Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Nashukuru kwamba mapendekezo ya bajeti yametambua kabisa kwamba kipaumbele ni sekta za uzalishaji, mimi nitajikita kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba changamoto ya ajira Tanzania ni changamoto inayofahamika na ni changamoto ambayo haiwezi kumalizwa kwa mwaka mmoja. Pamoja na kwamba tumeona kwamba fedha imetengwa kwa kiasi kikubwa kwa sasa imeongezeka kwenye bajeti ya kilimo, lakini kwenye Serikali yetu kutenga ni jambo moja na fedha kupelekwa ni jambo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia leo kwamba kilimo kikawe mbadala au kikapunguze changamoto ya ajira lazima tuachane na utaratibu wa kilimo cha msimu kwa kutegemea mvua, lazima tuelekeze fedha na mitazamo kwenye utaratibu wa umwangiliaji, namaanisha nini? Leo tunachangamoto ya mafuta, tuna changamoto pia ya mazao tunajua msimu wa safari hii siyo mzuri sana, lakini Mungu ametujalia tuna Maziwa Makuu. Haya Maziwa Makuu tunayategemea kwa ajili ya uvuvi peke yake wakati pale tunaweza kuyatumia kwa kuchukua hayo maji yakatusaidia kwenye kilimo cha umwagiliaji, badala ya kulima alizeti mara moja kwa mwaka, tunaweza kulima zaidi ya mara tatu tukijipanga. Kwa hiyo, badala ya kufikiri tu ndani kumaliza changamoto ya mafuta wakati tuna changamoto ya ukali wa maisha tunaweza kutumia mbadala kwa sababu tumepata mafuta ya kutosha ya kupikia, tukauza yakaja kupunguza ukali wa maisha kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nijikite zaidi kwa sababu tumeamua kujiwekeza kwenye kilimo lazima tuje na mkakati wa ziada wa kumaliza changamoto ya mbolea ambayo inawakumba wakulima walio wengi.

Mheshimiwa Spika, unapozungumzia ruzuku kabla hujapeleka ruzuku lazima ujue mahitaji ya mbolea kwenye Taifa ni kiasi gani. Msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022, makadirio yalikuwa ni tani 698,000, lakini hadi Machi zilipatikana tani 480,000, sawa na asilimia 69 peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba nia asilimia 69, lakini katika hiyo asilimia 69 uzalishaji wa ndani ilikuwa ni asilimia 6.0 peke yake. Waziri anapokuja anataka kulinda viwanda vya ndani vinazalisha kiasi gani na mahitaji ni kiasi gani. Changamoto ya hapa ya kwanza tuna taasisi ya kwetu wenyewe ya Serikali ya kuagiza mbolea TFC, TFC ina hali mbaya sana, ina changamoto kubwa mbili; changamoto ya kwanza ni suala la mtaji na changamoto ya pili ni madeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ili twende kwenye malengo na matarajio ambayo tumejiwekea ya kufanya mapinduzi makubwa kwenye kilimo ni lazima tuwezeshe taasisi hii, TFC inadaiwa bilioni 15 na taasisi za kifedha tofauti tofauti, TFC inadaiwa na taasisi za kifedha lakini makampuni ya waagizaji wa mbolea, lakini pia inadaiwa na watoa huduma. Wakati huo TFC inadaiwa lakini bado TFC yenyewe inadai na hapo unazungumza suala la management, ni suala la usimamizi mbovu wa shirika hili.

Mheshimiwa Spika, madeni yaliyopo ambayo TFC wakiamua kuchukua hizo fedha wanaweza kumaliza badala yake Serikali ijikite kuwapa fedha ili wajiendeshe kibiashara. Ruzuku ni bilioni tano ambayo wanadai na Serikali haijapeleka, lakini vyama vya ushirika vinadaiwa bilioni tatu, wadaiwa binafsi bilioni tisa. Hili jambo halihitaji muujiza, linahitaji uthubutu wa wale waliopewa dhamana. Vyama vya Ushirika vipo vinafanya kazi kila siku, ni suala la usimamizi wa waliopewa dhamana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mazingira hayo ambayo yamejitokeza kwenye hili shirika, Mheshimiwa Waziri kama tunataka kuwasaidia vijana wetu waingie kule lazima tujue kwamba sisi hatuna shida ya ardhi, ardhi ipo hatuna shida ya nguvu kazi, shida iliyopo ni namna gani tumeamua kwa dhamira ya dhati kuwekeza kwenye kilimo. Nataka kushauri mambo kadhaa, huko nyuma tulikuwa na mfumo wa uagizaji wa mbolea kwa pamoja. Mfumo uliopo leo hata tukiweka ruzuku haiwezi kuwa suluhisho la changamoto ya mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa kwanza lazima turudi kwenye mfumo ule, kwa sababu walikuwa wanaweza kununua kiwandani badala ya kwenda kwenye soko la dunia. Leo ukizungumzia bei ya tani moja kwenye soko la dunia ni Dola 800 mpaka 1,000 kwa tani, lakini kiwandani ni Dola 300 mpaka dola 400. Lengo ni kuwasaidia wakulima na kama lengo ni hilo lazima turudi kwenye mfumo ambao unakwenda kuwasaidia Watanzania ambao ndiyo tunaamini asilimia 70 ni wakulima ambao watakwenda kuinua na kuleta mapinduzi ya uchumi kwenye nchi yetu. Serikali wasikwepe waende wakalipe madeni, walipe hili shirika fedha, walipe hayo madeni kisha lijiendeshe kibiashara, hapo tutakuwa tunakwenda kutafuta suluhisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ajili ya muda naomba niende kwenye suala la ukali wa Maisha. Natambua juhudi za Serikali ambazo zimefanyika kwenye ile fedha iliyotolewa, lakini ile fedha imetolewa tulikuwa tunalenga ikamsaidie nani? Tulilenga ikamsaidie mwananchi wa kawaida kabisa, lakini pamoja na fedha hiyo kuwekwa kwenye mafuta, bei ya nauli haijashuka, bei ya gharama vifaa vyovyote vile ambavyo vinakwenda kwa wananchi wa chini haijashuka, tulikuwa tunataka kuwasaidia wamiliki wa magari au tulitaka kuwasaidia wananchi wa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili kwenda huko lazima tujikite kuondoa tozo ambazo tunaamini hizo ndizo zinapelekea bei kubwa ya mafuta. Kwenye petroli peke yake kuna tozo ya shilingi 920, dizeli 813, mafuta ya taa 577, pamoja na mazingira yote yale kwa kuwa Serikali imeonyesha nia ya kwenda kupunguza ukali tujikite kwa suluhisho la kudumu, siyo la muda mfupi, lazima tutafute suluhisho la muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda na haya mambo tumeshazungumza sana, naomba niende kwenye suala ambalo Serikali imechukua kuondoa ada kwa kidato cha tano na cha sita kwa maana hiyo kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha sita elimu itakuwa bila ada, Wabunge lazima tujue siyo elimu bila malipo ni elimu bila ada. Tunashukuru kwa hatua ya awali ambayo Serikali imechukua, lakini changamoto ya wazazi ambayo inawakumba huko siyo ada peke yake, changamoto kubwa ni utitiri wa michango iliyopo kwa hao wanafunzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua kuwekeza kwenda kulinda ndoto za watoto wetu wa Kitanzania na kama hiyo ndiyo nia ya Serikali pamoja na kwamba tunakwenda kumsaidia huyu mtoto kwa kuondoa ada. Naomba nizungumzie hakuna kitu ambacho hata wafanyabiashara wanawekeza ili wapate faida Serikali imeamua kuwekeza kwenye elimu ili kuwalinda wototo wakiwemo watoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na nia njema wote tunajua kwamba mahakama ilishatoa hukumu juu ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, ilitoa na ikatoa mwaka mmoja sasa ni miaka mitatu. Tunamshukuru Mungu leo Rais tumempata ni mwanamke na Spika wa Bunge ni mwanamke, wote tunaamini ndoto ya mtoto wa kike, jambo hili litakwenda kupata suluhisho kipindi hiki, naamini ndiyo dream yangu. Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama mahakama imeamua na sote tunajua kwamba mahakama ndiyo chombo cha mwisho na lengo letu ni kumsaidia mtoto wa kike, najua kwamba Serikali ina nia njema ndiyo maana imeondoa ada, sasa hiyo nia njema ionekane kwa dhamira njema ya kumaliza kuondoa hiki kifungu cha 13 na cha17 ili kumlinda mtoto huyu wa kike wa Kitanzania tuwapate akina Samia wengi, tuwapate akina Tulia Ackson wengi na akina Aida wengi ili na wao waweze kuweza kufanya kazi ambayo sisi tumeianzisha, kwa kuwa lengo ni kumlinda mtoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ajili ya muda naomba nizungumzie suala la asilimia 10. Lengo la asilimia 10 ilikuwa ni kwenda kuwasaidia wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. tunahitaji fedha ziongezeke badala ya kuwakopesha watu milioni tatu. Tulitegemea leo Mheshimiwa Waziri wa Fedha aje na utaratibu wa kwenda kuwapatia watu fedha, kufungua viwanda awape milioni 100 kwamba baada ya mwaka mmoja tuone wanawake waliokopeshwa mwaka jana sasa wanaweza kama walikuwa na mtaji wa milioni 10, wanaweza kuwa na mtaji wa bilioni. Hatuwezi kufikiri kurudi nyuma lazima tufikiri kusonga mbele, badala ya kuindoa hiyo asilimia tano, haisaidii chochote. Tunataka fedha ziongezeke kwa sababu mahitaji ni makubwa. Wanawake wapo tunawaona wanavyofanya kazi na wote hapa tunajua kwamba umesema wamekuwa ni waaminifu kurejesha, kama ni waaminifu tukaongeze fedha tuwasaidie wanawake wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)