Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kipekee namshukuru Mungu aliyetuweka hapa leo, tuna afya njema na tunazungumzia jambo muhimu sana katika nchi yetu, bajeti ya Serikali ya Tanzania mwaka 2022/2023 iliyowasilishwa hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Rais wetu mpendwa, Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea bajeti ambayo ni ya viwango. Watanzania wanajua, dunia nzima inajua kwamba sasa hivi mwanamke anayeongoza Tanzania anafanya vitu vyake kwa hali ya juu na kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana mwasilishaji wa hoja hii ambaye ni Waziri wetu wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba na timu yake yote; makamu wake, Katibu Mkuu na watendaji wote. Jambo hili limefanyika vizuri na nitamke rasmi, naunga mkono hoja japo pia nina michango ambayo nataka aboreshe na aipokee na wengine waliyoyasema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze tu kwanza kwa kusema jambo hilo la kusoma Form One mpaka Form Six bila ada ni jambo jema, na wote wameyasikia, wavulana kwa wasichana. Wakati tunaenda jeshini miaka hiyo, mwaka mmoja ukiwa umetoka Form Six, maafande wale wanakwambia hao ni wasomi mpaka wakakuta no class, yaani unagonga no class ndiyo Form Six.
Mheshimiwa Spika, sasa nawaomba watoto wetu walio Tanzania nzima wasome mpaka wakute no class, hakuna mbadala. Jambo hili linaenda kupunguza mimba za utotoni, kwa sababu kama wewe ni mwanafunzi na mtu akija akigusa mwanafunzi kifungo ni chake. Hiyo ndiyo adhabu. Sasa sijui mabinti zetu nini kitawazuia wasisome mpaka wamalize? Vile vile hao vijana wasichezecheze na watoto wa wenzao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kushukuru kwa jambo hilo, nije na lile ambalo limeleta taharuki kidogo, ni hili jambo la asilimia 10. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, jambo hili ameliongelea vizuri sana mwenzangu aliyenitangulia kabla, alikuwa ni Mheshimiwa Husna. Kwamba hii asilimia 10 ilipowekwa ilikuwa na madhuni maalum. Ukienda kule library ukasoma Hansard miaka hiyo ya 1994 hili jambo halikuwa rahisi wala jepesi. Ilikuwa ni asilimia 10 kwa wanawake na wanawake hao ni wale wanawake ambao hawakopesheki, hawana dhamana yaani hawana security, hawezi kwenda kwenye benki kukopa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati huo waliotutangulia wakaona kwamba basi tuwawezeshe akinamama na ikafanyika hivyo. Pia ukizingatia ukiiwezesha kaya, umewezesha kata, umewezesha tarafa, umewezesha wilaya, umewezesha mkoa na Tanzania nzima. Sasa iweje leo Serikali inataka kuwajengea wajasiriamali miundombinu, wanaona waje pale kwenye ile asilimia 10? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, juzi juzi, miaka michache iliyopita, mwaka 2008 wali-beep wakaitoa ile asilimia 10 ikaenda kwenye 4,4,2. Wanawake walivyo wasikivu wakanyamaza. Kelele zilipigwa za kichinichini na mnajua wenyewe, kwa sababu wote hapa ni Wabunge na hata yeye ni Mbunge, anajua jambo lililokuwa linaendelea. Ile hela nyingine ilikuwa sasa watu wasaidie, Wabunge wasaidie kutoka mfukoni. Sasa mnakuja tena kugusa pale pale. Yaani unaweka chumvi kwenye kidonda. Unawagusa tena wale wanawake, unataka tena kuondoa utamu, iweje? Kwani mwanamke akipata nani kapata? Inakupunguzia mzigo wewe baba, inamwezesha mwanamke. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana Serikali yangu sikivu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi, isikie jambo hili, waachieni wanawake hiyo asilimia yao ilivyokuwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo na maombi hayo, sasa naomba nizungumzie sekta binafsi. Sekta binafsi ni eneo ambalo sasa linatakiwa lifanye kazi kwa kukimbia kabisa. Mheshimiwa Rais wetu amesema, Serikali ipo tayari kuweka miundombinu mizuri ya wafanyabiashara au ya sekta binafsi kufanya biashara zao vizuri. Hili ni kweli, amedhamiria. Sasa hii sekta binafsi nayo inatakiwa pia isaidike.
Mheshimiwa Spika, unakuta kwamba kama watakuja wafanyabiashara wa sekta binafsi kutoka nje tu wakafanya na haupati hiyo faida yao, huku ndani hatutaweza kui-feel vizuri, lakini kama wafanyabiashara wa kwetu wa sekta binafsi watafanya vizuri, basi kila mtu atai-feel yale maendeleo au wata-feel biashara yao waliyofanya hapa kuwa wamepata chochote. Itasikika vijijini na itasikika mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba wafanyabiashara hawa wawezeshwe. Wawezeshwe katika njia nyingi, mpaka sasa Serikali imeshafanya kiasi kikubwa sana. Imewawezesha kwenye miundombinu; barabara, reli, na viwanja vya ndege. Hiyo yote Serikali imeshafanya, lakini sasa tunakwenda kuwawezesha zaidi katika kule kwenye zile ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utakuta kwamba mfanyabiashara anapokuja kwa kuajiri mishahara inatofautiana na pia kodi zinatofautiana, sasa inatakiwa watu wetu tuwaelimishe wanapoenda kufanya kazi kwenye sekta binafsi wawe na nidhamu ya sekta binafsi, kuna mambo yamezoeleka business as usual hapana siyo kwenye sekta binafsi! Amefunga safari au mtu amefungua shughuli yake iwe ni hoteli iwe ni nini, anatarajia wewe unaenda kufanya kazi kwake uwe na nidhamu ya kutosha ili aweze kuzalisha kama anavyotarajia.
Mheshimiwa Spika, miaka 94 wakati TBL imetaifishwa ilibidi yale mashamba ya kuzalisha shayiri na ngano kule West Kilimanjaro itolewe kwa wakulima au sekta binafsi, kweli walikuwepo Watanzania waliojiotolea, wakati huo walikuwako Watanzania wanne waliungana, lakini ukaja kutokea mgogoro yale mashamba wakanyang’anywa sasa walipokuja baadaye, kuja watu wa kutoka nje kuwekeza hawalimi tena ile shayiri na ngano katika kile kiwango kikubwa, matokeo yake ni nini, ni kwamba matokeo yake ni kwamba sasa mashamba yale yamebaki hivyo hivyo na ukienda kule unakuta wana-import ngano kutoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa BASUTA imeenda wapi? West Kilimanjaro imeenda wapi? Kwa nini tuna maeneo makubwa hayo na hatuwezi kuzalisha kama tunavyotaka, kwa hiyo nilikuwa naomba sana Serikali iweke jicho la ziada kwa hao watu wa sekta binafsi ili waweze kupata ushindani, ushindani kwa huku huku ndani wenyewe lakini pia ushindani na wale wanaokuja ku-invest katika nchi yetu na ikiwezekana hawa wa ndani wawazidi hata wale.
Mheshimiwa Spika, sekta binafsi ninayoweza kuzungumzia ni sekta ya hawa Makandarasi. Tumeona kwamba Makandarasi wa nchi kwetu wanapata kikwazo sana pale kwa ule mtaji wa Bilioni 10, wao hawaruhusiwi kwenda zaidi, sasa matokeo yake wanaopata hizo kazi za REA, wanaopata kazi za kwenye maeneo makubwa mengine ni hawa contractors kutoka nje, lakini nilikuwa naomba iletwe hapa ile Sheria ya PPRA ibadilishe kile kiwango cha Ten Billion kiweze kwenda juu waruhusiwe hawa ma-controctors waungane hata kama ni barabara kubwa wao waweze kupewa kwa jumla halafu wagawane hiyo barabara kwa sababu kama ni viwango vinavyopimwa kwa wale wa nje ndio hivyohivyo vinavyopimwa kwa watu wa ndani.
Mheshimiwa Spika, haina maana mtu amsomeshe kijana wake afanye engineering miaka minne halafu afanye tena field, aje aajiriwe aambiwe hapana uwezi kupata kazi mpaka waje hao ma-contractor wa nje! Sasa mkumbuke tu kwamba wakishapata wale zinakwenda kuliwa nje na sio hapa. Kwa hiyo, hilo namuomba sana Waziri aweze kuliangalia.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ni kwenye huo uwezeshaji niliozungumza nyingi ni Commercial Banks zinakopesha sisi tuna benki yetu Tanzania Investment Bank, ni benki ambayo ilikuwa ni ya kuwawezesha wananchi wakope ndani, lakini ni benki ambayo katika nchi nyingine any Investment Bank ni benki kubwa na hapa ndani miaka iliyopita walisema kuwa Serikali ilisema ingewasaidia mtaji, lakini tuna miaka kadhaa hawajaweza kupata mtaji, pia hatujaweza kujua nini kinaendelea TIB mpaka sasa hatuoni kama wanatoa mikopo ya kutosha, hata Serikali yenyewe ingeweza ikakopa huko hela za kujenga hiyo reli – SGR, hela za kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere, matokeo yake unakuta tunakwenda kukopa mahali ambako Tunadaiwa faida kubwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuunga mkono hoja niwaombe wenzangu nao waunge mkono hoja ili Waziri huyu aachiwe mapema akatekeleze hayo majukumu na wote tuweze kupata hii keki ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru nilishaunga hoja mkono. Ahsante sana. (Makofi)