Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ziwani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Vile vile kwa namna ya pekee namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa Watanzania na kutufanya sisi Watanzania leo kutembea kifua mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vitabu vyetu vya dini vinasema, mtu asiyemshukuru mtu, basi hamshukuru Mungu. Kwa sababu mtu anamwona, na kama hamshukuru, basi hawezi kumshukuru Mungu ambaye hamwoni. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Mama Samia kwa kila jambo jema analolifanya katika nchi hii. Mwenyezi Mungu atampa heri, atampa umri mrefu na atamjalia kila jambo jema katika maisha yake yote. Amina. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia kitabu cha bajeti cha Wizara ya Fedha ukurasa wa 75 mstari wa tano kutoka chini, Waziri wa Fedha anasema, namnukuu: “nitumie nafasi hii kuwahakikishia Watanzania kuwa tutaweka nyasi bandia kwenye viwanja vitano kwa kuanzia Mwanza, Arusha, Tanga, Dodoma na Mbeya kwa ajili ya kukuza michezo.” Huu ni mpango.
Mheshimiwa Spika, pia ukichukua kitabu cha bajeti cha Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, ambayo inaeleza dhamira, napenda kumnukuu Waziri na ningependa angekuwepo lakini hayupo, bahati mbaya sana; anasema yeye, katika kuhakikisha Tanzania inakidhi vigezo vya kuandaa mashindano ya Kimataifa na Kikanda, Serikali katika mwaka 2022/2023 imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya viwanja vya Dodoma, Sheikh Amri Abeid, Sokoine Mbeya na pia Uwanja wa Uhuru pamoja na Benjamin Mkapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa malengo na mpango haviendani, ni vitu viwili tofauti kabisa. Kwa sababu leo kwenye soko ukienda kununua artificial turfs (nyasi bandia), kwenye soko leo ukiangalia unakuta square foot moja ya hizo turfs ambazo ni supreme utaipata kwa Dola 3.39, na hizo ndiyo zenye kiwango cha juu kabisa. Kwa kiwango cha chini kabisa ambayo tunaita TFD utaipata kwa Dola 1.65. Maana yake nini? Maana yake, uwanja mzima wa mpira una-square feet 76,900, maana yake itakuwa ni sawa na Dola za Kimarekani 260,691, na hiyo nyingine itakuwa kama Dola 126,885. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ukizi-convert hizo zinakuwa kama Shilingi milioni 600 kwa supreme, na mpaka tufanye installation kwenye viwanja, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nasema na wewe! (Kicheko)
SPIKA: Mheshimiwa Ngwali!
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Sawa, sawa!
SPIKA: Mheshimiwa Ngwali!
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Ah, nazungumza Mheshimiwa. (Kicheko)
SPIKA: Unasikilizwa.
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Aah, sawa.
SPIKA: Unasikilizwa.
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Sawa, sawa.
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Wewe unazungumza na mimi humu Bungeni, huzungumzi na Waziri. Hata ukiwa unaongea nitazame mimi hapa, ndiyo kazi yangu kukusikiliza. (Makofi)
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Spika, haya sawa. (Kicheko/Makofi)
SPIKA: Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, kwa kiwanja kimoja kuwekwa hiyo artificial turfs ni kama Shilingi milioni 800 na kidogo hivi. Sasa ukivichukua viwanja vyote ambayo Serikali wameeleza kwamba wataweka hizo nyasi bandia, utakuta sasa, ukiweka hizo nyasi bandia (artificial turfs) katika hivyo viwanja, hivyo viwanja huwezi kutumia katika international level. Kwa hiyo, kama una lengo la kuandaa AFCON hivyo viwanja vitakuwa havifai kwa sababu Regulation za FIFA haziruhusu artificial turfs kufanyika mashindano ya international level. Kwa hiyo, lengo ni kuweka fedha katika hivyo viwanja na utakuwa huna kiwanja, maana yake viwanja vyote vya Jamhuri, Sokoine, CCM Kirumba, Mkwakwani, vyote hivyo ukiviweka nyasi bandia, maana yake umebakiwa na kiwanja kimoja cha Benjamin Mkapa. FIFA wanatumia natural. Kwa hiyo, hata kiwanja chako cha Sokoine kitakuwa hakiwezi kuchezewa katika international level. Kwa hiyo, malengo na mipango ni tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, juzi tu FIFA wamekataa viwanja artificial. Marekani Canada pamoja na Mexico wanaandaa hiyo World Cup ya mwaka 2026 na CAF wanafuata viwango vya FIFA vya viwanja. Viwanja vilivyokataliwa naomba nivitaje; MetLife Stadium ya New York pamoja na New Jersey imekataliwa kwa sababu ina-artificial. SoFi Stadium ya Los Angels imekataliwa kwa sababu ina-artificial. Tena wamewataka Marekani wabadilishe. Siyo wamevikataa kabisa, wabadilishe kupeleka katika natural. Levi’s Stadium ya San Francisco viwanja 11 vimekataliwa. Lumen Field ya NRG Stadium ya Huston imekataliwa. Lincoln Financial Field ya Philadelphia imekataliwa, yaani viwanja 11 vimekataliwa na FIFA kwa sababu FIFA wanatumia natural na CAF wanatumia viwango vya FIFA. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata uwanja wa Azam Complex, ule preliminary unaruhusiwa kucheza, lakini hauruhusiwi kucheza robo fainali. Ukifika kiwango cha robo fainali ule uwanja haufai kuchezea. Kwa hiyo, ukiweka nyasi bandia (artificial turfs) unazuia huo uwezekano wa Tanzania kuwa mwenyeji au ku-host mashindano ya AFCON. Ndiyo maana nasema mpango na dhamira ni vitu viwili tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeona wametaja viwanja vingi ambavyo watavifanyia ukarabati, siyo ukarabati huo wa kuweka nyasi bandia, nitatoa ushauri baadaye; lakini kwa nini Zanzibar, Amani Stadium na Gombani Pemba havipo? Tena napendekeza hivyo viwanja Mheshimiwa Waziri vikae katika mpango wako. Kwa sababu kile ni kituo na pia ni kituo rahisi, na vile viwanja ni vya Serikali, hatuna haja ya ku-negotiate na mtu yeyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Zanzibar ni viwanja vya Amani pamoja na Gombani Pemba kama kituo, basi viweke katika mpango wako Mheshimiwa Waziri, lakini siyo mpango wa kuweka nyasi bandia. Kwa sababu uwanja wa Amani hauwezi kutumika sasa hivi katika international level kwa sababu una nyasi bandia, tena grade four, kama shamba la bibi; na kama ambavyo kiwanja cha Gombani Pemba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba, kuna njia mbili tu, au kuna njia moja ya kufanya, kwamba, high brick system ndiyo inayotumika sasa hivi hasa kwa viwanja vya IPL. Maana yake na FIFA wanavitambua kama ni natural turf. Unachukua grass master ndiyo walioweka turfs zile katika uwanja wa Stamford Bridge na Emirate pamoja na viwanja vingi vya Uingereza. Pia Swiss grass wao ndio walioweka turf katika uwanja wa Man City ambapo wao ndio walioshinda Kombe la Dunia last time kuweka viwanja vya Urusi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia Atlas Turf International, wao ndio wameshinda Qatar kuweka turfs ambapo aina zao za nyasi wanaziita Platinum TE Paspalum. Hizo ndiyo nyasi ambazo wanatumia. Kwa hiyo, tutumie makampuni makubwa ya nje yaje yaweke nyasi katika viwanja vyetu hivi. Siyo nyasi bandia watutengenezee hivi viwanja, tutangaze tenda international, kwa sababu hakuna watu wa ndani ambao wanaweza ku-deal na huo utengenezaji wa viwanja ili tukidhi hicho kiwango cha FIFA na CAF wanachokitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja mia kwa mia. Ahsante sana. (Makofi)