Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Alfred James Kimea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii jioni ya leo ya tarehe 09/11/2023, na mimi kuchangia kwenye Mpango huu wa mwaka 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijatoa ushauri wangu hasa nimejielekeza kwenye Sekta ya Kilimo. Ninaomba nitumie fursa hii kueleza mambo machache sana ya nyumbani kwetu nikimaanisha kwenye Jimbo langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya miaka mitatu kama siyo minne tuliahidiwa kujengewa barabara kwa kiwango cha lami, barabara ambayo inaunganisha Majimbo muhimu matatu kwenye Mkoa wa Tanga Jimbo langu la Korogwe Mjini, Jimbo la ndugu yangu Timotheo Mnzava Korogwe Vijijii lakini Kimbo la Kaka yangu Dunstan Kitandula. Barabara hii tumeahidiwa mara nyingi, Serikali ilituahidi kwamba mwaka huu wataenda kumaliza upembuzi yakinifu ili barabara ile iweze kutangazwa. Mwezi wa Sita walituahidi watamaliza mwezi wa Sita umepita hawajamaliza, wakasema mwezi wa Tisa, mwezi wa Tisa umepita haijamalizika baada ya hapo wanatuambia mwezi wa Kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ahadi zimekuwa nyingi tunaomba Serikali itimize ahadi hiyo, upembuzi yakinifu umalizike barabara hiyo itangazwe ili ianze kujengwa kwa kiwango cha lami kama tulivyoahidiwa. Kibaya zaidi Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri Mkuu kwa nyakati tofauti walimuahidi Kiongozi wetu mkubwa kabisa wa dini kwenye nchi hii kwamba wataenda kujenga barabara ile, Mufti Mkuu wa Tanzania. Tunaweza tukaacha kutimiza ahadi lakini mpaka kwa Viongozi wetu hawa wakubwa wa dini haileti picha nzuri. Kwa hiyo, naomba Serikali iweze kwenda kufanyia kazi barabara ile haswa kipindi hiki cha mvua imeharibika sana haipitiki kwa hiyo waende kuingalia na waone namna gani wanawasaidia wananchi wa Korogwe Mjini kwenda Magoma, kwenda Mabwepande ambayo inaunganisha Majimbo matatu muhimu na ndugu zangu Mheshimiwa Kitandula na Mheshimiwa Mnzava pamoja na mimi tumekuwa tukiliongelea mara nyingi. Ahsante nimeanza na utangulizi huo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mkubwa ni kwenye Sekta ya Kilimo siku ya leo, nimejipanga kuchangia sehemu saba kwenye Sekta ya Kilimo, muda ukinitosha nitachangia zote muda ukiniishia katikati hapo nitakapoishia nitaishia hapohapo, kikubwa ninachotaka kuchangia moja ni Mikopo kwenye sekta ya kilimo, riba ya mikopo ya sekta ya kilimo, pembejeo kwenye sekta ya kilimo, bima ya kilimo, masoko, miundombinu ya umwagiliaji, uongezwaji wa thamani kwenye mazao ya kilimo. Hayo ni mambo saba ambayo nataka kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na jambo la kwanza ambalo ni mikopo kwenye sekta ya kilimo. Kwanza nitumie fursa hii kumshukuru Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan jinsi anavyoendelea kuongeza bajeti kwenye sekta ya kilimo tunaona miundombinu mingi kwenye sekta ya kilimo ikiwemo miundombinu ya umwagiliaji ikijengwa siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ni uwekezaji mkubwa ambao Mama Samia Suluhu Hassan anaifanya kwenye sekta ya kilimo lakini bado tuna changamoto kubwa kwa wakulima wa nchi hii kukosa mitaji ili waweze kujikita kwenye sekta ya kilimo. Tumekuwa tukihubiri sana kwamba Benki zetu za Biashara pamoja na Benki yetu ile ya Kilimo inatoa mikopo kwa wananchi lakini kwenye ground hali haiko hivyo, vijana wetu, wamama na wakulima wadogo imekuwa ni vigumu sana kupata mikopo kwenye taasisi hizi za mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali moja kuendelea kuongeza bajeti au fedha kwenye Benki yetu ya Kilimo ili kuhakikisha tunaongeza wigo wa wananchi wa Kitanzania ambao wanapenda kulima wapate mikopo ili waendeleze sekta ya kilimo. Nilikwisha kushauri kwenye Bunge hili kwamba hizi Benki za Kibiashara zinafanya biashara na hazitaki kupata hasara.

Mheshimiwa mwenyekiti, sekta ya kilimo ni kati ya sekta ambazo risk iko kubwa hivyo ili kuongeza appetite ya hizi benki kuweza kukopesha wakulima ni lazima Serikali ije na bajeti na fund kuwepo na mfuko ambao risk ambayo inatokana na kukopesha sekta ya kilimo iwe inakuwa covered na hiyo fund ambayo Serikali imeiweka. Tukifanya hivyo benki zetu za kibiashara zitaongeza mikopo kwa wakulima kwa kuwa wanajua endapo wakulima wata-default mikopo hiyo kuna fund kutoka Serikalini ambayo ita-cover risk hiyo. Nilikwisha kushauri ninaomba ndugu zetu hawa Waziri wa Fedha pamoja na Waziri wa Mipango waone namna Mfuko huo unakuja ili kuongeza mikopo kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba mbili kama nilivyosema ni riba. Tunashukuru Serikali kupunguza riba kwenye sekta ya kilimo kushuka mpaka single digit asilimia tisa lakini bado tunaweza tukafanya zaidi riba ikapate kupungua benki zetu zinapata faida kubwa, tupunguze riba kwenye sekta ya Kilimo ili tupunguze gharama ya kilimo, hilo ni jambo la pili tuangalie namna tunapunguza riba kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo nataka kuchangia ni pembejeo kwenye sekta ya kilimo hasa pembejeo muhimu kama mbegu pamoja na mbolea. Watanzania wengi, wakulima wengi wa nchi wanashindwa kuingia kwenye kilimo kwa ajili ya kukosa Pembejeo muhimu haswa Mbegu. Mheshimiwa Bashe atakuwa shahidi mwaka jana msimu uliopita nilikuwa nikimsumbua sana wananchi wangu wa Korogwe Mjini ambao walikuwa wanatafuta mbegu bora za mahindi kwa ajili ya kupanda hawakupata mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali ije na mkakati ili pembejeo hizi muhimu mbolea na mbegu ziwe za kutosha nchi hii na gharama ipate kupungua lakini ushauri wangu angalau najua watu wengi wanaweza kupinga kusema gharama ni kubwa lakini nchi hii ina uwezo wa kufanya mbegu kuwa bure kwenye nchi hii, mtu yeyote ambaye anataka kulima akapate kupata mbegu bure. Kama haiwezekani basi wakati wa kilimo wananchi wakopeshwe mbegu wakati wa mavuno wapate kurudisha fedha hizo walizokopeshwa kwa ajili ya kupata mbegu. Kama hilo haliwezekani basi ruzuku kwenye mbegu na mbolea ipate kuongezeka ili gharama ya pembejeo hizi muhimu kwenye nchi hii zikapate kushuka ili gharama ya kilimo ikapate kupungua, hilo ni jambo langu la tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne la muhimu ni bima kwenye sekta ya kilimo. Watanzania wakulima ambao wamekuwa wakilisha Taifa hili kwa muda mrefu, wamekuwa wakilima bila uhakika, wanalima kwa kubahatisha, hawajui watavuna au hawatavuna. Wakulima wamekuwa wakiingiza fedha nyingi wamekuwa wanaingiza nguvu nyingi kwenye kilimo..

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa

MWENYEKITI: Taarifa

TAARIFA

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nimpe taarifa. Kwa bahati mbaya wakulima hata watakapovuna hayo mazao ambayo wamelima kwa shida, Serikali ikinunua haiwalipi fedha kwa wakati.

MWENYEKITI: Hiyo ni taarifa kweli? Endelea na mchango. (Kicheko)

MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru. Kwa hiyo nilichokuwa nataka kuongelea hapa wakulima wamekuwa wakiingiza nguvu, wakiingiza fedha kwenye kilimo lakini kukija na majanga kama wadudu, majanga kama ukame na vitu vingine wanakuwa wanapoteza kila kitu kwa kuwa hatuna bima ya kilimo kwenye nchi hii, tuna makampuni machache sana yanayotoa bima na hawa wanatoa bima ni aghari sana wananchi hawawezi ku-afford lakini watanzania wengi hawana uelewa wa jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoshauri moja ni kwamba, tuje na mikakati ambayo itasaidia kuwa na taasisi nyingi zinazotoa bima lakini bima hizo zikapate kutolewa kwa bei rahisi ili wakulima wengi wakapate ku-cover risk ambazo zinatokana na kilimo. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante kengele ya pili.

MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)