Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuhitimisha hoja ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu ripoti za CAG kwa Hesabu za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2022. Aidha, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchangia hoja hii kwa ukamilifu, weledi na uzalendo wa hali ya juu, nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jumla ya Waheshimiwa Wabunge takribani 78 wamechangia kwa kusema na wengine kwa kuandika na naomba kwa sababu ya muda nitasema tu mambo machache lakini kabla ya kuendelea nifanya masahihisho katika lile Azimio ambalo tulikuwa tumependekeza. Katika moja ya eneo ambalo nataka kufanya marekebisho kidogo ni lile eneo linalohusu zile fedha za IPTL kwenye taarifa tuliyokuwa tumesoma tulisoma bilioni 148.4 badala yake siyo bilioni tulikosea tukatumia Tshs. Ni Dola za Marekeni milioni 148.4. Kwa hiyo, naomba katika maeneo yote ya taarifa kuu pamoja na yale niliyoyasoma yafanyiwe marekebisho ili yasomeke hivyo.
Mheshimiwa Spika, katika uchangiaji, wachangiaji wamezungumza mambo mengi sana na yote kwa kweli ni mazuri na sisi kama Kamati tumeyakubali, lakini nataka nitoe ufafanuzi katika maeneo machache.
Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza Serikali kwa hatua ilizochukua katika ufungaji wa hesabu. Hapo ukizungumzia kufunga hesabu, kuzingatia Kanuni za Kimataifa za Ufungaji wa Hesabu kuzingatia Sheria na Miongozo kwenye kufunga hesabu wako vizuri sana sasa hivi. Hali ni nzuri na ndiyo maana utakuta Hati za Ukaguzi ni nzuri na zinaonesha hali nzuri. Hati za Ukaguzi Hati zenye Mashaka zimepungua kwa kiwango kikubwa, ni kazi kubwa ambayo imefanywa na Serikali tunaitambua. Sasa kupata Hati inayoridhisha haina maana kwamba huko ndani mambo yote yako safi ni bahati mbaya hatuna neno zuri la kulitumia tunatumia “Hati Safi” hakuna neno “safi”, kwa kiingereza ni unqualified opinion ni Hati Inayoridhisha, hakuna taasisi ambayo ni safi 100 percent hakuna! kwa hiyo ni Hati Inayoridhisha, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo nilitaka kuliweka vizuri kaguzi zipo za aina nyingi, hapa tunayoiwasilisha ambayo tumeifanyia kazi kwa kiwango kikubwa ni Ukaguzi wa Masuala ya Kifedha, kuna Ukaguzi wa Masuala ya Kifedha kwa mujibu wa Katiba yetu, kuna Ukaguzi wa Ufanisi ambayo ni Performance Audit Report, hizo hatujazifanyia kazi nyingi bado. Kuna Ukaguzi wa Kiufundi (Technical Audit), kuna Ukaguzi Maalum na kuna Ukaguzi wa Kiuchunguzi au tunaita Forensic Audit. Sasa Waheshimiwa Wabunge naomba muelewe tofauti ya Kaguzi zote hizo.
Mheshimiwa Spika, hapa tunachokichambua kwa leo ni ukaguzi wa kifedha kuangalia kama taratibu zilizingatiwa. CAG anapokagua kuangalia hayo, anaangalia kama kuna upungufu na anatoa taarifa mbili; ya kwanza anatoa maoni yake ambayo yapo kwenye hati ya ukaguzi. Yale ni maoni (expression of opinion on the financial statement), ndiyo hiyo ya kwanza mpaka anatoa hati.
Mheshimiwa Spika, cha pili, analeta barua inayoonesha upungufu uliopo kwenye taasisi, ambao siyo sehemu ya financial statement, lakini yale aliyokutana nayo, hayo yanakuwa kwenye kitu tunaita Management Letter na hayo ndiyo yanayotusaidia kujadili. Sisi Kamati tunapokutana, yale mazuri yote tunaya-note, lakini siyo sehemu ya ripoti yetu. Kwa mujibu wa Kanuni zetu, zinatuelekeza tujadili na tulete humu Bungeni maeneo yenye upungufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunayoyaleta hapa ndani ni yale maeneo yenye upungufu. Kama yana upungufu, nataka niseme, kama nilivyosema, hesabu zimefungwa vizuri, zimetayarishwa kwa kiwango kikubwa tu, na tukiangalia katika uzingatiaji wa taratibu za Kimataifa, kuna maeneo mawili tu yanaonekana yana upungufu kwenye Serikali. La kwanza liko kwenye upande wa Kanuni ya Kimataifa Kanuni 17 (IPSAS 17) kwenye namna ya kutambua mali za kudumu na namna za kuzifanyia revaluation ili zitumike kwenye kufunga hesabu. Hilo katika taasisi nyingi kuna upungufu.
Mheshimiwa Spika, pili, ni ku-comply na maelekezo ya Wizara ya Fedha yaliyoagiza kila taasisi inapofunga hesabu ihakikishe mali zake zote za kudumu ziko katika mfumo wa kieletroniki wa GAMIS. Nataka niseme, tulipoangalia hakuna taasisi hata moja iliyoweza ku-comply na hiyo 100 percent, zote zina matatizo kwenye hilo eneo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nizungumzie kwa kifupi sana maeneo ambayo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamechangia. Kuhusu hasara ya TANOIL, nashukuru baadhi ya Mawaziri wamefafanua. Tulichoambiwa sisi ni kwamba, kama nchi tunahitaji tuwe na shirika ambalo kama ikitokea emergency lazima liweze kufanya kazi ya Serikali. Ndiyo maana Serikali iliamua kuanzisha TANOIL. Hilo sisi hatuna tatizo nalo. Tatizo tulionalo, ni kwa nini ipate hasara? Hasara iliyoripotiwa mwaka ule na hasara itakayoripotiwa mwaka huo ambao wamefunga hesabu ni vitu viwili tofauti, sasa hivi nafikiri imekuwa ni kubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa sisi hoja yetu ni kwamba kwa nini hasara ilitokea? Wanasema hawakufuata bei zilizotangazwa na EWURA, waliweka discount. Discount ni kitu cha kawaida, kinaruhusiwa kibiashara, lakini unapoweka discount, lazima uhakikishe kwamba kweli unapata faida. Sasa hawa wamepata hasara na Serikali imekiri wamepata hasara. Kwa hiyo, hapa tunachosema ni kwamba lazima sasa tuchunguze kwa undani, hatua zichukuliwe. Hilo sidhani kama lina mjadala. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo limezungumziwa kwa kirefu sana na ninamshukuru Mheshimiwa Waziri wa Kilimo amelizungumzia, hili suala la madeni ya Mfuko wa Pembejeo (AGTIF). Bahati nzuri ameshakupa orodha, nasi tuliiomba hiyo orodha, tuliipata, na tuli-note kwamba kweli wapo baadhi ya Waheshimiwa hawajalipa. Kwa hiyo, tunachosema, Bunge lifanye uamuzi, kwa sababu zile fedha zikirudishwa kwenye ule mfuko, ule mfuko utakuwa hai, utaendelea kufanya kazi ile iliyokusudiwa. Kwa hiyo, hilo hatuna matatizo nalo.
Mheshimiwa Spika, kuna madeni ambayo yapo ambayo viongozi na Serikali imetoa ufafanuzi. Sisi tunakubaliana kama Kamati, madeni ya Serikali kwenye mifuko ya hifadhi za jamii, tume-note hatua ambazo zimechukuliwa, wamelipa; lakini sisi concern yetu tunaiomba Serikali iseme italipaje hayo madeni, na kwa kipindi gani? Kwamba kila mwaka itakuwa inalipa kiasi fulani, basi kuwe na commitment ambayo inaonekana kabisa ambayo tunaweza kuifuatilia ili ikija mwakani, tunasema Serikali ilisema itafanya hivi, haikufanya. Kwa hiyo, hilo tunadhani kwamba itatusaidia sana.
Mheshimiwa Spika, suala la riba limezungumziwa sana. Kwenye Taarifa ile ya CAG kubwa, suala la riba ni shilingi bilioni 418. Riba zinazotokana na ucheleweshaji wa mikataba mbalimbali kutokulipa, lakini tuliyoyafanyia kazi kwenye Kamati katika kipindi hiki, kumbuka Kamati inachukua ina sample, hatufanyi yote 100 percent kwa sababu ya muda. Tuliyoyafanyia kazi ni taasisi mbili tu ndio tumezifanyia kazi, moja ni TANROADS ambayo tumekuta riba kwa mwaka huo pekee yake wana shilingi bilioni 36 wanadaiwa lakini TANESCO wanadaiwa riba na kampuni ya Pan African Energy shilingi bilioni 113. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ukichambua zile nyingine na hizo taasisi ambazo hatukuzichambua, ndiyo maana CAG anasema zinafika shilingi bilioni 418. Sasa hizo fedha concern yetu sisi, ni fedha nyingi. Hizo kama kweli tunge-save badala ya kulipa riba, zingefanya kazi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, japo kuna suala la madawa, wameshaeleza na Mheshimiwa Waziri nashukuru kwa maelezo uliyoyasema. Maeneo mengi kama uzingatiaji wa sheria, taratibu, nimewasikia Mawaziri walivyosema, na mmesema mambo mengi, lakini ninachotaka niseme Waheshimiwa Wabunge, kwa michango namna mlivyochangia kwa muda wa siku hizi tatu mmeitendea haki Kamati yetu na mmelitendea haki Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, michango ni mizuri na inaleta uchungu. Tunapoona Mheshimiwa Rais anapambana huku na huko kutafuta fedha ili zitekeleze miradi, halafu nyingine haziendi kutekeleza ile miradi iliyokusudiwa, inaumiza sana. Hiyo Waheshimiwa Wabunge tume-note concern yenu na mmechangia vizuri sana. Tunawapongeza sana kwa hilo. Vile vile mmefanya jambo la Kikatiba. Katiba yetu inatutaka tuisimamie Serikal. Kwa hiyo, mlichokifanya leo ni kuisimamia Serikali, na maazimio mtakayoyapitisha ni ya kuisimamia Serikali. Kwa hiyo, naamini maazimio yatakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa maeneo mengine yote ambayo wameyasema yanayohusu KADCO, na kadhalika, kila mtu ameyasikia; yanayohusu kila taasisi, tumeyasikia. Kwa hiyo, nina imani Wabunge tutafanya uamuzi, lakini nataka nitumie muda huu kuleta kwa uchache mapendekezo ya maazimio ambayo Bunge hili sasa tunatakiwa tufikie kuamua. Mapendekezo hayo, nataka niseme mwishoni nikishamaliza kuyasema haya; nimeletewa mapendekezo na Waheshimiwa Wabunge wawili katika kuongezea maazimio ambayo tunayapendekeza kwenye Bunge. Nayo nitayatolea ufafanuzi baadaye nitakapokuwa naendelea.
Mheshimiwa Spika, naomba kwa heshima kubwa niseme mapendekezo ya Kamati kama ambavyo tunafikiria na kama ambavyo tulipendekeza. Mabadiliko ni kidogo sana.
Mheshimiwa Spika, kuhusu nakisi ya ukusanyaji wa mapato kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kiasi cha shilingi bilioni 887.3:-
Kwa Kuwa, Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini nakisi ya kiasi cha shilingi bilioni 887.3 cha mapato ambayo hayakukusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa mwaka wa fedha 2021/2022, kutokana na upungufu mbalimbali ikiwa ni pamoja na usimamizi usiokuwa thabiti wa mafuta yaliyosafirishwa kwenda nje ya nchi na kisha kutumika hapa nchini na kuchelewa kusajili mapingamizi ya kikodi;
Na Kwa Kuwa, kutokukusanywa kwa mapato hayo kunasababisha upotevu wa mapato ya Serikali na pia kunapunguza uwezo wa Serikali kuwa na rasilimali za kutosha katika kutimiza majukumu yake;
Kwa Hiyo Basi, Bunge linaazimia kwamba:-
(a) TRA ihakikishe ndani ya mwaka wa fedha 2023/2024 inakamilisha usimikaji na utekelezaji wa mifumo yote muhimu ya usimamizi wa udhibiti wa kodi ili kuhakikisha mapato stahiki ya Serikali yanakusanywa kwa ukamilifu;
(b) TRA ihakikishe kesi zote za mapingamizi ya kodi kama zilivyoletwa na walipa kodi zinashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali;
(c) TRA ihakikishe inaweka mifumo dhabiti ya usimamizi wa kodi katika michezo ya kubahatisha na mafuta ambayo yanapitia hapa nchini kwenda nchi za nje. Katika kutekeleza azimio hili, hatua kali zichukuliwe kwa wanaokiuka sheria na umma ujulishwe ipasavyo; na
(d) TRA itengeneze mfumo maalum wa kusimamia makusanyo ya mizigo, yaani ile mizigo ambayo wanatakiwa kui-consolidate (consolidators) ili kuhakikisha mapato ya Serikali yanayokusanywa kwa mujibu wa sheria yanakusanywa. Aidha, kodi yoyote ambayo ilikuwa haijakusanywa ikusanywe kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi zilizopo.
Mheshimiwa Spika, hilo ndilo azimio letu la kwanza, azimio la pili Waheshimiwa Wabunge kama mtaniruhusu linabaki kama lilivyo lile lilokuwa linahusu hasara ya shilingi bilioni 7.8 la TANOIL. Kwa sababu ya muda, kama mtaridhia kama tulivyolipendekeza awali linabaki kama lilivyo.
Mheshimiwa Spika, azimio la tatu, mapato yasiyokusanywa ya dola za Marekani 599,000 katika Wizara ya Maliasili na Utalii, linabaki kama tulivyopendekeza pale awali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la nne linahusu IPTL kutotimiza wajibu wa kimkataba na hivyo Serikali kuwa hatarini kupatiwa madai ya dola za Marekani milioni 148.4 yanayotokana na IPTL kutotekeleza majuku yake. Hili azimio kama nilivyosema pale awali, figure tulikuwa tumeandika bilioni badala ya milioni; ni dola za Marekani milioni 148.4.
Kwa Kuwa, Taarifa ya CAG ilifafanua kwamba Kampuni ya IPTL imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kimtaba kwa kinga ya kisheria iliyotoa dhidi ya madai ya Serikali;
Na Kwa Kuwa, kutotekelezwa kwa kinga hiyo ya kisheria kunasababisha Serikali kuendelea kudaiwa madai mbalimbali yanayotokana na IPTL ikiwemo madai ya Dola za Marekani milioni 148.4.
Kwa Hiyo Basi, Bunge linaazimia kwamba:-
(a) Serikali itekeleze kwa ukamalifu masharti yaliyoambatanishwa kwenye kinga ya kisheria (indemnity) iliyotolewa na IPTL dhidi ya madai yoyote ambayo yangetokea kwa Serikali baada ya kutolewa kwa fedha hizo katika akaunti ya Tegeta ESCROW; na
(b) Serikali isifanye malipo mengine yoyote kwa mshauri yanayofunguliwa dhidi ya mmiliki wa IPTL ili kutopoteza fedha za umma kwa sababu ina kinga ya kisheria kwa suala hili.
Mheshimiwa Spika, huu ndiyo msimamo ambao tunafikiri ubaki vilevile. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge hilo azimio kama mtaridhia libaki hivyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la tano ni upungufu katika utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Mwanga - Same hadi Korogwe. Hili nalo tunaomba libaki kama lilivyo. Hapa nimemsikia Mheshimiwa Waziri amezungumzia kwamba kulikuwa na special audit ilikuwa imeshafanyika. Kilichofanyika ni technical audit, tunayokwenda kuifanya ni special audit na itaambatana na forensic audit, kufanya uchunguzi. Kwa hiyo, hicho ndicho kinachoenda kufanyika. Tunaomba kama nilivyopendekeza pale mwanzoni, Kamati inapendekeza bado ibaki vilevile bila mabadiliko yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la sita, manunuzi ya mita za umeme bila kukaguliwa na Wakala wa Vipimo, tunaomba hili azimio nalo libaki kama lilivyo. Eneo la saba ni Tume ya Madini kutokusanya madeni ya kiasi cha shilingi bilioni 30.7, tunaomba nalo hilo libaki kama lilivyo. Bohari Kuu ya Dawa, tunaomba libaki kama lilivyo, tulivyopendekeza pale awali. Taarifa ya Ukaguzi Maalum kuhusu uendeshaji na usimamizi wa mikataba ya maridhiano, yabaki kama tulivyopendekeza pale awali. Taarifa za matumizi ya fedha ya mkopo wa IMF, yabaki kama yalivyo. Kutozingatia ipasavyo kwa Kanuni za Kudumu za Utumishi wakati wa mchakato wa ajira katika Benki Kuu ya Tanzania, tunaomba azimio libaki kama tulivyopendekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla niseme, mapendekezo ya maazimio tunaomba karibu yote kama tulivyoyawasilisha pale juzi yabaki kama yalivyo, isipokuwa tumepata mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge wawili. Tumepata mapendekezo kutoka kwa Mheshimiwa Ole-Sendeka na Mheshimiwa Luhaga Mpina. Sasa naomba nitoe maelezo kidogo.
Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya Mheshimiwa Mpina bahati mbaya yametufikia wakati karibu nasimama kuja huku, sasa hatukuweza kuifanyia kazi. Kwa hiyo, mapendekezo yake yote hatujaweza kuyatafakari na kujadiliana na Wanakamati wenzangu. Kwa hiyo, hiyo kidogo inanipa ugumu kuyaleta kama mapendekezo ya Kamati.
Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya mabadiliko ya hoja ambayo yanapendekezwa na Mheshimiwa Ole-Sendeka, anapendekeza kama ifuatavyo na Waheshimiwa Wabunge kama mtaridhia naomba niwasomee. Anasema hivi, “Kwa kuwa ukaguzi uliofanya na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)…
SPIKA: Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti hayo mapendekezo yameshawekwa kwenye vishikwambi. Kwa hiyo, wewe endelea na hoja yako.
MHE. JAPHET N. HASUNGA – MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI (PAC): Mheshimiwa Spika, okay, nashukuru sana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Waheshimiwa, Mheshimiwa Ole-Sendeka amependekeza azimio la kwanza, kwamba Serikali ihakikishe inaokoa fedha zote zilizobainishwa kwenye Taarifa ya CAG. Sisi kama Kamati tunaona hili ni la msingi na tunafikiri kwamba ni kitu cha msingi sana kama tunaweza tukali-adopt tunaweza kuliongezea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili anasema, Mawaziri, Makatibu Wakuu na Watendaji wote walioguswa na Taarifa ya CAG na Kamati wajitafakari kabla ya Mamlaka ya Nidhamu kuchukua hatua dhidi yao, hilo tunaliachia Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine, Bunge iunde Kamati Teule kwa mujibu wa Kanuni ya 139 ya Kanuni za Kudumu na mambo mengine yanayoelekezwa kama alivyopendekeza wakati anachangia, tumeiangalia lakini tumeiachia Bunge kwamba liendelee kutafakari.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Luhaga Mpina ameleta mapendekezo mengi, hatujayapitia, lakini nimeyapata. Kwa sababu hatujayajadili na wenzagu, naomba nisiyatamke, maadamu yapo kwenye vishikwambi, basi Waheshimiwa Wabunge watazingatia wakati wanatoa maamuzi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo na ufafanuzi huu mdogo ambao nimeufanya, kwa heshima kubwa niwaomba Waheshimiwa Wabunge, nawashukuru sana kwa michango yote na kazi kubwa mliyoifanya. Sasa naomba kutoa hoja ili maazimio haya yawe ni sehemu ya Bunge letu zima.
Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba kutoa hoja. (Makofi)