Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Robert Chacha Maboto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwanza kwa kupata nafasi hii ili nami niweze kuchangia kwenye Wizara ya Fedha na Mipango. Awali ya yote namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya kwa ajili ya Taifa letu. Suala la bajeti yetu ya nchi 2022/2023, imeenda mpaka shilingi trilioni 41. Fedha hizi, shilingi trilioni 41, kuna fedha ambazo zinakwenda kwenye Wizara ya Kilimo na Chakula.

Mheshiiwa Spika, juzi wakati Wizara ya Kilimo inawasilisha bajeti yake hapa nilitoa mchango wangu na nikashauri kwamba ikiwezekana Wizara ya Kilimo na Chakula ijiweke tayari au ijipange ili kutuwekea akiba ya chakula nchini takribani miaka miwili.

Mheshimiwa Spika, bajeti yetu hii ili iwe imara, na iwe yenye uhakika, lazima wananchi wetu wawe na uwezo wa kupata chakula; na nchi kama nchi iwe na uwezo wa kujiwekea akiba ya chakula kwa muda walau hata miaka miwili ijayo. Leo kukitokea tatizo la njaa kwenye nchi yetu, kwa bajeti hii tunayoipanga leo hapa au tunayoipitisha hapa leo, kukitokea njaa kwa wananchi wetu, mipango yote itakayokuwa imepangwa kutekelezwa kati ya 2022/2023 haitafanyika kwa sababu wananchi watakuwa na njaa na nchi itaingia kwa ajili ya kuwanusuru wananchi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Wizara ya Kilimo na Chakula wamepewa bajeti kubwa kwa mwaka huu, lakini bado jambo la akiba ya chakula nchini ni la muhimu sana. Tusipolizingatia hili, kuna siku Bunge litakaa, litatoa maamuzi na kupitisha bajeti, lakini katikati ya safari wakati tunaendelea kukitokea njaa kwa wananchi wetu, bajeti ile itavurugika kwa vyovyote. Leo tukipata shida ya chakula hapa, lazima mipango mingine yote ile ambayo ilikuwa inapangwa kwa ajili ya utekelezaji wa maendeleo ya wananchi kwenye nchi yetu itavurugika. Taifa litageuka kufanya na kutafuta suluhu kwa ajili ya kuwapatia wananchi wake chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Wizara ya Kilimo na Chakula jambo hili ilichukue na ilifanyie kazi. Wenzetu wa nchi za nje wamejiwekea akiba kwenye mambo yao; mafuta na vitu vingine, sisi Tanzania ardhi tunayo, mvua tunapata ya kutosha, na watu wapo. Tunakosaje kujiwekea akiba ya chakula cha nchi cha miaka miwili? Tukijiwekea akiba ya chakula cha miaka miwili, aidha miaka mitatu, yale yote ambayo tutakuwa tunakaa kwenye Bunge humu tukayapitisha, tuna hakika yatatekelezwa kwa sababu hatutapata mtikisiko katikati ya safari. Haiwezi kutokea.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni Mamlaka ya Mapato Tanzania. Mimi ni mfanyabiashara, lakini wafanyabiashara walio wengi hapa nchini kwetu sio wafanyabiashara ambao wamesomea mambo ya biashara. Sisi tunafanya biashara kutegemeana na kile ambacho umekiona kiko mbele yako, aidha kwa namna ambavyo umepata mtaji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Wizara ya Fedha kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania na kwa sababu wafanyabiashara wetu walio wengi hawakusomea mambo ya biashara, ni vizuri mamlaka ikaweka zile kodi za wafanyabiashara wazi ili kuongeza tija kwa walipakodi. Ila wafanyabiashara wale kwa sababu hawana elimu ya biashara, halafu yule anayekuja kuwafanyia hesabu ya kulipa kodi amesomea, kwa hiyo, anabaki kumsikiliza kila atakachomuamulia yeye. Wizara ikitengeneza mpango wa kutengeneza kodi ya uwazi, kwanza itawavutia wafanyabiashara wengi na kujua viwango halisi vya kodi zao wanavyotakiwa kulipa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huwa najiuliza, kwa mfano, kwenye bajeti hii ya Shilingi trilioni 41, labda fedha ambazo zinatoka kwa wafanyabiashara labda ni Shilingi trilioni 12 au 13, halafu wafanyabiashara na walipakodi wale wote ambao wanalipa, kama ni wafanyabiashara mle kwenye idadi yao, inajulikana wako wangapi? Kila mtu analipa kiasi gani? Kama kweli tunataka kuondoa hii sintofahamu iliyopo kati ya wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato, pangewekwa utaratibu kila mmoja akawa anajua kodi yake atakayoilipa kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, wakati mwingine linatolewa jedwali tu ambalo linamwonyesha Maboto mwaka huu fedha zitakazotakiwa kuchangia kwenye kodi ya Mamlaka ya Mapato ni kiasi fulani kwa mwaka, na ikishatolewa hiyo hakutakuwepo na mazungumzo tena na mtu mwingine. Watu wa Mamlaka ya Mapato watabaki kuja kukaa kufuatilia namna ya ulipaji wa zile fedha ambazo zimetolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili linapoachiwa tu kwao wenyewe wakaenda kuzungumza na watu ambao wao kwenye biashara wameingia tu kufanya biashara, jambo hili wakati mwingine linaleta sintofahamu kwa wafanyabiashara, halafu linawafanya pia nao wasione kwamba kile wanachofanyiwa ni haki kwenye kodi zile wanazokuwa wanakadiriwa.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, nataka kuzungumzia suala la madini. Jambo hili naona bado lina matatizo makubwa, kwa sababu wananchi wetu kwenye maeneo yao wanayoishi, wanakuwa ndio wa kwanza kuvumbua sehemu hii kama ina madini. Wao wenyewe wananchi wa kawaida tu, wakishavumbua lile eneo ambalo lina madini, hawa wataalam wetu wakijua kwamba wananchi wamegundua eneo ambalo lina madini, wanachokifanya ni kwenda kutafuta watu ambao wanakata leseni kwenye eneo lile, bila kuwahusisha wananchi wenyewe, wahusika. Jambo ambalo bado linaleta mgogoro mkubwa.

Mheshimiwa Spika, ukija kuangalia, kiongozi wa wasimamizi wa wachimbaji wadogo wa madini nchini, yeye mwenyewe ni mfanyabiashara wa madini, halafu yeye ndio anawasimamia wachimbaji wadogo, halafu yeye mwenyewe huyo ndio akawatafute wenye mashamba akazungumze nao. jambo hili halikai vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli kama Kiongozi wa Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini, anatakiwa atokane na watu ambao hana interest yoyote na uchimbaji wa madini ndiyo ataweza kuleta haki kati ya wenye mashamba, wenye leseni na wachimbaji wadogo. Anapewa mtu kusimamia wachimbaji wadogo aidha wenye mashamba na sehemu ya kuchimba madini ambaye yeye mwenyewe ana-interest na uchimbaji wa madini.

Mheshimiwa Spika, jambo hilo linaleta migogoro mikubwa sana kwa wananchi wetu linawafanya wao waone, wao kama raia wa kawaida wamevumbua eneo lile la uchimbaji wa madini, huyu yeye kwa sababu anakuwa yupo ngazi ya juu anakwenda anatafuta leseni anakuja kuwaambia kwamba eneo hili tulishapata leseni miaka mitano iliyopita. Wakati madini yamevumbuliwa labda zaidi ya mwaka mmoja au miaka miwili iliyopita. Sasa jambo lile linaleta mgogoro mkubwa sana kati ya wananchi na Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Spika, wale Wasimamizi wao na Viongozi wa Wachimbaji Wadogo nchini, wanasababisha migogoro iendelee kuwa mikubwa jambo hili lisipowekwa vizuri kuna siku ninaamini litaleta mgogoro mkubwa kwa sababu wale wananchi wanaona kama wananyimwa haki zao, madini ya kwao, eneo la kwao, ardhi ya kwao, Babu yake na Bibi yake wamezikwa hapo halafu leo… (Makofi)

SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa kengele la pili imeshagonga.

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)