Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi pia kuweza kushiriki kuchangia katika mpango huu. Natamani leo nitumie nafasi yangu vizuri kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo amefanya kazi nzuri sana ya kuleta fedha nyingi kwenye mikoa yote na hususan kwenye Mkoa wangu wa Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona ambavyo madarasa mengi yamejengwa, vituo vya afya vingi vimejengwa. Kiukweli ukiangalia unaona kabisa ile ni nguvu ya ziada ambayo Mheshimiwa Rais anastahili pongezi, lakini pia katika barabara tumeona ametoa fedha nyingi kwa majimbo yote ambazo ni fedha nyingi kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kama ni kufanya kazi Mheshimiwa Rais Mama yetu Dkt. Samia anajitahidi sana. Pia, amshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuweza kuanzisha dry port katika Mji wetu wa Tunduma, Mkoa wa Songwe. Tumeona kuna hatua ambazo zinaendelea. Kwa hiyo nisipotumia nafasi hii kumshukuru nitakuwa simtendei haki yeye pamoja na timu yake nzima ambayo wanaratibu suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kama dry port ikijengwa pale Mpemba tutaongeza wateja wengi wanaotumia bandari yetu ya Dar es Salaam lakini pia barabara zetu hazitaharibika. Pia, ajali zinazotokea katika ukanda huu wa barabara ya Tanzam zitapungua sana. Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha ujenzi wa barabara nne katika Mji wa Vwawa, Tunduma ambapo mkandarasi yupo na wanaendelea na utaratibu. Kwa hiyo, hili pia natumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais, sitaacha kumshukuru kwa ruzuku aliyoweka kwenye mbolea. Bado tuna-appreciate kwamba alitusaidia sisi kama wakulima. Mkoa wa Songwe una wakulima wengi sana. Natumia forum hii pia kumwomba kaka yangu Bashe atusaidie kwenye suala la pembejeo za mbegu na viuatilifu pamoja na viua magugu na viua wadudu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama ilikuwa ni kubwa sana na tuliweza mbegu feki nyingi kiasi kwamba katika mikoa hii ambayo inazalisha mahindi wananchi wengi waliingia hasara. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Bashe aangalie ni namna gani ambavyo atafanya kuhakikisha wananchi mwaka huu hawatumii mbegu ambayo ni feki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza kusema kwamba Serikali yetu imekuwa ikiendelea kufanya kazi nzuri, tunafurahi, lakini kumekuwepo na maboma mengi ambayo wananchi wanajitolea kufanya kazi; wanafanya wanayajenga yanachukua muda mrefu kumaliziwa. Nawaomba Mawaziri wetu wenye dhamana ya afya, hususan TAMISEMI watusaidie kuhakikisha maboma haya yanaisha. Yamekuwa ni kero na wananchi wanapoteza ile morale ya kujitolea kujenga maboma mapya katika maeneo mengine. Kwa hiyo, hilo pia namwomba Mheshimiwa kaka yangu Mchengerwa aweze kuliangalia na kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitakuwa sijajitendea haki nisipozungumza suala la maadili, shule zetu nyingi hazina walimu wanawake. Nimefanya ziara kwenye Kata 30 katika Mkoa wangu, changamoto niliyoikuta ni shule nyingi za msingi na sekondari walimu hawapo. Mfano mzuri niliukuta katika Shule ya Kanga katika Wilaya ya Songwe. Walimu wapo 22 halafu walimu wanawake wapo wawili na ile shule takwimu inaonyesha mabinti ni wengi kuliko watoto wa kiume. Kwa hiyo, kwa hili pia namuomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana Kaka yangu Mchengerwa waangalie namna ya kuwa na distribution nzuri ya walimu wanawake, kama hawapo basi ufanyike mkakati maalum wa kuajiri walimu wanawake ili waweze kusaidia ku-maintain maadili katika shule zetu ambazo zina watoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kabla sijachangia mchango wangu namuomba Dada yangu Ummy, Waziri wa Afya, alinipa miezi sita ya Sera ya Lishe na katika mpango huu niliposoma sijaona sehemu inayoeleza suala la lishe. Namuomba anisaidie suala la lishe liweze kukamilika, Sera ya Lishe ni muhimu kwa Taifa hili kwa sababu hali ya utapiamlo katika nchi hii haijakaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa narudi katika mchango wangu ambao nilidhamiria siku ya leo, niongelee masuala yanayohusu fedha zinazoletwa katika maeneo yetu. Tunajua Serikali inajitahidi kutenga fedha nyingi na inajitahidi kutoa maelekezo ya fedha nyingi iende kwenye miradi ya maendeleo. Wanatenga hizo fedha na wao wanaleta hizo fedha kwenye maeneo yetu, tunawashukuru sana. Kwa hili kwa kweli Wizara ya Fedha wamekuwa waaminifu kuleta fedha kwenye maeneo yetu. Nampongeza Mheshimiwa Mwigulu kwa hili wanatutendea haki sisi kama Wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inayokuja kujitokeza katika maeneo yetu ni kwamba kumekuwa na usimamizi duni wa hizi fedha kwenye maeneo yetu. Ninarejea kwenye kipengele cha udhibiti wa matumizi ya fedha katika huu mpango ambao Mheshimiwa Waziri ametupatia. Anasema fedha zote kutumika kwa wakati, kumekuwa na miradi ambayo inavuka mwaka wa kwanza, mwaka wa pili, mwaka wa tatu tunamuomba Mheshimiwa Waziri na timu yake waangalie namna njema ya kufanya hii miradi isiweze kuvuka muda mrefu na wawe wanaibainisha tuwe tunaiona ili tujue kwamba ni miradi gani imekuwa sugu haitekelezeki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachokuja kusikitisha ni kutoa fedha sawa katika maeneo tofauti lakini maeneo mengine miradi inaisha na maeneo mengine miradi haiishi. Maeneo mengine wanaongeza fedha nyingi juu yake wakati maeneo mengine unakuta hawajaongeza hata fedha kidogo. Natamani iwe hivi, kwenye kudhibiti fedha zetu hata ongozeko linaloongezeka liwe na uwiano. Haiwezekani uniambie wewe Halmashauri yako Engineer alikosea estimation kwa kiwango hicho mpaka wewe uwe na ongezeko kubwa namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona nilivyopita kwenye miradi mbalimbali katika ziara yangu. Unakuta shule inajengwa kunakuwa na ongezeko la zaidi ya shilingi milioni 150, sasa unajiuliza hivi hiyo shilingi milioni 150 ina maana kweli Engineer alikosea kwa kiwango hiki? Kwa hiyo na hili namuomba Mheshimiwa Waziri aweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ombi maalum kwa hawa Wakaguzi wa Ndani (Internal Auditor), hawa watu wanahitaji kujengewa uwezo wa kina, kwanza ni wachache. Mimi nashauri katika maeneo yetu, Halmashauri zetu, Wakaguzi wa Ndani waongezeke. Mbali ya hivyo watengewe fedha ya kutosha kuweza kuzunguka kwenye hiyo miradi zaidi wapatiwe vifaa vya usafiri ikiwa ni pamoja na magari ili waweze kufika maeneo hayo ya ukaguzi na kuweza kujua value for money ya hela zetu inakuwa ikoje.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia nasema hivi, force account imekuwa ni kichaka cha uharibifu wa fedha zetu. Miradi mingi iliyotekelezwa kwa force account ni dhaifu na fedha nyingi inaharibika.

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naunga mkono hoja.