Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie katika hotuba ya Serikali. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kunijaalia uhai kuweza kusimama hapa leo.

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa bajeti nzuri ambayo hakika inaenda kutibu kiu ya Watanzania. Pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, wamekuwa wasikivu kweli kweli, nasi ambao tumepata nafasi ya kuwasikiliza kwenye Kamati ya Bajeti, hakika wamekuwa waki-accommodate mawazo ambayo yanatolewa na Wajumbe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kipekee kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameitendea haki sekta ya utalii. Utakubaliana kwamba Royal Tour duniani zimefanyika katika maeneo machache na Tanzania ikiwa mojawapo. Inahitaji ujasiri kwa Mheshimiwa Rais kushiriki. Kimataifa nchi ambazo zimeweza kufanyiwa na huyu Bwana Peter Greeberg ni pamoja na Israel, New Zealand, na kwa Afrika ni Rwanda na Tanzania. Kwa hiyo, hizi kelele ambazo unazisikia nyingine zinaanzia ndani na nyingine zinatoka nje ni kwa sababu ya mafanikio ambayo tunaenda kuyapata kutokana na utangazaji ambao umefanyika. Tuna kila sababu ya kumuunga mkono Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni wajibu sasa kwa Wizara; Mheshimiwa Rais ameonesha njia, tunayo maeneo mengi sana ya vivutio ndani ya nchi yetu, tuna vivutio vilivyozoeleka na sasa ni high time twende na maeneo mengine, twende Mbeya, Songwe, na Rukwa, vipo vivutio vingi, ili watalii kama ambavyo wamekuwa wakienda nchi kama Israeli, waweze kuja Tanzania. Itakuwa siyo rahisi kumwomba tena Mheshimiwa Rais ashiriki Royal Tour nyingine; ameonesha njia, ni kazi ya Wizara husika kuhakikisha kwamba kazi nzuri ambayo imeanzishwa na Mheshimiwa Rais inaenda kuleta mafanikio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema bajeti hii ni ya kimapinduzi, maana imepeleka fedha kwenye kilimo, kutoka shilingi bilioni 294 mpaka shilingi bilioni 954. Tumekuwa tukisema Bunge la Kumi na Mbili linatakiwa liache legacy yake ya kuhakikisha kwamba transformation inafanyika kwenye kilimo ambapo kwenye kilimo huku ndiko tunaajiri Watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Spika, zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wanashiriki kwenye shughuli za kilimo, lakini kilimo kimekuwa kama vile mtu ambaye anakosa kazi ya maana ndiyo anaambiwa aende kwenye kilimo, lakini kwa uwekezaji wa fedha hizi na ambavyo tumeambiwa na Serikali kwamba bajeti itaendelea kukua hadi kufikia asilimia 10, hakika kilimo kitakuwa kivutio na Watanzania wengi wataona namna pekee ya kuwa na uhakika wa kiuchumi ni kujiingiza kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali, ni wakati muafaka wa kuhakikisha kwamba benki ya Kilimo inafufuliwa, inawezeshwa kimtaji ili Mtanzania ambaye anaenda kukopa kwa ajili ya kilimo waongee lugha ya kuelewana. Tukiongea digit moja katika interest iwe ni jambo linaeleweka kiurahisi, ukitaka kilimo kikakopewe kwenye Commercial Bank, hakika hatuwezi kufika.

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kushirikiana na Waziri wa Kilimo, ni muda muafaka kama siyo bajeti hii, katika bajeti zinazokuja tuhakikishe kwamba benki ya kilimo inawezeshwa kimtaji na pia kuwa na manpower na structure ya kutosha ambayo itahakikisha kwamba siyo lazima mwananchi atoke Kalambo aje hadi Dar es Salaam au Mbeya ndiyo aweze kusikilizwa kwa ajili ya masuala ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, naiomba Serikali yangu, tuna wajibu wa kufufua benki ya kilimo, lakini benki yetu ya TIB, hapa katikati imeunganishwa na Benki ya Posta, ni vizuri kama Serikali tukawa na benki yetu ambayo tuna uhakika kama ambavyo benki nyingine katika nchi kama za China, kuna benki ya Serikali ambayo muda wote Serikali inaweza ikaiwezesha na wakati mwingine inakwenda yenyewe kukopa. Ni wakati muafaka kuhakikisha kwamba Benki ya TIB pamoja na Benki ya Posta, kwa jina lolote lile ambalo mtakuja nalo, kuhakikishe kwamba inawezeshwa kimtaji na kimuundo ili Watanzania au Wakandarasi wadogo wadogo wawe na uhakika kwamba wanaenda kukopa na kufanya miradi kwa ajili ya Taifa leo.

Mheshimiwa Spika, naomba pia niongelee suala la TRA. Naomba niipongeze TRA, imekuwa ikifanya vizuri mwaka hadi mwaka, wamekuwa wakiongeza makusanyo katika mapato yao; lakini itoshe, ifike wakati kwamba ni vizuri kama Taifa tuhakikishe kwamba tunawekeza kwenye mifumo.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kuwapongea vijana wa Kitanzania ambao wamekuwa wakiibua mifumo mizuri ya Kimataifa. Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba vijana hao wa Kitanzania ambao wanaibua mifumo na inakubalika Kimataifa, wanalindwa na wanakuwa motivated, kwa sababu anayefanya vizuri, hakuna dhambi ya kuhakikisha kwamba unampa incentive. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haipendezi wanafanya kazi nzuri lakini huoni namna ambavyo Serikali inawapa motisha ili waendelee kuwa Serikalini na badala yake baada ya muda mfupi, wanaondoka kwenda kwenye private sekta, kwa hiyo, inakuwa kila wakati Serikali inakuwa na kazi ya ku-train wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe TRA, top management system ambayo imekuwa ikifanyika katika kukusanya kodi imeonesha ufanisi mkubwa, hasa maeneo ya Majiji, bahati nzuri mmepata watumishi kama 2,000, hakikisheni kwanza mnaanza kuwatumia hao katika maeneo ambayo ni oevu kwa maana ya uhakika wa fedha kwenda huko tuhakikishe kwamba tunapata mapato mengi kabla ya kuanza kuwatawanya. Ikiwezekana hebu tuanze na hili eneo ambalo linaonekana kwamba halijafanya vizuri, katika property tax, kwa kushirikiana na TAMISEMI huku kuna fedha za kutosha. Tuondokane na ule utaratibu wa flat rate, kwamba mwenye ghorofa na nyumba ya kawaida eti wanachangia kiasi sawa, hii siyo sawa hata kidogo. Ni kukiuka sheria za kodi, kodi inataka uwe progressive na yule ambaye ana kingi achangie kingi, aliyekuwa na kidogo achangie kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo naomba niongolee, nilikuwa naongea na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, nalirudia kwa mara nyingine. Namna pekee ya sisi kama Taifa la Tanzania kuweza ku-access Congo DRC, ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na njia iliyokuwa fupi kuliko njia zote. Na ikiwezekana twende Congo tukitoka Tanzania bila kulazimika kupita nchi nyingine na route nilishawapa.

Mheshimiwa Spika, upo uwekezaji ambao umefanywa na Serikali unakwenda mpaka Kasanga Port na pale kuna maboresho makubwa sana ya Bandari. Ukivuka straight bila kugusa nchi nyingine yoyote unakwenda eneo la Mlilo ambalo tayari utafiti ulishafanyika, panafaa kuwa na bandari.

Mheshimiwa Spika, siyo lazima kwamba Serikali ndiyo iende kuwekeza, ni private sector kwa sababu malori yakipita nchi nyingine yanaacha Dola 700 kwa kila lori moja. Kwa hiyo, hata kama tukawa na straight njia na wakawa wanalipishwa hata Dola 400 wataona ni nafuu kwa sababu kwanza wamepunguza umbali, lakini wakati huohuo tuna-access Congo ya Lubumbashi ambayo ndiyo iliyokuwa na madini.

Mheshimiwa Spika, narudia kwa mara nyingine, Mheshimiwa Waziri, ulisema ni-share na wewe documents, nita-share na wewe ili muone kama Serikali, kwa kushirikiana na Serikali ya Congo tunakwendaje Congo ya Katanga kwa maana ya Katanga Province na kule kwingine ili kama tunajenga reli kwenda upande wa chini kule sawa, lakini Congo ya Lubumbashi namna pekee ya kufikia huko ni kwa kupitia Katanga na jiografia haiongopi. Kwa hiyo ni vizuri tusije tukashindwa kwenda na jiografia inavyotutaka.

Mheshimiwa Spika, kuna suala lingine ambalo limeibuka kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri na ikaleta kelele kweli. Inaonekana kwamba sasa hivi kodi eti mtu kuanzia umri wa miaka 18 inabidi apate TIN Number kwa sababu inabidi aanze kuchangia kodi, jambo ambalo siyo sahihi.

Mheshimiwa Spika, hakuna kodi yoyote duniani ambayo ilishawahi kutozwa kwa ku-base kwenye umri wa mtu. Kinachotozwa ni fedha. Kwa hiyo ni vizuri Serikali mkafafanua vizuri, kwamba hata angekuwa mtoto mdogo amerithi kampuni ambayo ina wealth, anatozwa kodi. Kwa hiyo kinachotozwa kodi siyo umri wa mtu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kumekuwa na misconception kwamba umri wa miaka 18 watu wawe na TIN ni kwa sababu ya takwa la kisheria tulilonalo sasa hivi kwamba kitambulisho cha NIDA anapewa mtu mwenye umri kuanzia miaka 18. Kwa hiyo, upotoshaji ambao umekuwepo kwamba eti sasa Watanzania whether ana kazi, ana kipato au hana kipato akishafika umri wa miaka 18 anaanza kutozwa kodi siyo sahihi. Kinachotakiwa ni kwamba anayetozwa ni yule ambaye ana kipato, kinachotozwa ni kipato na siyo umri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, naomba niunge mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)