Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na mimi kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja hizi tatu za CAG zilizoko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naunga mkono hoja za Kamati zote tatu na pia naunga mkono mapendekezo yote ambayo Kamati hizi tatu zimependekeza.

Mheshimiwa Spika, hii Taarifa ya CAG, CAG mwenyewe anasema ukaguzi anaoufanya kwa sasa, ni kwa asilimia 16 peke yake. Waheshimiwa Wabunge, haya ambayo tunayaona na tunayasikia ni kwa asilimia hizo peke yake, wakati atakapokuja kufika kwa asilimia 50 hali itakuwaje? Kama hii ni 16% peke yake ukaguzi huu alioufanya haya ndiyo tunayaona, akija kufika asilimia 50 hali ya nchi yetu itakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo amekuwa akipeleka fedha nyingi katika Halmashauri zetu. Wabunge wengi nilivyokuwa nawasikia wakichangia, hakuna mtu anayekataa force account. Hapa Kamati tumesema na tumetoa mapendekezo kwenye Kamati ya LAAC lakini fedha hizi zinazokwenda miradi mingi iliyopo ya force account haina ubora. Hata kama imekamilika mingine ukipita madarasa yana nyufa, madirisha hayafai, ceiling boards ni za hovyo, kuna vitu vinavyotendeka kule ni vya ajabu kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi naomba niseme, hakuna aliyekataa suala zima la force account lakini mimi binafsi nilikuwa kwenye Kamati ya LAAC na nimeshawahi kutembelea miradi mbalimbali, ipo Halmashauri moja ambayo sisi tuliietembelea, wanasiasa miongoni mwetu tunasababisha ubadhilifu wa hizi fedha kwenye maeneo yetu baadhi ya maeneo. Kuna hiyo Halmashauri na nimpongeze huyu Mkurugenzi wala sitamtaja, baada ya kuona sintofahamu ya hizi fedha wanasiasa wameingia humo, watendaji wanagambana, Mkurugenzi huyu aliamua kutafuta Mkandarasi na kukaa naye chini. Akamwambia Mkandarasi nimeletewa milioni 500, sina hela ninataka kujenga majengo moja, mbili, tatu, fedha niliyonayo ni hii hapa, angalia unaweza kuchukua mradi ama huwezi kuchukua mradi, kazi inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge kwenye Kamati tumeiona kazi inafanyika, kwa sababu Mkurugenzi huyu aliona hali inapoelekea ni mradi kutokukamilika na mwisho wa siku yeye ndiyo atakayekuwa responsible, akaamua kufanya alichokifanya. Kwa hiyo, kuna uwezekano yapo maeneo ambayo unaweza ukafanya negotiation na Wakandarasi na wakaweza kufanya kazi vizuri kama ambavyo wanafanya hawa watu wengine ambao tunasema ni wa bei nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unakuta Mkandarasi amekaa miaka mitatu, minne, mitano, hana kazi, anakuja kuambiwa kuna milioni 500 kuna Mkandarsi atakayekataa? Hayupo. Kwa hiyo, zipo kazi zinafanyika na wapo Wakurugenzi ambao wanaamua kufanya maamuzi hayo ili yeye aweze kuwa salama na zile fedha zilizopelekwa ziweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa iliyopo katika Halmashauri hizi ni usimamizi wa fedha hizi. Watu wamesema hapa, ni ukweli usiopingika fedha nyingi zinakwenda, miradi inafanyika lakini fedha nyingi zinapigwa. Watu wanakula fedha kweli kweli huku chini lakini yote hii ni kwa sababu ya usimamizi mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mnaenda Kamati mnafika mnakuta mradi, Wabunge tuliokwenda kwenye Kamati tunashangaa, timu ya TAMISEMI tuliyoongozana nayo inashangaa, timu ya Mkuu wa Mkoa tuliyonayo inashangaa, timu ya Mkuu wa Wilaya tuliyonayo inashangaa, Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi ambao ndiyo wenye Ilani na wenyewe unashangaa kwa hali ambayo tunakutana nayo kwenye maeneo hayo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, jiulize sisi Wabunge tumuulize nani? Kama wote walioko hapa na wote ambao ni wahusika wanashangaa, sisi Wabunge ambao tunatoka huko tukamuulize nani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapozungumza kuhusu suala zima la Wabunge ni kweli Wabunge tupo kwenye Halmashauri lakini siyo Wabunge wote ambao tuko kwenye Kamati ya Fedha. Hata hao walioko kwenye Kamati za Fedha tumeshaomba Bunge hili kila mara, ratiba zibadilishwe, ratiba zisiwekwe kipindi ambacho Bunge linaendelea. Ratiba nyingi zinawekwa kipindi ambacho Bunge linaendelea, kule Halmashauri kwetu kuna vikao, unaenda kule unakimbia huku, unarudi huku, jamani! Yapo mambo mengine hata Wabunge wakisema na wapo Wabunge ambao wanazungumza hapa wengine ni wenzetu Wabunge ambao ni Mawaziri. Majimbo yao na Halmashauri zao ni hovyo kweli kweli. Tumekagua tuomeona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna maeneo hizi POS…

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Hawa Mwaifunga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jesca Msambatavangu.

TAARIFA

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, nilitaka kumpa taarifa ni kweli kwamba Wabunge ni Wajumbe wa Kamati za Fedha kule, sisi tunapokea tunapitisha ile miradi lakini sisi hatuendi kusimamia mifuko ya cement inayoachwa kuoza, hatuendi kusimamia hela zimeibiwa au panajengwa vipi, wapo wataalam, ipo Serikali.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Chama cha Mapinduzi kinashangaa, chenyewe ni bosi kimeweka Serikali ndiyo contractor wa kuhakikisha anatekeleza mradi. Kwa hiyo anayeharibu ni yule contractor aliyepewa kujenga siyo sisi. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Hawa Mwaifunga unaipokea taarifa hiyo? (Kicheko)

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, usimamizi kwenye suala zima la miradi ni changamoto na hilo tulikubali. Kwanza tukushukuru na tukupongeze kwa kuamua kuboresha mambo mbalimbali kwenye hizi Kamati tatu wakati wanapokuwa wanafanya majukumu yao.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika tulikuwa tunakaa mpaka saa sita za usiku, lakini tulikuwa tunataka kuhakikisha tunapokuja na taarifa tuje na taarifa inayokamilika. Ni kweli kuna mambo ambayo tayari yanafanyiwa kazi, mengine tayari hatua zimeshachukuliwa lakini tulikuwa tunapata changamoto kubwa sana. Unakuta kuna Mkurugenzi amefanya ubadhilifu wa hali ya juu baada ya taarifa ya CAG ya Mama aliposema, Mkurugenzi huyu kashachukuliwa hatua, ameshapelekwa kwenye Muhimili mwingine unakuja hapa unataka kuhoji ujue nini kilichoendelea humpati yule mwizi. Unampata mtu mwingine ambaye hawezi kukueleza chochote ambacho kimeendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiyo nayo pia ni chagamoto na ni tatizo ambalo tulikuwa tunakutana nalo. Kitendo cha kuongezea muda Kamati hizi kimesaidia kuweza kuhoji Halmashauri nyingi kwa wakati mmoja, kiasi kwamba tumegundua Halmashauri nyingi zina mambo mengi kwa sbabau haziitwi na Kamati ya Bunge kwa muda mrefu hivyo kupelekea mambo mengi zaidi kuharibika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninakupongeza lakini pia tunaendelea kuomba utusaidie hizi Kamati ziweze kufanya kazi zake kwa ufanisi kwani mambo yaliyoko huku chini na hizi Kamati ikiwepo Kamati ya LAAC ndiyo Kamati ambayo ina TAMISEMI kwa wananchi na wananchi hao ndiyo wanaitegemea Serikali iweze kufanya mambo mazuri.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)