Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kutamka rasmi kwamba naunga mkono hoja hii ya bajeti ya kufurahisha.
Nakushukruu sana kuniruhusu na mimi nichangie hoja hii ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/2023. Nianze kwanza na pongezi na shukrani. Mimi nampongeza sana Mama Samia Suluhu Hassan kwa alama nyingi alizotuwekea katika Jimbo langu la Tabora Kaskazini. Niruhusu nizitaje baadhi ya alama ambazo kila mtu anaziona na ndiyo maana ninasema Mama Samia tunamuona kila siku Jimbo la Tabora Kaskazini. Mama Samia hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna miradi ya maji Ziwa Victoria Vijiji 58 vitapata maji kutoka Ziwa Victoria kutoka kule Mwanza hadi Tabora Vijijini tuna maji, pia umeme tulikuwa hatuna sasa tunavyo vijiji 41 umeme unawaka tunamshukuru Mama Samia. Kuhusu afya tulipewa fedha za kujenga zahanati Nne tumejenga tatu na moja inaendelea kujengwa, pia vituo vya afya vitano tayari vitatu, bado viwili vinaendelea kujengwa kikiwemo kile cha Marehemu Benjamini Mkapa pale Usagali. Tunampongeza sana Mama Samia Suluhu Hassan, pia tumejenga hospitali kubwa ya Wilaya hongera sana Mama tunakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhsuu elimu, sawa tuna elimu ya bure kuanzia darasa la kwanza hadi Form Six, tuna kuunga mkono na tunampongeza sana Mama Samia Suluhu Hassan, lakini pia tumejenga madarasa 17 ya shule za Sekondari na shule mbili shikizi, tunampongeza sana Mama Samia Suluhu Hassan. Pia tunayo shule mpya inayojengwa tumepewa Milioni Mia Nne itakayoitwa Almas Maige kule Gilimba tunampongeza sana Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan. Pia kipo kituo cha VETA ambacho kimegharimu karibu Bilioni Mbili kinakaribia kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa niende kwenye bajeti, kabla ya bajeti kuna barabara sita zinajengwa kwa fedha ya bajeti iliyopita, kuhusu bajeti ya sasa tunao pia utawala bora ambao tumejengewa jengo la Halmashauri ya Wilaya jipya kabisa Shilingi 1,750,000,000.
Mheshimiwa Spika, kuhusu bajeti ya sasa Serikali inatakiwa ipongezwe sana na wananchi, tumeona kwamba bajeti ni ya wananchi kwa sababu imeongeza fedha za sekta ya kilimo kutoka Milioni 254 mpaka Milioni 954 hii haijapata kutokea, na sisi tumeona kwa sababu asilimia 75 karibu ya Watanzania wote ni wakulima bajeti hii imewagusa wakulima moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa nina ushauri wangu ninaomba Serikali ifanye jukumu kubwa sana la kufanya kilimo cha umwagiliaji na siyo kilimo cha mitaro, ni kilimo cha kumwagilia kwa mashine na ichimbe mabwawa au ipate maji kwa kukinga kwenye mabwawa ya mito wakati wa mvua au mito ya msimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu upatikanaji wa mbolea nashauri kwakweli turudi kama tulivyokuwa kule nyuma, tujenge viwanda vyetu vya mbolea ambavyo itafanya mbolea ipatikane kwa urahisi na kuwafikia wananchi na hasa wananchi wa Uyui.
Mheshimiwa Spika, lipo suala la ruzuku nchi zote duniani inatoa ruzuku kwa wakulima wao, tungependa pembejeo za wakulima wa Tanzania zipatikane kwa ruzuku na kwa mtandao wa nchi nzima kwa hiyo tutaongeza tija ya kilimo nchini kote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu kukuza bajeti ya kilimo hadi kufikia asilimia 10 mwaka 2030, jambo hili ni la kupongezwa na Serikali itilie mkazo, isiwe porojo ya bajeti hii tulione linakua kila mwaka hadi mwaka 2030 tupate asilimia 10 ya Bajeti ya Kilimo iwe sawa na asilimia 10 ya bajeti ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu uchumi wa Bluu, tuna bahati kubwa ya kuwa na mito na maziwa mengi sana lakini bahati mbaya sana hatupati faida ya uchumi wa bluu na hapa ninapendekeza kuwa moja, tumekuwa tunaongelea bandari ya Bagamoyo ipo haja ya kusema sasa tunaijenga hiyo bandari ili iweze kuwa kitega uchumi chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono mawazo ya Serikali katika bajeti hii ya kujenga Bandari ya Bagamoyo, lakini pia tunaomba uendelee ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kule Lindi ili tuweze kupata mazao ya uvuvi kutoka meli mbalimbali ambazo zitatua pale.
Mheshimiwa Spika, lipo pia suala la kufufua TAFICO, TAFICO lilikuwa ndiyo shirika kubwa linalotengeneza faida hapa Tanzania tukaliuza, sasa nimeenda kutembelea juzi TAFICO unaweza ukalia hakuna chochote, lakini Serikali ina nia ya kufufua TAFICO ninaiomba Serikali yangu iweke nia ya kuweka fedha za kutosha ili TAFICO ilete faida hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika bajeti iliyopita tulikusudia kununua meli nane lakini mwaka huu bajeti imepungua kutoka meli nane hadi meli mbili, hata hivyo ninaipongeza sana Serikali kuwa na wazo la kununua meli za uvuvi mbili. Ahsante sana naipongeza sana Serikali.
Mheshimiwa Spika, suala kubwa la mwisho niliongee kwa kituo ni kuhusu kodi, wigo wa kodi ni mdogo sana, watu Milioni Tatu tu ndiyo wanaolipa kodi nchi hii katika watu Milioni Sitini, wigo huo hautoshi! Yapo maeneo mengi ambayo najua kwamba yakifanyiwa kazi yanaweza kuingiza fedha na wananchi wakalipa kodi. Kwa mfano, Sekta ya ulinzi binafsi hapa nchini ilianza na makampuni mawili sasa ina makampuni 3,500, imeajiri watu chungu mzima askari, kama ingesimamiwa vizuri kama ambavyo Serikali inasimamia SUMA guard wanapatiwa kazi lakini pia wanalipa kodi na kwa kufanya hivyo kama sekta ingesimamia Makampuni yote 3,500 tungepata fedha nyingi sana lakini hatuwezi kusimamia sekta ya ulinzi binafsi kama hakuna sheria wala GN ya kuanzishwa kwa sekta ya ulinzi binafsi. (Makofi)
Kwa hiyo, nashauri Serikali sasa ije na nia bora ya kuleta Muswada wa Sekta ya Ulinzi Binafsi hapa Bungeni ili iweze kuundwa mamlaka ya kusimamia makampuni haya ya ulinzi ya sekta binafsi ambayo itazaa hela nyingi na itakuwa chanzo rasmi cha mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nikushukuru tena na naunga mkono hoja kwa mara ya pili. (Makofi)