Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii kuchangia kwenye bajeti.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuleta bajeti nzuri sana, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mwigulu, kwa kuileta hii bajeti hapa Bungeni. Kusema ukweli hii bajeti imekidhi ni nzuri sana kwa wananchi wote, wote wanaipenda sana.

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la kuondolewa ada kwa kidato cha tano na sita. Hii imepokelewa vizuri na inaonekana kuwa wanafunzi watasoma bure bila ya kulipa ada kuanzia shule za msingi mpaka Kidato cha Sita, hii ni nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, inaonekana kuwa mikopo ya Vyuo Vikuu imeongezewa fedha katika bajeti hii. Kwa hiyo, jambo ninaloomba na kushauri ni kwamba vyuo vya kati viangaliwe ili na vyenyewe ulipaji wa ada uweze kuwa nafuu kwa wanafunzi hawa na kwa wazazi. Kwa hiyo, huo ni ushauri wangu, kuwa na vyenyewe viangaliwe, visiachwe katikati peke yao.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo ninapenda kuongelea ni kuhusu hii asilimia 10. Kwa kweli hii asilimia 10 Mheshimiwa Waziri ukija kuhitimisha naomba uitolee ufafanuzi ili tuweze kuelewa. Hii asilimia 10 umesema kwenye hotuba yako kwamba asilimia tano imependekezwa kuwa iende kwa wamachinga ili kuboresha miundombinu. Miundombinu hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa masoko.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia Wamachinga tayari kuna fedha ambazo zimeshatengwa, lakini hii asilimia 10 umesema asilimia mbili ndiyo itakwenda kwa vijana na asilimia moja ndiyo itakwenda kwa watu wenye ulemavu kwa kweli hapo haieleweki!

Mheshimiwa Spika, ninachoomba hii asilimia 10 ibaki kama ilivyokuwa, kuwa asilimia nne ibaki kwa akinamama, asilimia nne ibaki kwa vijana na asilimia mbili ibaki pia kwa wale watu wenye ulemavu. Kwanza kilichokuwa kinaombwa hapa ni kuongeza hii bajeti kwa upande huu wa asilimia 4:4:2, sasa badala ya kuongeza inaonekana kuwa inapunguzwa. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri aingalie vizuri sana kusudi isipangwe kama anavyokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la kufurahisha kwa wananchi wote na hasa wakulima na wafugaji na wavuvi ni kujali sekta za uzalishaji na hizi sekta za uzalishaji hasa ni Sekta ya Kilimo, Sekta ya Uvuvi na Sekta ya Mifugo ambapo asilimia 65.5 ya wananchi inategemea kilimo. Asilimia 100 ya chakula tunachokula Watanzania inategemea kilimo. Kwa hiyo, kwa kuongeza bajeti ya kilimo kutoka bilioni 274 mpaka bilioni 954, ni jambo la neema sana. Pia fedha za mifugo kutoka bilioni 168.2 mpaka 268.2, nalo ni jambo safi kabisa na hapo hapo kuna mchanganuo kuwa bilioni 92 ni fedha za mifugo na bilioni 176.2 ni fedha za uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye kilimo jambo linalotakiwa hapa ni kilimo chenye tija, ufugaji wa tija pamoja na uvuvi wenye tija. Kwa upande wa kilimo nashauri na nampongeza Waziri wa Kilimo kama walivyosoma sekta zao pamoja na uvuvi na mifugo. Nashauri mipango iliyopangwa kwenye Wizara hii iende kama hivyo hivyo ilivyopangwa. Jambo la muhimu ni utekelezaji, ufuatiliaji na kuona kuwa mipango yote inaenda kama ilivyopangwa. Kwa mfano, nikija kwenye upande wa kilimo cha mbegu, sasa hivi tunamashamba ya mbegu 17 lakini unakuta mashamba mengine hayafanyi kazi vizuri. Kwa hiyo, nashauri mashamba yote ya mbegu yafanye kazi vizuri na yaweze kutumia kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi mashamba hayatumii kilimo cha umwagiliaji, naamini tukizalisha mbegu sisi wenyewe za hapa ndani tutatokana na tatizo la mbegu. Kwa mfano, mbegu za alizeti na michikichi, Tanzania tuna ardhi kubwa sana hatuna sababu ya kuagiza mafuta ya kula kutoka nchi za nje, tunaweza kulima mbegu zetu za alizeti, tukaweza kuwatosheleza wakulima wote, tukaeneza elimu ya kulima michikichi kwenye mikoa ambayo imepangwa na tukaweza kuzalisha kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kilimo cha ngano; tuna ardhi, tuna mikoa ambayo pia bado haijaangaliwa kuwa inaweza ikalima ngano. Kwa hiyo, hakuna sababu ya kutoa ngano kwenye nchi za nje, tunaweza tukalima sisi wenyewe tukajitosheleza. Nashukuru Wizara ya Kilimo ambayo tayari imetoa vitendea kazi kwa Afisa Ugani. Kwa hiyo, Maafisa Ugani hawa wakisimamiwa vizuri naamini kuwa tutaweza kutoa na kuzalisha mbegu za kutosha na kuweza kujisimamia kupata mafuta ya kutosha ya kula badala ya kupeleka fedha zetu kununua mafuta nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, nikija kwa upande wa mifugo, tayari kuna elimu ya uimilishaji; wananchi wengi hawatumii elimu hii, elimu hii ni nzuri sana ikitumika vizuri bajeti itakwenda vizuri na watu wataweza kupata mazao bora ya mifugo. Kwa upande wa uvuvi nilikuwa nataka wananchi waweze kufundishwa vizuri elimu ya ufugaji wa samaki.

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye ukusanyaji wa mapato; mapato mengi yanapotea tungeweza kupata fedha nyingi za kutosha kwenye ukusanyaji wa mapato. Tuje kwenye ukusanyaji wa mapato, hata sisi tulio humu ndani tunasema yule anayeuza aweze kutoa risiti na yule anayenunua aweze kudai risiti, lakini unakuta hiyo njia haitumiki. Kwa hiyo, naomba uwepo mfumo mzuri kama ulivyo kwenye sheli zetu za kuuzia mafuta, whether unaomba risiti, huombi risiti, lakini tayari mahesabu yanaonekana kuwa umechangia Serikali. Kwa hiyo, hata kwenye maduka yetu ya wafanyabiashara ionekane kuwa hizo EFD machines zinafanya kazi na zimewekewa mfumo wa kukusanya ada zetu ambazo tunaweza tukaongeza bajeti ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo naongelea ni kuhusu TEHAMA. Hii TEHAMA ikienda mpaka vijijini vijana wetu kupitia kilimo, mifugo na uvuvi wanahitaji kutumia TEHAMA, wanahitaji kutumia umeme, wanahitaji maji safi na salama, wanahitaji mambo ya afya. Naamini hivi vyote vikiwa huko vijijini vijana watatamani kukaa vijijini na wataweza kuendesha maisha yao huko vijijini, watajiajiri huko vijijini, hakutakuwa na sababu ya kuvutiwa kuja mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo naomba kuongelea baada ya kuwavutia vijana kukaa huko vijijini, nashukuru kwa upande wa kilimo, tayari na uvuvi na mifugo wameshaweka mazingira mazuri ambayo yatawavutia lakini yasimamie kwani kuwatengea ardhi, kuwapa matrekta ya kulimia ni jambo zuri ambalo litawavutia hawa watu hukohuko.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo naomba kuendelea ni kuhusu miundombinu ya SGR. Nashauri Mheshimiwa Waziri anasema SGR inakwenda vizuri, naipongeza Serikali ujenzi wa SGR unakwenda vizuri kipande cha Dar es Salaam kuja Morogoro kinakwenda vizuri, Waziri amesema kuwa tumefika asilimia 96.5. Kwa hiyo, naomba kipande hicho kiweze kukamilika na kiweze kufanya kazi kusudi na vipande vingine viendelee vizuri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru, lakini mambo hasa niliyosema kuwavutia vijana ikiwemo TEHAMA na kila kitu, hivyo naomba kifanyiwe kazi.

SPIKA: Muda wako umeshaisha Mheshimiwa.

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja, na bajeti hii ni nzuri naomba itekelezwe na isimamiwe. Ahsante sana. (Makofi)