Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na wewe nikushukuru sana kwa kunipa fursa ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu leo kwa ajili ya kuweka mchango wangu kwenye Bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, leo nimepanga kuzungumzia mambo matatu. Jambo la kwanza ni kuhusiana na hili ambalo limewasilishwa kupitia bajeti hii kwa maana ya kupunguza gharama za uendeshai Serikalini. Kupitia fursa hii naomba nimpongeze sana Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa maono, namna ambavyo bajeti hii imeletwa na kukidhi mahitaji ya maeneo mengi, hasa kwa watu wale wenye kipato kidogo kwa maana ya wenzetu kule chini.

Mheshimiwa Spika, ukizungumzia kupunguza gharama za uendeshaji maana yake unataka kuleta tija katika wale ambao wanategemea huduma za kijamii zinazotolewa na Serikali huko kwenye ngazi za chini. Nimeona katika bajeti hii, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amekuja na mkakati wa kupunguza matumizi Serikalini kwenye magari, kwa watumishi, vilevile jambo kubwa ambalo nimeliona ni lile la kupunguza vikao na kuhamia kwenye TEHAMA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhamia kwenye TEHAMA kwa ulimwengu tulio nao sasa ni kama vile tumechelewa, ni jambo ambalo ningeshauri liende kwa spidi kubwa sana. Nitakupa mfano, wakati wa maandalizi ya bajeti zetu za halmashauri, halmashauri zetu almost zote huwa zinahamia Dodoma.

Mheshimiwa Spika, wanakaa kwa zaidi ya wiki tatu, wiki tano na wengine miezi miwili, hapa Dodoma kwa ajili ya maandalizi ya bajeti, jambo ambalo lingeweza kufanyika huko kwenye Halmashauri zao taarifa zikaletwa kwenye Kamati za Bunge, michakato ikaenda kimtandao kutumia TEHAMA na mwisho wa siku tukatengeneza tija kubwa sana na tukabana matumizi, fedha hizi tukapeleka kwenye maeneo mengine ambayo yana uhitaji. Kwa hiyo, ninaipongeze sana Serikali na Wizara ya Fedha kwa kuona namna gani tunaweza tukabana matumizi kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Spika, kipindi kifupi kilichopita tuliona Katibu Mkuu Hazina alitoa tangazo la kuongeza hizi posho za viongozi. Hizi ukiziongeza na bado ukaendelea ku-entertain vikao vingi, tunapeleka mzigo mkubwa sana kwa Mtanzania. Ili kuweza kupunguza huu mzigo, pamoja na kwamba hizi posho zimeongezwa, ni vizuri sana Mheshimiwa Waziri akaona namna nzuri ya kutekeleza hili jambo kwa haraka kuleta tija na nafuu ya maisha ili kuendeleza kupeleka fedha kwenye miradi ya maendeleo na kuboresha maisha ya Watanzania zaidi.

Mheshimiwa Spika, eneo hili naona changamoto moja tu, kwamba tumezoea kutumia mtandao wetu kwenye mawasiliano ya Serikali, hata kwenye mifumo ya fedha tunatumia TTCL, lakini TTCL haifanyi vizuri sana, maeneo mengine hayana mtandao kabisa, maeneo mengine mtandao ni hafifu, jambo ambalo litatusababishia sasa kusuasua tunapokwenda kutekeleza vikao kwa kutumia TEHAMA.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ili tuende kwa ufanisi, jambo la kwanza ningeishauri Serikali kuangalia namna bora ya kuboresha mfumo wa mawasiliano kupitia TTCL. Wakiboresha mtandao wa TTCL ukawa unapatikana, bado itakuwa tena ni fursa, badala ya fedha kutumika kwenye mitandao mingine ya kibiashara, hiyohiyo fedha ambayo tunakwenda kufanyia TEHAMA itarudi tena kwenye Mfuko wa Serikali kupitia TTCL. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ninapenda kulizungumza siku ya leo ni namna ya kuongeza mapato. Wakati inawasilishwa Bajeti ya Afya nilisimama katika Bunge lako na nikaiomba sana Serikali kuangalia namna ya kuboresha huduma ya mama na mtoto.

Mheshimiwa Spika, katika kuzungumza hayo tuliona mifano mbalimbali, kwamba pamoja na sera nzuri za Serikali na maelekezo ya Wizara kwamba akina mama na watoto wapate matibabu bure, lakini maeneo mengi akina mama wanafanyiwa operesheni kwa gharama kubwa sana wanapojifungua, watoto bado wanatozwa, ukiuliza wanasema ni uwezo mdogo wa kifedga lakini muda mwingine vituo vyetu vinakosa kabisa dawa.

Mheshimiwa Spika, namna bora ambayo nimeiona ya kwenda kuongeza mapato kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya ni kufunga mfumo wa GoT-HoMIS. GoT-HoMIS ni mfumo ambao unaunganisha utoaji wa huduma kwenye kituo cha afya tangu mgonjwa anasajiliwa mpaka anakwenda kwa daktari, anakwenda maabara, mpaka anarudi tena kwa daktari kwa ajili ya majibu. Kwa hiyo, huo mfumo ukiwekwa vizuri maana yake hakutakuwa na uvujaji wa mapato kwenye kituo cha afya.

Mheshimiwa Spika, tumeona kwenye maeneo mengi ambapo huo mfumo umefungwa mapato yameongezeka zaidi ya mara tano, mara sita. Kituo ambacho kilikuwa kinakusanya 100,000 kwa siku kikifungiwa GoT-HoMIS kinakusanya mpaka 500,000, 600,000 kwa siku.

Mheshimiwa Spika, jambo hili likiwekewa mkazo, pamoja na maelekezo ya Serikali, lakini bado Halmashauri hazijatekeleza vizuri huu mfumo, yakipelekwa maelekezo mahususi wakafunga huu mfumo, ninaamini hata yale malalamiko ya kukosekana kwa dawa au kutozwa fedha kwenye vituo vya afya yataondoka kwa sababu tayari kutakuwa na uwezo wa kupata fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ninataka kulizungumza siku ya leo ni hii asilimia 10. Naifahamu dhamira njema sana ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, kwamba angetamani kuwawezesha na wamachinga, na mimi najua. Kwenye asilimia 10 ya halmashauri imewataja akina mama, vijana na watu wenye ulemavu, kwenye kundi la vijana wametajwa wenye kuanzia miaka 18 mpaka miaka 35 wakati Baba kwa maana ya mwanaume ambaye anatamani kupata huo mkopo wa halmashauri wa asilimia 10 lakini hawezi kuupata kwa sababu tayari pengine amevuka miaka 35. Changamoto inakuja hapa, Baba mwenye miaka 35 akikosa huo mkopo nadhani inawezekana ndiyo sababu Serikali imefikiria sasa waone namna ya kutengeneza miundombinu kwa ajili ya wamachinga na watu wa namna hiyo.

Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie, chanzo cha mikopo hii ya wanawake na vijana ilianzishwa mwaka 1993 na Kanuni zake nadhani zilianza mwaka 1994, lakini maboresho yaliyofanyika 2018 na kanuni za 2019 yalitoa malengo kwamba kwa mwanamke siyo mtu ambaye ana msuli, baba kwenye familia au kijana mwenye nguvu angalau hawezi kufa njaa kwa sababu ana uwezo wa kwenda kubeba gunia, ana uwezo wa kwenda kuchimba sehemu kazi yoyote ya kutumia msuli na akawezesha familia yake kupata mlo wa siku hiyo. Lakini kwa mama uwezo huo hana.

Mheshimiwa Spika, sasa ili aweze kujikimu, aweze kuendeleza familia, mama ambaye anategemewa na familia, ilionekana ni vyema apewe mkopo ndiyo tukaenda kutenga hizo asilimia 10 tukazigawanya zilivyogawanywa kwa ajili ya kuwezesha yale makundi maalum.

Mheshimiwa Spika, sasa changamoto inayokuja hapa ni kwamba hii fedha haitoshi, kuna halmashauri za pembeni, kwa mfano Halmashauri za Wilaya za Lushoto, Kilindi, Korogwe, Mkinga na kadhalika na pengine nchini halmashauri nyingi ambazo pengine kwa mwaka hata zinakusanya chini ya Bilioni Moja. Sasa kama mapato ya ndani yako chini ya Bilioni Moja, maana yake ni kwamba asilimia 10 inaweza isifike hata Milioni 200 lakini wananchi wanaohitaji pale ni zaidi ya inavyotegemewa, kwa hiyo mwisho wa siku wanazigawanya zile fedha kwa kuwakopesha wengine Milioni Moja, Milioni Mbili, hela ambayo haileti tija au tija yake inachelewa sana kwa sababu mkopo huo unakuwa na fedha kidogo.

Mheshimiwa Spika, sasa nini kifanyike? Kwa kuwa mwaka 1993 lengo lilikuwa ni vijana na akina mama, na kwa sababu mwaka 1993 ulianzishwa mfuko wa vijana na unafanya kazi mpaka leo kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, ninashauri kwamba pamoja na asilimia 10 kubaki kama ilivyo kwenye Halmashauri zetu kwa ajili ya kuwasaidia akina mama, vijana na watu wenye ulemavu, lakini uanzishwe Mfuko mwingine na uwe unatengewa fedha kama unavyotengewa huu wa vijana kwa kila bajeti kwa ajili ya kuwasaidia hawa wamachinga kujenga miundombinu, vilevile mfuko huo uwasaidie akina mama kupata mikopo kama ambavyo wanapata hili kundi la vijana, kwa sababu wanapata ile asilimia 10 ya halmashauri, at the same time wanapata mikopo kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ninapenda kulizungumza siku ya leo ni upande wa watumishi. Ni dhahiri kwamba tuna upungufu mkubwa wa watumishi katika sekta mbalimbali, Wizara imeona na imeleta namna ambavyo wanaweza wakakabiliana na namna ambavyo wanaweza wakaajiri kadri muda unavyokwenda gradually. Mimi naona kuna haja ya kufanya kitu kwenye eneo hili. Kwa mfano, unakuta kwenye Halmashauri ya Wilaya tunazo taasisi zetu kama Halmashauri, kuna RUWASA, TARURA, kuna taasisi nyingi zipo kwenye Halmashauri, unaweza kukuta pengine kuna Mhandisi wa Ujenzi mmoja yupo pale Halmashauri pengine upande wa RUWASA, ni vizuri tukaenda kwenye kanuni zetu za utumishi wa umma tukaangalia namna ya kuwaazima watumishi kwenye taasisi zingine waende wafanye kazi kwenye taasisi mojawapo ili kuweza angalau kupunguza upungufu wa watumishi na mwisho wa siku kuleta tija katika utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, vilevile inaenda pamoja na upande wa Madaktari. Tumezoea kuona Madaktari wengi wameajiriwa kwenye hospitali zetu za Serikali, wakimaliza ule muda waliopangiwa kuwepo pale unamkuta yuko part-time kwenye hospitali binafsi, lakini huwezi kumkuta yuko part-time kwenye hospitali nyingine ya Serikali. Kwa nini, pengine kuna mgongano hapo wa kikanuni na kimaadili kwenye Kanuni za Utumishi wa Umma, kwa hiyo tuki-harmonize haya mazingira ya utumishi wa umma tutawaruhusu watumishi wetu kutumika kwenye taasisi au kwenye maeneo zaidi ya moja na mwisho wa siku kupunguza uhaba katika utumishi wa umma.

Mheshimiwa Spika, nimeliona hili kwa upande wa TRA pia. Kwa mfano, unakuta kwenye maduka yetu anakwenda kutembelea mtu wa TRA kwa ajili ya kukagua kama kuna EFD machine inatumika vizuri, lakini kama huyo mwenye duka analipa kodi vizuri, akitoka anakwenda mtu wa mapato wa Halmshauri, anachokwenda kufanya yeye ni kuangalia service levy peke yake, akitoka atakwenda Afisa Biashara, anachokwenda kufanya ni kuangalia leseni peke yake, akitoka ataenda mtu wa Zimamoto anakwenda kukagua mtungi peke yake, sasa badala yake yangeunganishwa haya yote akienda mmoja wao akapewa nafasi ya kukagua hayo mengine yote kuliko kulazimu kila ofisi, kila idara, kila taasisi kutembelea duka moja. Hii naona kama vile ni matumizi mabaya ya ofisi na kushindwa kutumia watumishi wachache tulionao, ku-utilize resources tulizonazo katika kuleta tija kubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ninapenda kuzungumzia, hapohapo kwenye utumishi wa umma, tuna idara kwenye elimu inaitwa Quality Insurance (Wathibiti Ubora wa Shule). Kwa mujibu wa Waraka wa 2015 hawa ni watumishi viongozi na waraka umewaelekeza kwamba wao watalipwa mishahara yao kwa LSSE II lakiniā€¦.

Mheshimiwa Spika, naomba sekunde mbili tu niweze kuhitimisha.

SPIKA: Endelea.

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, mpaka tunapozungumza sasa wao hawajapelekwa kwenye hiyo ngazi mpya ya mshahara. Ninaiomba Serikali ione namna ya kuwatia moyo watu hawa. Kwa sababu Waraka umetoka tangu 2015, ni nini kinazuia hawa watu wasipelekwe kwenye mishahara mipya kwa miaka Sita ya kubaki kwenye mishahara ya zamani?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)