Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Tauhida Cassian Gallos Nyimbo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia bajeti yetu. Kwa namna ya kipekee nampongeza Waziri na Naibu Waziri na Mawaziri wote kwa kutuletea bajeti ambayo ni bora na nzuri, yenye majibu na matumaini kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza na Royal Tour. Tumshukuru kwa namna ya kipekee Mheshimiwa Rais wetu wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kutangaza utalii wa Tanzania. Hizi kelele zote tunazoziona zinazohusisha Longido, Ngorongoro ni matokeo na jibu la Royal Tour. Tunamshukuru kwa namna ya kipekee Mheshimiwa Rais wetu ameifungua Tanzania. Kila kona na kila milango ya Tanzania iko wazi. Tuna matumaini makubwa kuona kwamba Tanzania inaenda kufunguka.

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Royal Tour kwa matokeo makubwa yanayoenda kutokea. Utalii wetu unaenda kugusa vijana na wanawake wa Tanzania. Hii itaenda kuongeza vipato vyao na kuendelea kuongeza shughuli walizokuwa nazo. Tulitegemea kuona Watanzania, hususan Wabunge wanaowakilisha Watanzania, ambapo sisi tuliokuwemo humu ni wachache ambapo wengine hawakupata fursa ya kuwepo hapa. Pale kwenye masuala ya Kitaifa kuona kwamba tunaunga mkono Serikali yetu na kuunga mkono jitihada za Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee kabisa ambayo sijawahi kuifanya, nampongeza Ndugu yangu Mheshimiwa Kishoa kwa uzalendo wake aliyouonesha hapa. Kwenye suala la Kitaifa lazima Watanzania tuwe wamoja. Kwenye suala la maslahi ya wananchi, lazima Watanzania tuwe wamoja. Tukiungana kwa namna hii, hii ndiyo siasa inayotakiwa kuwa nayo ndani ya Tanzania. Hii ndiyo siasa tuliyoitegemea kwa miaka mingi kuiona ndani ya Tanzania. Suala la maslahi ya nchi, lazima tuungane na tuwe wamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitegemea kuona Wabunge wote tukiunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais. Royal Tour inaenda kukuza uchumi wetu, inaenda kupandisha kipato cha Watanzania. Sikutegemea kuona vikwazo. Vikwazo venyewe inabidi sasa tuwaambie Watanzania, ni vikwazo ambavyo watu wa nje wanatutumia baadhi yetu wanasiasa, wafanyabiashara na mbaya zaidi wanawatumia wananchi waliokuwemo ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, tumesimama hapa tuseme kwamba tuko pamoja na Mheshimiwa Rais wetu. Kwenye hili hatuna mjadala na mtu. Kwenye hili hatutamung’unya maneno. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa, lengo na dhamira ni moja tu, kukuza kipato cha Watanzania. Lengo ni moja tu, kukuza uchumi wa Tanzania. Kwenye hili, haturudi nyuma na hatutamwangalia mtu usoni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matamanio yetu na matarajio yetu, mambo mazuri anayoeleza Waziri Mkuu kwenye mikakati ya kupunguza watu kwenye maeneo haya, Watanzania wote wakiwa wamesikia, tulitegemea kuona wameunga mkono. Hili kwetu limekuwa ni fumbo, lakini tunasema wa kulifumbua ni sisi Wabunge. Jibu letu ni moja, tuko pamoja na Mheshimiwa Rais wetu. Tanzania kwanza, wananchi wa Tanzania kwanza, mengine yatafuata baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bajeti yetu ina mambo mengi, Serikali yetu ina mambo na mambo wanayotupangia ni mazuri. Kuna suala la wanafunzi wa Form Five na Form Six sasa kusoma bure. Kama ni Mtanzania mzalendo lazima afikirie kwamba ndani ya nchi hii ya Tanzania kuna wanafunzi walikuwa wanafaulu lakini wanashindwa kwenda kusoma kwa sababu ya vipato vya chini walivyokuwa navyo ndani ya familia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa Rais amesema watoto hawa wasome bure, sisi ni nani wa kutokumpongeza Rais kufanya jambo zuri kama hili? Tuchukue fursa hii tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa bajeti ya mfano iliyomjali mnyonge, iliyomgusa mtu wa chini. Hakuna mtu wa juu aliyeshindwa kusomesha mtoto wake. Waliokuwepo juu wengi wao watoto wao wanasoma ma-private toka Darasa la Kwanza mpaka wanamaliza wanalipia fedha. Mnyonge aliyekuwepo chini, kijijini mtoto wake anafaulu.

Mheshimiwa Spika, juzi tuliona mfano, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alimtoa mtoto kashindwa kusoma kaenda kufanya kazi, lakini akamwambia acha, njoo usome. Wako wangapi kama wale? Wanahitaji msaada; Mheshimiwa Rais amesikia, ameona, naye ni mama mlezi, tunamshukuru. Hatuna maneno makubwa ya kumpa zaidi ya ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuje kwenye suala la Shirika la Bima, Shirika letu la Taifa. Hili Shirika likionekana kwa undani ni kama limesuasua, sidhani kama lina fedha ya kutosha ya kuweza kufanya kazi, kuingia kwenye ushindani uliyokuwepo. Lazima Shirika hili liongezewe fedha liweze kuingia kwenye ushindani. Haiwezekani tunakuwa na Shirika ambalo unaliona; tatizo siyo watu waliyokuwepo pale, tatizo fedha za kuwawezesha watu kufanya kazi vizuri. Lazima Shirika liwe na fedha ya kutosha liweze kufanya kazi zake vizuri. Namwomba Mheshimiwa Waziri, nalo hili liingie kwenye suala la fedha ili liweze kupata ushindani mzuri kuweza kufanya majukumu yake vizuri.

Mheshimiwa Spika, vilevile naishauri Serikali, Shirika la Zanzibar la Bima linafanya kazi mpaka Tanzania Bara, basi nami niseme angalieni sheria, mikakati, utaratibu, nalo pia liwe na uwezo wa kufanya kazi Zanzibar. Tanzania ni moja na Watanzania ni wamoja.

Mheshimiwa Spika, nije kwenye asilimia 10 za wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum. Kwenye hili, naishauri Serikali yangu, hapa tupaache kama palivyo. Tunaposema tuchukue asilimia tano tuipeleke kwa Wamachinga, hili suala halijakaa vizuri. Ili likae vizuri, hawa watu tunaowazungumza, Wmachinga wanapatikana kwenye kundi la wanawake. Mheshimiwa Waziri wa Fedha utusikilize kwenye hili.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, hawa wanapatikana kwenye kundi la wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum. Huu mfuko haujawazuia wao kutokufanya kazi, hawajazuiliwa na wao kuingia kwenye mikopo kwa mfumo uliyokuwepo. Hebu Mheshimiwa Waziri pata muda ufuatilie huu mfuko, unafanya kazi vizuri? Kuna Halmashauri imelimbikiza fedha chungu mzima zipo, wanawake hawapatiwi mkopo, vijana hawapatiwi mikopo, sasa tunaposema tunanyofoa asilimia tano, zinabaki asilimia tano, wakati hata hizo zilizokuwepo watendaji wetu wanatuangusha, hawazifanyii kazi ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza tuangalie mifumo vizuri, tuangalie utekelezaji wake kama uko vizuri ndipo tuone tunakuja na maamuzi gani? Kwa sasa ni mapema mno na tumefanya haraka. Turudi tuache mfuko ulipo. Mheshimiwa Rais amesema zitakwenda Shilingi milioni kumi kumi, atapeleka. Vilevile kwenye bajeti yako ukurasa wa 69 imeonesha kuna Shilingi bilioni 45 ambapo zitakwenda Shilingi bilioni moja moja kila Mkoa. Nadhani bado kuna fursa na namna ya kuangalia, ile asilimia 10 iachwe kama ilivyo, iwasaidie wanawake na vijana wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii tena kuishukuru Serikali yangu kwa kutenga fedha katika bajeti kwa ajili ya vifaa tiba. Waaguzaji ni wanawake. Baba leo akiumwa muugazaji ni mwanamke, mtoto akiumwa muugazaji ni mwanamke. Tunapoona vifaa tiba vimepatikana, tunasema ahsante na tunaishukuru Serikali yetu, inatuangalia kwa jicho la kipekee, inatuangalia kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakwenda kumalizia. Kuna migogoro, wananchi wetu wanatuletea malalamiko. Mheshimiwa Waziri aangalie, kuna migogoro ya mabenki, hususan kwa wawekezaji wazalendo. Waangalieni, kweli!

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)