Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HALIMA J. MDEE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI ZA MITAA (LAAC): Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi niliyopata ya kuweza kufanya majumuisho. Lakini vilevile nichukue nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe/Wabunge mliochangia ambao mliochangia kwa kuzungumza ni zaidi ya 78 na wengine ambao mmechangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Spika, nitajibu hoja kadhaa halafu nitakuja kwenye Maazimio. Jambo la kwanza ambalo nilikuwa nataka kulizungumza ni kuhusiana na haja ya upande wa Serikali na watendaji kuchukulia Taarifa za CAG kwa uzito wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, umesema hapa mwezi Juni tulikuja hapa kupitia utekelezaji wa Serikali wa maagizo ya CAG. Kwa upande wetu sisi Serikali za Mitaa mpaka tunatoa taarifa hapa, kulikuwa hakuna agizo hata moja lililotekelezwa kwa ukamilifu wake. Kwa hiyo tunavyosema Serikali muwe makini tunasema muwe makini na muwe serious kwa sababu sisi tunakutana na maafisa masuuli kwenye vikao vya Kamati. Ni muhimu ikaeleweka kwamba majibu ambayo yataua ama kumaliza hoja za kaguzi siyo majibu ambayo Mawaziri mnatupa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, majibu yatakayomaliza hoja za kaguzi ni majibu ambayo Mkaguzi atayapata kwenye vikao lakini vile vile wakaja kufanya verification kwamba tumesema tumekwama hapa, Serikali mnajibu hapana hatujakwama tumeenda hapo; unayetakiwa kumpa uthibitisho ni Mkaguzi wa hiyo hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo maelezo waliyokuwa wanayatoa Mawaziri hapa na sisi ambao tulikuwepo kwenye vikao mpaka juzi, mock LAAC za mwisho kwenye LAAC, mock LAAC yaani vikao kati ya Ofisi ya CAG na upande wa Serikali vilifanyika kuanzia Oktoba 3, Oktoba 2, Septemba majibu yaliyokuja ndiyo yamepelekea Taarifa zetu hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivyo basi ndugu zangu; kama kweli tuna dhamira ya kusaidia hii nchi iende, hayo majibu mnayoyasema kwa sasa hayana maana mpaka CAG aka-verify. Kwa hiyo, ni muhimu mzingatie hilo Mawaziri na mimi kwenye Kamati yetu wamekuja Mawaziri wa TAMISEMI, wawili Naibu Mawaziri wanamuwakilisha Waziri wanakuja na Makatibu Wakuu. Kwa hiyo, ninashangaa Waziri anasimama hapa anasema yeye kwake anakuja anakuta hapa ni kitu kipya, hili ni jambo ambalo mnatakiwa mjue wote. Waziri aje na Katibu Mkuu wake aje; akituma mtu aje akupe mrejesho. Ndiyo tunasema hakuna connectivity ya kazi au utendaji kazi hakuna connection. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni bahati mbaya sana watu waliopewa dhamana ya kusimamia fedha za nchi hii hawana uchungu wa kusimamia fedha za nchi hii. Kunahitajika nguvu ya ziada, kunahitajika mkono wa chuma kusimamia watu waliopewa dhamana ya kulinda fedha zetu; kwa nini nasema hivi? Tunataarifa hapa ya madeni kwa mfano ambayo hayakupelekwa kwenye mifuko ya hifadhi (makato).
Mheshimiwa Spika, unakuta Halmashauri ya Mpanda kwa mfano, hawakuwasilisha shilingi milioni 56.52 lakini kwa sababu mifuko yetu inavifungu vya adhabu vya faini inayotolewa kila mwezi kwa watu ambao hawapeleki michago; leo Mpanda adhabu ni shilingi milioni 514. Tuje Bunda, walitakiwa wapeleke shilingi milioni 56, hawakupeleka; faini shilingi milioni 114. Shinyanga, walitakiwa wapeleke shilingi milioni 205 hawakupeleka. CAG anasema eti faini imeenda mpaka shilingi bilioni 45, sisi tunajiuliza hawa watu walizembea muda gani mpaka faini zika-accumulate to this sum? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wamepewa dhamana. Hivi ni vitu ambavyo kama chain ya Serikali inafanya kazi ipasavyo, kuanzia Wakurugenzi, kuanzia Wakuu wa Mikoa, kuanzia Mawaziri wangeviona hivi vitu; huwezi kukaa usubiri CAG aje aone hivi vitu. Nilisikia hapa watu wakizungumza kuhusiana na CAG jukumu la controllership la CAG kwa mujibu wa Ibara ya 143(2)(a) ya Katiba kwa sababu kuna maeneo matatu ambayo ni majukumu ya CAG.
Mheshimiwa Spika, udhibiti wake uko kwenye (a) kuhakikisha kwamba fedha zozote zinazokusudiwa kutolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali matumizi yake yameidhinishwa na kwamba zitatolewa kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 136 ya Katiba hii na iwapo watatosheka kwamba masharti hayo yatatekelezwa ipasavyo basi ataidhinisha hizo fedha zitolewe. Hiyo ndiyo udhibiti, role aliyopewa CAG. Sasa mnataka CAG akafanye kazi ambazo wanatakiwa wafanye Wakurugenzi huku ya kukimbizana hela? Come on! (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, hivi tunsema tumeajiri watu wa kazi gani? Ndiyo maana nikisikiaga eti imeundwa task force, nasema task force ya nini? Yaani mmeajiri watu, mnalipa watu mishahara, wamesababisha tatizo, kuenda ku-rectify tatizo mnaunda task force? For what? For what? Kuna tatizo kubwa sana la mfumo ambao lazima wafanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili; ni bahati mbaya natakiwa nijibu zangu tu, yaani ningekuwa nachanganya na nyingine watu hawajali. IPTL, hizi fedha hizi wanazoenda kulipwa ni za watu kutokujali, ni deal tu, kwa sababu Serikali ilienda kuweka fedha kwenye Escrow Account. Ule mkopo ulitakiwa ulipwe Escrow Account haikulipiwa. Si mfuate maneno ya mtaani wakati ana watu. Nimesema tu nachanganya; watu hawajali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, SYMBION katika taarifa ya mwaka jana alilipwa zaidi ya milioni 300 ambazo hakutakiwa apewe, watu hawajali. Tunataka mjali. Siyo sifa kupanda VX na kuwa Waziri pekee, siyo sifa kupanda VX na kuwa Katibu Mkuu, sifa tendea haki nafasi yako.
Mheshimiwa Spika, Kamati yako ya LAAC, nawashukuru wajumbe wangu tunafanya kazi mpaka saa sita usiku. Siku moja niliwaambia, wa TAMISEMI niliwaambia kazi inayofanywa na LAAC basically ni kazi iliyotakiwa ifanywe na wakurugenzi, ni kazi iliyotakiwa ifanywe na TAMISEMI. Sasa mnatuletea vitu ambavyo vimeshindikana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi vitu vinauma, vinakera, vinachefua. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge mmechangia vizuri. Hivi nchi hii wakurugenzi tunawapataje? Yaani mtu ambaye mmempa dhamana ya kwenda kusimamia halmashauri kitendaji kuwa accounting officer kupokea mabilioni ya shilingi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo kule kwenye halmashauri zinaenda billions of money, ukiuliza mkurugenzi amepatikanaje? “Kashindwa kura za maoni”, wapambe. Maana nimegundua nchi hii yaani ukishakuwa kiongozi, yaani kabla hujawa mtu mkubwa wapambe hawapo ukishapata nafasi zenye uteuzi wapambe wanakuzunguka. Mamlaka ya uteuzi inawezekana group hili la wakurugenzi ninaamini linavurugwa na wapambe zaidi.
Mheshimiwa Spika, naomba sana, kama nchi tuangalie upya namna wakurugenzi wetu wanavyopatikana. Nilikuwa napitia kitu kinaitwa the local government financial memorandum ya mwaka 2009. Kuna kitu kinaitwa responsibilities of the director. Yaani kuna responsibilities hapa kama 12, ni nzito ambazo zinahitaji mtu mwenye weledi na taaluma na uzoefu wa hali ya juu katika usimamizi wa fedha, katika kusimamia watu, katika utawala na mambo mengine.
Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia wakurugenzi tuliokutana nao huko unakuta kakurugenzi yaani katoto, DT ni kama baba yake. Ukiuliza umetokea wapi? “Nimetokea sekta binafsi”, hasemi sekta binafsi wapi. Kwa hiyo, ukiangalia hata wage bill, muulize Mheshimiwa Mwigulu hapo. Wage bill inaongezeka kwa kiwango kikubwa kwa sababu moja kubwa, tunaokota watu nje ambao hawakuwa kwenye mfumo, tunampa nafasi ya kulipwa mshahara mnono. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, turudie utaratibu wa kila wenye vigezo vilivyowazi watu washindanishwe. Mimi nina mifano yangu hapa, mtiririko wa makusanyo ya mapato. Unakuta halmashauri kama Kigoma DC, nadhani, ilikadiria kukusanya shilingi milioni 700 ikakusanya shilingi milioni 688. Kigoma DC, OC iliyotoka Serikali Kuu; yaani hapa kuna watu wameshiba, watu wazima na akili zao, shilingi milioni 688 mwaka mzima. Yaani akili zao zote zile milioni mia 688 makusanyo ya ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukija kiasi cha OC, matumizi ya kawaida walichochopewa na Serikali Kuu ni shilingi bilioni 16.3. Yaani kuna watu wazima wamekaa kule chini wanalipwa mshahara. Hiyo ni OC, sijazungumzia miradi ya maendeleo fedha ilivyoshushwa. Sasa unajiuliza hivi kuna faida gani ya kuwa na wakurugenzi, maafisa mipango na ma-DT kule chini ambao hawako creative ku-deal na vyanzo vya mapato, ama kuhakikisha vilivyopo vinatosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unakutana na mkurugenzi anakwambia kwamba sisi tunafanya shughuli ya kilimo. Kwa kuwa mvua hazijanyesha mapato yetu yameshuka, mkurugenzi! hivi hizi ni akili? Kwamba ameweka pale kusubiri mvua? Sawa, si lazima uwe mbunifu, kama unasubiri mvua kuwa mbunifu na umwagiliaji. Kama huna, tafuta vyanzo vingine, tengeneza fedha itengenezwe. Tuna wakurugenzi ambao hawana uwezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana Serikali iweze kutekeleza wajibu wake ipasavyo. Madeni ya wazabuni, tumeweka maazimio yetu naamini hayajabadilika, ni yale yale tu, kwa hiyo, tutayapitisha tu haraka haraka.
Mheshimiwa Spika, madeni ya wazabuni ni crisis nyingine, alisema Mheshimiwa Hawa Mwaifunga hapa, kwamba hii ni sampling. Si mkaguzi amesema bilioni nane point kadhaa, sisi tumekutana na halmashauri takriban 79 kwenye hii mikutano miwili. Hii juzi tumekutana na 39. Kwa fedha tu za ndani za halmashauri pekee hii taarifa ya CAG inazungunguka mara mbili. Si alisema shilingi bilioni nane, tunazungumza hizi halmashauri ambazo tumekutana nazo sasa hivi, na hazifiki 40; hamlipi fedha za wazabuni. Sasa tumeingia sisi kufanya kazi ya Serikali. Mnajua mlichofanya? Mkiambiwa mdawaiwa shilingi ngapi na wazabuni? shilingi kadhaa, mwaka huu mmefunga kiasi gani? Wakasema hapana tumetenga kidogo. Ndiyo allocation mnaenda kufanya Disemba? Ndiyo; fanyeni reallocation, mwaka ujao shilingi ngapi.
Mheshimiwa Spika, yaani sisi tunaweza kuwa na vikao vya Kamati kuwafanyia mambo ambayo mlitakiwa mfanye ninyi. Kwa hiyo, kila mkurugenzi aliyekuja kwenye Kamati yetu tumeshampa mpango wa kwenda kulipa wazabuni wote. Lakini najiuliza; kwa nini sisi wajumbe wako tukeshe, yaani sisi tukeshe halafu jamaa wapo hapo, haiwezekani. Natambua kazi ambayo Mchengerwa ameanza nayo, natambua, lakini tunasema hivi, kama Mheshimiwa Mchengerwa hamtatatua dudu la wakurugenzi wa hovyo wanaopatikana, wasiokuwa na uwezo; siyo wote, kuna ambao wanaweza, niseme neno baadhi, wasiokuwa na uwezo. Nakwambiaje, utaishia kutumbua. Yaani itakuwa miaka yako inaisha unatumbua, ukimaliza kutumbua huyu, unakuja unatumbua mwingine halafu fedha ya umma imepotea. Tuanze kutibu tatizo from the core tuangalie source.
Mheshimiwa Spika, sasa nashauri, yeye ni Waziri bwana, mimi sina access na Mheshimiwa Rais; akamshauri Mheshimiwa Rais ili aliangalie hili eneo kwa mapana na mawanda yake kwa sababu kuna impact kubwa sana tukiwa na wakurugenzi wazuri kule chini. Yaani impact kubwa ya kimapato ya kiutendaji na kiufanisi. Tufikirie nje ya box. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni la madai ya wafanyakazi, bilioni 119. Sasa ndugu yangu Simbachawene naona hayupo; amekuja hapa katutajia figure zake kaondoka. Sasa hajatwambia katika figure zake zile Serikali Kuu ni ngapi, halmashauri ni ngapi. (Kicheko/Makofi)
SPIKA: Usiwe na wasiwasi Waziri Mkuu yupo.
MHE. HALIMA J. MDEE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA Bunge YA HESABU ZA SERIKALI ZA MITAA (LAAC): Mheshimiwa Waziri Mkuu yule kijana wako; amekuja ametutajia figure zake kaondoka, si ndiyo? Sasa mimi na timu yangu kwa taarifa ambayo mpaka tunawasilisha taarifa yetu Bungeni na kwa Spika na ambayo Mock LAAC zilivyokaa zimethibitisha ni kwamba kwenye halmashauri kuna bilioni 119 hazijalipwa. Hii taarifa imeeleza kila halmashauri inadai kiasi gani. (Kicheko/Makofi))
Mheshimiwa Spika, wanakuja watu wa Wizara tunawaambia okay, Wizara ya fedha ninyi si mmesema mmelipa bilioni ngapi, wanatutajia figure za kutisha ili kukupoteza confidence. Sawa basi twambie hivi, halmashuri hii mmelipa nini, halmashauri hii mmelipa nini, wanakimbia, hawana majibu. Sasa sisi tunasema hivi, mpaka sasa licha ya majibu aliyoyatoa kaka yangu Simbachawene hapo, ya kwake, ambayo hayajawa verified, Serikali inatakiwa ilipe madai ya watumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jesca amezungumza hapa, tulikuwa Kigoma nadhani kama siyo Kigoma ni halmashauri moja wapo. Yuko DT…
(hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie. Halmashauri mojawapo, Kigoma DT amekaa pale anatujibu maswali amenyong’onyea. Sasa Jesca akafanya utundu kidogo, akachukua kile kitabu akaanza kuchambua baada ya kusikia watu wamejitambulisha. Kumbe yule jamaa DT anaidai Serikali shilingi milioni 40, yaani amekaa pale ndiye DT halafu ndiyo tunategemea yeye atupe majibu, kalipeni watumishi wa umma. Kujisifu kwa mbwembwe hakusaidii, mbwembwe zitajijibu zenyewe kwa matendo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa sehemu ya tatu, tunaomba sasa Bunge likubali mapendekezo yale ya Kamati kama nilivyoyasoma na kama ambavyo Hansard imeyaingiza. Baada ya kusema hayo nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja ili mapendekezo yetu ya Kamati yaweze kupita. (Makofi)