Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Omar Ali Omar

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Wete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa jioni hii ya kuchangia katika bajeti yetu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nataka mchango wangu niuelekeze zaidi kwenye lugha ya Kiswahili. Nianze kwa maneno aliyoyazungumza Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania. Mwalimu alizungumza kwamba Uhuru wa Tanganyika ulichochewa sana kwa kutumia lugha hii ya Kiswahili. Kwa hiyo, uliharakishwa kutokana na kutumia lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo, lugha ya Kiswahili ilisaidia sana kupata uhuru wa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 1962 lugha ya Kiswahili iliamriwa kwamba ni lugha ya kutumika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwaka 1964 lugha ya Kiswahili ndiyo ilitangazwa rasmi kwamba ni lugha ya Taifa. Kwa hali hiyo basi, lugha ya Kiswahili ni moja katika lugha ambayo tunatakiwa Watanzania tuienzi, tuitukuze na tuhakikishe kwamba tunaitumia ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi nyingi za Ulaya ikiwemo China, Korea, Uturuki na kadhalika, zimepata maendeleo makubwa kwa sababu ya kutumia lugha zao. Sasa sisi Watanzania bado hatujajikita kutumia Kiswahili kama ni lugha yetu ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawapongeza sana tena sana Wizara ya Katiba na Sheria kwamba wameanza angalau kuonesha mwanga kwenye hukumu wanazozitoa kwenye Mahakama. Ila ni jambo la kushangaza, Wizara mama ya Elimu ambayo ina mitaala ya kutosha, ina uwezo wa kubadilisha kuitumia lugha ya Kiswahili katika shule zetu za sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli hili linahuzunisha sana, kwa sababu hata somo la historia jamani! Hata somo la historia ya nchi yetu tunalizungumza kwa lugha ya Kiingereza! Lugha ya Wakoloni ambao wametutawala kwa sababu ya kuitumia lugha yao? Ukitaka mtoto ajisikie katika nchi hii, basi azungumze Kiingereza. Ila ukitaka aonekane kadhalilika, basi azungumze lugha ya Kiswahili. Hii ni kuonesha kwamba lugha yetu ya Kiswahili bado hatujaipa kipaumbele katika kuhakikisha kwamba lugha hii ndiyo lugha halisi tunayotakiwa kuitunza na kuhakikisha kwamba tunaitumia ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna wataalam wengi wamezungumza lugha ya Kiswahili. Kama mtunzi mmoja Ibrahim Hussein, alizungumza katika tamthilia yake ya “Mashetani” kwamba Tanzania tunajiamini kwamba mkoloni katuachia kisu sasa, na kisu kile ndiyo tunachotumia kujikata sisi wenyewe. Siku zote tunaona kwamba lugha ya Kiswahili ndiyo lugha ambayo inaweza kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waingereza hao hao wanasema don’t bite the hand that feeds you. Usiule mkono unaokulisha, ukiula mkono unaokulisha utakulia nini? Naomba sana lugha ya Kiswahili itumike kwamba ni lugha ya Taifa kweli kweli na tuhakikishe kwamba vizazi vyetu tunawarithisha lugha yetu ya Kiswahili kwa kuitumia ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niende kwenye ukurasa wa 75 ambapo Mheshimiwa Waziri wa Fedha alizungumza juu ya mkakati wa uchumi wa bluu. Ni dhahiri kwamba Tanzania tuna watu ambao wanategemea sekta ya uvuvi wasiopungua milioni tano. Watu hawa wote wanategemea sekta ya uvuvi, lakini uvuvi huu unategemea vyombo vinavyohusika kwenda bahari kuu. Ni-quote speech moja ambayo aliitoa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Spika, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alisema kwamba kipindi cha miaka mitano, mwaka 2020 Novemba 15, alisema maneno haya yafuatayo: Kwamba, kipindi cha miaka mitano sekta ya uvuvi itakuzwa ikiwemo uvuvi wa bahari kuu kwa kununua meli nane zitakazofanya kazi katika ukanda wa Pwani ulioko Zanzibar na Tanzania Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiyo haitoshi. Mheshimiwa Waziri katika bajeti iliyopita ya 2021/2022 aliizungumza kwa kinywa kipana kwamba tunanunua meli nane za uvuvi. Naomba atakapokuja Waziri, atueleze, hizi meli nane zilipotea wapi kwenye bajeti hii ikawa haionekani? Hazionekani kabisa, wala hakuzungumza kwamba kutakuwa na meli nane zitakazofanya shughuli za uvuvi. Angalau angesema kwamba tushanunua meli mbili zimebaki sita, lakini hata moja hajaizungumza katika bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee katika kilimo cha mwani. Mikoa inayozalisha mwani kwa Tanzania Bara haipungui minne; Lindi, Mtwara, Mkoa wa Pwani, Mafia; nadhani ni mikoa hiyo. Kwa Tanzania Visiwani, Zanzibar, karibu mikoa mitatu inazalisha mwani ikiwemo Mkoa wangu wa Kaskazini Pemba.

Mheshimiwa Spika, asilimia 90 ya wanawake wanajishughulisha na kilimo cha mwani. Ni masikitiko makubwa sana kwamba wanawake hawa wanadhalilika mpaka sura zao zimebadilika, nywele zimenyonyoka vichwani kwa kushughulikia kilimo cha mwani. Nadhani hata kiwanda kile cha kutengeneza nywele bandia kinaweza kikajengwa Pemba sasa, kwa sababu nywele hazimo tena kwa kilimo cha mwani. Zimepotea kabisa kwa sababu ya kilimo cha mwani. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini? Ni kwa sababu mwani haujapewa kipaumbele na nchi yetu. Kilimo cha mwani kinasaidia sana kukuza uchumi wa wanawake nchini, lakini changamoto kubwa ni jinsi bei zinazopangwa na mashirika yanayonunua mwani. Mashirika haya yote, hakuna ambalo linawaonea huruma wakulima wa mwani. Maana wananunua kati ya Shilingi 600/= mpaka Shilingi 1,800/=, kiwango kidogo kabisa cha fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake wakae kutafakari na kupanga bei ya mwani kama vile inavyopangwa bei ya korosho, kahawa, karafuu kwa kule Zanzibar na maeneo mengine. Hii itaweza kuwakomboa wanawake wabaki salama kwenye mwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyo, mwani huu tunauuza sisi kama malighafi. Inakera sana. Tanzania ni nchi ya viwanda, ina uwezo wa kujenga viwanda vidogo vidogo, lakini mpaka sasa hivi hakuna kiwanda hata kimoja kinachochakata mwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwani unatusaidia sana kwa kutengeneza mboga mboga, mwani ni chakula, mwani tunatengenezea mafuta, lakini hutoamini rasilimali inayotoka kwenye mwani. Mwani unatengeneza mpaka hii mitambo yetu wanaume tunayoitumia inatokana na kilimo cha mwani. Hii ni kuonesha kwamba mwani kumbe una faida kubwa kwa nchi yetu. (Makofi/Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Omar, hoja ya msingi sana hiyo, dakika moja malizia muda wako umeisha. (Makofi/Kicheko)

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante. Penye watu wazima wengi hufahamu lugha nzuri. Mitambo ya wanaume mnaijua, na mkifanya mchezo basi wanaume tunaweza tukapoteza mabibi zetu kwa sababu ya mitambo haifanyi kazi kutokana na kwamba hatuutumii mwani vya kutosha. Kwa hiyo, mwani una faida kubwa na tuendelee kuutumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi/Vicheko)