Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mikumi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuendelea kuchangia Mpango.
Kwanza nianze kwa kumshukuru Rais wetu, Mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa utekelezaji mzuri wa bajeti hii ambayo tunaendelea kuisimamia katika utekelezaji wake, lakini kwa nafasi nyingine pia ya kushauri Serikali maeneo muhimu ya kuwekeza katika bajeti inayokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mikumi, nimshukuru Mheshimiwa Rais na Bunge lako kwa msaada mkubwa ambao mmempatia mtangulizi wangu Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Mheshimiwa Joseph Haule (Profesa Jay). Kimsingi kwa niaba ya wananchi wa Mikumi tunashukuru sana kwa mapokeo lakini pia utayari wa Bunge hili ku-support course ambayo anaenda ku-fight kwa ajili ya watu wenye matatizo ya figo, tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ambayo tunaendelea nayo na mpango huu ambao tunaujadili sasa, tunaujadili katika wakati ambapo dunia ipo katika hali ya sintofahamu kiuchumi na kisiasa. Changamoto kubwa za kimfumo zinaendelea dunia nzima. Tanzania siyo kisiwa, nasi pia ni sehemu ya dunia hii. Tunaathirika moja kwa moja ama kwa namna moja ama nyingine. Ni vyema mipango yetu na bajeti yetu katika maandalizi yake, tukaangalia mwenendo wa dunia unavyoenda na jinsi gani unaenda ku-impact watu wetu hasa wakulima ambao ni 70% ya wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunavyozungumza, kuna vita Middle East, kuna vita Ulaya, kuna vikwazo kila sehemu, lakini kimsingi tunaona kabisa kila dalili kwamba mfumo wa soko huria kwa maana ya policies na capitalism ambapo sisi ni sehemu ya dunia hii na mifumo hii ya kiuchumi inasimamia shughuli zote za kijamii, kiuchumi na kisiasa katika dunia yetu tunaona imetetereka. Kwa sababu siri ya mfumo wa kibepari na soko huria ni ulinzi wa mitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vikwazo na confiscation ya private property ambayo ndiyo roho ya ubepari, roho ya mfumo wa soko huria; tunaona Warusi mali zao zinataifishwa kwa sababu tu ni Warusi, kwa sababu tu Werikali yao imeingia vitani. Yeye sio mwanasiasa, sio mshiriki wa Serikali, wala hajashiriki katika maamuzi ya kwenda vitani, lakini mali zake zinabinafsishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo ni ndwele ambazo zinaashiria jambo kubwa kwa sisi Waafrika ambao kazi yetu ni kuchukua fedha ndani na kwenda kuwekeza nje. Fedha hizo hazitakuwa na maisha kesho kwa sababu uchumi wa dunia yetu wote tunaujua, umejengwa katika hali ya primitive accumulation of capital. Sheria zimejengwa kwa ajili ya ku-confiscate mitaji ya watu kwa njia ambayo ni legally. Kwa mfano hiyo ya kuweka vikwazo na kuchukua mali za watu binafsi kwa makosa ya Serikali zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linatupeleka kwenye kile ambacho Francis Fukuyama alizungumzia Clash of Civilization, kwamba baada ya migongano kati ya Ubepari na Ujamaa, kitakachofuata ni migongano ya imani, kiitikadi na kimtazamo. Ndiyo maana tunaona dunia hailali kwa sababu damu ya watu fulani inamwagika, lakini wakati huo huo inalala damu ya watu fulani ikimwagika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria na mipango na mifumo imejengwa kwa ajili ya kumuumiza asiyenacho. Ndiyo maana mwaka 1837 Bunge la Uingereza lilipitisha sheria ya kuzuia biashara ya utumwa, pia ilipitisha sheria ya ku-compensate wale Waingereza wote ambao wanakwenda kupoteza mali zao kwa maana ya watumwa, yaani Waafrika katika makoloni ya Mwingereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, walitenga zaidi ya pauni 20,000,000 ambayo ni sawa sawa 40% ya bajeti yao, sawasawa na 5% ya GDP ya nchi kwa ajili ya ku-compensate watu ambao walikuwa wanamiliki watumwa. Deni hilo lilikuwa ni kubwa na la kihistoria, na Serikali ya Uingereza kwa maana ya walipakodi wa Uingereza wakiwemo Wabunge ambao wamesoma Uingereza, wameshiriki kwenye kulipa deni hilo mpaka 2015, ndipo wamemaliza kulipa deni hilo. Mwaka 2015, maana yake ni miaka saba iliyoisha, ndiyo wamemaliza kuwalipa wale ambao walikuwa wanamiliki watumwa kuwaachia huru watumwa hao. Kwa hiyo, tumeshikiri katika kampeni ya kuwapa uhuru babu zetu na bibi zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii ilipitishwa kwa ajili ya ku-compensate loss kwa hawa wamiliki wa watumwa, lakini katika kuwajengea mitaji Waingereza, mitaji ambayo sasa hivi tunaitumia kama mikopo ambayo tunailipa kwa riba kubwa kwa nchi zetu. Hilo linaonesha kwamba kuna umuhimu wa sisi pia kwa bajeti yetu tusione aibu kutenga fedha kiasi cha kutosha kwa ajili ya kuwaweza watu wetu kwa kisingizio chochote kile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutegemea Sheria za Kimataifa kutupa fedha ama leeway ya kupendelea watu wetu katika ku-accumulate capitals hazitatufikisha mbali. Pamoja na hayo yote, naomba nizungumze kitu kimoja. Sheria nyingi ambazo zipo, hata hizi Mahakama za Kimataifa ambazo Serikali inakosa haki na tunapaswa kulipa mabilioni ya hela, zinaturudisha nyuma badala ya kutupeleka mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ambazo tunalipa kama compensation kwa sababu ya kuvunja mikataba ni aina nyingine ya unyonyaji ambayo imejikita katika mifumo ya unyonyaji ya dunia yetu. Hatuwezi tukaa hapa tukapanga mipango ya kukusanya fedha za walipakodi wetu kwa ajili ya kulipa fidia au kwa ajili ya kuendelea kuimarisha mifumo ya kinyonyaji duniani. Ni lazima mipango yetu iangalie pia jinsi ya kudhibiti mianya ambayo inavujisha fedha zetu kwa ajili ya kuimarisha masoko ama mitajji ya mabepari. (Makofi)
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dennis, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Christopher Ole-Sendeka.
TAARIFA
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa Taarifa Ndugu yangu Londo kada wa chama chetu kwa maneno mazuri sana anayozungumza. Tusipochukua tahadhari sasa dhidi ya watu wanaotuingiza kwenye mikataba ambayo sasa tunakuja kudaiwa kupitia Mahakama za dunia ambayo sasa ni kiwango cha mabilioni ya fedha, kesi nyingi tumeshapigwa na kesi nyingine zipo njiani na tutashindwa, lakini waliotuingiza kwenye hasara hizo bado wapo kwenye Utumishi wa Umma na hawaondolewi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri umefika wakati sasa tukilipa fedha za mikataba hii, wahusika wenyewe wachukuliwe hatua ikiwa ni kuondolewa wao na wale madalali waliokuwa wanapita Wizarani kuwaombea kazi hao.
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Dennis Taarifa hiyo unaipokea?
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea kwa mikono miwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko tunakoenda, hatuwezi kubeza kilimo, lakini hatuwezi kukaenenda na mwenendo huu tukategemea matokeo ya tofauti. Tuna ekari zaidi ya milioni 26 ambazo tunaweza tukamwagilia kilimo cha umwagiliaji, lakini tuna highly suitable land ekari zaidi ya milioni 2.3. Kiasi ambacho tutatumia sasa hivi kwa ajili ya umwagiliaji ni 1.6%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama 70% ya Watanzania wamejikita kwenye kilimo, ni vizuri bajeti yetu ikajikita kuona ni namna gani tunaenda kumkwamua huyu mkulima maskini wa Kitanzania, kilimo chake kiongeze tija kwa kumpunguzia gharama za uwekezaji, kwa maana ya kumjengea miundombinu ya uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara za TARURA ambazo zinaunganisha mashamba na masoko, mashamba na barabara kubwa ni lazima zipatiwe bajeti ya kutosha. Mwaka jana 2022 tulipitisha hapa shilingi bilioni 11 kama dharura. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishuhudia mvua zikinyesha, zikiondoa madaraja na Barabara, fedha hizo sidhani kama zilienda. Mwaka huu kuna fedha ambazo tulipanga kwa ajili ya ujenzi wa Barabara, kuna zaidi ya shilingi bilioni 350 ambazo zilipangwa kwenda, sina hakika kama zimeenda. Barabara hizi ni muhimu, siyo kwa ajili ya luxury ya wakulima, ni kwa ajili ya kumpa mkulima uhakika wa kuondoa mazao yake mashambani kwenda sokoni ili Serikali ipate mapato yake na huyu Mtanzania apambane na umaskini wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki ambacho tunakiona katika sekta ya kilimo, tuna wafanyabiashara wakulima zaidi ya milioni mbili. Asilimia 94 ni wazalishaji, ni 1.4% tu ambao unaweza kusema kwamba wanashiriki kikamilifu katika zoezi la kuongeza thamani mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ndiyo msingi kwa wakulima. A certainty ambayo inatokea inatokea migogoro ya mipaka, a certainty ambayo inatokea katika suala zima la umiliki wa ardhi katika maeneo mbalimbali, siyo suala la kupuuza. Kama tunataka tumwezeshe Mtanzania kiukweli, ni lazima tusimamie migogoro yote na vyanzo vya migogoro ikiwemo kuchukua hatua watumishi wote ambao wanasababisha kuingia katika migogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunaingia kwenye migogoro hii ya ardhi? Sheria Na. 8 ya Ardhi inaitaka TAMISEMI kupima, kupanga na kumilikisha. Nani anapitisha hayo? Ni Afisa Kamishna wa Ardhi kule juu, lakini msimamizi wa sera ni Wizara ya Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro ukitokea unaenda Baraza la Ardhi ama Mahakamani, lakini huku kwenye halmashauri ambapo ndiyo wana sheria ya kusimamia hii ardhi unaona kabisa kuna makampuni yanaenda yanapima pale, yakishapima pale yalipeleka mchoro huku juu baada ya kuwalipisha wananchi, wanaambiwa kwamba hapo tayari hilo eneo lilishapimwa na lilishatwaliwa tayari na mtu. Kwa hiyo, tumeingia kwenye mgogoro mpya.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumaliza…
MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa dakika 30.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Kilosa kuna barabara ya kutoka Kilosa – Mikumi kile kipande kinaunganishwa na SGR Stesheni ambayo yamewekezwa mabilioni ya fedha pale. Kile kipande cha kilometa 72, hii sasa hivi ni bajeti ya tano kinaingia na hakijawahi kushughulikiwa. Barabara mpya zinakuja, zinatangazwa, zinajengwa. Kipande hiki kuna nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, imefikia hatua wananchi wa Mikumi wameanza kukata tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. Naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)