Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Kwanza, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Wizara ya Mipango, lakini pia nampongeza sana Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuiongoza Wizara hii. Vilevile, nawapongeza wawasilisjhaji wote wawili ambao ni Mawaziri wetu, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Waziri wa Mipango kwa uwasilishaji wao mzuri na kimsingi tumeelewa ambayo wametueleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kugusia kidogo tu maeneo mawili ya kiuchumi ambayo tumeyaona katika mawasilisho yao, la kwanza ni kuhusiana na export ambapo ukisoma yale majedwali ambayo ametuonesha Mheshimiwa Waziri wa Mipango, utaona kwamba kuna mabadiliko kwa miaka 20 kuna mabadiliko ya export zetu. Kuna bidhaa ambazo zimeongezeka volume zake, lakini kuna bidhaa ambazo zimeshuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuchukulie mfano mmoja ni dhahabu. Dhahabu miaka ya 2000 ilikuwa iko chini sana, kwenye 5% hivi, lakini kwa miaka ya 2020 tunaona dhahabu imeongezeka imefikia 39%. Sasa tukija kwa upande wa zao la korosho mazao kwa ujumla lakini hasa zao la korosho utaona linasuasua na export imepungua kidogo. Hapa nataka kusema nini? Ni kwamba mifumo na testimony yetu nzuri ni dhahabu kwa sababu ukiangalia kwa mfano miaka ya nyuma dhahabu ilikuwa inauzwa kiholela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo kulikuwa hakuna takwimu zinazopatikana, lakini mapato mengi yalikuwa yanapotea hatujui kimeuzwa kiasi gani. Baada ya kuimarisha mifumo yamewekwa masoko ya dhahabu na kodi zake zimekuwa ni reasonable na kwa maana hiyo wafanyabiashara wamehamasika sana na wanapeleka bidhaa zao au dhahabu zao kwenye vile vituo vya kuuzia dhahabu na tunaona sasa exports zimepanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kushauri kwa upande huu wa exports, tuangalie mifumo, tuimarishe mifumo, lakini tufanye utafiti wa kina na kwa maeneo haya utaona kwamba hata zile nchi ambazo walikuwa ni wateja wetu mwanzoni, kuna wateja ambao tumewapoteza lakini tumeongeza wateja wapya. Kwa hiyo tunahitaji tafiti zaidi katika eneo hili kusudi tuweze kuimarisha exports zetu ambazo pia ndiyo nguzo kubwa ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee eneo la pili ambalo ni matumizi ya gesi asilia. Tuna gesi nyingi kwa takwimu ambazo tunaambiwa tuna trilioni 57 cubic feet reserve ya gesi ambazo ni nyingi sana. Sasa hivi tuna mradi ambao unataka kuanzishwa wa LNG ambao naamini kabisa tukiitumia vizuri gesi yetu tunakwenda kupanda kiuchumi, tutaboresha maisha ya wananchi kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza matumizi ya gesi, yataokoa kwa kiasi kikubwa matumizi ya fedha za kigeni kuagizia mafuta nje. Pili, itapunguza matumizi ya Serikali kwa upande wa fedha. Gharama ambazo zinatumika kununua mafuta zitapungua kwa sababu gharama ya gesi ni ndogo. Kwa mfano mmoja tu, mtu anatumia karibu Sh.80,000 kutembea kilomita 600 ambapo ukitumia Diesel kwa bei ya Sh.3,500 kwa lita unaweza ukatumia Sh.350,000 ambapo sasa utakuja kuona matumizi ya gesi ni almost robo ya matumizi ya mafuta. Hii itasaidia pia kupunguza gharama za usafirishaji na gharama za usafiri kwa wananchi wetu na itasaidia sana kupunguza gharama za maisha ambazo sasa hivi wananchi wetu wanalalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kidogo upande wa afya. Naishukuru sana Serikali, tuna miradi 49 ya afya kule Mtwara inayoendelea, lakini nashukuru tumepata MRI na tumepata CT scan katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Kanda ya Kusini na tumepata digital x-ray, tunaendelea vizuri, lakini tuna tatizo moja, vifo vya wanawake. Kule Mtwara vifo vya wanawake kwa mwaka jana, mwaka huu wa fedha 2022/2023 ni 84 kati ya vizazi hai 39, ambapo ukipiga average kati ya vizazi 100,000 utakuta kwamba ni juu ya ile average ya Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa namna ya pekee kabisa Serikali ituangalie kule Mtwara, watuletee Madaktari au wataalam wa afya kwa sababu tuna upungufu wa 69% ya wataalam wa afya. Kwa hiyo, naomba sana pamoja na yote ambayo Serikali imefanya tupatiwe wataalam wa afya na hasa wakunga. Wakunga ni muhimu sana katika kutatua tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo suala la mazingira, tuna usafirishaji wa makaa ya mawe ambayo yanatokea Mkoa wa Ruvuma, yanasafiri kwa Bandari ya Mtwara. Tunapata adha kubwa sana, vumbi lile lina athari kubwa sana kwa afya za wananchi. Naomba tena, nilishawahi kuomba humu ndani, tuna taarifa kwamba kuna ujenzi wa bandari ambao unakaribia kuanza. Bandari ambayo itashughulikia usafirishai wa makaa ya mawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ule usafirishaji uzingatie basi kuwekwa kwenye makasha ili kusudi kuzuia lile vumbi wakati wa usafirishaji barabarani. Hata wakati wa kupakua ule mzigo na kupakia kwenye meli shida ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kidogo suala la tembo ambalo tumesikia mauaji ni mengi sana. Naomba nishauri kidogo, tuweke mpango mzima wa kutumia drones ili kufukuza tembo …

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante, mwandikie Waziri.

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)