Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Uchambuzi wa Taarifa ya CAG ambao umewasilishwa hapa na Kamati zetu za PAC, LAAC na PIC, umethibitisha ukiukwaji wa kanuni, sheria, taratibu na miongozo kwenye ukusanyaji wa mapato, usimamizi wa mikataba, ufanyaji wa malipo mbalimbali na hata utunzaji wa Mali za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa ya CAG imeweka bayana udhaifu ambao umeonekana kwenye ukusanyaji wa mapato hususani kwa mfano, TRA kutokusanya shilingi karibu bilioni 890. Kwa kweli hili ni jambo ambalo ni kubwa na Bunge linatakiwa ku-note na kufanyia kazi. Vilevile umebainika udhaifu mkubwa katika usimamizi wa mikataba. Kwa mfano, eneo moja tu ukilitaja la ucheleweshaji wa malipo ya wakandarasi na wataalamu washauri ambao kwa mara nyingine umesababisha riba ya zaidi shilingi bilioni 36. Hii ni eneo mojawapo ambalo kwa kweli linatia ukakasi uendeshaji wetu wa kazi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, taarifa ile imeonesha udhaifu mkubwa katika utekelezaji wa masharti ya sehemu ya 17 ya viwango vya uhasibu vya kimataifa (IPSAS). Katika baadhi ya taasisi unaona kabisa kwamba, watu wanakuja pale kwenye Kamati hawajajiandaa kujibu maswali ya Kamati, wanaonesha kabisa kuna upungufu wa watumishi kwenye kada hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, kwa nini ije kubinika upungufu wa watumishi kwenye hizo kada mpaka watu wengine wanasema tutatafuta mtaalamu mshauri (consultant) wa kuja kufanya review ya asset. Yaani, ni kazi ndogo ambayo inaweza ikafanywa na mhasibu mdogo tu ambaye ametoka shule, haijafanyika. Kwa hiyo, kuna udhaifu mkubwa sana kwenye eneo la utunzaji wa mali za Serikali kwa sababu tu ya kutokufuatiliwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo kama hayo ndiyo yamesababisha Kamati hizi zije na maazimio na mapendekezo ambayo mimi kama Mbunge wa Sikonge ninayaunga mkono na ninaomba Wabunge wote tuyaunge mkono ili tuweze kuwezesha Serikali kufanya maboresho na marekebisho mbalimbali ambayo yatasaidia na kuwa tija katika uendeshaji wa kazi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa mfano halisi, kwamba yamefanyika kwa bahati mbaya, sikubali kama yamefanyika kwa bahati mbaya. Mengi yamefanyika kwa makusudi, mengi yaliyoonekana, yamefanyika kwa makusudi. Haiwezekani wewe kutojua sheria, kanuni, taratibu na miongozo kwa sababu miongozo hiyo ukiwauliza wanasema tunafahamu miongozo hiyo ila tutarekebisha. Kwa hiyo, maana yake wengi wamefanya kwa makusudi, na kufanya kwa makusudi inasababisha hasara kwa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana, haya yafanyie kazi na Bunge likubali maazimio na mapendekezo ambayo yamewasilishwa na Wenyeviti wetu watatu wa Kamati zetu tatu za usimamizi ili kuweza kufanya maboresho. Nitatoa mfano halisi mmoja tu wa hasara ya shilingi bilioni 7.840 katika kampuni ta TANOIL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni ya TANOIL ni kampuni tanzu ya shirika la maendeleo ya petrol Tanzania (TPDC). Kampuni hii imepewa kazi ya kuagiza na kusambaza mafuta. Sasa kilitokea nini mpaka kampuni hii ikapata hasara hii? Kabla hatujaingia kwenye hizi point kuwa kilitokea nini, tushangae kwamba haiwezekani kwamba hasara ya Mwaka 2020/2021 ilikuwa shilingi milioni 166 tu. Sasa ime-jump kutoka shilingi milioni 166 mpaka shilingi bilioni 7.840 kwa mwaka mmoja tu. Ina maana hapo kuna watu waliona pengine labda kuna fursa labda ya transition, wakaona pengine labda hawatathibitiwa na mambo kama yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya tunayoyasema hapa mengine yanasaidia Serikali kuweza kuangalia kwa kina. Hivi kwa nini hasara ipande kutoka shilingi milioni 166 hadi shilingi bilioni 7.840 kwa tofauti ya mwaka mmoja tu. Hilo ni jambo ambalo liweke alarm kwa kila mtu. Ukizichunguza sababu kwa nini ilipatikana hasara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya kwanza, Menejimenti ya TANOIL kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ilikuwa haifanyi usuluhisho wa kila mwezi wa mafuta yaliyokuwa yananunuliwa na kusambazwa. Matokeo yake ilipata mafuta yenye thamani ya shilingi bilioni 1.8, hayakufanyiwa reconciliation na hiyo kusababisha hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, menejimenti haiwezekani isisimamie reconciliation. Lazima kulikuwa na sababu za makusudi. Sasa, Serikali huko watakapokaa wafanye uchambuzi kwa kina, kwa nini hawakufanya reconciliation?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya pili, Menejimenti ilikuwa hainakili mapato yatokanayo na bishara ya mafuta kwenye vitabu. Kwa mfano, shehena mbili za mafuta zenye thamani ya shilingi bilioni 16.2 yaliyopokelewa mwezi Juni, 2022 hadi Mwaka wa Fedha unaisha, tarehe 30 Juni, 2022 yalikuwa hayajaingizwa kwenye vitabu vya hesabu. Maana yake ni nini? Haya yalikuwa ni makusudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya tatu. Menejimenti ya TANOIL iliamua kuuza mafuta kwa makampuni ya ndani kwa bei ya chini kulinganisha na bei elekezi. Maana yake ni nini? Vilevile nyaraka za malipo za makampuni zilipopitiwa na CAG, aligundua malipo yenyewe halisi, yaliyofanyika yalikuwa na bei ndogo kuliko hata bei ambayo ilikuwa imeidhinishwa na menejimenti ya TANOIL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa maana yake ni nini? Hasara hii ambayo ilisababishwa na kutokuwa na kutonakili kwenye vitabu vya hesabu, hasara iliyosababishwa ilikuwa shilingi bilioni 53.7 na hasara ya kwenye nyaraka ambayo inaonesha bei ya chini kuliko hata ile ya menejimenti, shilingi bilioni 30.9. Huu ni upotevu mkubwa sana wa mapato ya Serikali na hii umetokana na ukiukwaji wa makusudi wa sheria, kanuni, miongozo, na taratibu za Serikali. Wale mabwana ni watu wadogo sana lakini waliamua kusababisha hasara kama hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ndiyo sababu Kamati zimekuja na mapendekezo. Kwa mfano, kwenye hiyo ya TANOIL, Kamati imependekeza kwamba tufanye ukaguzi wa kiuchunguzi. CAG afanye ukaguzi wa kiuchunguzi (forensic audit) ambayo itabaini nani alifanya nini kwa jina na makusudi gani. Ikiwa ni kwa makusudi basi hatua zitachukuliwa kipindi hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli lazima sababu za kina zibainike kupitia uchunguzi huu utakaofanyika kwa hao ambao wamehusika, lakini kuna mambo madogo madogo ambayo yanatakiwa yaangaliwe. Hivi kulikuwa na sababu yeyote ya kuanzisha TANOIL wakati tuna TIPER? Pengine TIPER angeweza kupewa kazi hiyo akaifanya vizuri, na pengine tusingeweza kuingia kwenye hasara; au pengine labda Idara ya Serikali ingeweza kufanya kazi hizo. Yaani huu uchungzi utatusaidia kubaini mambo mengi, si haya tu yaliyobainika kwenye hesabu, mambo mengi ili kuwea kuisaidia nchi na kuweza kupata tija ambayo ilitarajiwa kutokana na kuanzishwa kwa hii kampuni ya TANOIL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa kweli naliomba Bunge, kwa sababu mimi kama Mbunge wa Sikonge naunga mkono mapendekezo yote na maazimio ambayo yamelewa hapa na Kamati zote tatu. Basi naliomba Bunge nalo katika deliberations zake liunge mkono ili tuweze kuisaidia nchi kusonga mbele. Tumsaidie Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hawa ambao wanafanya mambo kama haya ni watu tu ambao kwa kweli wameaminiwa kwenye ofisi. Inawezekana asiwe hata afisa masuhuli, lakini wamefanya haya na yanonekana kwenye hesabu ambayo inasababisha hasara kwa nchi. Kwa hiyo ni jambo ambalo ni lazima tuchukue hatua za makusudi ili kuweza kujanga tija katika nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii.