Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Kwanza nianze kwa kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Mwigulu na Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, kwa kuwasilisha hotuba zao zote mbili hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba niseme, kiongozi mzuri hajitengenezei ubinafsi. Narudia, kiongozi mzuri yeyote duniani hajitengenezei ubinafsi, bali anatengeneza mambo ya kuleta mabadiliko chanya ya maendeleo kwa watu anaowaongoza na kuleta legacy. Sasa hii imejidhihirisha kwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote Tanzania, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutengeneza na kuwafikia wananchi wa kawaida vijijini. Kuwatengenezea huduma za kijamii, shule, afya, maji na barabara na anatengeneza legacy kwa kuwafikia wananchi wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo anatengeneza shule na tumeona wote katika kila jimbo madarasa yamejengwa vizuri, anajenga vituo vya afya na hospitali. Naamini kwamba ukitaka kumfikia mwananchi wa kawaida maskini kijijini, wape elimu watoto wake. Ukitaka kufikia familia maskini kijijini, wape mazingira bora ya afya katika maeneo yao. Haya ndiyo anayoyafanya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa narudi kwenye hoja, kwenye suala la Mpango ulio mbele yetu. Uchumi duniani unapodorora unaathiri pia Taifa letu. Tunaambiwa sasa hivi utaathiri upatikanaji wa fedha za mikopo, kupanda kwa riba ya mikopo huko duniani na uwezekano wa kupungua au kukosa misaada kutoka katika nchi hizo. Nchi hizo marafiki zetu kihistoria, ambao wamekuwa wakitupa misaada na mikopo, Marekani, Japan, Uingereza, Canada, Ujerumani, Ufaransa, Italia, Hispania na maeneo mengine ya Ulaya; kiwango cha ukuaji wa uchumi wao kinatarajia kushuka kutoka asilimia 2.6 mwaka 2022 mpaka asilimia 1.5 mwaka huu 2023, lakini ukuaji wa uchumi utaendelea kushuka tena mwaka 2024 mpaka asilimia 1.4. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hayo yote lazima tuyatafsiri kwa kukaza mkanda na kujiimarisha katika kazi zetu na kuona mpango wetu huu unajielekeza katika kukabiliana na hali hii ya mabadiliko ya kudorora kwa uchumi duniani hasa kwa nchi hizi nguli za magharibi. Kwa kuwa watu hawa tumekuwa na mahusiano nao mazuri, ya mikopo na misaada mbalimbali na sasa riba kwao zimepanda za mabenki yao, lakini pia hali ya ukuaji wa uchumi wao umeshuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie, je, ni nini itakuwa athari yake kwetu sisi kama Tanzania, lakini tukikopa pia kwa wakati huu athari yake itakuwa nini kwa riba kubwa kwa nchi zile? Mpango utuoneshe maeneo yale ya misaada kutoka kwao tutakayokosa katika kipindi hiki yatatuathiri kiasi gani na tumejipangaje kuziba pengo hilo la misaada ambayo tunaipata kutoka kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, tuongeze uzalishaji mali katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji wa kilimo, lakini bidhaa mbalimbali zitakazoongezwa thamani kuuza nje. Tuongeze thamani katika bidhaa mbalimbali, nitatolea mfano katika mazao haya ya biashara ya kilimo, lakini kutokana na muda nitalisemea moja la tumbaku. Zao la Tumbaku limekuwa ni zao ambalo linauzwa kwa dola. Kwanza ni zao la kimkataba, mkulima kabla hajaingia shambani, unafanika mkataba wa ununuzi na ununuzi ule ni kwa dola lakini zao hili pia lilishanunuliwa kwa mkulima kwa dola, linaenda kuwa processed. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna viwanda hapa vya ku-process tumbaku, semi-product ambao wanafanya blending ya ile tumbaku. Ikishafanyiwa blending, asilimia kadhaa kubwa inauzwa nje ikiwa imekuwa processed kiasi kwa kufanyiwa blending. Inauzwa nje kwa dola lakini asilimia nyingine inauzwa ndani katika viwanda vya ndani, inatengeneza final product ambayo ni sigara. Pia, nayo hiyo sigara inauzwa nyingi asilimia kubwa nje kwa dola. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi nchi yetu sasa hivi tuna uhaba wa dora na tunakazania sana tupate dora. Tulitazame sana zao hili. Zao hili ni zao la kimkataba na kwa mwaka huu tu limeuza zaidi ya dola milioni 400. Takwimu zaidi sina za uhakika, lakini Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, watafute takwimu vizuri. Mwaka huu tumeuza tumbaku kwa dola nyingi, lakini mwaka huu pia msimu unoakuja tumeingia mkataba wa uzalishaji wa tani nyingi zaidi za tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu hili zao tuliangalie kwa karibu sana, kwa sababu kama nilivyosema, linauzwa kwa dola kwa mkulima, linapokuwa processed linauzwa nje kwa dola, lakini pia linapokuwa processed hapa na kupata final product ya sigara nyingine kwa wingi, zinauzwa nje kwa dola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunachoomba, tuliangalie hili zao katika uzalishaji wake. Leo hii zao hili, mbolea yake inalipiwa ruzuku. NPK hailipiwi ruzuku, inauzwa kwa bei ghali Sh.160,000 mpaka Sh.170,000, lakini mbolea nyingine zozote za mazao, zinapewa ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, Serikali itoe ruzuku katika zao la hili la tumbaku ili tuweze kupata dola nyingi zaidi. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, aliwahi kutuambia hapa Bungeni, ukitaka kula, lazima uliwe. Kwa hiyo, haya madola yote wanayoyasema haya ili Serikali iyapate mengi zaidi, ni lazima tuliwe. Lazima tutoe ruzuku ya NPK kwa zao la tumbaku. Pia, naomba mpango ujielekeze kwenye hilo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tunashukuru sana mpango hapa umetueleza katika Aya ya 31, Ukurasa wa 14, mafanikio yale. Serikali imetoa ruzuku katika mazao ya kilimo. Pia, ongezeko la uzalishaji wa mazao, limeongezeka kutoka tani milioni 17 mpaka 20, lakini pia wameimarisha masoko. Wameyasema wazi NFRA wamenunua mazao. Tunashukuru sana imenunua kweli na mazao mchanganyiko wamenunua NFRA, lakini bado wakulima walikuwa wanawadai Serikali bilioni 40. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ni kipindi cha wakulima kwenda kulima na kilimo kinataka maandalizi na maandalizi ni fedha. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali, nashukuru mpaka Ijumaa Serikali imeshalipa bilioni 19 kwa wakulima waliouza mahindi kupitia NFRA. Sisi Mkoa wa Ruvuma tunadai bilioni 9.9 na tumeshalipwa bilioni 4.0, bado wakulima wanadai bilioni 5.9 (Bilioni tano na milioni mia tisa). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali kupitia NFRA iwalipe wakulima hawa warudi tena shambani waweze kuzalisha, mazao yaweze kuongezeka. Kwa hiyo, tunaomba sana hili walichukue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine. Mipango yote hii tunayoifanya, yote inahitaji usalama. Ni lazima eneo la usalama tulizingatie sana katika mipango yetu ya Taifa. Tuhakikishe kwanza tunalinda mifumo yetu ya fedha. Eneo hili la usalama tuhakikishe tunalinda mifumo yetu ya fedha kwani sasa hivi kumekuwa na ushamirishaji mkubwa sana wa wizi kupitia mifumo yetu ya fedha za Serikali. Kwa hiyo, lazima kuwe na fedha za ziada ambazo zitakuwa zinalinda wakati wowote kubadilisha mifumo ili kukabiliana na wizi huu wa fedha za Serikali kupitia mifumo. Kwa hiyo, tunaomba sana uhalifu wa mifumo yetu ya Fedha za Serikali na mwingine umeongezeka sasa hivi ambao udhibiti wake… (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa…

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, lakini naomba unipe nusu dakika. Mifumo ambayo udhibiti na ufuatiliaji wake wa mifumo hii, unahitaji teknolojia na teknolojia inahitaji fedha. Kwa hiyo, sasa katika mpango huu ni lazima tuweke fedha za kulinda mifumo yetu kwa ajili ya usalama wa fedha za Serikali na kuzuia hawa wahalifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)