Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, nitaanza mchango wangu kwa kuzungumzia suala la usimamizi wa fedha za umma. Kama kuna jambo ambalo inabidi tuliangalie kwa makini na ikiwezekana tulifanyie mabadiliko ni muda ambao CAG na Bunge tunautumia katika kufanya ukaguzi, kujadili na kuchakata hizi taarifa za ukaguzi na hatimaye kutoa maelekezo na maagizo kwa Serikali juu ya matumizi yasiyofaa kwa fedha za umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali ilivyo sasa, kuanzia mwisho wa mwaka wa fedha tarehe 30 Juni, muda ambao Wakuu wa Taasisi, Maafisa Masuuli wamepewa kuandaa taarifa za mwaka na baadaye kuziwasilisha kwa CAG na CAG anazikagua na halafu anawasilisha taarifa kwa Mheshimiwa Rais na baadaye Bungeni; baada ya hapo, Kamati za Bunge za LAAC na PAC zinajadili na baadaye taarifa zinaletwa Bungeni, Bunge linajadili na kutoa maagizo juu ya mambo yaliyopatikana, tunatumia miezi 17.

Mheshimiwa Spika, huu ni muda mrefu mno, kwamba fedha za umma zimetumika na mtu ambaye ametumia vibaya fedha za umma anakuja kujua kwamba ametumia vibaya na maagizo yanatoka baada ya miezi 17. Muda huu ni mrefu mno na kuna haja ya kufanya mabadiliko. Maafisa ambao sio waoga wanakuwa na ujasiri wa kufanya matumizi mabaya ya fedha za umma kwa sababu wanajua mpaka aje agundulike na maelekezo yatoke ni miezi 17 ambao ni muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali ilivyo sasa ni kwamba mwaka wa fedha unaisha tarehe 30 Juni na baada ya hapo, Sheria ya Ukaguzi wa Umma kifungu cha 31 kimewapa Maafisa Masuuli wa Taasisi zote za Serikali miezi mitatu kuanzia tarehe moja Julai mpaka tarehe 30 Septemba kuandaa hesabu za mwaka ili wazipeleke kwa CAG kukaguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hali ilivyo sasa ya kiteknolojia, taasisi zote za Umma zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa zinafanya transactions zote za kifedha kwenye mifumo. Kama ni makusanyo ya mapato, kwa mfano, Mamlaka za Serikali za Mitaa kama ni makusanyo ya ushuru wa mazao, ushuru wa masoko, ushuru wa stendi, yote yanafanyika kwenye mifumo. Kama ni malipo ya wakandarasi, wazabuni, yote yanafanyika kwenye mifumo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tujiulize, kwa hali ilivyo sasa, pengine hii Sheria ya Ukaguzi wa Umma ilitungwa wakati hii miamala inafanyika manually kwa mikono, lakini kwa hali ya kielektoniki ilivyo sasa, kuna haja gani ya Afisa Masuuli ambaye amemaliza mwaka tarehe 30 Juni, kuna haja gani ya kumpa miezi mitatu yote hiyo kufunga hesabu? Wakati sasa hivi kwa mifumo ya kihesabu iliyopo kwenye taasisi za umma unaweza ukafunga hesabu za mwaka kwa siku mbili tu au siku moja, is a just ku-press burton tu. Kwa hiyo, hakuna sababu yoyote kwa level ya teknolojia iliyopo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuipongeza Serikali kwa kuboresha mifumo, na sasa hivi taasisi zote zinatumia mifumo. Kwa hiyo, hakuna sababu yoyote ya Maafisa Masuuli kupewa miezi mitatu kufunga hesabu za mwaka, ni muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri wangu kwenye eneo hili ni kwamba tubadili kifungu Na. 31 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ambacho kinampa Afisa Masuuli miezi mitatu, turudishe mpaka angalau mwezi mmoja, ingawa najua hata siku mbili zinatosha kuandaa hesabu ambazo zimeandaliwa kwenye mfumo, lakini tumpe mwezi mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi baada ya miezi mitatu, taarifa ikifika kwa CAG anatumia miezi sita kufanya ukaguzi mpaka mwishoni mwa mwezi Machi ambapo ndiyo anakabidhi taarifa kwa Mheshimiwa Rais na baadaye inakuja Bungeni. CAG sasa hivi amewezeshwa na naipongeza Serikali kwamba imeji- commit kumwezesha na kumpa fedha. Kwa hiyo, akiwa na workforce ya kutosha na mifumo mizuri ya kufanya ukaguzi, hana haja tena ya kutumia miezi sita, anaweza kutumia miezi mitatu na kufanya ukaguzi na baada ya hapo kwa Mheshimiwa Rais na baadaye Bungeni na Kamati zetu za LAAC na PAC kuweza kuchakata na baadaye kujadiliwa na kutolewa maagizo ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mapendekezo yangu ambayo yatapunguza hii process kutoka miezi 17 mpaka miezi nane, ni kwamba tubadilishe kifungu cha 31 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma, Maafisa Masuuli wapewe mwezi mmoja badala ya miezi mitatu, CAG apewe miezi mitatu badala ya miezi sita na taarifa ije Bungeni na immediately LAAC na PAC waanze kukagua na maagizo yatoke. Kwa hiyo, tutakuwa tunatoa maagizo kwa muda wa miezi nane badala ya miezi 17 ya sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza bajeti hii kwa kuongeza bajeti ya kilimo. Sisi Wabunge tunaotoka vijijini shughuli yetu kuu ya wananchi wetu ni kilimo. Kwa hiyo, kuongeza bajeti kutoka Shilingi bilioni 294 mpaka Shilingi bilioni 954 ni jambo la kupongezwa na hapa nawapongeza sana. Shilingi bilioni 150 ya ruzuku ya mbolea itakwenda kuwasaidia wakulima wetu kupata mbolea hii kwa bei nafuu na kuongeza tija ya kilimo chao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nimeliona ni mapendekezo ambayo yamo kwenye hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri ambayo yamependekeza kubadilisha kifungu cha 6(1) ambacho kinapendekeza kuhamisha majukumu ya usimamizi wa mifumo ya mawasiliano kutoka TCRA kwenda TBS.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuwa Mbunge mimi nilikuwa mtumishi wa Airtel ambayo ni Kampuni ya Simu. Ushauri wangu hapa ni kwamba jukumu la kusimamia mifumo ya mawasiliano libaki TCRA na kama kuna maboresho yanahitajika, basi yafanyike huko huko TCRA badala ya kupeleka TBS. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niungane na Waheshimiwa Wabunge, hotuba imezungumzia kuwezesha kampuni zetu binafsi ili ziweze kushindana na kampuni nyingine kwa mfano Shirika la Bima la Taifa ambalo linashindana na kampuni nyingine binafsi za bima, liwezeshwe kimtaji na kiuwezo kwa maana ya watumishi ili Shirika hili la Bima la Taifa liweze kutoa huduma za tija ambazo zinaweza kushindana na kampuni binafsi na hatimaye kuweza kutoa huduma za kiufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono uamuzi wa kufuta ada Kidato cha Tano na Kidato cha Sita, jambo hili litapunguza mzigo kwa wazazi ambao wanahangaika sana kuhakikisha kwamba watoto wao wanapata elimu ambayo inahitajika sana, pia naungana na Wabunge wote ambao wamependekeza asilimia 10 ibaki vilevile ilivyo, labda kama yatatoka maelekezo ya kutosha lakini kama yalivyo kwamba asilimia tano zitumike kujenga miundombinu ya ujasiriamali, kwa tunaotoka Halmashauri za eneo kubwa la vijiji ambavyo viko mbalimbali hoja hiyo haiwezekani kabisa. Kwa hiy,o tunashauri asilimia 10 zibaki kama zilivyo na ikiwezekana hata ziongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nipongeze pia Serikali kupandisha bajeti ya mifugo na uvuvi, wote tunafahamu kwamba mwaka huu ambao tunamaliza tulikuwa na Bilioni 168 lakini tunakwenda kupata Bilioni 268.

Mheshimiwa Spika, nakushuru naunga mkono hoja asilimia 100, ahsante sana.