Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. DEUS C. SANGU – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI NA MITAJI YA UMMA (PIC): Mheshimiwa Spika, naomba kwa moyo wangu wa dhati kwanza nitoe shukrani zangu kwa waheshimiwa Wabunge wote waliochnagia hoja ya Kamati yetu ya PIC, Kamati muhimu ambayo inasimamia uwekezaji wa mitaji ya umma. Nitambue michango ya Waheshimiwa Wabunge wote ambao idadi yao ni takriban Waheshimiwa Wabunge 30 michango yenu tunaithamini na kama Kamati imetupa nguvu ya kusonga mbele, tumeona kweli Waheshimiwa Wabunge mnatuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaenda kwenye kutoa ufafanuzi wa hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge na hoja zangu za msisitizo kuna jambo ambalo naomba nifanye kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameweka msukumo wa pekee katika kuwekeza mtaji katika mashirika ya umma.

Mheshimiwa Spika, hadi ninavyokuja hapa kuwasilisha ripoti ya Kamati yetu Serikali imewekeza katika mashirika ya umma mtaji wa trilioni 73.36. Na kwa miaka mitatu ongezeko lilikuwa ni shilingi trilioni 8.17. Ni uwekezaji mkubwa. Huu uwekezaji umewekwa kwenye mashiirika 304. Mashirika yameongezeka kutoka 298 yamefika mashirika 304.

Mheshimiwa Spika, taifa kuwa na state enterprise mashirika yake ni jambo ambalo ni muhimu sana; na mashirika haya yana maana kubwa katika ku-drive uchumi wa nchi wa nchi. Moja katika jambo ambalo Serikali iliamua kuanzisha hakuna shirika hata moja lilianzishwa kwa bahati mbaya. Kila shirika la umma lililoanzishwa lilikuwa na misingi yake na lina maana kwa ajili ya kusukuma jambo fulani katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nitaongelea swala ambalo ndilo jambo la msingi ndilo core objective, hasa yale mashirika yanayofanya biashara kuhakikisha kwamba yanaleta faida na kupeleka gawio kwa Serikali. Hapa katika Kamati yetu tulitumia muda mwingi kuchambua haya mshirika umma. Kati ya mashirika 66 ni mashirika 25 tu yanayofanya biashara ambayo yako chini ya sheria ya makampuni sura ya 188, ni mashirika 66 tu.

Mheshimiwa Spika, kati ya mashirika 66, ni mashirika 25, taasisi 25 tu ndizo zimeweza kupeleka gawio kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Hapa naomba nitoe ufafanuzi. Shida ni kwamba sheria zipo lakini kuna taasisi zinakaidi kupeleka gawio kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Sasa katika hizo taasisi 25 kichekesho ni taasisi tatu tu ndizo zinachukua asilimia 93 ya fedha zile shilingi bilioni 372 zilizowekezwa kwenye Mfuko wa Serikali. Hapa nakupa task Mheshimiwa Waziri wa Fedha; yaani una taasisi 66 taasisi 25 hizo zilizojitoa kimasomaso, na hilo si jambo la kufanya kama ni charity contribution, ni jambo la kisheria, ni takwa la kisheria, ni taasisi tatu tu ndizo zimepeleka asilimia 93.

Mheshimiwa Spika, kuna category ya pili ni wale wanaotakiwa kupeleka mapato ghafi, mashirika, taasisi zile ziko 25, hawa nao ni taasisi chache zilizopelekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, watu wanajifanyia wanvyotaka. Kuna category ya tatu ni taasisi zile zinazobaki ambazo hazijawekewa utaratibu. Hizi ni kwa hiyari, wanavyojisikia hapa napo kuna kichekesho.

Mheshimiwa Spika, taasisi hizi kuna taasisi nitawapa, na siku natoa taarifa hapa uliniambia rudia mwenyekiti sehemu hiyo. Kuna taasisi inaitwa Bodi ya Chai Tanzania. Hawa wao kwa miaka mitatu kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali walipeleka shilingi milioni mbili. Pale nilipokuwa nasoma ulidhani labda kuna error, milioni mbili. Maana yake ni average ya shilingi laki sita na nusu kila mwaka ndiyo wanapeleka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Huu ni utani na hauwezi kukubalika; na ndiyo maana unaona state enterprise nyingi zinakufa kwa sababu kuna mizaha mingi.
Mheshimiwa Spika, nataka niseme tena kwa uchungu mkubwa, yule binti ni DG sina maana ya kum-offend amekuja pale ana timu ya wataalam wafikao 20, wamekuja pale Kamati tume-raise maswali zaidi ya 15, 16; alifika pale aliweza kujibu maswali mawili tu. Nilimtimua nikasema wewe sasa hujui majukumu yako, nikawaambia sasa huyu timu aliyoleta hapa imetumia zaidi ya shilingi milioni 10 anapeleka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali shilingi milioni mbili ni utani kwa Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo haya mambo yanafanyika na hapa tusiposimama madhubuti na hapa Kamati yetu mbele ya Bunge lako Tukufu nasema kwa haya mashirika ambayo kisheria yanatikiwa hayapeleki wasiwe wanakuja hata kwenye Kamati yetu maana wameshindwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo haya mambo yanafanyika na hapa tusiposimama madhubuti mbele ya Bunge lako Tukufu na hata kwenye Kamati yetu nasema, kwa haya mashirika ambayo kisheria yanatakiwa kupeleka, lakini hayapeleki wasiwe wanakuja hata kwenye Kamati yetu, maana yake wameshindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili jukumu tunapotoka hapa ndiyo kazi ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwenda kufanya. Wakiacha zile fedha zibaki kule maana yake ni nini? Watu si fedha zinabaki kwao, hawajapeleka kwenye Mfuko ambao ungeenda kujenga zahanati na vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanaanza kugawana honorarium, wanaanza kugawana bonus, wanaanza kutafuta safari za nje, wanaanza kutafuta semina yaani wanatafuta wafanye tu nugatory expenditure, matumizi yasiyo ya lazima, kwa sababu hela ziko kule hamna anayejali kwenda kuzifuata. Baadaye tutakuja hapa tuunganishe mashirika, tutakuwa tunafanya biashara ya kuunganisha, tutaunganisha baadaye state enterprises zote zitaisha hatutakuwa na taasisi ya Serikali. Kwa hiyo, hili jambo naliongea kwa uzito wake na kwa uchungu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la gawio, category ya wale wanao-fall kwenye Sheria ya Makampuni, ile Sura 180 waka-comply wote. Kama hao 66 wote waliopata faida na wanatakiwa wapeleke, wakapeleke hiyo kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na tuje tupate taarifa ndani ya Bunge hili, la sivyo tutakuwa tunafanya mchezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wale ambao wanatakiwa kutoa asilimia 15 ya mapato ghafi, gross revenue wanatoa asilimia 15, hao nao ziko taasisi 25. Waziri wa Fedha akafanye yeye ndiyo anamsimamia Msajili wa Hazina, akahakikishe pia mashirika hayo yanapeleka fedha kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bila kufanya hivyo tutakuwa tunacheza dilly-dally na haya mashirika tutaona watu tu wananenepa, wanatembelea magari mazuri, wanaishi maisha ya raha na starehe, kumbe kuna wananchi huko kwenye zahanati wamekosa dawa. Kuna wananchi huko kwenye vituo vya afya wanakufa kwa sababu hatujatimiza wajibu wa kuyasimamia haya Mashirika ya Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala hilo la Mashirika ya Umma ambayo shilingi bilioni 272 katika uwekezaji wa trilioni 73.32 ni utani. Sawa, kuna yale yanayotoa huduma, hata haya yanayofanya biashara? Yanaweza yaka-raise trillions of monies zikaingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo hii ni assignment ambayo kama Kamati tumei-pose na tutakuwa wakali na ukali wetu watauona, Waheshimiwa Mawaziri watapata message kwamba kuna moto unawaka huko PIC. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naondoka kwenye suala la gawio, naingia katika suala la mikopo chechefu. Mikopo chechefu nitaanza na suala la SUMA JKT. SUMA JKT ni kampuni iliyoanzishwa, kwanza ni kampuni ya mkakati, ilikuwa kama shock absorber. Inapotokea taasisi nyingine zinafeli za private tuwe na state enterprise inaweza ika-take off. Sasa hapa kuna shida, SUMA JKT tuliamua kuiua, SUMA JKT ilipewa mradi wa matrekta na zana nyingine za kilimo wa shilingi bilioni 61. Waliletewa, yaani hawakupewa fedha walipewa mkopo in terms ya vifaa.

Mheshimiwa Spika, lengo lilikuwa ni ku-boost sekta ya kilimo inayoajiri Watanzania zaidi ya asilimia 70. Kwa bahati mbaya pale palienda kufanyika uhuni wa ajabu. Yale matrekta yaligawiwa kama sadakalawe. Waheshimiwa Wabunge wa wakati huo na wengine wapo walichukua matrekta yale, ma-DC, Wakuu wa Mikoa na viongozi wengine wa Serikali waligawana. Mtu mwingine alikuwa anaenda kuchukua hadi matrekta matatu. Madhara yake ni nini? Ndani ya SUMA JKT pale kwenye kipengele tu cha mkopo wa matrekta tumezalisha shilingi bilioni 38.77 kama mkopo chechefu, haulipiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, orodha hii ipo na tumewaomba SUMA jana nilitaka nije nao hapa mimi ninge-display kwa majina. Kwa haraka haraka ningepiga sampling hapa. Naomba Bunge lako tupate orodha ile kwa rejea, kama Kamati tunayosimamia mitaji ya umma tuone ni namna gani Serikali ita-recover hizi fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, category ya pili, ilikuwa ni vifaa. Kuna vifaa pale SUMA JKT vya shilingi bilioni 11, vipo pale haviuziki. Katika hiyo pesa waliyopewa ya vifaa vya shilingi bilioni 61, vifaa vya shilingi bilioni 11 haviuziki. Mkulima akienda pale vimepitwa na wakati, haviwezi kutumiwa. Madhara yake ni nini? Madhara yake ni kwamba sasa vile vifaa tunaenda sijui kupima chuma chakavu? Sijui tunavifanyaje? Yaani tunaenda ku-sank, tunaenda ku-establish sank cost ya shilingi bilioni 11, yaani shilingi bilioni 11 hivi hivi, vipo pale SUMA JKT.

Mheshimiwa Spika, category ya tatu, ndiyo hayo madeni mengine, wanajitahidi. Naomba jambo moja katika hili na Serikali wako hapa. Kwanza, wakapambane na mkopo wa SUMA JKT. Pili, kwenye kupambana na jambo hili kusiwe na mzaha na asionewe mtu yeyote aibu. Hata kama kwa upande huu ndugu zangu Mheshimiwa Waziri kuna watu wapo wakarudishe hizi fedha za matrekta. Kwa sababu hizi fedha ni revolving fund ambayo itakuwa na-multiply effect ya kwenda kukopesha wakulima wengi na tuta-boost sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumei-paralyze SUMA JKT na hatujaishia hapo, tunaendelea kuiua SUMA JKT. Wametoa huduma Serikalini za kufanya ulinzi, usafi na mambo mengi wanafanya hawa SUMA JKT, wanadhulumiwa hawalipwi. Pale SUMA JKT anapompeleka mlinzi hampeleki bure, Askari yule analipwa mshahara na mnaona askari wa SUMA JKT wanavaa uniform safi sasa SUMA JKT hiyo hela ya kuwavalisha askari na kuwalipa mshahara anatoa wapi? Serikali na taasisi nyingi za Serikali hawalipi. Madhara yake ni nini? Madhara yake ni kwamba hii kampuni inaenda kufa na ikija hapa tutaomba sijui tu-merge, tufanye nini, tufanye liquidation, mambo kama hayo, litakuwa ni jambo la kufanya post-mortem. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili jambo linatokana na kwamba mashirika haya yapo yote 304, hayana instrument ya kuyasimamia. Yupo mtu anaitwa TR, yaani TR ni mtu tu anaenda kutembea, hana instruments, hana meno ya kusimamia hizi taasisi, yaani ukitoa hivi tumekuja PIC kama Kamati sisi ndiyo angalau tuna meno ya kuya-screw haya mashirika. Baada ya hapo Bodi zinajiendeshea mambo. Kuna taasisi zina mambo ya ajabu, bodi fulani iliidhinisha Mkuu wa Shirika moja hivi aliidhinisha bima ya maisha ya Board Members wake na anaulizwa anasema, nimeona niwakinge na risk Board Members wangu, yaanio ametumia billions of monies. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hatuwezi kufanya mambo haya, mashirika yetu yatakufa. Hapo ukiwa na bodi hivi itatokea tu CAG akija tutakuwa tunafanya post-mortem. Lazima TR, Sheria hii Sura 370 ya Msajili wa Hazina irekebishwe, TR apewe meno, asiwe mtu wa kwenda kutembelea na mtu anasema haya yako kwa TR. Yako kwa TR, sawa lakini hawezi hata kuziwajibisha Bodi, hawezi kufanya periodic review performance. Hata KPI zile tunazowapa Wakuu wa Taasisi na Wenyeviti wa Bodi, TR hawezi kufanya, yeye anaenda kutembea tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru Bunge lako kuanzisha hii Kamati ya PIC. Ni moja kati ya Kamati muhimu sana za kusimamia hizi taasisi za umma. Naamini kama Mwenyekiti na Wajumbe wangu wa Kamati tutafanya kazi hii kwa weledi mkubwa ili kuyanusuru mashirika yetu ya umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeongelea deni chechefu hilo la SUMA JKT. kuna mtu anaitwa TEMESA, SUMA JKT anamdai TEMESA alichukua huduma ya ulinzi na usafi shilingi bilioni 1.11. Yaani shilingi bilioni nzima TEMESA wanayo ya SUMA JKT. Mwaka huu SUMA JKT ameingia kwenye competitive tendering, amekosa tenda ameingia private operator. Yule private operator yeye hana shida analipwa vizuri ila SUMA JKT ndiyo hatakiwi kulipwa. Tafsiri yake ni nini? Huku SUMA JKT huwezi kuchukua ten percent lakini ten percent kwa private operator utaipata. Sasa hiyo logic ndiyo hiyo hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana unaona DAWASA watu wametumia maji, Taasisi za Serikali zimetumia maji ya DAWASA ya bure ya shilingi bilioni 13. Shilingi bilioni 13 na Vyombo vya Ulinzi na Usalama tuko hapa, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika eneo hili Waziri anahusika sana, akasimamie vyombo vyake vya Ulinzi na Usalama vikalipe bili ya maji waliyotumia DAWASA. Sisi kama Kamati hatutakubali jambo hili liendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sababu inayokuja kutolewa hii DAWASA yenyewe wanaenda ku-collapse, itakufa. Wanatumia huduma bure, Bunge hili tunapitisha matumizi kwa hiyo sisi tutazipitisha hizi OC za maji unapeleka wapi? Kwa nini wasilipe bili za maji? Hizi OC za ulinzi tunapitisha kwa nini hawalipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona nitolee ufafanuzi wa jambo hili, narudi palepale kwenye mikopo chechefu. Ameongea ndugu yangu Mheshimiwa Bashe hapa AGITF – Mfuko wa Pembejeo wa Taifa. AGITF ilianzishwa tangu miaka ya 90 na lengo lilikuwa kwenda kukopesha wakulima zana za kilimo na pembejeo. Huu Mfuko ukageuka kwanza ukawa unaendeshwa na political interest. Waziri Bashe nikiwa Waziri wa Kilimo nitafanya ninavyojua, nitaenda kwenye sehemu yangu nitawagawia na watu ukiwapelekea kwa misingi hiyo bila kufuata credit policy na mambo mengine umewapa hiyo ni kama umefanya bonus tu watachukua.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana hii AGITF imefika na portfolio yake ya shilingi bilioni 26, shilingi bilioni 20 ni mikopo chechefu. Mpaka Juni 30, shilingi bilioni 20 ni mikopo chechefu, sawa na asilimia 81. Takwa la kisheria ni ku-maintain portfolio ibaki, tunasema portfolio at least ibaki asilimia tano. AGITF nashukuru na napongeza uamuzi aliochukua Mheshimiwa Bashe wa kuvunja management. Bodi mpya namwamini CEO mpya yule ndugu yangu engineer Omary kwa maana ya Mwenyekiti wa Bodi na CEO, amemtoa kwenye private sector, bank wata-drive, lakini wale aliowaondoa haitoshi, hela za umma zimepotea. Kachukue hatua zaidi za kinidhamu na kisheria tuwaone wengine kwenye kesi za uhujumu uchumi, tuwaone watu wanawajibika huko kinidhamu, siyo tu kuishia kuwatengua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kama ukinitengua mimi nimeshajipa tayari gratuity ya shilingi bilioni 20 nimeshajitangulizia mbele, nina shida gani? Wataendelea tu na maisha mengine. Kwa hiyo, Mheshimiwa Bashe katika hili mimi ni mmoja ambaye nime-discuss naye zaidi ya masaa matatu juu ya AGITF. Nimekuja na proposal na ndiyo maana watu walishangaa kwa nini una-propose baadhi ya mikopo ifutwe.

Mheshimiwa Spika, ni principle ya kihasibu, kuna mikopo imeishi pale zaidi ya miaka 30, yaani ilikopeshwa miaka ya 90. Ime-accumulate inasomeka kule kama non-performing loans. Zile hakuna possibility yoyote ya kuweza kuzi-recover zaidi ni ku-write off. Tuki-write off tuna clean vitabu, tunafanya aging analysis ya mikopo. Tukifanya aging tunaya-cluster yale ambayo hayawezekani, we write off hakuna option, hatuwezi kukaa nayo miaka, 100 yale yanayokusanyika tunayakusanya, ndiyo jitihada unayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, USAID wametusaidia IFAD wanatusaidia, TaDB wanatusaidia lakini ili uje upate potential investor kwenye taasisi zetu, hakuna potential investor atakayekuja ku-invest kwenye taasisi yako wakati mizania ya vitabu vyako iko hatarini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nani anakuja kuweka hela kwenye mikopo chechefu asilimia 86? AGITF hii ilikuwa almost a dead state enterprise. Kwa hiyo, sisi kama Kamati tunaosimamia Mitaji ya Umma tutampa Mheshimiwa Bashe backup, tutampa support. Tunaomba tu mambo haya tunayoshauri wakayafanyie kazi na next time wenzangu wamekuwa popular wanaongea mambo ya CAG, lakini huku kwenye Mitaji ya Umma huku tukisimamia vizuri kuna tija kubwa sana. Huku hatutaji wizi, lakini nimekuja na namba, najaribu kutoa vitu hivi, namna gani tunaweza tukaandaa taasisi zetu za umma ili kesho na kesho kutwa ziwe na tija na zisaidie kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwenye Taifa hili. (Makofi)

SPIKA: Haya Mwenyekiti malizia.

MHE. DEUS C. SANGU – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI NA MITAJI YA UMMA (PIC): Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa muda, nina mambo mengi, lakini kwa sababu ya muda naendelea kusisitiza yale mambo ya muhimu. Suala la GPSA ni jipu kubwa kwa sababu taasisi hizi zinaagiza magari yanachukua hata zaidi ya miezi 28, CAG kasema hapa.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa ruhusa yako niseme jambo moja. Lengo la kuanzisha hii bulk procurement ya magari kwa pamoja ilikuwa ni tuwe na volume kubwa ili tukiagiza tupate discount. Sasa hivi hiyo theory haipo, ndiyo maana kila taasisi tulivyoinyang’anya tukampa GPSA tulitamani kupata unafuu, value for money tutaiona. Badala yake sasa imekuwa disaster, bei zimekuwa juu sasa tukatathmini upya jukumu hili GPSA bado analiweza? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda naomba kusema nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na naomba mapendekezo yetu yote 14 tuliyoyatoa kwenye Kamati ya PIC yawe ni maazimio ya Bunge lako.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)