Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Issa Ally Mchungahela

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lulindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, lakini pia nikushukuru wewe kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utakapoanza nimeamua moja kwa moja kuondoa takwimu, kwa maana ya kuhakikisha kwamba mchango huu unaishi kwa muda mrefu miongoni mwetu.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyowahi kuzungumza hapo mwanzo, siku za nyuma, kwamba Taifa hili linakosa uzalendo. Tatizo hili limekuwa ni changamoto kubwa ambayo nafikiri tunahitaji kujitathmini na kuangalia jinsi gani ya kuenenda ili kuhakikisha kwamba, uzalendo unapatikana na mambo yanakwenda kama vile tunavyotarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, licha ya kuaminiwa tulikoaminiwa na wananchi, lakini pia wale walioteuliwa na Mheshimiwa Rais au na watu mbalimbali bado kumekuwa na changamoto, kwamba hatuzitendei haki teuzi hizo, wala hatutendei haki kuchaguliwa huko. Kumekuwa na shida ambayo ni ya wazi inayoonesha upotevu wa maadili, hususan katika taasisi mbalimbali ambazo zinafanya kazi zilizopewa mamlaka ya kutenda kwa niaba ya wananchi au kutenda kwa ajili ya Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu itajielekeza katika taasisi mbalimbali, hizi zikiwapo pamoja na taasisi za halmashauri, lakini na taasisi nyingine za kiserikali. Lengo kubwa ni kuwagusa maafisa masuuli ambao wao ndio wamepewa jukumu la kuendesha taasisi hizi kwa ajili ya ustawi wa nchi na ustawi wa wananchi pia.

Mheshimiwa Spika, uzoefu wangu nilioupata baada ya kujadiliana na kuhoji taasisi mbalimbali, kwa maana ya halmashauri tulizohojiananazo katika kipindi hiki kumeonesha kwamba, maafisa masuuli walio wengi aidha hawajui majukumu yao au kwa makusudi kabisa wameamua kukaidi kutoyatekeleza. Hali hii inasababisha athari nyingi sana, athari ambazo zinajitokeza katika sekta nyingi zilizoko hapa nchini, lakini katika taasisi hizo.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa majukumu waliyopewa maafisa masuuli ambao wao ndio wanaendesha hizo taasisi, majukumu makubwa sana. Majukumu hayo mojawapo kwanza ni kutafuta fedha popote ilipo. Lakini jukumu jingine ambalo afisa masuuli analo ni kuhakikisha kuwa fedha hii aliyoitafuta kwa maana ya aliyoikusanya katika maeneo husika, lakini pia fedha ambayo ameipata kupitia Serikali Kuu na vyanzo vya wafadhili mbalimbali kwamba, fedha hizi zinatumika kama inavyostahiki na matarajio ya walio wengi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia, afisa masuuli anahakikisha kuwa anapata mapato kwa kadiri ya jinsi alivyojipangia, kwa maana ya bajeti. Afisa masuuli ahakikishe kwamba, bajeti yake amepata kiasi kinachostahili kwa ajili ya kuiendesha halmashauri au taasisi yake kwa ajili ya ustawi wa wananchi na nchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, afisa masuuli yeye ni msimamizi wa fedha alizokasimiwa kutoka Serikali Kuu au wafadhili mbalimbali; kuhakikisha kwamba fedha hizi zinatumika ipasavyo, lakini pia hazitumiwi isivyokuwa sahihi. Kutokana na uhalisia ulioko sasahivi ni kwamba, maafisa masuuli walio wengi wanalipuuza jukumu hili au tuseme kwamba hawajui kabisa jukumu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maafisa masuuli wamepewa nyenzo nyingi sana, bora na muhimu sana katika kutekeleza majukumu yake. Hata hivyo, inashangaza kwa jinsi gani wanashindwa kutekeleza majukumu haya. Kwa mfano, maafisa masuuli wamepewa mitaji, kwa maana ya nguvu kazi na vyanzo vya kukusanyia mapato hayo. Maafisa masuuli pia wamepewa wasaidizi, kwa maana ya wakuu wa vitengo na wakuu wa idara.

Mheshimiwa Spika, lakini afisa masuuli pia, amepewa mifumo mbalimbali wezeshi ambayo itamuewezsha yeye kufanya kazi kwa umakini na kufanya kazi kwa jinsi anavyotakiwa. Afisa masuuli anacho kitengo cha ukaguzi wa ndani, pia kamati ya ukaguzi wa ndani, anayo pia bodi ambayo inampa ushauri jinsi gani ya kufanya kazi zake. Halikadhalika afisa masuuli kupitia RAS anacho kitengo cha ukaguzi, ufuatiliaji pamoja na tathmini.

Mheshimiwa Spika, hivi vyote vimewekwa kwa ajili ya kumuwezesha afisa masuuli kufanya kazi yake kwa weledi, kama nilivyosema hapo mwanzo. Hivyo, inashangaza kwa nini afisa masuuli anashindwa kuwajibika na kufanya kazi kwa weledi kama si kukosa uzalendo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi kama ni yule mwakilishi aliyepita, yule aliyetoa ushauri hapa, kwa maana ya mchangiaji aliyepita alivyouliza kwamba, kama ingekuwa ni biashara binafsi ambayo mtu anayo kwa resources hizi zote alizopewa afisa masuuli kweli angeweza kushindwa kuifaya kazi yake kwa kiwango hiki? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa ndipo tunapozungumza kwamba, uzalendo katika nchi hii haupo. Sasa, tunayo kila sababu kuhakikisha kwamba tunapambana kurudisha uzalendo.

Mheshimiwa Spika, hali hii ipo katika kila mahali, miongoni mwa wengi waliochaguliwa wanahisi kwamba wakishachaguliwa tu basi kazi yao imekwisha. Wengi hawafikiri kwa niaba ya nchi hii au kwa maslahi ya nchi hii. Walio wengi wanafikiri juu ya maslahi yao binafsi. Wengi tunaendekeza matumbo yetu kwa kweli. kweli tunahitaji kujirekebisha na kubadilika kama kweli tunaitakia mema nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyowahi kusema huko nyuma kwamba, nchi bila wananchi walio bora haiwezi kwenda popote, nchi bila wafia nchi haiwezi kwenda popote. Basi sisi tuliopewa majukumu na madaraka kwa namna yoyote ile tunatakiwa tufikirie jinsi gani ya kufia nchi, na huo ndio uwananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, malalamiko ya ufujaji wa fedha ambazo zinatoka aidha kutoka Serikali Kuu au maafisa masuuli wanazikusanya wenyewe katika maduhuli yao ni mengi sana. Takribani kila halmashauri katika nchi hii ina changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano nilkitolea kwangu kabisa, kwenye halmashauri yangu maana mimi si Malaika na kwamba halmashauri yangu haina shida hiyo; nataka niseme kwamba, ni miongoni mwa halmashauri zenye shida hiyo, tena kubwa. Hivi ninavyosema Mkuu wa Wilaya ametoa maelekezo kwa TAKUKURU kuichunguza Halmashauri ya Masasi DC kwa madai na malalamiko mbalimbali ya ubadhirifu yanayohusiana na fedha za maendeleo ya walizozikusanya, halikadhalika fedha wanazozipata kutoka kwenye vyanzo vingine.

Mheshimiwa Spika, jambo hili si jema. Na ninafanya hivi kwa nia ya kufanya nini, kwamba, tujirekebishe na mimi nikiwapo miongoni mwa hao wanaotakiwa kujirekebisha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja. Nakubaliana na maazimio yote ya kamati zote zilizokuja kuwasilisha hapa. Ahsante. (Makofi)