili waweze kutengeneza barabara nzuri, nilikuwa nikiuliza maswali hapa na hasa Bukoba Vijijini katika Wilaya ya Bukoba.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Bukoba ni miaka mingi tangu tupate uhuru hatuna barabara ya lami. Sasa tunasema uchumi wa Mkoa wa Kagera umekufa kwa stahili hiyo wameuua wao wenyewe kwa sababu kama hawawezi kutujengea barabara, madaraja, vivuko ambavyo watu wanaweza kusafirisha mazao yao, tutawezaje kupata maendeleo. Pamoja na mambo mengine lakini hata miundombinu katika Mkoa wa Kagera na hasa Bukoba Vijijini kwa kweli wametuweka mahali pabaya na tumelalamika sana hapa, tunapewa majibu mengine kwa kweli ambayo siyo ya kuridhisha. Tunaamua Kwenda tu, basi bora liende, lakini tunaomba watufikirie zaidi katika kutujengea barabara Bukoba Vijijini, barabara ya lami, watufungulie Jimbo letu, watufungulie wilaya yetu, tunalima migomba, tunalima mbao sasa hivi tunalima miti sana, lakini hatuwezi kusafirisha kwa sababu hatuna hata daraja pale Kalele, nimesemasema sana hapo Waziri Kasekenya ananisikiliza, alikuwa akinijibujibu maneno. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.