Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Bakar Hamad Bakar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ninakushukuru siyo tu kwa sababu ya kunipa nafasi hii, lakini pia kwa namna bora ambavyo unaongoza Bunge hili kwa hekima na busara nyingi sana. Kwa hiyo, nikupongeze sana na nikushukuru sana kwa namna bora ambavyo unaongoza Bunge letu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninampongeza na ninamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyoendelea kutupigania Watanzania na maendeleo ambayo anaendelea kutuhangaikia na tunavyopiga hatua hizi za kimaendeleo. Bajeti hii ambayo iko mbele yetu ni bajeti ambayo inaenda kutatua changamoto za Watanzania, inaenda kumgusa kila Mtanzania. Bajeti hii imewagusa wamachinga, bajeti hii imewagusa wakulima, bajeti hii imewagusa watumishi wa umma, lakini bajeti hii imeyagusa makundi yote, vijana, walemavu, wanawake, hata wanamichezo bajeti hii haiwaacha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunasema kwamba, bajeti hii imekuja katika right time, lakini pia ni bajeti ambayo inaenda kutatua changamoto za Watanzania. Nikupongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha, wewe na timu yako, kwa namna ambavyo umewasilisha na umeandaa bajeti hii nzuri sana kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja ya industry ambayo inakua kwa kasi ya kiuchumi sasa hivi duniani ni Islamic Financing System. Islamic Financing System sasa hivi inakadiriwa taasisi karibia 400 duniani tayari zinafuata mfumo wa Islamic Financing duniani, lakini pia inakadiriwa ukuaji wa system hii kwa mwaka ni karibia asilimia 20 kwa mwaka, lakini na nchi nyingi ambazo sasa hivi zinatumia siyo tu zile nchi za kiislamu, lakini hata nchi ambazo siyo za Kiislamu zinatumia mfumo huu. Ukienda South Africa wanatumia Islamic Financing System, ukienda UK, ukienda Nigeria na nchi za Afrika nyingi hata Kenya wanatumia mfumo huu, lakini kwetu sisi Tanzania bado hatujaweza kuu-recognize mfumo huu uweze kutumika katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, bado tunahitaji kufanya mabadiliko kwenye sheria zetu. Kwa mfano, Banking Act, hii inatakiwa pia ifanyiwe marekebisho ili kuutambua mfumo wa Islamic Financing ili uweze kutumika Tanzania kwa sheria, pia tufanye marekebisho kwenye Insurance Act ili pia iweze kutambua takaful kama ni Islamic Insurance ambayo inakwenda kutatua matatizo mbalimbali yanayohusiana na insurance za kiislamu, pia tunahitaji tufanye mabadiliko kwenye capital market and security ili kuweza kutambua Islamic bond ambayo inaitwa sukuk ambayo itawawezesha wawekezaji wengi ambao hawatumii mifumo iliyoko sasa, wanatumia mifumo ya Kiislamu kuja Tanzania kupiga hodi na kuweza kuwekeza kwa bond hizo ambazo na zikonchi nyingi ambazo zinatumia Islamic Bond kuweza kutekeleaa miradi yao mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda Nigeria wanatumia mfumo huo, ukienda UK pia wanatumia mifumo hii ya Islamic Bond ambayo ni Sukuk, lakini Tanzania bado hatujaweza kuitambua mifumo hii kisheria. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri tuende tukapige hatua.

Mheshimiwa Spika, siyo kwamba tunakwenda kulitekeleza jambo hili from nowhere, kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ukienda Ibara 159 (f) imezungumzia juu ya mifumo ya Islamic Finance na CCM imeahidi kwamba, ifikapo 2025 jambo hili tayari litakuwa limeshafanyiwa kazi. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, nakupongeza sana kwa sababu umeshapiga hatua kwenye bajeti yako hii umeweka, umefanya amendment kwenye TRA Act ile ya mwaka 2008 tayari kuna kipengele umekiweka pale, lakini kile kipengele bado hakijatosha. Financing System ina faida kubwa sana kwa Tanzania, lakini pia ina faida kubwa sana kwa uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna hofu sana kwenye jambo hili na Watanzania wengine wanahofu kwamba, aah, kwa nini Islamic System? Islamic System hizi benki ni huduma kama huduma nyingine. Ukienda kwa Tanzania tunazo system za kidini ambazo zinafanya kazi bila ya ubaguzi na zinatumika kwa watu wote. Ukija tuna shule mbalimbali za kikristo, tuna shule pia za kiislamu, lakini tunasoma kwa pamoja bila ya kubaguana. Pia, tuna hospitali na vituo vya afya mbalimbali ambavyo ni vya kidini, tunaenda kutibiwa kwa pamoja bila kubaguana kidini. Hii pia ni huduma kama huduma zingine na watatumia watu wote au yule ambaye anahitaji na ambaye hahitaji halazimiki kutumia huduma hii. Ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu 2025 tutaenda kuhojiwa na Watanzania kwamba, kwa nini hatukutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwenye jambo hili. Nikuombe sana tuende tukalitekeleze jambo hili kama ambavyo limeahidiwa na Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa nini sasahivi mifumo hii inakwenda kwa kasi sana? Ni kwa sababu ya faida zinazopatikana kwenye products ambazo zinazalishwa kwenye Islamic Banking. Kwa mfano, miongoni mwa products ambazo zinazalishwa kwenye Islamic Banking ni product ambayo inaitwa Mudharaba. Mudharaba ni product ambayo benki wanampa mtaji mteja anaenda kufanya biashara, lakini kwa kugawana faida. Product kama hii ipo kwenye conventional bank kwa maana wao wanapewa mkopo, wakishapewa mkopo wanachokijua wao ni riba na marejesho ya mkopo ule. Hawashughuliki na biashara yako wanavyofanya, vyovyote itakavyokuwa, umepata hasara, umepata faida ni wewe mwenyewe, lakini mudharaba ambayo ni product ya Islamic hii benki na wewe, benki na mteja wanashughulika pamoja kwenye biashara yako na mwisho mnagawana faida.

Mheshimiwa Spika, endapo imetokea hasara kwenye biashara yako hiyo, haulazimiki kulipa isipokuwa kwamba, isiwe negligence ya kwako wewe kama mteja, lakini kama imekwenda vizuri biashara kwa misingi ambayo mmekubaliana na benki na haikutengeneza faida, hulazimiki kulipa. Leo ukiangalia mifumo yetu ya conventional kama hukwenda kulipa ama watakuja kukufilisi au watakupiga mnada yale ambayo umeweka kama dhamana ya mkopo wako, lakini kwenye Islamic Banking haipo hivyo, kama umepata hasara, ukipata faida mnagawana na benki na hiyo ni moja katika product. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini zipo products nyingi. Kuna mudharaba, kuna musharafa, lakini pia kuna murahaba, ziko nyingi sana. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri jambo hili tulifanyie kazi na tulifanyie kazi kwa wakati na kwa haraka sana.

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwenye suala la ushirikiano au ushirikishwaji wa taasisi zetu za Serikali zote mbili; ziko taasisi za Zanzibar ambazo sasahivi zinafanya kazi zake huku Tanzania Bara. Kwa mfano tunayo taasisi ya ZIC, Zanzibar Insurance Company, lakini pia tunayo PVZ ambayo pia inafanya kazi huku tunakuomba sana Serikali kwa pamoja tuendelee kushirikiana na taasisi hizi, bado mashirikiano ya taasisi hizi kwa taasisi ambazo ziko Bara ni madogo sana. Kwa hiyo, nikuombe sana na niiombe sana Serikali tuongeze ushirikiano kwenye taasisi zetu hizi za Zanzibar kwa sababu zote hizi ni taasisi za Serikali na zinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 kwa hiyo, hatuna haja ya kuziwekea hofu au kuzijengea hofu. Tuzitumie taasisi hizi kama ni taasisi zetu za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie jambo moja, kuna suala la Foreign Currency Exchange Market. Ni jambo ambalo limefungiwa sasa kwa muda mrefu na sasa hivi huduma hii inahitajika sana. Mama Samia amekwenda mbio sana amefanya Royal Tour kutangaza utalii, watalii watakuja na wameanza kuja, kwa hiyo, tunaziomba hizi taasisi za foreign exchange kwa maana ya Bureau De Change zirudi na zirudi katika masharti ambayo siyo yale kandamizi kama ambavyo yako sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano eneo maalum la Zanzibar, kumuwekea mzanzibari mtaji wa Bilioni Moja ndiyo aanzishe taasisi hii ya Bureau De Change kwa kweli, si jambo rahisi kwa wazanzibari kwa mujibu wa uchumi ambao tukonao bilioni moja ni hela nyingi sana hatuwezi tukapata hata kampuni moja ambayo itaweza kufungua, itakidhi sharti hili la kuweza kufungua hii Bureau De Change kwa Zanzibar. Kwa hiyo, nikuombe sana masharti haya yalegezwe, hasa kwa upande wa Zanzibar, kwa kweli Bilioni Moja ni nyingi sana kuweza kufungua Bureau De Change kwa upande hasa wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii, ninaunga mkono hoja hii, ahsante sana. (Makofi)