Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge kuhusu Wakala wa Kimataifa wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (International Renewable Energy Agency - IRENA) na Azimio la Bunge kuhusu mapendekezo ya kuridhia Mkataba wa Kuanzisha Taasisi ya Dawa ya Afrika wa Mwaka 2019 (Treaty for the Establishment of the African Medicine Agency - AMA)

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge kuhusu Wakala wa Kimataifa wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (International Renewable Energy Agency - IRENA) na Azimio la Bunge kuhusu mapendekezo ya kuridhia Mkataba wa Kuanzisha Taasisi ya Dawa ya Afrika wa Mwaka 2019 (Treaty for the Establishment of the African Medicine Agency - AMA)

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninaunga mkono Azimio. Kama ambavyo Mwenyekiti wetu amewasilisha sisi kama Kamati tumepata muda wa kutosha kupitia wasilisho la Serikali lakini kuwasikiliza wadau mbalimbali ambao walikuja kuwasilisha maoni yao na ninaomba kutumia fursa hii kuunga mkono hoja na kuomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuridhia ili nchi yetu iweze kuwa mwanachama wa IRENA.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ilikubali kuwa mwanachama mwaka 2009 lakini imetuchukua miaka takribani 13 leo kuja kupitisha Azimio. Zilikuwepo sababu za msingi, tuliuliza kwa nini tumechukua miaka yote hiyo wakati tumeendelea kushiriki? Serikali ilisema, ilikuwa inajipa nafasi ya kuona wale walioingia wamefaidika kiasi gani na baada ya kujiridhisha kwamba walioingia wamefaidika sasa nimegundua ni muda muafaka wa kuingia. Jambo hili ni jema ingawa kuchelewa kwetu kumetuchelewesha kwenye kufaidika na faida ambazo wanachama wengine wamepata.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ndilo eneo ambalo lina umeme wa bure au lina nishati ya bure. Amezungumza hapa Mheshimiwa Masache aina za umeme unaopatikana kwenye eneo hili pamoja na solar energy. Afrika jua lipo la bure, ziko nchi duniani wanavizia jua litoke, siku jua likitoka wanashangilia. Yaani jua linatoka kwa mwezi mmoja kwa mwaka mzima, sisi tuna umeme wa bure kutoka kwenye jua lakini tuna upepo wa kutosha (wind energy). Tuna joto ardhi (geothermal), yako maeneo yamepimwa na umethibitika kwamba yanaweza kutoa umeme wa kutosha lakini tuna maeneo mengi yanaweza ku-generate hydroelectric power.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza Serikali kwa sababu sehemu kubwa ambayo tunataka kutumia ni hydroelectric power lakini bado hatujatumia kiasi cha kutosha fursa hii tuliyonayo. Bado tuna umeme mwingine wa bioenergy sehemu kubwa ya uharibifu wa misitu inatokana na utafutaji wa nishati na watafutaji wengi wa nishati ni wafugaji. Wafugaji wana uzalishaji mkubwa wa kinyesi cha ng’ombe ambacho kinaweza kutumia kutengeneza biogas.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa uzembe ambao tunao ni kwenye ku-transform hizi fursa tulizonazo kupelekea hao wanaotumia zaidi ukataji wa kuni waache kutumia watumie biogas. Kwa hiyo, nadhani huu ni muda muafaka ambao Serikali kwa kuridhia Azimio hili, sio twende kama ceremonial, tuweke mkakati wa kutosha kuhakikisha kwamba sasa tunakwenda kupambana kuvuna hizi fursa ambazo tunazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi jirani wanazalisha zaidi ya megawatt 1000 kutoka kwenye geothermal. Mtu anaweza kufikiri kwamba Serikali itapata wapi pesa kwa ajili ya kufanya jambo hili. Tumeshauri Wizara tutumie zaidi PPP au tuhamasishe watu binafsi kuingia kwenye eneo hili na kazi ya TANESCO iwe kuhamasisha wawekezaji lakini kutengeneza mazingira ambapo wao wanaweza kuwa recipient wa umeme na kuhakikisha watanzania wanapata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuna upungufu wa umeme kwenye nchi yetu na kwenye Kamati tuliambiwa kwamba hata baada ya Mwalimu Nyerere kuingia mahitaji ya umeme wa majirani zetu ni makubwa sana wataendelea kuhitaji umeme. Ni muda muafaka sasa kwa sababu kujiunga kwa Azimio hili kunafungua milango ya teknolojia, kunafungua milango ya mitaji, lakini kunafungua milango ya uzoefu ambao majirani zetu tayari wanao na tayari wateja tunao ambao tunapaka nao kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo tayari yamekwishathibitika, Singida kuna upepo, Kishapu kuna joto lakini Same kuna upepo na maeneo mengine ya geothermal ambayo utafiti unaonesha tayari Wizara ilikwishafanya kazi kubwa lakini shida imekuwa ni kuvutia teknolojia, kuvutia mitaji na kutengeneza sera ambayo inakaribisha watu waje.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, sera tunayo ya ujumla lakini tunapungukiwa sheria mahususi kwenye eneo hili. Tumemweleza Mheshimiwa Waziri na tutaitaka Serikali kutengeneza sheria ambayo wawekezaji ambao wana historia ya kuona kwamba tuna sera zinabadilikabadilika, tuwe na sheria ambayo mtu anaweza kuwa na uhakika nayo. Anapokuja kuwekeza asitarajie kesho au kesho kutwa kujikuta anakosa soko la kuuza umeme au anajikuta anaamuriwa kufunga biashara yake. Tuwe na sheria na sera ambayo Wizara tunaiomba iitengeneze na tuitangaze kuvutia maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naunga mkono Azimio. (Makofi)