Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie kwenye Wizara hii muhimu ya Fedha na Mipango. Nianze kwa kusema, wakati naanza kuwa Mbunge tuliambiwa maneno yafuatayo: Ukiwa kama Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, la kwanza ni maslahi ya Taifa lako, la pili ni maslahi ya wananchi wako Jimboni kwako, la tatu ni maslahi ya chama chako, na la mwisho ni maslahi yako binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ameinuka leo Mbunge mmoja, tena Mbunge Mwandamizi ndani ya Bunge hili Tukufu akamnukuu Baba yetu wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, nami nimeona tu nimnukuu Hayati Kambarage Nyerere kwenye Azimio la Arusha la mwaka 1967. Alisema kwamba, “ili kuhakikisha kuwa uchumi wa wananchi unakwenda sawa, Serikali lazima iwe na mamlaka kamili juu ya njia muhimu za kukuza uchumi.@ Akaenda mbali akasema, “Mheshimiwa Mbunge anaposimama, (ukurasa wa 11) kuomba barabara, au shule, au hospitali, au vyote; je, Serikali ina mpango gani?” Majibu, anategemea Serikali iseme, anasema, “naye pia jibu ambalo anagependa kupewa ni kuwa, Serikali inao mpango safi kabisa wa kutengeneza barabara au kujenga shule au hospitali au vyote kwa wananchi wa sehemu Mbunge Mheshimiwa huyo na watafanya hivyo kwa kutumia fedha.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo tunajadili bajeti ya Wizara ya Fedha. Sisi Wabunge moja kati ya jukumu letu kubwa ni kuisaidia Serikali kupata vyanzo vya fedha. Tutafanya hivyo kwa namna yoyote ile ikiwa ni pamoja na kuwaruhusu wananchi wetu kuachia maeneo muhimu ambapo maeneo hayo yataipatia Serikali fedha. Sheria ya Ardhi ya nchi hii Kifungu cha 4 kinasema, ardhi ni mali ya umma na Rais ndio mwenye dhamana; na inaruhusu Rais huyo huyo kuweza kutwaa ardhi ile kwa ajili ya maslahi ya umma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunalo eneo letu very potential na nilisema humu ndani, suala la Ngorongoro atapigwa mwingine, atalia mwingine. Ngorongoro kwa mwaka 2018/2019 imeipatia Serikali yetu mapato ya Shilingi bilioni 150. Ngorongoro ndiyo urithi wa dunia. Leo wananchi wa Ngorongoro wanahamishwa kwa namna ambayo Wabunge wengi humu ndani tunaona wivu, wanahamishwa. Anasimama Mbunge anasema, wanateswa, wanaonewa.
Mheshimiwa Spika, ipo haja ya kupima uzalendo wa Watanzania ambao tunawawakilisha sisi humu ndani, tupimwe uzalendo wetu kwenye Taifa letu. Haiwezekani tuungane na raia wa kigeni kulichafua Taifa letu kwa propaganda zinazofanya tushindwe kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Watanzania tunajuana. Viingereza vyetu vya Rasi Simba, tunajuana. Leo anasimama mwanaharakati eti Mmasai wa Ngorongoro, wa Loliondo, eti mwanaharakati anaongea Kiingereza cha Malkia. Kiingereza cha ndani kabisa yaani, anasema anawatetea Wamasai wenzie wa Ngorongoro. Tanzania ni yetu, tutaachia rasilimali. Kama kwa kufanya hivyo inasaidia kujenga nchi, inasaidia kukuza uchumi, inasaidia kuongeza biashara, inasaidia kuboresha maisha ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 1999 wananchi wa Kata ya Bulyanhulu, Kakola kule, uliko Mgodi leo wa Barrick ambao sasa hivi unaitwa Twiga, walihamishwa kwenye maeneo yao, wakakiri kuhama kwenye maeneo yao. Leo wananchi mwaka 2008, 2010, wananchi wa Mgodi wa Buzwagi ambao leo ndiyo upo mgodi ule walikubali kuhama kwenye maeneo yao. Wengine mpaka leo wanadai fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama hali ndiyo hiyo, mimi wananchi wa Shinyanga wamenituma, wanamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, kauli yake aliyoitoa ya kusema anawapa pesa wananchi wa Ngorongoro kwa kuhama, anawajengea nyumba na kuwakabidhi hati, eti mpaka mtu mwenye wake wa tatu atapewa hati tatu, wananchi wa Shinyanga Mwendakulima na wenyewe wanataka hiyo privilege waliyopewa watu wa Ngorongoro. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni yetu sote. Haya mambo ya kubembelezana; Mgodi wa North Mara watu waliondolewa pale kwa mabomu. Haiwezekani leo jamii moja ya Watanzania iwe very much privileged, ionekane yenyewe ndiyo kila kitu, propaganda ziendelee kufanyika eti tunawabembeleza watu kupisha eneo ambalo ni potential, ni urithi wa dunia, eneo ambalo ni rasilimali kubwa duniani, siyo Tanzania. Tunawagopa kwa sababu ya propaganda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi wakati najifunza siasa, niliambiwa propaganda hujibiwa kwa propaganda. Hawa wanasema leo eti Mawakili, wanakwenda Mahakama ya ICC kwenda kuishtaki Tanzania kwa kuwapiga watu wanaoenda Ngorongoro, tutapambana nao Mahakamani. Wale watu wa propaganda wapambane nao kwa propaganda. Haiwezeki tukae kimya ardhi yetu inatumika vibaya, haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wa Shinyanga na sisi tunataka haki yetu. Wananchi wa Shinyanga, ilifika hatua, Kahama peke yake imekuwa ya nne Kitaifa kwa kuchangia pato la Taifa kwa sababu wananchi wa Shinyanga walikubali kutoka kwenye maeneo ya madini na kuwaachia wawekezaji ambao leo hii tunapiga kelele hapa, lakini ndiyo pesa za watu wa Shinyanga waliyotoa kwenye maeneo yao wameachia nchi inapata kipato. Nasi tunaidai haki hiyo kwa wivu mkubwa.
Mheshimiwa Spika, wanatoa sababu eti maeneo yale wameyazoea. Wale maeneo wameyazoea walikuwa wanakaa tu na kuchunga ng’ombe. Shinyanga wananchi wa Mwime, Mwendakulima, Chapua, hawana shughuli nyingine yoyote ya kuwaingizia kipato zaidi ya kuchimba dhahabu. Hawana shughuli nyingine. Ukienda Ibadakuli, Bulyanhulu, wananchi wa Bulyanhulu kule Nyangalata, Namba Tatu, Namba Nne, hawana shughuli yoyote ya kuwaingizia kipato. Asilimia 99 ya wananchi wale shughuli yao ilikuwa ni uchimbaji. Kama suala ni maeneo waliyazoea, na sisi tuliyazoea. Hoja hizi ni batili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaposimama ndani ya Bunge hili sisi kama Wabunge, kazi yetu ni kutafuta vyanzo vya mapato. Tumesikia hapa Wabunge wanasema, wale watu walikuwa wananufaika, tumeinua Taifa hili kwa sababu wanawake walikuwa wanapewa asilimia nne, vijana wanapewa asilimia nne, watu wanaoishi na ulemavu wanapewa asilimia mbili. Leo inapunguzwa mpaka asilimia mbili, mbili, moja, pesa nyingine wanapelekewa Wamachinga. Kakeki kenyewe ni kadogo, tunakagombania, watu wengine wanatetea maslahi binafsi kwenye maslahi ya umma, hiyo haikubaliki. (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Salome Makamba, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tabasam.
T A A R I F A
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, Sengerema wananchi wanaachia eneo la Sotta Mining, kaya 1,600 mpaka sasa hivi tunavyozungumza wanatakiwa kuondoka, wapishe mgodi bilioni 740. Wao siyo watu? (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Salome Makamba, unapokea taarifa hiyo.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, taarifa ya mjomba wangu Mheshimiwa Tabasam Hamis naipokea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mustakabali huo, na bahati nzuri wewe ni Mwalimu wetu mzuri sana. Kanuni za Bunge zinakataza kujadili jambo ambalo limeshajadiliwa na mjadala wake ulishafungwa. Mjadala wa Ngorongoro tulizungumza humu ndani, tukajadili na huo mjadala umeshafungwa. Naomba kwa Mwongozo wako suala hili lisisemwe tena, kwa sababu watu wameshakubali kuhama, watu wameshakubali kwenda kwenye maeneo yao mapya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasisitiza, zile ng’ombe za wale wawekezaji ambazo wameziweka kwenye Hifadhi, wale watu watoe. Nimeangalia kwenye taarifa ya Habari, zile ng’ombe mlizoziweka kwenye malori ni chache mno. Wekeni zile ng’ombe zote zilizoko kwenye Hifadhi ziende na wale watu kule Handeni. Ndiyo utajua, tangu lini Mtanzania wa kuzungumza Kiingereza cha Malkia, eti amekuwa Mmasai wa Ngorongoro, eti amekuwa Mmasai anatetea wananchi wa Ngorongoro! Hiyo haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya issue ya Ngorongoro natumai umeifunga, nami naishia hapo, sitaisema tena. (Kicheko/Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Muda umeshaisha Mheshimiwa. (Makofi)
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)