Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisesa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa. Awali ya yote, nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha ya wazazi wangu. Vile vile nachukua nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge, ndugu jamaa na marafiki, viongozi wa madhehebu ya dini, Baba Askofu Peter Kisenha na Mtume Boniface Mwamposa, kwa maombi na Faraja; pia viongozi wengine wote wa dini kwa namna katika kipindi chote hiki cha msiba ambavyo walinitia moyo na kunifariji. Wazazi wangu; Mama Ceflen Kabula Masaga na baba, Mzee Mpina, Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani. Amina. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimepitia hotuba ya Waziri hapa, nimesoma vitabu vyote viwili vya hali ya uchumi na bajeti yake. Kuna mambo mazuri ambayo ni ya kupongezwa na hii Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inaongozwa na mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Kuna mambo mengi ambayo yamefanyiwa maamuzi lakini mambo mazuri ya kupongezwa ni ule uwezo wa kusimamia fedha yetu ya Kitanzania, kuimarika kwa wastani wa 0.03 kuimarisha kwa uimarikaji chanya, ni jambo zuri sana la kupongezwa kwa Serikali yetu. Pia kuna mipango mizuri pale ambapo tumeweza hata kulipia advance ya ndege tano ikiwemo ndogo ya mizigo, ombi ambalo tuliliomba kwa muda mrefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni jambo zuri na la kupongezwa sana katika maamuzi ya Serikali yetu. Pia pongezi kwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba. Hapa ameweka bayana, kuna mambo ambayo hayatajwi na watu wengine, yeye ameamua kuyasema. Katika ripoti yake ameweka wazi juu ya udhaifu wa baadhi ya watendaji wa Serikali ambavyo wanatumia vibaya na kufuja mali za umma. Ametueleza hata namna baadhi ya watendaji wanavyoitumia Sheria ya Manunuzi kupora fedha za umma; ameweka wazi hilo. Pia ameeleza hata baadhi ya mashirika ya umma kugeuzwa kuwa mali ya watu binafsi. Ni maneno ambayo sio Mawaziri wengi wanaoweza kuyataja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wapo Mawaziri wenzake ambao baadhi ya Wabunge walipojaribu kueleza baadhi ya changamoto za Serikali waliambiwa hawaipendi Serikali ya Awamu ya Tano, waliambiwa ni wapotoshaji. Sasa hali hii ya Waziri wa Fedha kusema huu udhaifu ambao ni lazima tuuseme ili tuurekebishe tuweze kupata namna ya kuendelea ni uzalendo na kielelezo cha hali ya juu sana. Hongera sana Waziri wa Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa tunayo mambo tuliyoyazungumza hapa, nami nataka nianzie na suala la mapato. Suala la mapato hapa, Waziri wa Fedha wewe unajua, watu wamepiga sarakasi hapa, watu wamelia hapa kwenye Bunge, watu wamepiga magoti hapa kwenye Bunge lako Tukufu; hii yote ilikuwa ni hali ngumu ya mahitaji ya fedha kwa wananchi wake. Tuna bajeti ndogo sana ambayo haiwezi kukidhi mahitaji ya wananchi wetu. Sasa tunatokaje hapo? Nimesoma hotuba ya Waziri wa Fedha juu ya namna ya kukusanya mapato inavyostahili.
Mheshimiwa Spika, sisi sasa hivi tuna average ya kukusanya mapato ya Serikali asilimia 11.4 ya pato la Taifa. Wwenzetu wa Rwanda na Kenya wanakusanya hadi asilimia 16 ya pato ya Taifa. Nini kinachotukwaza kufikia hapo?
Mheshimiwa Spika, yapo mambo mengi hapa. Kwa mfano, suala la malimbikizo ya madeni. Ni jambo la ajabu na la kusikitisha, tumefikia hatua malimbikizo ya madeni, zile arrears kufikia Shilingi trilioni 7.54 kwa mwaka wa fedha. Unawezaje kuwa na arrears za Shilingi trilioni 7.54 halafu ukaweza kukusanya mapato ya kutosha ku-support bajeti yako?
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tuna kesi zilizoshikiliwa na mamlaka ya rufani trilioni 5.19, nazo hizi ni kesi ambazo zinatakiwa kuamuliwa tu, lakini haziamuliwi, matokeo yake mapato haya ya Serikali hayawezi kukusanywa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulisema mwaka jana na sasa tunaendelea kusema kwamba tuna makampuni ya 504 (multinational companies) ambazo assessment yake ya kodi ni lazima uwe na wataalam ambao wanaweza ku-assess properly ili uweze kukusanya kodi properly. Uwezo wetu sasa hivi ni asilimia 1.2 wa kuya-asses haya makampuni. Maana yake ni kwamba hayawezi kulipa kodi properly. Sasa ni lini utakusanya mapato ya kuwatosheleza wananchi wako?
Mheshimiwa Spika, sasa hivi kama una mapato ambayo hayajakusanywa kwa maana ya arrears, kwa maana ya kushikiliwa na mamlaka za rufani, ni Shilingi trilioni 12.6 hazijakusanywa. Fedha hii zingeweza kutusaidia kupiga hatua kubwa sana, lakini hayo yote hayajafanyika. Sasa Waziri wa Fedha ni vizuri akajipanga vizuri zaidi katika kushughulikia hili suala.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie kidogo kuhusu marekebisho ya sheria na ni zungumzie eneo la Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ambapo 5% zinapendekezwa kwenda kujenga miundombinu ya masoko ya wamachinga. Hapa suala langu ni moja. Hizi fedha zilikuwa zinakopwa kwa ajili ya mitaji. Asilimia 10 yote hii ilikuwa inakwenda kwenye mitaji; na hawa wamachinga walikuwa wanakopa kwenye hizo asilimia 10, unaenda kuzipunguza fedha za mtaji kuzipeleka kujenga miundombinu, halafu miundombinu unayokwenda kujenga unasema tu asilimia tano. Unajua Meatu kuna machinga wangapi? Unajua wanahitaji soko lenye ukubwa gani? Unajua nature ya biashara wanazozifanya? Unaidhinisha tu asilimia tano ziende huko, nadhani hii siyo sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mtaji tungeuacha, asilimia 10 ziende kwenye mtaji. Kama tunahitaji kujenga miundombinu ya Wamachinga na masoko tutafute vyanzo vingine vya fedha tukajenge na tufanye tathmini ya uhakika tunaenda kujenga eneo lenye ukubwa wa aina gani? Pia tuzifahamu biashara. Muuza soksi huyu anayetaka kutembea kuwapelekea wateja wake unamjengea jengo! Ni lazima pia tujue watu tunaowajengea nature yao tujue tunawajengea miundombinu ya aina gani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni deni la Taifa. Deni la Taifa hapa limeelezwa katika hotuba ya Waziri wa Fedha, limeongezeka kwa Shilingi trilioni 8.72, unajiuliza maswali, deni la Serikali linaongezekaje? Limeongezeka kwa Shilingi trilioni 8.72. Kama deni la Serikali limeongezeka kwa Shilingi trilioni 8.72 katika mwaka mmoja wa fedha, wakati katika mwaka husika deni hilo tulili-service kwa zaidi ya Shilingi trilioni 7.2? Kama ndiyo hivyo, maana yake tumekopa kuliko tulivyoahidi hapa Bungeni. Maana yake tumekopa mkopo mkubwa wa zaidi ya kile tulichoji-commit hapa Bungeni. Kama tulifanya hivyo, ni kwa ridhaa ya nani? Kwa ajili ya kazi gani?
Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakapokuja hapa atueleze vizuri katika hili suala la Deni la Serikali ili kuondoa mkanganyiko uliopo. Kwa sababu ukifanya hesabu za kawaida, tumekopa zaidi ya Shilingi trilioni 15, wakati huku tunaelezwa kwamba tumekopa kama Shilingi trilioni 9.3. Sasa huu mkanganyiko wa takwimu unatokana na nini? Ni lazima Waziri wa Fedha aeleze vizuri juu ya jambo hili ili kuujua usahihi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni ranchi ya Kongwa kugeuzwa kuwa shamba la alizeti. Hili shamba lilianzishwa kwa ajili ya ranchi za mifugo, kuendeleza kosafu bora ya mifugo, kuendeleza mifugo, na kama shamba darasa la mifugo. Leo tunaenda kulibadilisha eti kuwa shamba la alizeti kwa sababu mifugo humo ni michache. Anayesema hayo ni Waziri wa Fedha. Kama mifugo ni michache, si upeleke fedha ukaongeze tu mifugo mle? Kuna tatizo gani? Kama mifugo ni michache katika ranchi ya Kongwa, kwa nini usiongeze mifugo humo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna miundombinu ya maji mle, tuna miundombinu ya majosho, tuna miundombinu ya malisho, tunaenda kuibomoa tugeuze kuwa shamba! Kwani hakuna mashamba mengine yaliyo wazi alizeti ikaenda kulimwa katika nchi hii? Mbona tunaelezwa mapori kwa mapori! Hii yote ni kutokuona umuhimu wa mifugo nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huku tunasema tunaongeza fedha kwenye mifugo, huku unaenda kunyang’anya mashamba ya wafugaji kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha alizeti. Mbona hamjaenda Tabora; mashamba ya mifugo yapo mengi ambayo hayajalimwa, ni mapori, kwa nini msiende mkafyeke mapori huko mpande alizeti? Kwa nini mkapande alizeti kwenye shamba la mifugo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika na Wabunge kataeni mpango huu na msikubali mambo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni hili la sheria. Waziri wa Fedha anapendekeza kupewa mamlaka ya kutoa vivutio vya ziada vinavyotokana na vikao vya NISK, anaweza kusamehe VAT, anaweza kusamehe kodi ya mapato kwa ajili ya wawekezaji mahiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tujue tuna ushindani sawa katika biashara (fair competition). Kuna watu walioweka viwanda hapa. Leo unasema tu, huyu ni mahiri anakuja, tunamsamehe; hawa waliowekeza mapema unawapeleka wapi? Tuna hiyo fair competition ambayo ni global issue ambayo ni lazima ui-tackle globally! Unakuja huyu una m-exempt kwa makundi ya watu. Tunapotaka ku-exempt ni lazima tuwe na ile exemption ya pamoja. Kwamba hili kundi lote tumelisamehe, lakini hizi exemption za mtu mmoja mmoja hazitufikishi mahali popote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nami naomba sana, Waziri wa Fedha sio leo atakuwa Waziri wa Fedha wa kudumu, watakuja Mawaziri wa Fedha wengine; tusikubali na Waziri wa Fedha asikubali kuingizwa kwenye mitego ya kutoa exemption ya group la watu. Asikubali! Nasi Wabunge tusikubali kuruhusu sheria ya namna hiyo ikaingia hapa Bungeni ya kumruhusu Waziri wa Fedha hapa eti hawa ni mahiri tunawasamehe, wakati tuna wawekezaji wengine wana viwanda hapa nchini, wasiposhindana kwa haki si watafunga viwanda kwa ajili ya huyo uliyem-favour wewe! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukatae sheria hizo na tuzikatae hapa Bungeni, Kwa kweli Finance Bill itakapokuja, tuta-move amendment kuhakikisha kwamba sheria za namna hii hazipati nafasi kwenda kuharibu uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa kabisa, sikuwepo, lakini nimefuatilia sana katika Hansard mjadala wa Bunge baada ya kumaliza msiba. Naomba tu kusema kwa kifupi kwamba, kuna maeneo muhimu sana ambayo ni lazima tu twende kwenye kuunda Tume ya Bunge. Nami nakuomba ukubali uweke hii rekodi, utashukuru. Utakapounda Tume ya Bunge, utakayoenda kuyaona na mchango utakaoleta kwenye Taifa, utanishukuru kama mmoja wa Wabunge wako waliokushauri hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, moja ya jambo ambalo naomba liundiwe tume ni ucheleweshaji wa ukamilishaji wa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. La pili ninaloomba liundiwe tume ni kupanda kwa bei za mafuta kwa kisingizio cha vita ya Ukraine na Russia; na tuweze kujua yale makandokando mengine yaliyomo humo ndani ambapo mchezo uliofanywa wa bei za mafuta kupanda nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ninalotaka liundiwe tume ni bei za mbolea nchini na biashara inavyofanywa. Tulikuwa tunafanya vizuri sana zamani, tulikuwa na mpango wa kufanya requalification, tulikuwa tuna-visit hata viwanda vinavyozalisha mbolea. Tulikuwa tunatumia mfumo wetu ule wa bulk procurement system tukawezesha mbolea kuagizwa kwa bei ndogo na kusambazwa kwa bei ndogo. Mfumo huo umeuawa. Sasa leo hii tukajue kwamba hizi bei za mbolea tunazopewa hapa nchini, kweli zina uhalisia? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili suala la mbolea nataka liundiwe tume kwa sababu moja, hata Waziri wa Kilimo mwenyewe alivyoingia hapa Bungeni, mchana akatoka na takwimu nyingine, kwenye kuhitimisha akatoka na takwimu nyingine. Kwa hiyo, tutakuja tuone ukweli na uhalisia wa mbolea wanazouziwa wananchi imekaa vipi hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nataka tukaangalie suala la malimbikizo haya ya kodi, hivi ni kweli taasisi zetu za kodi wanafikia mpaka malimbikizo ya Shilingi trilioni 7.54 za kodi, mnashindwa kukusanya, halafu uwezo wa kukusanya hizo kodi ukawa asilimia 10 tu, halafu tunakaa kimya katika hilo! Hili jambo ni kuhusu malimbikizo ya kodi na mapingamizi yaliyopo kwenye Mahakama ni muhimu sana yaundiwe tume sasa, kwa sababu Serikali kila tukiiambia haitekelezi hilo.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)