Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Ally Anyigulile Jumbe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, timu bora sana duniani zinazocheza mpira zina mifumo ya uchezaji mpira na mfumo mmojawapo ni 4-4-2 lakini ipo na mifumo mingine ambayo wanaibadilisha inakuwa 4-3-3 na sisi katika kujenga vijana wetu, wakina mama pamoja na walemavu tulichagua mfumo bora kabisa ambao unashinda mfumo wa 4-4-2. Mimi leo nataka nishangae wakati tunataka kushinda tunaletewa mfumo wa 5-2-2-1 mfumo huu ni wa ku-defend haujawahi kushinda hata siku moja. Maana yake ni kwamba, nasema hivi turudi kwenye mfumo wetu ambao umekuwa ukitushindia ambao umekifanya Chama cha Mapinduzi kiweze kushinda, ambao tuliwaahidi wananchi wetu kwamba tutafanya hivi ili waweze kushinda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka kusema hivi asilimia 10 ninataka nilishawishi Bunge ibaki kama ilivyo, lakini tunasema asilimia tano iende eti ikajenge miundombinu, miundombinu ipi? Miundombinu ambayo tunataka kuijenga haijatolewa ufafanuzi, lakini hata tukijenga miundombinu hivi ni lini mmachinga yaani huyu mmachinga ambaye tunamuangalia akafanya biashara ya kukaa badala ya kwenda kutembea kuuza bidhaa zake? Mimi nasema hapana, hili tuliangalie vizuri.

Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kazi nzuri inayofanywa na Waziri wetu, kwa kuhakikisha sasa hivi tunapata fedha za kulipa elimu bure kuanzia shule ya awali mpaka Kidato cha Sita. Hivi tunapofanya haya tumewafikiria watoto wa kike ambao tunataka kesho wawe wakina Mama Samia, kesho wawe wakina Tulia, kesho wawe wakina Mama Abdallah tumewafikiria ni watoto wangapi hawaendi shule kwa kukosa taulo zao za kike? Mimi nilitaka nilishawishi Bunge hili kwamba tuoneshe mfano, kwa mara ya kwanza tusimchoshe mama yetu Samia Suluhu Hassan hebu twende tuongeze katika hii asilimia 10 hata iwe asilimia 12 au asilimia 11. Asilimia moja itolewe ruzuku kila shule watoto wa kike wapate mataulo ya kike.

Mheshimiwa Spika, yaliyopo huko vijijini ni mengi unajua sisi hapa Wabunge wako tunaongea mambo yaliyoko site hatuongei mambo yaliyoko Mjini, huko site watoto wa kike hawaendi shule wengine wanafikia hatua ya kuweka mawe kwa sababu wamekosa fedha. Kwa hiyo, ninaomba hili lifanyiwe kazi na Wizara yetu ninajua ni sikivu inataka Bunge hili litoke na vitu vipya kama inavyofanya sasa. Nashukuru sana kwa usikivu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapoongelea mambo ya site ni mengi sana katika vitu ambavyo ni muhimu kwa nchi yetu pia ni viongozi wetu. Usalama wa viongozi wetu ni kitu muhimu sana, lakini tunapozungumza usalama wa viongozi wetu kuna sehemu ambapo wananchi wetu tunawakwaza. Kiongozi wetu anaposafiri au anapita sehemu utakuta atapita Saa Tano, lakini magari yanaanza kufungiwa kuanzia saa 12 asubuhi! Hili halikubaliki katika teknolojia ya sasa, hivi ni nani amewahi kufanya utafiti wa madhara yanayotokea? Kwa mfano, mtu alikuwa anakwenda Mahakamani halafu akafungiwa mnajua ni watu wangapi ambao wameshindwa kufika Mahakamani? Mimi ninaomba tutumie njia rahisi sana, kuna mambo mengi viongozi wetu wanaweza wakaenda kwa helikopta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa majuzi Mheshimiwa Nape alikwenda kwa helikopta well done! lakini viongozi wetu sisi tunao uwezo wa kufanya TEHAMA nzuri kabisa na sasa hivi kwenye mitandao tunao uwezo wa kufikia, kwa nini hazitolewi taarifa kwamba leo barabara fulani na barabara fulani hazitapitika, ili kama mtu unawahi basi mtu uanze saa 10 uwahi sehemu unayokwenda ili ikiwezekana hata wale ambao wanataka kusafiri wajiandae.

Mheshimiwa Spika, katika uchumi tunaokwenda nao, uchumi huu tunaoujenga muda ni kitu muhimu sana tusiuchezee muda. Hapa majuzi mimi nimeshuhudia tumesimamishwa round about hapo tunakuja Bungeni, tumekaa dakika 40 halafu hakuna kiongozi aliyepita magari yakaruhusiwa kweli hii ni haki? Hii siyo nchi ya kujenga uchumi ambao ni wa blabla! tujenge uchumi uliokamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mazuri sana yaliyopo kwenye bajeti hii, pamoja na hotuba nzuri sana, lakini kuna suala la pendekezo la kufuta baadhi ya vifungu vinavyoiwezesha TCRA kusimamia baadhi ya huduma na miundombinu. Hivi kwa nini tuna-rush sana kwenda huko kitu gani kinachotukimbiza mpaka tukahangaike na kubadilisha kanuni sasa? Hata ambao tunasimamia Wizara hiyo hata hatujui hivi vifungu vina-conflict gani, vina faida gani na wala hatujui ni sababu gani ambazo zinatupelekea twende tuvibadilishe. Kazi kubwa ya TBS ni ku-formulate, mimi nilidhani sasa hivi tunatakiwa tuiwezeshe TBS ilete viwango vya ujenzi wa nyumba zetu. Sasa hivi tunatumia viwango vya watu wa Ulaya, kwa mfano standard temperature ni 20 je, Tanzania standard temperature ni 20? Hivi utafiti umefanyika? ndiyo kazi ya TBS! TBS kuna sehemu tumewahi kufeli, tuliwapa wakague magari Japan hivi hilo limefika wapi? Matokeo yake Serikali imepata hasara sasa. Mimi ningeomba tusikimbilie huko Mheshimiwa Waziri, tuende tufanye mijadala ya kina na kuangalia kwa kina zaidi kuna mambo mengi. Haya mambo tunayokwenda kuyafuta ni globally harmonized, ni mambo ya Kimataifa. Wizara yetu ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeingia mikataba ya Kimataifa kwa ajili ya kusimamia haya. Mimi ningeomba hili tuachane nalo tulifanyie utafiti wa kina ili lilete tija kwa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la kubana matumizi limeongelewa sana hapa, mimi nitakuwa kinyume sana na kubana matumizi mpaka kufikia eti vikao na semina vifanyike kwa sinema Hapana! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu uchumi wake unategemea fedha za Serikali na jinsi tunavyokula maisha ndivyo mzunguko wa fedha unavyozunguka kuwafikia kila mtu. Tukisema tubane hilo Wakurugenzi wakae huko eti aje huku hatutafika popote. Haya mahoteli tunayojenga sasa hivi ambayo ndiyo uchumi lakini uchumi wa Dodoma utakufa, wanaoleta fedha ni hao ambao tunataka tuwabanie tuwaangalie kwa sinema. Lakini exposure tu DED akitoka huko anakutana na mwenzie, akifika hapa anabadilishana mawazo, anakuwa na mawazo mapya lakini pia ana-refresh. Mimi nataka kusema mlowee kwa kubana matumizi ya kuangalia semina kwenye ving’amuzi hapana, tusifike huko, tunaharibu nchi! acha watu wale maisha wapate fedha Mama amefungua zipu. Jambo kubwa hapa tumsaidie Waziri atafute vyanzo vizuri vya mapato na kuna wakati waliwahi kusema uchumi tunao lakini tumeukalia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru ulituruhusu Kamati yetu tukaiangalie barabara bora kabisa inayotoka Njombe kwenda Ludewa mpaka Manda kilomita zaidi ya 200 inayojengwa kwa zege. Barabara ile tukifikia hatua ya kwamba tunataka tuache kubana matumizi watu wale maisha nataka niseme ile barabara acha tuimalizie sasa. Ile barabara ikifika Manda itaunganisha na Itungi Port ambapo meli zikibeba makaa yatafika pale Itungi Port mpaka Manda. Manda yatabebwa kwa magari kwa barabara bora nzuri sana kabisa, lakini kule ndiko Mchuchuma na Liganga iliko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini leo hii tuache kuvuna yale makaa sasa, ndiyo uchumi ambao tunasema hebu tuende tujielekeze huko, tutafute vyanzo vizuri vya uchumi tuache haya mambo ya kubana bana matumizi madogo madogo haya ambayo hayana maana kwa kweli. Fedha yetu tunayohitaji ni kubwa matumizi tunayobana ni kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la kilimo tumefanya kazi nzuri sana na Waziri amefanya kazi nzuri sana, lakini tunakwenda kutoa zaidi ya Bilioni 900 Je, tumewaangalia Maafisa kilimo waliopo huko wanafanya kazi gani? Hivi ninavyosema inawezekana tunakwenda kutoa ruzuku kwenye mbolea lakini hata idadi (database) ya wakulima hapa hatuna! Ni sababu gani? hatujawaangalia Maafisa Kilimo waliopo mimi nataka kusema tuweke maafisa kilimo walio bora ili waweze hata kusimamia haya tunayoyasema yaweze kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe mfano mwingine, kuna suala la kilimo cha umwagiliaji hapa tumezungumza lakini kuna mradi mkubwa ambao siuoni popote. Wizara ya Mambo ya Nje siuoni, Wizara ya Fedha siuoni, Wizara ya Kilimo siuoni, Wizara ya Maji siuoni ni ule wa Songwe River Basin ambao unakwenda kufanya kazi kubwa. Nataka niseme Mheshimiwa Waziri hebu liangalie hili ni Dola Milioni 577 zinahitajika, ili watu wa Kyela walime mpunga kwa kumwagilia ili kule kuwepo na mambo ya umwagiliaji mazuri.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii, naunga hoja mkono. (Makofi)