Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Lindi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa uwasilishaji wa bajeti yake ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo imeelekeza nguvu kubwa katika sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, nishati lakini kutekeleza miradi ya kielelezi, tunajua ya kwamba Serikali ina lengo kubwa la kukuza uchumi lakini hatimaye kukuza ajira katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuridhia kutekeleza mradi mkubwa wa LNG lakini kwa kuridhia kusaini mikataba kwa wabia wetu kwa makubaliano yale ya awali. Wananchi wa Lindi tumepata faraja kubwa sana na tumepata matumaini makubwa ya kutekelezwa kwa mradi mkubwa ambao utanufaisha Taifa letu katika kukuza uchumi, lakini katika kukuza ajira katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, tuna kila namna ya kuhakikisha kwamba tunaendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu kwa yale mema mazuri anayotuletea kwa faida ya Taifa letu. Katika mkutano wa kusaini mkataba yako maagizo ambayo Mheshimiwa Rais aliyatoa, naomba niwakumbushe watakao simamia katika utelekezaji.
Mheshimiwa Spika, katika agizo lake la kwanza alisema kwamba wahakikishe kwamba barabara zinaboreshwa katika eneo la mradi wa LNG, katika agizo lake la pili aliagiza ujenzi wa hospitali za kisasa katika eneo la mradi. Ninashukuru ya kwamba Manispaa yetu ya Lindi tuliiongeza baada ya kupata fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, tulielekeza moja kwa moja ikajengwe katika eneo hili la Kata ya Mbanja kule Kikwetu ambako mradi wa LNG utatekelezwa.
Mheshimiwa Spika, pia agizo lake lingine aliagiza ujenzi wa shule nzuri za kisasa lakini na agizo la nne ni huduma ya maji kupelekwa katika eneo hili ambako mradi wa LNG utatekelezwa, mimi ninaamini kwamba Mheshimiwa Waziri wa Maji ni msikivu sana na hata hakikisha kwamba maji yanafika katika eneo la Kata ya Mbanja. Agizo lake la tano ni kuhakikisha kwamba huduma ya umeme inafika katika eneo la mradi wa LNG, pia sekta ya mawasiliano kuhakikisha kwamba mawasiliano pale yanafika na agizo lingine la mwisho ni kuhakikisha kwamba upimaji wa ardhi kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi ufanyike.
Mheshimiwa Spika, ninaishukuru sana Serikali kupitia Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kuridhia katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kupata mkopo wa Bilioni Moja katika kuhakikisha kwamba tunakwenda sasa kupima ardhi kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi na fedha hizi zimefika wakati muafaka sasa wa kuhakikisha kwamba Lindi Manispaa sasa tunakwenda kuwekeza katika upimaji wa ardhi na kukaribisha sasa uwekezaji katika maeneo ya Lindi Manispaa.
Mheshimiwa Spika, katika maeneo hayo yakuboresha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, tunazo Km. 2.4 tumefanya maombi maalum kuhakikisha kwamba kutoka barabara kubwa ya lami kwenda ilikojengwa Hospitali ya Wilaya tuweze kupata fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Km. 2.4 tunaboresha na huduma ya afya iweze kufikiwa kwa urahisi.
Mheshimiwa Spika, bado tuna ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa, nayo kutoka barabara kubwa kwenda kule ndani ni kilometa 2.5 tumefanya maombi maalumu kuhakikisha kwamba barabara hiyo inaboreshwa. Pia tuna ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Mkoa ambayo imeshakamilika tuna Km. 300 kutoka barabara kubwa ya lami kuekelekea kule kwenye Mahakama hiyo, tumefanya maombi hayo maalum kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha eneo hilo kuhakikisha kwamba wananchi wetu waendelee kupata huduma bora lakini tuhakikishe kwamba uwekezaji huu wa mradi mkubwa wa LNG tunakwenda nao sambamba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufuta ada, kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wenzangu wameongelea kuanzia Darasa la Kwanza, Form Four, Form Five mpaka Form Six ni jambo jema sana kuhakikisha kwamba watoto wetu sasa wanapunguziwa mzigo wa mkubwa wa kushindwa kumaliza masomo kwa kushindwa kulipa ada, kwa hiyo mimi ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti yetu tunajua kwamba mwaka huu ni mwaka wa sensa, na muda siyo mrefu mwezi wa Nane Tarehe 23 maana yake tunaingia kwenye sensa, muda uliobakia kufanya maandalizi ni muda mfupi sana na siyo muda mrefu, tukimbizane na wakati uliobaki tuhakikishe kwamba fedha inafika kwa wakati na vifaa ili kuhakikisha kwamba tunafanikiwa wananchi wetu kuingia kwenye kuhesabiwa ili tuweze kupata takwimu halisi.
Mheshimiwa Spika, ninasema hivi kwa sababu Lindi Manispaa tumeathirika na sensa ya mwaka 2012, wananchi wengi hawakuhesabiwa tuliingia kwenye matatizo makubwa na ndiyo maana hatupati fedha nyingi za maendeleo katika eneo letu la Lindi Manispaa, kwa hiyo nina kila namna ya kusisitiza fedha pamoja na vifaa vifike kwa wakati kuhakikisha kwamba tunajipanga kuingia katika tukio hili la sensa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la haki na usalama wa raia wetu. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutuwezesha fedha zaidi ya milioni 900 kujenga Kituo cha Polisi Daraja A. Wilaya ya Lindi ina Majimbo Matatu na tulikuwa hatuna Kituo cha Polisi cha Daraja A, kwa hiyo nimshukuru kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wetu, kutuwezesha fedha hizi kujenga Kituo kikubwa cha Polisi cha Daraja A. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, licha ya hayo, bado tuna changamoto, ni muhimu sana kuweka Vituo vya Polisi kwenye Tarafa, Vituo vya Mahakama kwenye Tarafa ili iwe rahisi wananchi wetu kuweza kupata huduma hizo kwa wakati. Inapotokea kwenye Tarafa kunakosekana kuwa na mahakama, ni mzigo mkubwa na kumfanya mwananchi huyu asafiri umbali mrefu kwenda kupata huduma ya mahakama. Kwa hiyo nina hakika yako maeneo mengi ambayo hayana mahakama na hayana vituo vya polisi.
Mheshimiwa Spika, tunaona sasa hivi wezi na vibaka wamekuwa wengi sana kwa kukimbilia hatuna kwa wakati, kwa sababu vituo vya polisi vimekuwa mbali mno na maeneo ambayo wananchi wanaishi. Kwa hiyo tufanye kila namna kuhakikisha kwamba katika maeneo yetu ya Tarafa tupate vituo vya polisi lakini tuwe na mahakama zile za mwanzo kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanaendelea kupata haki na huduma huko wanakoishi bila kutembea umbali mrefu.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la TRA, suala la kulipa kodi ni uzalendo na bila kodi maana yake hatuwezi kuendesha nchi bila kuwa na mapato ndani ya nchi yetu. Hata hivyo, niseme kwamba maduka mengi ukipita kununua vifaa suala la utoaji wa risiti wa EFD machine hazipo, limetoweka kabisa. Niwaombe sana ndugu zangu wa TRA kuhakikisha kwamba wanafanya kazi kupita huko na kukumbushana na kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wanaendelea kutumia mashine hizi za EFD kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato.
Mheshimiwa Spika, tumeona changamoto kubwa ya makadirio ya viwango vya kodi, mathalani mtu ana mtaji wa milioni 50, lakini kwa mwaka mzima anapelekewa kodi ya milioni 200. Sasa unajiuliza nina mtaji wa milioni 50, nawezaje kulipa milioni 200! Kwa hiyo, kwanza nashukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameliona hili na kwenye taarifa yake ameliandika, tuhakikishe kwamba tunalisimamia suala la uzalendo ni suala muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika eneo ninaloishi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Muda umeshaisha Mheshimiwa, kengele ya pili imegonga.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nizungumzie suala la kodi ya mabasi ya abiria na malori ya abiria, hili linatupa maswali mengi.
SPIKA: Kengele ya pili imegonga Mheshimiwa.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wakati ana-wind up atuambie ni kwa namna gani tunaweza kusimamia hili kwa sababu mabasi yanatofautiana ukubwa wa mabasi na abiria na mizigo.
Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)