Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia katika Bajeti Kuu. Kwanza, naipongeza Wizara kwa kuandaa bajeti ya wananchi na kwa mara ya kwanza katika nchi hii tunapata bajeti ya kijamaa, lakini nasikitika kwamba Waziri wakati anakuja kuiwasilisha ile bajeti hakuja kijamaa lakini nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nataka nianze na Bandari, bandari ni mlango ambao tumepewa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya sisi kutokupata shida, uwekezaji wa bandari kwa mwaka jana tu Mheshimiwa Rais Samia wakati anaingia madarakani kulikuwa kuna mradi pale ulikuwa unahitaji shilingi bilioni 210, baadaye mwezi Desemba ikatolewa shilingi bilioni 290, tukapata shilingi bilioni 500 katika kutengeneza kupanua bandari.

Mheshimiwa Spika, bandari ndio mlango pekee ambao unatakiwa kutusaidia kupata fedha nyingi, kwa mfano kwa mwaka huu tunapata Trilioni Moja na katika hiyo Trilioni Moja ambayo tunakuja kuipata katika bandari kwa magati 12 tu, sasa tukiangalia nchi ambazo zinatuzunguka, tukiwaangalia Kenya, wenzetu Kenya wanajenga bandari ya pili Lamu ambayo itakuwa ina magati karibu 40, wana bandari yao ya Mombasa ina magati 25, leo tuna mtu mwingine ambaye ni mshindani wetu Beira ana magati 17 anapanua magati Sita kupata 23. Pia tunae mshindani wetu mwingine wa nne ambaye sisi tunamuona siyo mdogo ni mkubwa ana magati 52 Durban.

Mheshimiwa Spika, sasa ukichukua wenzetu wanapakua meli za kutosha, kwa mwezi Mombasa anapata meli kama 240 kwa siku anapata meli sita hadi nane. Dar es Salaam tunapata wastani wa meli mbili au tatu kwa siku, sawa na wastani wetu sisi ni meli 60 hadi 70 kwa kipato cha Trilioni Moja. Wenzetu Bandari ya Beira wanapata meli nne hadi tano, wenzetu Bandari ya Durban wanapata meli kuanzia10 hadi 15 kwa siku.

Mheshimiwa Spika, sasa tunakwama wapi Mheshimiwa Waziri? Ni kwamba tunao uwezekaji wetu Kwala kutoka Dar es Salaam kwenda Kwala ni kilometa 90, lakini Kwala kama tutasafirisha reli yetu hii tuliyonayo ambayo siyo ya mwendo kasi, hii reli yetu tu ya Mjerumani tuliyoirithi, kutokea Dar es Salaam tukaweka vichwa vipya vikachukua yale makontena kutuletea Kwala kwenye eneo ambalo limekwenda kuwekezwa na Bandari ni hekta kama tano ambalo linaweza likakaa na makasha kontena zaidi ya 3,600, bandari inakuwa wazi tunapata nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri hapa leo mimi naomba nikushauri nachukua ndani ya Katiba Ibara ya 72 inasema Kazi ya Mbunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali, leo pokea ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umeniteua kuwa Balozi wa mafuta nitakuja kwenye mafuta leo nipo kwenye bandari halafu nitakuja kwenye mafuta. Sasa kule Kwala nakushukuru mmetenga eneo la kuwapa wenzetu Warundi mmetenga eneo la kuwapa Wazambia, Wakongo, mmetenga eneo la kuwapa Wanyarwanda na Waganda, sasa…

SPIKA: Mheshimiwa Tabasamu, hiyo mmetenga unaniunganisha mimi na nani?

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nasema Serikali.

SPIKA: Maana wewe unazungumza na mimi na kama unasema Serikali sema Serikali imetenga.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga.

SPIKA: Mheshimiwa Tabasam kwa sababu ukisema mmetenga na Spika wako unamuweka huko, maana wewe unaongea na mimi hapa.(Kicheko/Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru endelea kunilinda.

Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga eneo kwa ajili ya kuwapa wenzetu sehemu ya kushushia mizigo na hiyo itakuwa fursa kupakuwa mizigo mingi, sasa kwa hatua hiyo mwendelezo wa lile eneo la Kwala toka mwaka 2017 eneo linatengenezwa haliishi, na kutokea Vigwaza kwenda kule Kwala ni kilometa 15, kutokea Ruvu kuja Kwala pale ni kilometa moja na nusu. Reli tayari imeshatengenezwa pale, kwanini kunakuwa kuna mlundikano wa makontena Dar es Salaam tunashindwa kushusha mizigo kwa wakati? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, meli ukipita nenda kule Sea Cliff, ukiwa eneo la Msasani Dar es Salaam unaona meli zimefunga gati kule, zile ni demurrage charges tunapata hasara Watanzania. Kwa mfano, meli ikisimama kule kwa ajili ya kushusha mafuta demurrage charge peke yake tunapaka kwa mwezi Bilioni Mbili, Bilioni 24 tunapoteza kwa ajili ya demurrage charge. Bilioni 24 ukizipigia hesabu kama Kituo cha Afya kimoja kinajengwa kwa Milioni 500 angalieni Billioni 24 tunapoteza vituo vingapi vya afya. Leo bado Waziri unakwenda kuchukua asilimia tano kwamba uitoe kule wakati kuna fedha tunakaba hapo bandari tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa hatua hiyo ni kwamba tukiimarisha bandari yetu, tukawekeza katika bandari kwenye mifumo na teknolojia pale bandarini, tutashuka hadi reli 300 kama leo meli 70 tunapata Trilioni Moja, kwanini tusishushe meli 300 tukapata Trilioni Nne. Naomba Waziri wa Fedha uzingatie jambo hili tukiwekeza katika bandari tunaweza kufaulu, na hizi kodi ndogo ndogo zinatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niongelee kuhusu suala la ushindani. Suala la ushindani kama wenzetu wana magati mengi kiasi hiki hatutaweza kuja kupata hizi fedha, tuangalie nafasi yetu ya kusafirisha haya makasha, tufanya haraka kwa ajili ya uwekezaji wa Kwala, tukiifungua Kwala bandari itakuwa wazi, tutaweza kushusha mizigo yetu vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo bandari ina miaka 75 imeanzishwa mwaka 1947 lakini leo bandari zinazoanzishwa mpya zinatuzidi sisi wenye miaka 75. Pale bandarini kuna mifumo 36 yaani uki-log ili utoe kontena mifumo 36 unaingia kwanini usiwe na mifumo mitatu, huko na kwenyewe tunakwenda kuvujisha pesa. Tunakuomba ukija kwenye majumuisho yako utueleze lini Mheshimiwa Waziri utarejekebisha hilo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la mafuta. Kuna bwawa la kushushia mafuta kule Kigamboni - Mji Mwema, wanaita SPM. Bomba lile lipo tunaweza tukashusha mafuta pale metric tani 120,000 lakini tukilisogeza mbali kidogo tu kwa kilometa mbili meli itakayoweza kushusha pale ni meli ambayo inaweza ikabeba metric tani hadi tani laki tano za mafuta. Tunaweza tukachanganya mafuta ya petroli na dizeli tuweke la pili litakalopakia petroli kwa sababu ndani kule Kurasini meli zinazoingia kule ni metric tani 39 zina oda moja ya mafuta inatolewa Tanzania vimeli vidogovidogo vya metric tani 40. tender moja inatoa meli nane, lazima wananchi wanakuja kuumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri uliniteua mimi kuwa Balozi wako wa mafuta, hebu tukae tuongee sasa na mimi nitakuletea na watu wengine tuje tukae tuzungumze tunaumizwa wapi kuhusiana na suala la mafuta, ukiniita tukaja na hao wanaokataa kwamba hatuumii katika mafuta, tuje kwenye mjadala wa Kitaifa kimya kimya tu utaona tunaokoa hizi fedha nyingi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu TPDC ukiona watu wanapinga TPDC isiwezeshwe ujue hao ni maadui wa Taifa hili. Yapo makampuni duniani makubwa ngoja, nivae miwani naona hata macho sioni vizuri sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika kuna makampuni kwa mfano kama Abu Dhabi kuna kampuni inaitwa ENOC - Emirates National Oil Company ni kampuni giant kampuni kubwa kuna ENOC kuna Malaysia wale wanajiita PETRONAS kuna Saud Arabia ARAMCO kuna SONATRACH ya Algeria, kuna kampuni ya Nigeria inaitwa NNPC kuna Oman OTI, kuna Urusi wanajiita Rosneft, lakini wapo wale mpaka Brazil. Brazil wana kampuni kubwa za mafuta ambazo zinafanya kazi zote. Mheshimiwa Waziri, Kampuni hizo zinatafiti mafuta, kampuni hizo zinasafirisha zinauza, sasa sisi tunafeli wapi kuiongezea mtaji?

Mheshimiwa Spika, leo TPDC inaidai TANESCO Bilioni 552 hiyo ilikuwa hadi mwezi wa Machi, hadi leo kama deni lile bado linaendelea kwa Bilioni 50 kila mwezi leo limefika Bilioni 700, hivi tunavyozungumza na wewe kama wataiwezesha TDPC tunatoka,. (Makofi)

SPIKA: Muda umeisha Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, naomba dakika moja nizungumzie Hazina tu tuwasaidie kuwafungua TPDC naomba.

SPIKA: Sekunde thelathini.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, ahsante TPDC Mheshimiwa Waziri ni kwamba…

SPIKA: Ongea na mimi Mheshimiwa unavyomwongelesha Waziri ndiyo maana muda wako unaenda haraka zaidi.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Mheshimiwa Spika, kuna TIPER, TIPER kule tumewekeza tuna asilimia 51 ya kwetu kwa ORYX lakini kuna hawa watu wa BP ambao wameuza PUMA tuna asilimia 50 ile ni mali ya Serikali, PUMA wale watu wa PUMA tunakuomba tu hawa watu wa Wizara ya Fedha, Msajili wa Hazina achukue zile hisa akamkabidhi TPDC.

SPIKA: Haya ahsante.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa mchango wangu.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)