Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuweza kuchangia taarifa za Kamati hizi muhimu sana; Kamati ya TAMISEMI na Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla kwamba wamepeleka fedha nyingi sana majimboni kwetu kufanya kazi ya kuhudumia watu wetu katika sekta mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naunga mkono Taarifa na maazimio ya Kamati zote mbili, nami ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi taarifa ni muhimu sana kwa sababu zina cut across katika maeneo yote katika nchi yetu, sasa zikishasomwa napendekeza kwamba kuwe na utaratibu tu wa kujua kwamba yale tuliyotoa mwaka jana yametekelezwa mpaka leo kwa kiwango gani? Tusiwe tunasoma taarifa halafu tunafunika tu halafu tunaacha, hapana tuweke utaratibu wa kufuatilia mambo haya mazito ambayo tumeazimia kwa kila Kamati. Kwa sababu ni mambo ya msingi Wabunge wamechangia, na yameletwa katika Bunge lako Tukufu. Kwa hiyo, ni muhimu sana tupate mrejesho, maazimio ya mwaka jana, mwaka juzi na haya ya leo mwakani tupate mrejesho kujua utekelezaji wake umefikia hatua gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mapendekezo ya Kamati ya TAMISEMI tumesema ni vizuri Serikali ikaweka utaratibu. Mheshimiwa Rais, Mama Samia amepeleka fedha nyingi sana kujenga miundombinu ya elimu msingi, sekondari na afya, lakini unaweza ukashangaa shule ambayo imejengwa kwa zaidi ya shilingi milioni 500 mpaka shilingi milioni 600 na nyingine zimejengwa kwa shilingi bilioni moja na zaidi, lakini watoto wanakaa chini, hawana madawati, viti au meza, au shule inataka kufungwa kwa sababu wamefunga ya vyoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali iweke utaratibu wa kuhakikisha kwamba matundu ya vyoo isiwe ajenda ya kujadili kwenye Bunge hili, ni aibu. Habari ya madawati ya watoto kukaa chini tunapigiwa picha, tunaoneshwa, siyo sawa sawa. Kwa hiyo, jambo hili liwekewe nguvu na litekelezwe na tupate mrejesho kwamba hatua zimechukuliwa kwa kiwango gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya TARURA, kila Mbunge hapa jimboni kwake hata watu wa Dar es Salaam pia maeneo mengi hayapitiki. Sasa maana yake ni kwamba, kama hatutaki mwaka huu kupata ushindi mgumu wa uchaguzi, Serikali kwa makusudi iongeze fedha ya dharura ili wakarekebishe maeneo ambayo hayapitiki, warejeshe madaraja, wajenge mitaro, walete makalvati ili wananchi waweze kuwasiliana katika maeno hayo, na ni majimbo yote. Kila Mbunge akijieleza hapa, kuna malalamiko makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wabunge wengine sasa hivi wameahirisha kwenda majimboni kwa sababu ukifika pale hata nyumbani kwako huwezi kwenda. Kwa hiyo, ni vizuri hiyo hoja itolewe. Kibaya zaidi, fedha iliyotengwa, mwaka wa bajeti huu shilingi bilioni 808 ni asilimia ndogo sana imeenda na Serikali iliahidi kuongeza shilingi bilioni 350. Kwa hiyo, ni lazima kwanza fedha yote waliyobajeti iende na fedha ya dharura ambayo tuliahidiwa hapa iende ikafanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina Kata ya Matongo na Kibazuka ambako ng’ombe za watu zimeenda, mazao yameenda, watu wamepoteza maisha, hakuna mawasiliano kabisa katika Mto Tigite. Kwa hiyo, tunaomba fedha ikienda maeneo hayo pia ni muhimu kuzingatia na Wabunge washirikishwe katika kuboresha mawasiliano katika maeneo hayo. (Makofi)

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Vita Kawawa.

TAARIFA

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa msemaji, ni kweli anayoyasema namuunga mkono. Ni kwamba hata kwetu Jimbo la Namtumbo, barabara zinaharibika sana hasa barabara ya kutoka Lusewa kwenda Msisima na tulitengewa shilingi milioni 216 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo lakini fedha bado hazijaenda na kwa hiyo, mkandarasi hajaenda kazini. Kwa hiyo, barabara imekatika kabisa kutoka Lusewa kwenda Kata ya Msisima. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Waitara, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hiyo taarifa iwe ya mwisho kwangu, kwa sababu mimi siyo mzuri sana katika mambo hayo ya kutoa taarifa. Ndiyo maana huwa siwapi taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka kufanya kazi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa nimeipokea, lakini iwe ya mwisho hiyo. Sitaki nyingine tena. Nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unataka kufanya kazi ya maendeleo katika vijiji vyetu, vijiji na mitaa, yaani Serikali za Mitaa, imetambuliwa kwenye Katiba Ibara ya 145, lakini pia ikaongeza kazi zake Ibara ya 146, ambako kuna Umma wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mipango yote ya Serikali, hakuna mahali kwenye bajeti wamewahi kuonesha namna ambavyo wanasaidia vijiji, mitaa na vitongoji madiwani kufanya kazi yake. Hata namna ya kupata kazi za kawaida, hata posho ambazo wanafanya kwenda kusimamia miradi zinapangwa kutoka Ofisi ya TAMISEMI, zinaenda Mkoani, zinaingia kwenye Wilaya na Halmashauri. Kwenye vijiji pale watu wanashinda kutwa nzima hakuna hata maji ya kunywa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema asilimia 20 inaenda kwenye vijiji, tungeomba tupate takwimu ya Halmashauri ipi imerejesha asilimia 20 kwenye vijiji kusaidia viongozi wale kuendesha Halmashauri zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, posho za Madiwani zimeongezwa mara ya mwisho tarehe 16 Agosti, 2012, miaka 12 mpaka leo. Hao Madiwani, wanalipwa shilingi laki tatu na nusu, na Wabunge ni mashahidi. Madiwani kama kuna msiba, ni wao; iwe kuna sherehe ni wao, watoto kwenda shule, ni wao; kukagua miradi, ni wao; mvua imenyesha, ni wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni wakati muafaka, kwenye bajeti ijayo, Serikali iweke ongezeko la posho kwa Wenyeviti wa vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji, Waheshimiwa Madiwani ili na wenyewe wakafanye kazi. Kama maisha ni magumu kwa sekta nyingine na watu wengine, maisha ni magumu sana kwa Wenyeviti wa Mitaa, Wenyeviti wa Vijiji na Waheshimiwa Madiwani. Hili lizingatiwe na Waheshimiwa Wabunge naomba, kwenye bajeti hii, hicho kipengele lazima kiwekwe kwenye bajeti ya TAMISEMI, ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni vitendea kazi. Ninyi mmezungumza hapa Waheshimiwa Wabunge, watendaji kwanza ni wangapi? Hata asilimia 60 hawafiki. Kwa hiyo, vijiji vingi havina watendaji. Kata nyingi hazina watendaji, na kama wengine wapo, hawana sifa. Kwa hiyo, ukitaka kuimarisha Serikali za Mitaa, ni vizuri tuangalie hivi unampa nani aendeshe kata? Unampa nani aendeshe Kijiji? Hiyo inaenda sambamba pia kwenye na kwenye mikoa yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziara nyingi ambazo tunaangalia kwenye mikoa yetu, wanafanya Wakuu wa Mikoa, sasa waulize Makatibu Tawala, wanafanya ziara kwenda kusikiliza watendaji wenye kero kwenye mikoa na halmashauri? Kuna watu wanaonewa sana, yaani hawapati ziara, akienda ziara, posho mnagawana asilimia 80; hujampa posho, huendi. Huo ndiyo ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba Makatibu Tawala wafanye ziara kwenye Halmashauri zetu, wawasikilize Watumishi wa Umma, wapunguze changamoto, wapunguze malalamiko ili wafanye kazi kwa moyo. Vilevile katika eneo hili, ni vizuri tuweke utaratibu, hivi Mkurugenzi anapatikanaje? Kuna Wabunge hapa wanalalamika Mkurugenzi hana uwezo kabisa, yupo miaka mitano pale. Sasa wanasubiri maendeleo kwa mtu ambaye hana uwezo! Yaani wewe unapanda mahindi kwenye mwamba, unataka kuvuna! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tuangalie watumishi wale na SMT. Kama mtu hana uwezo katika eneo fulani asihamishwe kwenda sehemu ya pili, aondolewe pale awekwe mtu mwenye kwenye nafasi hiyo, mwenye uwezo wa kufanya kazi. Mkitaka matunda na matokeo mazuri, ni lazima muangalie mikoa, Watendaji wa Serikali wenye sifa wale wanaofanya kazi vizuri, wapongezwe. Wezi wote wawajibishwe. Hiyo itasaidia pia kufanya kazi ya utendaji mzuri, na pia kila mtu ajue kwa nini fulani kapata na kwa nini fulani kakosa? Kuwe na vigezo. Hii ni kazi ya Utumishi ya wataalam, hapa siyo siasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikifanyika hiyo, Wabunge hapa hatutalalamika, fedha inaenda kwenye Halmashauri inabadilishiwa matumizi kinapangwa kitu kingine. Mbunge ameahidi kazi ya maendeleo, kile ambacho kimesemwa hakifanyiki, halafu huwezi kumgusa kwa namna ambavyo setup imekaa. Kwa hiyo, nilidhani mambo haya yaondolewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ziara na semina, nililoliona kwa mfano Uchaguzi wa mwaka 2024, uwekwe utaratibu, Wenyeviti wa Mitaa wakishachaguliwa na vijiji wapewe semina, wapate mafunzo. Madiwani wakichaguliwa mwakani, bajeti iwepo, wafundishwe. Huyu sifa yake, anajua kusoma na kuandika, huyu mwenzake ana masters, ana first degree, ni mbingu na nchi, hawakutani. Kwa hiyo, kuwapiga sound ni rahisi. Ni vizuri tutengeneze watu wetu vizuri kuwajengea uwezo wa ku-perform na tunapodai miradi ikae vizuri, maana yake watu tumeandaa wa kusimamia na wenyewe wawe na uelewa pia wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho hapa ni namna ambavyo tunaweza kumalizia shule zetu. Imetengwa bajeti ya TAMISEMI na sasa kuna changamoto kubwa katika Taifa letu. Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI anafanya nzuri sana, hatuna shida naye, lakini tunamwomba na Serikali kwa ujumla, barabara ndiyo siasa, barabara ndiyo maisha, barabara ndiyo mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa majimbo ya vijijini mvua zimenyesha, hata aliyevuna kidogo hata sokoni hawezi kwenda. Kwa hiyo, ni lazima jambo hili kama Bunge tulichukue kama jambo mahususi, tupate azimio na liungwe mkono, na Waziri aje kwenye Bunge atuoneshe mpango wa muda mfupi wa kutengeneza barabara zetu, mpango wa muda wa kati wa kutengeneza barabara na mpango wa muda mrefu. Mpango wa muda mrefu ni kuongeza bajeti. Tunapendekeza iongezeke fedha kutoka shilingi bilioni 808 iende 1.6 trilion ili asilimia 70 ya barabara za vijijini ziweze kutengenezwa, na hivyo tutakuwa tumepeleka siasa nzuri na ushindi wa Chama cha Mapinduzi utakuwa shahiri dhahiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. (Makofi)