Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo ili kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/2023. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara hii kwa namna ambavyo wamekuja na bajeti inayolenga kutatua kero za wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wapo waliojadili kutaka kuifanya hii bajeti isionekane kama ni ya kulenga kero za wananchi, lakini nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Serikali, hawajafikia viwango vya bajeti hii. Hawajaonesha vyanzo mbadala, wanaizungumzia bajeti hii kwamba ni bajeti ambayo wanaishangaa, lakini wamefeli mapema kwa sababu hawana mbadala wowote. Nakumbuka nyakati zake Mheshimiwa Waziri alivyokuwa Mchumi Daraja la Kwanza aliwahi kuchanachana bajeti za aina hiyo. Nimpongeze na nasema kwa maoni yangu hii ni bajeti ya aina yake kwa sababu zifuatazo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza, sijawahi kushuhudia Bajeti Kuu ya Serikali ikionesha ongezeko la zaidi ya bilioni 660 kwa sekta moja ya kilimo, sijawahi kushuhudia kwa vipindi viwili. Sijawahi kushuhudia Bajeti Kuu ya Serikali ikiongeza bilioni mia moja kwenye ukomo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, sijawahi kuishuhudia. Sijawahi kushuhudia Bajeti ya Serikali ambayo imeonesha jitihada zote; kwanza, kubana matumizi na pili, kuwaondolea wananchi hali ngumu za kiuchumi ila ni bajeti hii. Sijawahi kushuhudia bajeti ambayo inategemea sekta mbalimbali za uzalishaji ili kuongeza mapato, ndio naiona bajeti hii. Tulikuwa tunasema hapa wigo wa walipakodi ni wachache, niipongeze Serikali kwa kuja na mkakati wa kutoa TIN kwa kuanzia umri wa miaka 18 na kuendelea.
Mheshimiwa Spika, hapa kama Balozi wa Kodi nataka niwatoe hofu Watanzania, hata sasa si wote wanaolipa kodi. Wale wenye vipato vya kuanzia zero mpaka milioni nne hawalipi kodi yoyote. Kwa hiyo, ni wazi ambao watakuwa na TIN wasiokuwa na vipato, msingi wa kodi utabaki palepale ni kipato. Kwa hiyo, niwatoe hofu Watanzania tunaelekea kuzuri kwamba, Serikali ikifanikisha kutoa TIN kwa Watanzania takribani milioni 19, tunaweza kuongeza wigo wa walipakodi kutoka milioni tatu na kitu hadi kufikia pengine milioni 10, tutakuwa tumeleta ukombozi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, moja ya sekta ambayo inategemewa kuchangia pato la Taifa, hasa pesa za kigeni ni sekta ya utalii, zaidi ya asilimia 25 ya pesa za kigeni. Naomba nichukue fursa hii nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ubunifu wake wa kuja na Royal Tour na kipekee kwetu Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Rais alifika wakati wa kurekodi Royal Tour, lakini matokeo ya Royal Tour yamezungumzwa ndani ya Bunge na mwenye macho haambiwi tazama tunayaona, ongezeko la wageni wanaoingia ndani ya nchi, ongezeko la safari za Mashirika ya Ndege ya Kimataifa; mfano Qatar wameongeza mpaka safari 15, Emirates mpaka safari saba na mambo kadha wa kadha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niseme filamu ilionesha vivutio mbalimbali kikiwemo kivutio cha mbuga yetu ya urithi wa Taifa Ngorongoro. Hapa asubuhi zimeelezwa hoja mbalimbali, naunga mkono, ikiwemo Mheshimiwa Kishoa amesema vizuri, lakini nataka niseme yapo maeneo kwa mfano, eneo la Likongo, Lindi ambako kunatarajiwa kufanyika Mradi wa LNG, wananchi wale wametoa ardhi yao kwa bilioni tano tu fidia, hawakupewa nyumba, hawakusafirishwa, lakini wametanguliza uzalendo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo pale kwetu Bagamoyo tumetoa eneo la ujenzi wa viwanda na bandari ya kisasa. Tumelipwa tu fidia hatukupewa eneo la maisha, hatukupewa eneo la nyumba, wala maeneo mbalimbali. Hawa wenzetu wa jamii ya kimasai wamepewa upendeleo wa kipekee, lakini hii inaonesha namna gani Mheshimiwa Rais Mama Samia anajua uchungu wa mwana na uchungu wa Taifa lake na ndio maana kwa jamii ya Kimasai amefanya mambo ambayo hayajafanyika nchi yoyote ya Afrika; kulipa fidia, kuwasafirisha, kuandaa mazingira wezeshi, kuwapa nyumba, kuwapa maeneo mbadala.
Mheshimiwa Spika, mimi ambaye natoka Wilaya ya Bagamoyo nina ushahidi wa kukaa na wafugaji Wamasai maeneo mbalimbali, Mkoa wa Tanga, Mkoa wa Pwani, tuna Wamasai ambao wanamiliki ardhi. Niwaombe wakazi wa eneo la Ngorongoro kwa kuwa, Serikali imewaomba kuhama kwa hiyari na kwa kuwa eneo linalokusudiwa hapa na wanaweka beacon ni eneo la kilometa zisizozidi 1,500, niwaombe Watanzania wenzangu tuunge mkono jambo hili la utalii linaweza kuiweka nchi yetu kwenye nchi ya kwanza kwa Afrika kwa vivutio vya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa niishauri Serikali vivutio viko vingi. Kama nilivyosema Mheshimiwa Rais alikuja Mkoa wa Pwani, kwetu Pwani tunacho kivutio Saadani, mbuga pekee ambayo Wazungu wanasema where the beach meets bush ni Saadani; tunacho Kisiwa cha Mafia ambako samaki mkubwa, Papa Potwe, anapatikana duniani; na tunayo mbuga Hifadhi ya Mwalimu Nyerere. Ninachoishauri Serikali ni kuharakisha ujenzi wa miundombinu ya kufikia vivutio hivi, ujenzi kwa mfano, kufikia Mbuga ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani, tunaomba Barabara ya Mandela – Miono – Mkange ijengwe kwa kiwango cha lami ili ikutane na Barabara inayotoka Tanga – Pangani – Mkange. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kukifikia Kisiwa cha Mafia tunaomba uwanja wa ndege uwekewe taa, kwani Mafia ni ya tano kwa ubora wa fukwe duniani. Kwa hiyo, unaona umuhimu wa Kisiwa cha Mafia; kuifikia Mbuga ya Hifadhi ya Taifa ya Rufiji, tunaomba Serikali iharakishe ujenzi wa kiwango cha lami cha Barabara ya Kibiti – Mloka na Barabara ya Ikwiriri - Mloka – Mtemele. Hata hivyo, kwa sasa nishukuru kwa hatua ya Serikali ya kutenga pesa kujenga Barabara ya Ubena Zomozi – Ngerengere. Naamini itaelekea Mvuha - Kisaki na hatimaye itaingia kwenye bwawa letu ambalo tunatarajia kuwa ni bwawa la kutalii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, niungane na wenzangu, hasa Wabunge wanawake kuomba Serikali ibaki na mtazamo huu kwamba, hizi pesa za halmashauri zibaki zichangie kundi la wanawake asilimia nne, kundi la vijana asilimia nne na kundi la watu wenye ulemavu asilimia mbili. Halmashauri zetu zimetofautiana, mpango huu waliokuja nao Serikali ni mzuri, lakini uanzie na majiji makubwa yale 16. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunatambua dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kulijali kundi hili la Wamachinga pia tunaipongeza Serikali kwa jitihada zake, imetenga bilioni 45 kwa ajili ya masoko haya. Kwa hiyo, tuombe hizi halmashauri nyingine tuendelee na huu utaratibu baadaye kidogo kidogo itafanyika tathmini.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo pia, niikumbushe Serikali suala zima la biashara ya vitenge. Nchi yetu kupitia soko la Kariakoo ilikuwa inafanya biashara ya vitenge kwa kiwango kikubwa na wanawake ndio waliokuwa wafanyabiashara hawa, lakini hatua za Serikali kwa mwaka wa fedha 2021 ya kuongeza kiwango cha malipo ya container kutoka dola 0.24 mpaka dola 1.0, lakini hatimaye wakapunguza mpaka dola 0.8 na kulifanya container kuwa na gharama zaidi ya milioni 300, imewafanya akinamama kushindwa kufanya biashara hiyo na hatimaye leo Kongo au Kariakoo imehamia Uganda, Kariakoo imehamia Tunduma na Kariakoo imehamia Kenya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo wafanyabiashara hawa wanaenda kununua vitenge nchi za jirani na wanarudisha hapa. Tumepoteza kiwango cha zaidi ya bilioni 204. Niiombe Serikali kupitia Mamlaka ya TRA irudishe kiwango cha kawaida ili vitenge hivi viingie hapa nchini, lakini hata hivi ambavyo vinazalishwa hapa ndani ya nchi pia, najua nia ya Serikali ya kuvilinda viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa, naiunga mkono bajeti ya Wizara hii. Naomba tuendelee kuwahamasisha Watanzania walipe kodi. Ndugu zangu bila ya kodi mambo yote mazuri haya ikiwemo elimu bure kwa kidato cha tano na cha sita, kutenga bilioni nane kwa familia maskini, Serikali yetu inaweza kupata ugumu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana na nawapongeza sana Wizara ya Fedha. (Makofi)